Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Thursday, December 29, 2005
KARIBU BARAGUMU, BLOGU MPYA INAYOFUNGUA MWAKA
NIMEFIKA Toronto njiani nilifarijika kukaa kiti kimoja na ndugu ya jamaa huyu. Tumelonga sana nitamshtukiza na picha ili ajue raha ya blogu inavyotuunganisha. Nimefika kwa mwenyeji wangu wa awali kabla sijamtafuta mheshimiwa Waziri Mkuu si Lowasa Edward aliyechaguliwa na Kikwete kulinda urafiki wao bali huyu katika Blogu za Watanzania.

Ninapofungua barua pepe zangu nakutana na Blogu jipya kabisa la ndugu Mwaipopo. Mnamjua huyu amekuwa mchangiaji wa mada katika Blogu kwa muda mrefu. Sasa amekuja na Baragumu lake hili hapa.

Mwaipopo karibu, umekuja kipindi muwali najua hili ni blogu la kwanza kuandaliwa katika mazingira tofauti tofauti maana maandalizi yalianzia New Jersey na sasa limefunguliwa Alabama.
 
© boniphace Tarehe 12/29/2005 11:43:00 AM | Permalink | Maoni 1
Wednesday, December 28, 2005
UKO WAPI MHESHIMIWA MBUNGE?
WIKI hii nimekuwa katika wakati mgumu sana. Sifahamu kama miaka inaenda hivi kama kweli nitakuja kukomboka na hali hii. Mawazo, fikra na kuchoka akili kumeniandama...sijui nifanyeje na kila nitazamapo sura ya mke wangu na baadaye wanangu nashindwa kuyapeleka macho yangu kukabiliana nao kama zamani.

Nilijiita mzazi bora miaka ya nyuma, nilikuwa nikijitapa sana mtaani hali hii ilitokana na ubingwa wa kujua mbinu za kupanga uzazi. Sikutaka itokee hatari ya mimi kuwa na watoto lukuki hivyo nilimpeleka mama Sikujua kuchukua dawa za kuzuia uzazi mapema baada ya kupata mtoto wa tatu. Maamuzi haya niliyafanya baada ya kumpata Mawazo kidume changu cha kulinda jina la ukoo wangu.

Tangu azaliwe Mawazo na hasa baada ya Mama Sikujua kuchukua dawa za kupanga uzazi, ameondokea kuwa na magonjwa yasiyoisha ya tumbo. Afya yake imekuwa ikizorota na kunipa simanzi. Furaha hapa nyumbani imegeuka taswira hasi, mkondo wa giza na kusudio lisilotazamika.

Wanangu ambao umri bado huu chini wamekuwa na kibarua cha kuambatana nami shambani na siku nyingine kwenda wao peke ya hasa siku ninazompeleka mama yao zahanati. Kila nikirudi hukuta vilio vya watoto hawa ambazo ukiwatazama nyuso zao utabaini kuwa walisahau bashasha karne nyingi zilizopita. Masha huyu mtoto wa pili ndiye hasa ambaye hakauki dimbwi la machozi. Analilia vyakula vitamu ambavyo siku hizi siwezi tena kujibana kuwanunulia hawa wanangu.

Wanatamani mboga iliyoungwa, hakuna mafuta ya kupikia hapa nadhani muongo unaelekea. Nilishasahau kuwa kuna nyama na samaki licha ya kuwa wanangu wanalitazama ziwa na mara kadhaa wameenda huko kuchota maji kila kisima chetu kinapokauka. Mwaka huu msimu wa mavuno umeambatana na kilio, hatukuweza kupata pamba kufuatia ukame, na hii ndogo iliyopo haina soko. Makampuni yanayonunua pamba yamegoma kuja kijijini kwetu kwakuwa hakuna mavuno mengi.

Inatubidi kutembea mwendo wa siku mbili kwa miguu ili kulifikia gari linalonunua pamba. Gharama za kusafiri kwa basi nadhani ni kubwa kuliko mauzo ya pamba yangu. Hakuna chakula cha akiba maana mahindi nayo yalikataa kuvunwa mwaka huu.

Sherehe za Krismasi nashukuru zimepita, ilikuwa ni wakati mgumu sana hapa nyumbani. Mama Sikujua mgonjwa huku watoto wakililia nguo mpya. Sasa nasikia kuna hizi za mwaka mpya. Kijijini kwetu kutakuwa na hotuba ya Mbunge tuliyemchagua ikisomwa na Mwenyekiti wa Kijiji. Ngoma ya mgambo imepigwa kuwa lazima tuwe katikia mti wa mikutano na familia zetu kusikiliza hotuba hiyo.

Nawaza siku hizo itakuwaje maana Mbunge huyo hatakuwepo ...amekwenda kusikiliza Bunge jipya. Nasikia tutaweza kumuona akizungumza Bungeni kupitia Tivii aliyoiweka hapa kijijini. Haka kachombo kalichangia sana mheshimiwa huyu kupigiwa kura. Baada ya kushinda ametuachia hapa kijijini lakini tangu atuachie hatujawahi kutazama picha kufuatia kijiji hiki kuwa kimojawapo katika vijiji vilivyowekwa katika ndoto ya kupata umeme. Wanasema haka kativii hakatumii betrii hizi za Matisushta ama zile za National. Kazi ipo na wanangu wanataka kuwa nadhifu siku hiyo ili wasichekwe na wenzao pale watakapokuwa mbele wakitazama picha za mheshimiwa mkombozi wa jimbo letu.

Wakati fikra hizi zinaujaza moyo wangu, namuona mwanangu Masha anakuja kashika kijibarua. Hapa nakitazama kinaonyesha kutoka shuleni. Hii ni michango mipya ya mavazi ya kumpokelea Mkuu wa Mkoa mara shule itakapofunguliwa. Nasikia Masha atakuwa miongoni mwa Chipukizi na hivyo natakiwa kununua sarawili jeusi na shati la kijani kwa ajili ya Masha. Nashika kichwa sijui nitapata wapi fedha za kutimiza matakwa ya Masha.

Ghafla nasikia kilio ndani, ni mama Sikujua anatoa kauli ya kuhitaji msaada, tumbo linamkata na sijui nitamfikishaje hospitalini. Mara ya mwisho tulijitahidi kufika na kuishia kuandikiwa karatasi ambalo siwezi kulisoma zaidi ya hizi herufi sijui ASP. Tuliambiwa twende na karatasi hilo katika duka la dawa la Daktari Nonino lililopo nje ya Hospitali ya mkoa. Kufika huko nilitajiwa fedha ambayo sikuwahi kuota kuisikia katika maisha yangu miaka hii kumi ya Rais Mkapa.

Tukaamua kurudi huku mama Sikujua akilia lakini tufanyeje. Akarudi nyumbani mwendo wa miguu siku mbili akijikokota na kilio cha maumivu. Safari ile ilimuweka kitandani wiki mbili na ni jana tu alipopata nafuu ya kutoa salamu kwangu. Najuta kwa nini nilimpeleka huko maana ilikuwa kumdhoofisha zaidi. Mama Sikujua analia na ninamtazama anatoa macho huku akionyesha kuniomba kitu. Namtazama na kumkaribia huku wanawe wakiwa karibu na machozi yanamtoka...

Nami nalilia moyoni huku nikiona mke wangu akiugulia mauti. Analia...analia,,,maumivu yanazidi kuwa makali. Nakumbuka ahadi za Mbunge wangu kuhusu afya bure kwa kila raia. Natamani awepo hapa atoe haki hii kwa mke wangu. Nakumbuka kukimbia kwa Mzee Matambala ili anipatie vijimizizi ili nimtulize mke wangu. Kabla sijaondosha mguu nagundua kuwa ananidai dawa alizotoa tiba zaidi ya mara tatu. Nashawishika kuchukua huyu kuku tuliyekuwa tumembakiza hapa ili aweze kuwa hazina yetu ya mwisho.

Ninapomfukuza kuku huyu ghafla inatokea pikipiki barabarani na kumgonga...kuku wangu anakufa na hapo nashangaa kuwa napaza sauti ya kulilia kuku huyu na kusahau maumivu na uchungu wa mke wangu! Mwenye pikipiki katimka na siwezi kumpata...nashia machungu machungu makali na sauti inanitoka ...uko wapi mheshimiwa Mbungeeeeee? Naanguka na kulia huku nikimkumbatia kuku huyu! Ninapoamka nakutana na sura za Sikujua, Masha na Mawazo wote wananitazama huku wakilia...wananionyesha kwa kidole kuwa niingie katika banda langu. Ninapoingia huko nakaukiwa na nguvu naanguka chini na kujikuta keshoye nimezingirwa na wanakijiji!

Nawauliza yuko wapi mheshimiwa Mbunge? Naona mwenyekiti wetu anaelekeza uso wake pembeni yangu...hapa machale yananicheza, kuna mtu kalala kafunikwa shuka jeupe...natoa kelele za uchungu bila kutazama kisha naishiwa nguvu na kuzirahi tena!
 
© boniphace Tarehe 12/28/2005 04:21:00 PM | Permalink | Maoni 0
NINI HATIMA YA UBABE HUU WA MAREKANI?
KUNA msemo wa Kiswahili usemao, "ada ya mja kunena, muungwana ni vitendo" Natumia msemo huu kuonyesha heshima yangu kwa wanaochangia mijadala katika KASRI. Kompyuta ninayotumia inatatizo katika kuweka viunganishi lakini naomba nikidhi ombi la Ndesanjo kwa kuweka makala hii hapa chini kama ilivyochapishwa na gazeti la Mwananchi Jumapili iliyopita. Waweza isoma sasa



NIMEKUWA katika safari wiki iliyopita na wahenga hawakukosea walipotoa msemo wa tembea uone. Niko katika pitapita za kuvuka mageti katika viwanja vya ndege na huko ninakutana na kizaazaa.

Msururu wa kuingia uwanjani katika njia ya wasafiri ni mrefu na inafika nafasi yangu nakutana na bibi huyu anayeonyesha sura ya tabasamu lakini tu na matendo yake ya kinyama kabisa. Haya ndiyo maisha yaliyopo Marekani, kila utakayekutana naye atakuonyesha tabasamu la usoni lakini moyoni si kuwa ana hamu na wewe.

Katika Tanzania sisi si wepesi wa kucheka cheka lakini tufanyavyo hivyo huwa ni kwa dhati kabisa kutoka moyoni. Hapa athari za ubepari zimegueza binadamu kuwa wanyama kabisa. Fikra zao ziko katika kujenga faida tu na utu umewekwa kando.

Napofika kwa huyu bibi ananiambia kukaa katika geti jingine, kauli hii anaitoa akiwa anatabasamu hali inayonipa mkuhisi kuwa huenda kaona nipewe njia bora zaidi. Nadhani unajua kuwa Afrika mgeni hupewa thamani ya kwanza, nadhani kuwa ni hili linalofanyika hapa...baadaye nang'amua kuwa sivyo!

Tangu kumeingia hili suala la ugaidi mataifa ya Afrika nayo mengi yamejumuishwa katika orodha ya nchi za kigaidi. Kisa eti ni umaskini wa nchi hizo. Nini maana ya umaskini wa nchi na ipi faida ya utajiri wa taifa moja ambalo raia wake wa hali ya chini wanalia katika hatari kubwa?

Hii ndiyo taswira ya Mrekani, taifa lenye uchumi bora kulingana na takwimu za Benki ya dunia na IMF lakini nchi yenye ufa mkubwa kati ya maskini na tajiri. Nasikia hii ilikuwa pia sera za awamu ya tatu katika Tanzania. Sera za kukuza uchumi kwa kufuata takwimu za Benki la Dunia na IMF. Vyombo hivyo ni makuwadi sawia wa Marekani na ili taifa liweze kukubalika kuwa linatanua uchumi wake na kuingizwa katikia takwimu zake lazima kuwe na hali ya kukubali magandamizo na manyanyaso ya Marekani.

Tanzania ilikubali, hoja ya kwanza ni huko kubadilishwa kwa Hati za kusafiri kwa lengo zikidhi matakwa ya kusomeka na kompyuta za Marekani. Tukabebeshwa mzigo wananchi bila kupenda na sasa cha moto tunakiona. La pili ni kupitishwa kwa kishindo sheria ya ugaidi. Sijui ugaidi ni nini hapo Tanzania, nadhani ni siasa za CUF na CCM!

Basi kutokana na haya masuala ya kukumbatia sera za Marekani basi nikaanza kupata adha ya kukaguliwa na kila kifaa cha teknolojia. Jamaa hawa hawakutosheka na baada ya kumaliza kuna huyu mjinga akaamua kabisa kuanza kunitomasatomasa, ni wazi alinipa mfadhaiko, sijatomaswa siku nyingi lakini hiin ilikuwa kero nyingine kwangu!

Nikajifanya kusahaun yaliyonikuta hapo San Antonio, nikaanza kusafiri na kufika uwanja wa Ohare, Ottawa, yakawa mengine. Hapo nikaanza kuhojiwa maswali makali na kwa tathmini yangu nikaanza kubaini vita vya wazi kati ya Marekani hata na Canada.

Nikaonekana mimi naheshimu sana sheria za Marekani na kutotilia mkazo hizi za Canada. Nikaonekana naona Marekani ni nchi zaidin kulikom ilivyo Canada na ikaja suala la kutoka Tanzania hapo Canada na Marekani zikawa na hoja sawa. Mimi kutoka Afrika nafata nini katika mataifa haya?

Mizigo yangu ikakaguliwa kwa kutoa kitu kimoja hadi kingine. Ikanikumbusha enzi zile elimu ya sekondari Tanzania ikitawaliwa na ubabe. Kipindi cha shule chache, kipindi cha walimu kuwa wafalme hali iliyowafanya kufukuza wanafunzi walivyopenda. Oma ufukuzwe enzi hizo, begi lako na mizigo yako ilikuwa ikiwekwa hadharani kwa ukaguzi ili wanafunzi wengine watizame kama kuna mali zao unataka kuondoka nazo...nakumbuka chuki hii japokuwa ikupata bahati ya klufukuzwa!

Naiita bahati maana kuna dhana niliyojiwekea katika maisha kuwa jambo baya ni muhimu sana likutokee ili uweze kukamilika. Kama mabaya hayakutokei huwezi kujiita fundi wa utatuzi wa matatizo. Fikra hizi zinanikumbusha tena kitabu cha Nelson Mandela "Long Walk to Freedom."

Ninapopita na kuruhusiwa kuingia sasa Canada, nakutana na swali kutoka Marekani. Marekani imekuwa katika mjadala wa kujenga kuta za kuzunguka mipaka yake. Moja ya sababu kubwa zinazotumiwa na wawakilishi wa Republican ambao ndio chanzo cha mjadala huo kupelekwa katika Kongresi ni kuwa hii itasaidia kupambana na ugaidi na pia kulinda kuingia kwa raia wa kigeni kinyume cha utaratibu.

Marekani chini ya George Bush huyu na si yule aliyewahi kusifiwa na Mandela nyakati za kupambana na ubaguzi wa rangi Afrika Kusini, ameamua kutokumbuka tena historia ya Mareakani. Hakumbuki kuwa majimbo kama Texas, New Mexico na sehemu ya Califonia yalikuwa chini ya Mexico. Hakumbuki kuwa nchi hiyo na majimbo yake yote 50 yaliwahi kuwa nchi huru...na tena hakumbuki kuwa umoja huu wa Marekani hautadumu miongo kadhaa ijayo!

Bush na chama chake kinatangaza kujenga ukuta, na swali hili limewashangaza wengi niliokutana nao hapa Canada. Kila mmoja anahoji ujinga wa serikali ya Marekani. Wanauliza je huu ndio mwisho wa ugaidi ambao chimbuko lake ni Marekani? Wanahoji tena vipi kuhusu mauzo ya madawa ya kulevya ambayo huratibiwa na wafanyabiashara wa Marekani ambayo husambazwa katika mataifa mbalimbali. Na je Bush na Republican hawana kumbukumbu ya Ukuta wa Berlin?

Raia wanatamkika kuwepo Mrekani kinyume na utaratibu wanafikia milioni 11. Hawa wanachangia nguvu zao kwa kasi kubwa sana kunyanyua uchumi wa nchi hii. Marekani haikuwahi kuondokana na mfumo wa kitumwa badala yake iligeuza utumwa na kuupatia majina mengine matamu katika taswira ya ulimwengu.

Mabepari wa Marekani wamejenga himaya za maisha yao kutokana na unyonyaji wa wazi. Mishahara wanayowalipa hao wanaoitwa wakimbizi katika Marekani licha ya kuwa ina unafuu kuliko katika mataifa yao ya awali lakini bado ni ya kiukandamizaji sana. Hali ya mabadiliko katika maisha ya Marekani imekuwa mbaya zaidi hasa kipindi hiki cha uongozi wa Republican.

Analaeuskas, mwandishi wa "Discivering America as it is," alifika Mrekani kutoka Urusi akiwa na ndoto tunazokuwa nazo wengi tukiwa nje ya Marekani. Analaeuskas alikimbia kipindi kile cha serikali za kikomunisti na akadhani kufika kwake Marekani ni kuingia katika mbingu ya dunia. Hakukuta hilo na katika kitabu hicho anachambua hali ya maisha ya Marekani na kuonyesha kuwa mazingira yab Urusi kulikuwa na unafuu mkubwa sana kuliko hali hii anayoitazama Marekani.

Mfumo wa kikomunisti tuliwahi kuuishi hapo Tanzania, bado wananchi tunauthamini lakini viongozi wetu tangu awamu ya pili walitamani ukubwa wa Kimarekani wakakimbia mfumo huo na hiki ndicho chanzo cha kupanuka ufa kati ya tajiri na maskini katika Tanzania.

Ubabe wa Marekani unapatikana katika mazingira mengi, nchi hii ndiyo hasa inayochangia Mexico kutokuendelea kutokana na kunyonya kwa wazi vyanzo vya kiuchumi vya Mexico. Licha ya kupakana na Marekani maisha ya Mexico hayana tofauti sana na Tanzania, rushwa ni mdudu mtamu kuliwa lakini sijapata taarifa kama nchi hii nayo ijna sheria inayohararisha rushwa kama Tanzania na sheria ya Takrima iliyowekewa mkono na rais wa awamu ya tatu!

Harakati za kujenga ukuta zinakuja wakati bado athari zilizosababishwa na kimbunga Katrina na Rita hazijaondoka. Mikakati ya kusaidia maskini hasa wenye ngozi kama yangu ni ndogo na sijui zitaonekana lini.

Hali ya kiusalama kwa vikosi vya Marekani katika Iraki na Afghanistan bado si ya kuridhisha. Mazingira ya kuepusha dunia katika janga la ugaidi hayaonyeshio mafanikio badala yake kunajengwa matukio yanayoweza kuhatarisha zaidi mahusiano katika ulimwengu na hivyo kuchochea ugaidi na matukio mengine ya kujitoa mhanga.

Serikali mpya imeingia madarakani hapo Tanzania. Inaweza nayo kufuata misingi ya kutaka sifa za takwimu za kiuchumi kutoka Benki ya Dunia na IMF. Nchi nyingi zilizopata kusifiwa na mashirika haya ni zile zinazokumbatia uchumi wa Kimarekani, uchumi unaotoa fursa kwa wachache kujigeuza mabwanyenye na kuwanyonya wengi. Haya si matarajio ya wapiga kura wa Tanzania.

Watanzania wanahitaji uchumi shirikishi, uchumi utakawaweka wamoja na sio kuwatenga kama awamu mbili zilizomaliza muda wake zilivyoweza kufanya. Sasa hivi kuna matajiri ambao hawakuwahi kuota shida katika Tanzania huku kukiwa na maskini anayefariki kwa kukosa shilingi mia za kununulia panadol.

Watanzania wanataka kuona usawa unaopatikana katika kupiga kura unaelekezwa katika uchumi pia. Hakuna maana ya kuwa na kura moja mtu mmoja huku ikifika katika kutumia rasilimali za umma kunakuwa na wachache kumiliki zaidi ya wengine.

Haya ni maisha ya kibabe ya Marekani na Tanzania inaweza kujifunza vema. Kukosekana ajira nchini kunatokana na kutokuwa na mikakati ya kujenga ajira mpya. Kukosa elimu bora kunatokana na kugeuza mfumo wa elimu badala ya kuwa haki ya watu sasa ni haki ya wenye mali. Kukosa madawa katika hospitali kunatokana na kukithiri kwa ubinafsi katika mifumo yetu ya afya. Wakubwa kuthamini kutibiwa Ulaya na kutotambua shida zinazowakabili wananchi wa chini.

Kuimarika rushwa nchini kunatokana pia na serikali kuona rushwa ni jambo muhimu kurahisisha utawala. Kama sivyo sitarajii kuona bunge jipya likishindwa kuikataa sheria inayoruhusu rushwa au hata mfumo wa mahakama ambao pia bado ni dhaifu katika Tanzania ukiipinga sheria hiyo kwa kuwa inapingana na haki za binadamu. Htujapata jemedari wa kupambana na rushwa na huyu mpya anaweza kuanza kwa kurejesha nyumba aliyojigawia sawa na wenzake katika awamu ya tatu.

Uongozi wa Tanzania sasa unataka vitendo, hakuna haja ya maneno maana tumezungumza sana zaidi ya miaka 40 na hakuna tulichofanikiwa! Tunahitaji kutooneana haya...tunahitaji mapambano mapya yasiyotazama sura!

Inawezekana wazi Tanzania ikajiendeleza na kujitosheleza kama tutakubali kusimamia misingi ya kujiendeleza na kulijenga taifa letu. Twatakiwa kuachana na kujisifu kuwa sisi ni halali kukopa na kuwa tunajenga heshima ya kukopesheka!Tangu lini mkopeshwaji akajisifu, kuwa mimi maskini safi sana hadi jamaa zangu wanakubali kunikopesha. Huo si ustaarabu wa Afrika, waafrika tangu awali tu waoga wa madeni na ndio maana tukakubali kuanza na siasa za kujitegemea.

Umakini unahitajika sasa kinyume na hivyo tutazidi kudhalilika kila tunapotembea katika uso wa dunia. Haya tunayoyaona tunapoingia katika mipaka ya nchi za wenzetu ni ishara kuwa tunatakiwa kuwaonyesha kuwa sisi nasi tu huru na tuna imani na misingi yetu na kimsingi tunajiongoza na sio kuburuzwa!
 
© boniphace Tarehe 12/28/2005 03:26:00 PM | Permalink | Maoni 0
SITTA SPIKA MPYA TANZANIA
KAMA utani hivi ndivyo imetokea hapo nyumbani Tanzania baada ya Spika wa miongo kadhaa Pius Msekwa kujikuta anaambulia aibu ya kushindwa kutetea kiti hicho. Alianza kama utani hivi miaka mitano iliyopita akiwahadaa wabunge kuwa hicho ni kipindi chaker cha mwisho, akadhani hawakumsikia, kisha juzi juzi akajitokeza tena kuomba nafasi hiyo, akisema Wabunge wamemuomba. Vyombo vya habari Tanzania vikaanika bila wazi na blogu nazo zikaweka bayana, ukawa mjadala mkubwa hali iliyoamsha ari ya kutazama mabadiliko na nafasi ya wengine katika utumishi wa umma.

Kuanguka kwa Msekwa kumetokana pia na makundi ya wazi yaliyomo katika chama cha Mapinduzi huku haya yakitokea tovuti ya CCM ilikuwa na picha zinazozunguka na moja ikiwaonyesha Rais Kikwete na Msekwa katika hali ya kuteta. Inaelezwa na wachunguzi wa masuala ya ikulu kuwa, Spika Mstaafu Msekwa aliomba nafasi kukutana na Rais Kikwete kuhoji kama analopendekezo lake katika nafasi ya Uspika. Hilo yaelezwa halikufanyika, lakini kundi lijulikanalo kama Wanamtandao, lililoongoza kampeni za uteuzi wa Kikwete, likiwa na mahasimu wakubwa wa Msekwa lilipinga wazi wazi kuteuliwa kwa Msekwa huku pia kundi lililokuwa likimpigia chapuo John Malecera likirejea tena na kumpigia chapuo Sitta na hivyo kujikuta mtandao wa Msekwa ukimong'onyolewa kama udongo mkavu utiwao maji.

Haya yanaanza kutokea wakati tayari Rais Kikwete amemrudisha bungeni Kingunge Ngombare Mwiru ikiwa ni katika viti anavyoteua Rais na hii ni moja ya zawadi kwa Kingunge kumuunga mkono Kikwete. Mfumo wa siasa za Tanzania saa chache zijazo utatazama jina jipya la waziri mkuu. Tayari picha imeanza kuonyesha kuwa awamu ya nne inaweza kutokuwa na jipya kufuatia misingi ya kubebana kuonyesha taswira ya awali kabisa. Majina mengine ya wabunge walioteuliwa na Rais Kikwete yanatabandikwa hapa baadaye.
 
© boniphace Tarehe 12/28/2005 09:08:00 AM | Permalink | Maoni 3
Saturday, December 24, 2005
MSEKWA ANATAKA NINI?
FIKRA Thabiti alituma bomu kwangu na Ndesanjo jana. Alitaka tuseme, nilichangia na kuahidi kutuma uchambuzi katika gazei la Mwananchi ili kiu yangu ifike kwa wapiga kura wa CCM wajue nini kinachowakabiri.

Materu
nimeandika na makala yangu mwaweza pia kuisoma hapa chini.

Msekwa anataka nini bungeni?

MAISHA ya wanasiasa matamu sana, hayafai kuigwa hata kidogo na kikubwa yamejisimika katika sifa moja kuu uongo. Ni katika sifa hiyo hiyo ambapo Mwanasiasa hugeuka kuwa kigeugeu.

Niombe radhi kwa mifano hii ninayoitumia leo, imekuwa karibu kwangu na hivyo nadhani itachangia kusimamisha hoja yangu. Waziri wa Afya serikali ya Benjamin Mkapa alitangaza mapema mwaka uliopita mkoani Tanga kuwa hatagombea tena ubunge.

Wengi tulifurahi maana tulitambua kukua na kuthamini nafasi ya wakati katika kuongoza. Tulijua sasa Tanzania inaanza kupata watu wanaobaini kuwa madaraka ya kisiasa si ajira bali utumishi.

Nimekatishwa tamaa kusikia huyu huyu sasa ni mbunge wa viti maalum kupitia CCM. Kumbe kutangaza kule kulikuwa geresha, alikuwa keshapata mlango mororo wa kuingilia madarakani, na kwa kuwa alikuwa karibu sana na kampeni za mgombea urais wa CCM, Rais Jakaya Kikwete sina swali kuhusu kuteuliwa kwake kuwa waziri tena.

Haya ndiyo maisha ya wanasiasa, geugeu sana, wanadhani jamii imelala haiwatazami, wanaamini kuwa nchi bila wao haiendi. Kauli za hivi karibuni za Rais Kikwete kurejea kutaja majina ya waliokuwa wakiwania urais naye kupitia CCM kuwa bado anawahitaji inatia maswali kadhaa. Mosi inaonyesha kuwa ukigombea unakuwa muhimu kuliko wengine au unapata nafasi ya kuwa na kura inayohesabika zaidi kuliko sisi akina kalubandika!

Mbona Rais hasemi kumtegemea Mbowe, Lipumba au Senkoro? Mbona hamtaji Mrema, Kyara na au Mvungi? Utajua kuwa siasa za Tanzania sasa zimekuwa sawa na maji ya mtungi mmoja. Wenye nguvu ya kuyanywa ni wale waliokaribu na mtungi huo. Na hapa ni chama cha Mapinduzi.

Moja ya masuala yaliyozungumzwa wakati wa mchakato wa kupata mgombea wa CCM ilikuwa utata wa John Malecera kutolewa mapema. Utafiti usio rasmi ulifafanua hoja ya umri maana kwa umri wake tayari ilishatosha kustaafu na kupumzika. Kwa kuwa siasa ni ajira Tanzania hakuna aliyekubali na sasa familia yake iko bungeni yale yale ambayo kama utachunguza utayakuta yalitawala katika bune lililopita.

Mwanasiasa mimi...sikumbuki ninalozungumza sasa. Nakumbuka ninalosema baadaye. Mwanasiasa mimi...mtalaamu wa hekaya za uongo na uzandiki. Mwanasiasa mimi....mtaalamu wa kulamba matapishi.

Mwezi uliopita nchini Marekani kulikuwa na taarifa ya Ikulu ikipinga kauli za Rais George Bush alizowahi kutoa kipindi cha nyuma. Bush kama muumini wa mfumo wa Kikonsevativu, aliwahi kukaririwa akimtumia Mungu kuwa, "alimtuma kuivamia Iraki jambo ambalo alifanya na sasa anasikia kuwa anamwambia kuingilia mgogoro wa Palestina na Islaeli na yuko radhi kufanya hivyo."

Nch za Mashariki ya mbali ziliogopa kauli hii maana wanamjua Bush kwa vita. Al jazeera ikatangaza na kuonyesha hofu ya mataifa hayo. Ikulu ya Marekani ikapinga na kusema Bush hakuwahi kutamka maneno yanayofanana na hayo. Kumbuka kuna mikanda ya video lakini hii nimeitumia kukupa tu picha ya maisha ya wanasiasa!

Kushindwa kupiga hatamu ya maendeleo kunachangiwa na uongozi wa kubebana. Kuchaguliwa kwa Kikwete kumekuja kama adhabu baada ya kuonekana kuwa Rais huyu anaweza kupambana na tabia za kupinga kubebana katika madaraka. Kama alivyowahi kusema Mkapa, ukitaka kumjua mtu mpe madaraka, sasa Kikwete ni Rais na tunasubiri kumpima baada ya kuchagua baraza lake la mawaziri kama atafuata mfumo ule ule wa funika kombe!

Hakuna chuo cha kuongoza, maarifa ya uongozi hupatikana kutokana na mazingira na hatab kizazi na kizazi. Hoja ya kuundaa watu kujitawala ilikuwapo wakati Tanganyika ikisubiri Uingereza ikubali ijitawale. Mtakumbuka tulivyokabiliana na hoja hii huku tukionyesha ari ya kutaka kujitawala.

Tulifanikiwa lakini sasa kuna wajanja wamegeuza kabisa madaraka ya kisiasa kuwa ajira zao. Inawezekana wamefanya mengi mabaya na sasa wanaogopa watajificha wapi na wanajuan utawala hata kama utabadilishwa hakuna atakayewagusa...lakini wasiombe nafasi ya wakati ikawapitia.

Maneno yangu yote huko juu ni kupuliza tarumbeta tu. Nimesoma maoni ya Watanzania wengi katika mtandao ambao wameonmyesha dukuduku lao kuhusu spika wa Bunge lililopita kuamua tena kugombea. Anasema, mosi ni haki yake kikatiba, je hatambui kwa kukalia kiti hicho kwa miongo mingi amevunja haki za wangapi waliokuwa na uwezo wa kukikalia?

Anasema, ameombwa na wabunge kuwa asisitaafu? Ni wabunge wapi, awataje sasa...nani hajuin kuwa alivunja bunge siku ile Mkapa alipotoa hotuba yake ya mwisho? Nani hajui kuwa tukio hilo liliambatana na Msekwa huyu kufuta uwakilishi wa Wabunge wa Tanzania katika mabunge mengine?

Nani hakumbuki sakata lake na Balozi Mongella, Rais wa Bunge la Afrika na ambaye inawezekana akawa Waziri mkuu ajaye wa Tanzania? Mmemsahau Msekwa inaonekana...alikutana na wabunge wapi maana hawa wapya wamechaguliwa juzi na hana madaraka ya kukutana nao ili hadi wamuombe kuwa spika wao?

Amesahau Msekwa kuwa moja ya hoja katika kampeni zake miaka mitano iliyopita na iliyomrahisishia kushinda ni kuwa alitangaza kuwa hicho ni kipindi chake cha mwisho? Alishinda na sasa amesahau, amekuja na kauli za wanasiasa zilizopitwa na zama za kutaka kuomba ridhaa ya kumalizia kazi walizozianza, kazi zipi hizo Msekwa ambazo zimekushinda kwa muongo sasa wataka kuzimalizia hapa na zama hizi za kasi, ari na nguvu?

Mila za kiafrika hazinipi fursa kutamka mengi, namuonea huruma babu yangu Msekwa lakini naomba kumkumbusha kuwa kwa mila hizo hizo, vijana wa kiafrika tumepewa jukumu la kuwatunza wazazi wetu. Msekwa aseme kama anataka kutunzwa tujue moja na hilo litafanyika.


Ukifatilia mbali utatambua kuwa kipindi cha utawala wa Msekwa kama Spika Tanzania imepitisha sheria mbalimbali na kwa sasa tunahitaji Rais wetu Mpendwa Kikwete kuzifuta. Moja ni hii iliyoidhinisha matumizi ya rushwa. Sheria hii imeipatia Tanzania rekodi ya kuwa nchi pekee inayoruhusu rushwa kwa kupatia sheria muwali iitwayo Takrima.

Haya ni matunda ya Msekwa na bunge lake, wabunge wapenda rushwa wamemuomba kugombea tena...amewaitikia na sasa amechukua fomu. Katika kinyang'anyiri hicho yupo Jamadin Akukweti, Naibu Spika wa Msekwa! Tazama hapa kituko kingine, yaani hawa walikuwa hawawezi kuketi na kuambiana kuwa mzee imetosha na sasa mimi naibu wako nipande kuchota maarifa zaidi?

Au Msekwa haoni kuna lojiki kwa Akukweti kugombea na yeye kwenda kumnadi. Antamani nini...au haamini kuwa Akukweti mgombea ubunge aliyepata pia kuzomewa mbele ya Kikwete, kuwa ameiva na anaweza kusimamia pale aliposhindwa Msekwa?

Katika kinyang'anyiro hiki pia yupo Phillip Marmo, huyu aliwahi pia kushika madaraka ya Akukweti na sasa ni mbunge. Amerudi na anaataka tena. Sina haja sana na mwanamama ambaye amejitokeza wala huyu kijana Elias Mnyeti.

Kwa zama hizi nadhani UVCCM ilipaswa kutangaza kabisa kuwa iko upande wa Mnyeti. Hili lilitakiwa kufanywa wazi na kutangaza kuwa haitatoa mchango wa wagombea ambao wametawala vya kutosha. Najua hili haliwezi kufanyika lakini hata kisirisiri tu.

Hkuna haja ya kukubaliana na wagombea wanaogeuza ofisi za serikali kuwa sawa na taasisi zao. Utakumbuka Waziri Mkuu aliyemaliza muda wake, Fredirick Sumaye aliwahi kutangaza wakati ule alimuachia jimbo mtu wake wa karibu, Marry Nagu tena katika kipindi kigumu baada ya kudondoshwa katika kuwania urais.

Kauli za Sumaye ziliwagusa pia akina Msekwa, ziliwagusa mawaziri wa serikali ya Mkapa ambao sasa wanabipu simu ya Kikwete kutafuta kuitwa tena kikosini. Ziliwagusa wengi wanaoamini madaraka ya umma ni ajira zaoi za maisha.

Huenda watanzania haawajui madaraka ya spika. Spika ni moja ya vyeo vinne vikubwa katika Tanzania. Kinaweza kuwa cha tatu au cha nne. Katika nchi yenye mgawanyo huru wa madaraka cheo hiki nadhani ni cha pili kutoka kwa Rais kufuatia madaraka ya Makamu wa Rais kubakia kama picha isiyo nakazi maalum hadi Rais asiwepo.

Msekwa amekalia kiti hicho kitambo, ameyaona matamu na hataki kung'atuka. Anasubiri aibu ya kushindwa na kwa kuwa ameshajua kuwa ni miongoni mwa vigogo vya CCM anaamini kuwa atapitishwa, na tena bunge kwa kuwa ni la CCM pekee atatangazwa mshindi kisha atatuambia akina mimi tunaoandika makala hizi tuache wivu wa kike?

Siku hizi nimekuwa muumini mzuri wa ahadi za TANU. Ni katika ahadi hizo nakumbuka hii ya kusema kweli daima na kuweka kando fitina. Msekwa anapaswa kuishi kauli zake, anatakiwa kuambiwa na watanzania wamseme...maana si yeye tu mwenye uwezo.

Wazee wasiojenga tabia ya kuamini kuwa kuna watoto wao wanaweza kutunza familia kama wao wanapata taabu sana katika siku za maisha yao. Msekwa anaweza kuwa katika kundi hili, yeye anaamini kuwa Uspika ni Msekwa na Msekwa ni Spika milele. Nadhani wakati muwali sasa akumbuke kuwa madaraka ya umma ni mali ya umma na aukishapewa kumbuka kuwa ni haki ya wengine nao kucheza karata zao ili apatikane manju bora ngoma iweze chezwa usiku kucha. Wasalaam Msekwa...jaribu karata yako!
 
© boniphace Tarehe 12/24/2005 05:58:00 PM | Permalink | Maoni 6
TAFAKARI ZA MAISHA, MIRUKO NA HATI ZA MUUNGANO
SI kawaida yangu kubandika habari fupi fupi lakini imenidi kufanya hivi kwa haraka haraka. Nipo vijijini na hiki kinaitwa Newfoundland nje kidogo ya Ottawa. Hivi ni vijiji vya Ulaya si kama kwetu na hapa nipo kwenye mtandao kuandika mada hii. Phabian Mjarifu atanisamehe kwa kuchelewa kutangaza blogu hii ya kwanza kuzaliwa katika nyumba aliyozaliwa Nyerere. Amekuja nami namkaribisha sana ili aweze kutupa hizi Tafakari za maisha kutoka hapo Musoma. Nadhani nafahamu nini kilichonifanya kushindwa na kutokana na leo kufanikiwa kuwa na viungo nimeweza kuja naye harakaharaka.

Wakati Tafakari za Maisha akiingia kuna mwezetu iliyenibidi kumpiga dongo baada ya kukimbia lakini sasa karudi tazama mavituvitu yake hapa. Nakushukuru Miruko kwa kurudi maana nilikukosa sana. Usikimbie hata kama Kikwete atakupa majukumu aah mzee Malecera maana unakaa naye karibu hapo anaweza kukuchukua umuanzishie blogu lake atakaloliita uzee busara.

Wakati hayo yakiendelea, hali ya Muungano wa Tanzania inazidi kusafiri na safari ya mashua. Inaweza isifike lakini kama ukweli ni kuwa hakuna hati za Muungano nini maana ya Muungano huo. Sasa ,jadala huu kabisa bado mbichi, Ndesanjo toka likizo njoo tuanze kazi.
 
© boniphace Tarehe 12/24/2005 05:33:00 PM | Permalink | Maoni 0
Wednesday, December 21, 2005
ANALALAPI MIRUKO?
U wapi ndugu Miruko, zamani umepotea
Umenifanya kituko, nduguzo kuhadithia
Mbali umetupa mwiko, twakosa wa kupikia
Jamani nielezeni, Miruko amefikwani?

Mavitu nayatamani, mwezi sijayaonea
Labda ameshikwani, Keko ndani kaswekewa
Mgonjwa anawezani, mahututi kalalia
Jamani nielezeni, Miruko amefikwani?

Ya Kikwete na Nyerere, ya mwisho alitokea
Nilimtolea gere, kwa njia alopitia
Nikatamka tawire, kisa kipya pulizia
Kila nilipopitia, Miruko kanyamazia.

Nikajipa hamasiko, utulivu kachukua
Ni kosa lamba ukoko, kwa wazee najulia
Lakini kaka Miruko, Dodoma kalalia
Aha yawezekana, mwanamke kamwibia.

Nikapiga darubini, machinjioni onea
Suraye sijabaini, ni wazi amepotea
Polisi nikafikani, ripoti nikatolea
Nao wakanijibia, suraye hawajatiya!

Huu ni wito wa mwisho, bloguni andikia
Hapa sitaki michosho, mwapaswa mtafutia
Kama anaye kidosho, tujue apoishia
Siwezi kimya kalia, blogiye kusinzia.
 
© boniphace Tarehe 12/21/2005 09:28:00 AM | Permalink | Maoni 3
Tuesday, December 20, 2005
NIPO NAMI DIAMOND
Nipo nami Diamondi, Rais namuonani
Tumekaa kwa makundi, kwa mbele kutazamani
Wamejazana Wahindi, utadhani Uhindini
Moyoni nauguani, kitendawili onani.

Sifa zinatangazwani, kila mtu achekani
Ni mimi nilobakini, machozi ninatoani
Kuna mtu akujani, kwangu nilipoketini
Hasira zamtolani, kisa mimi kuliani.

Namtazama Mkwinda, afike niepushani
Nambiwa nje kaenda, ndani hawezi ketini
Fulana hakuipenda, kwani rushwa yanukani
Wakamwambia huwezi, kuingia ukumbini.

Matangazo yaanzani, Rais kuapishwani
Walombele naonani, suti wamezitiani
Wako wapi masikini,tayari wameachwani?
Kwenye kura tuko sawa, baadaye twatengwani?

Natimka kwa ghadhabu, KASIRINI tuliani
Naona bora kujibu, hoja hii shairini
Hiki wazi kiarabu, ndo kisa sikisomani
Kero sijazisemani, hapa mwanzo naanzani.

Yaliyotokea Zenji, Qudusi atuonani
Mtazirudisha chenji, siku itapofikani
Natangazani rivenji, sina haja kufichani
Sitatumia mtutu, lakini mtajuani.

Nimelisimika jeshi, blogu lafunguani
Hapa hakuna ubishi, naona limeivani
Kwa kasi linashawishi, mawimbi kutimuani
Htutaweza kulala, hadi kazi malizani.

Ndesanjo unafanyani, kikosi kiko mbeleni
Changoja ukipangeni, kazi kianze fanyani
Amri kinatiini, siri yake kushindani
Nani natupa karata, Ndesanjo toa Amri.
 
© boniphace Tarehe 12/20/2005 05:25:00 PM | Permalink | Maoni 3
Sunday, December 18, 2005
HAPANA NIMEAMKA!
ASUBUHI mapema hivi anaamka mama Makene huyu ambaye ni mama yangu mzazi. Hiyo ni miaka ya huko nyuma wakati bado nasoma shule ya msingi. Anaamka katika nyumba ya shule iliyowekewa vioo kipindi cha ukoloni. Vioo hivi vilivunjika miaka kadhaa kabla hatujaamia nyumba hiyo. Ni nyumba ambayo imekuwa ikipiganiwa na Walimu wa shule ya msingi Mabuimerafuru, wanatamani kuishi katika nyumba yenye flemu za vioo huku wakiziba matundu na karatasi za nailoni.

Upepo unavuma kupitia dirishani, navuta shuka kujifunika zaidi na mama kishaamka anawaamsha sasa dada zangu. Hao nasikia wanatoka na dadangu mkubwa na mama wanaambaa hao kwenda kisimani kuchota maji. Ni mwendo wa kama kilomita mbili hivi na upepo unavuma. Hili linanitia simanzi...siwezi kutoka kitandani kumsaidia mama, maisha ya Afrika ukizaliwa Mwanamme basi umekabidhiwa ufalme.

Napitiwa na kausingizi katamu, simuwazi tena mama na ghafla nasikia mlango wa chumba chetu unagongwa na safari hii kwa nguvu. Mama huyo anakoroma kiasi maana tangu atoke kisimani nusu saa imepita na hatujaamka kwenda shamba. Ninawaza njia ya kufikia huko shambani. Njia hiyo imezungukwa na majani marefu kuzidi kimo changu. Hiki ni kipindi cha masika hivyo kuna umande mkali sana. Ili kufika shambani lazima ulowane na fikiri baridi ya asubuhi. Kuna suala la utelezi hili nalo ni jingine, nimeteleza sana lakini sikuwahi kusikia mama akiniambia waweza rudi nyumbani sasa ukapumzike lazima ufike shmbani na huku kazi ni ngumu, jembe la mkono...usisikie!

Kilimo cha mwaka huu kilikuwa safi, tulijituma sana maana ulikuwav mwaka wa uchaguzi, tumemaliza kumchagua Rais ambaye jina lake likifanana na Marehemu hapana nimesahau Hayati Kaka yangu Benjamin Nakuzerwa. Huyu kaka akawa shabiki mzuri sana wa sera za huyo bwana. Mkapa akapiga kelele kuhusun kufanya kazi kwa masaa mengi na kujenga nidhamu. Tukafuata kauli ya rais, tukalima kwa saa nyingi na kwav kujituma sana,

Sikujua haya na baada ya hapo ikawa hiki kinachonifanya kuchukia siasa za kifalme za Tanzania. Benjamin akatushawishi, familia yangu ikakubali kufanya kazi lakini baada ya msimu pamba yetu ikakosa soko. Tulipata mavuno mengi lakini soko hafifu halikuweza kulipa nguvu na nidhamu yetu. Ni mavuno hayo hayo yaliyotakiwa pia kutumika kumtibu Hayati Benjamin kwa ugonjwa wa Kansa, akamaliza vijisenti vile katika matibabu hafifu na mwisho kauli ikamtoka, akapumzika, akalala, akakimbia, akatutoka, akalalama akisema eloyi eloyi lamasabaktani! Kwa heri kaka nitakukumbuka sana milele!

Baada ya hapo nguvu kazi yetu katika kilimo ikafa, sikuona umuhimu wake lakini nikabaki na kilio cha uboreshaji wa huduma vijijini. Juzi kulikuwa na tatizo la maji Dar es Salaam, Rais mpya akatangaza katika sera zake kuwa hilo limeisha tuisubiri tu kuwa kura zetu zitatatua tatizo hilo. Nasikia watanzania wameamini kuwa kura zao zaweza kuondoa kero hiyo na wamezimpa kwa wingi mno.

Katika pita pita zangu nikaona bora kuwasiliana na mama, nikampata katika kile kijisimu chake alichotumiwa na mmoja wa wanae. Nikalonga naye akanieleza tena kilio cha kukosa maji kwani visima vimekauka hivyo wanatakiwa kutembea kilomita zaidi ya sita kutafuta maji ziwani pale kijijini Chumwi au Murangi. Nashika kichwa tena, nakumbuka nilipata taarifa za mradi mpya wa kupeleka maji Shinyanga na Dodoma kutoka ziwa Viktoria. Mradi huu haupiti kijijini Mabuimerafuru, hakuna kumbukumbu kama kutakuwa na mradi kama huu ili uweze kumnusuru mama yangu katika kilio cha kusaka maji maili nyingi huku akisumbuliwa na miguu kwa miaka mingi. Kipindi anachotoka kwenda kutafuta maji ziwani anakuwa kaacha wanafunzi bila mwalimu. Wanafunzi hao hushangilia tukio hilo maana nao huwa darasani bila kuoga kwa siku kadhaa. Tazama shida ya kukosa sabuni na mafuta ya kujipaka, sasa ongeza na maji ya kuoga na kufua huku darasa la kijijini likiwa bado ni lile lisilo na sakafu.

Nimekaa na kukumbuka kuwa kazi ya kuleta maji Mabuimerafuru, Mikuyu, Seka, Saragana na Nyambono imeshindikana kwa miaka 40 tangu uhuru. Ninatafuta njia ya kumtumia mama baisikeli ya kumsaidia kufika huko ziwani...lakini mama huyu mzee atawezaje kuendesha baiskeli nna uzee wote huo. Naogopa kutuma baiskeli hiyo maana yaweza geuka chanzo cha mauti ya mama yangu. Siwezi kujua nini iwe mbinu njema ila katika uchaguzi uliokamilika walipewa ahadi na mbunge wao kuwa kero zao zitaisha. Mbunge huyo aliahidi pia kujenga barabara ile mbaya kuliko zote nadhani katika Tanzania. Alisema jambo la awali litakuwa kupeleka mitambo ya simu bila kujua huko hakuna umeme. Alisema mitambo hiyo itawaunganisha watanzania walioko vijijini na walio mijini.

Akishakuweka mitambo ya simu, kitafuata kuweka viwanda kadhaa vya samaki. Samaki wote wamekuwa wakiuzwa katika viwanda hivyo huku wakazi wa vijiji vinavyolizunguka ziwa wakitangaza mabadiliko ya tabia za ulaji kuwa wanathamini sana makazi ya samaki hivyo hawataki kuwala kabisa! Wameamua kusaka majani na sasa hayapo kutokana na kiangazi, wananchi wanapigana na ng'ombe kusaka majani. Ni vita kubwa na mbunge nasikia ameshakimbilia Dodoma kuwahi kuapishwa. Hiyo ni sherehe kubwa na hatakiwi kuichelewa, Nasikia pia amewahi maana kuna kazi ya kuzungumza na Rais mpya kama anakumbuka kile kitita alichochangia chama wakati ule wa jkukomboa majimbo. Anataka sasa akumbukwe fadhila zake kwa kupewa walau kauwaziri.

Huyu mbunge hakuwahi kufika kumsabahi mama na hata wapiga kura wengine. Mara ya mwisho walimsikia alipotembelea pale Houston Texas kusalimia kimada wake anayemsomesha pale. Sakata hilo liliripotiwa na gazeti moja la udaku na hii ikachangia gazeti hilo kufungiwa. Mheshimiwa huyo amewahi kabisa Dar es Salaam ili kumnunulia kadi ya pongezi Rais mpya. Nani hajui kuwa alikuwa lazima ashinde lakini ndiyo Tanzania na hiyo ni geresha ya kuomba uwaziri na misamaha ya kodi katika biashara zake.

Nalalama na hasira hapa nasikia Melissa ananiita kumbe nilikuwa naota na katika ndoto hii nimetaja sana hofu ya barafu utelezi katika matope pale Ihungo. Nilikuwa pia nikizungumzia kule bondeni tulikokuwa tukichota maji palivyokuwa na utelezi huku giza totoro likigubika misitu ile ya Ihungo. Siku hizi misitu hii imekatwa kabisa, alikuha Mkuu wa shule mmoja mwenye uchu wa kutengeneza pesa, huyu alianzisha mradi wa kuuza mbao na akatumia msitu wa shule kutimiza haja zake. Sasa ukiwa mjini Bukoba waweza kuiona Ihungo juu ya kilima ikiwa tupu, uchi, si kama zamani ikimelemeta na kuzungukwa na kijani cha miti yenye bashasha. Natulia na kusema nimeamka na kazi imeanza.
 
© boniphace Tarehe 12/18/2005 05:50:00 PM | Permalink | Maoni 2
NIMEFIKA CANADA
SAFARI yangu kuja Canada naweza sema imekamilika. Nimeingia Canada baada ya visa kaisi. Nilicheleshwa kufika San Antonio kutokana na askari wa Mipakani kuingia katika basi letun mara kwa mara na kutukagua. Fahamu kuwa nilitoka ukanda wa Mexico na nchi hiyo imekuwa ikiingiza wananchi lukuki Mrekani. Sababu ni kuwa Marekani inachangia umaskini wa nchi hiyo hali inayowafanya raia wake kukimbilia Marekani kila kukicha.

Nilipofika pale nikapewa ndege ya kusubiri saa kama tisa hivi. Nikapita sehemu ya kukaguliwa, yakaanza...nikawekwa pembeni kwa ukaguzi zaidi. Sijui naonekana kama gaidi lakini nilikaguliwa hadin nikachukia. Sasa kuna huyu fala anaamua kunishikashika...nikaona huu mchezo hasa baada ya kumaliza nikampa nami kauli, thanks it was such a wonderfull massage! Ananitazama kwa hasira la kufanya hana nami nachoma ndani.

Kuingia Canada kulikuwa na shida, maswali kadhaa mengi nayajibu lakini kuna binti anasema kuwa nimeonekana kujjali zaidi sheria za Marekani na kukiuka hizi za Canada. Moja sina visa, wakati nilishaambiwa kwa matembezi mafupi sihitaji visa kuingia Canada na Mexico...wengi wamesafiri hivyo lakini kwangu mimi nimekwaa kisiki. Nimekalishwa saa kama mbili huku nikikaguliwa hiki na maswali mengi. Nayajibu sasa kisiasa huku nikitangaza na nia yangu ya kuwania Ubunge mwaka 2010 kwa huyu binti ili ajue Tanzania kwangu ni nchi ila suala sasa ni mtaji wa kufikia huo Ubunge na nimeashaanza na Blogu. Haya niache hizo propaganda, usumbufu umeisha naingia nche kwenye kifusi cha barafu. Kweli Jeff alisema na nimeyaona hapa. Nafika nyumbani na mwenyeji wangu, mkarimu huyu na kisha naanza kubandika maandishi haya huku nikijiapiza kuandika waraka mwingine kuashiria utamu wa barafu hii katika shairi.
 
© boniphace Tarehe 12/18/2005 12:00:00 AM | Permalink | Maoni 6
Friday, December 16, 2005
JEFF NAJA ! WAWEZA KUNYWA MVINYO NAMI?
SIJAANZA safari bado, itakuwa usiku huu. Siku hizi kuna mengi katika safari hizi na hiki kimekuwa kisa cha mimi kutangaza safari zangu. Utaratibu huu si kwa wabunge na marais tu hata nasi wanazuo tunao ili ijulikane wazi tupo wapi inawezekana kukutana na wale niliowasalimu katika shairi langu hapo chini.

Nitaondoka Edinburg usiku huu na kusafiri kwa Basi hadi San-Antonio. Kesho asubuhi sana nitasafiri kuanzia pale na kupitia miji ya Dallas, Chicago na kisha kushuka Ottawa majira ya jioni. Naamini Insharah Mnyezi Mungu Rabuka atajalia safari yangu kuwa salama. Nikiwa huko nitaweya kuwatembelea ndugu na rafiki zangu. Nitaweza kufika Toronto anakoketi Waziri Mkuu. Naweza kutana naye pale ili sambamba na masuala mengine ni kujadili nafasi ya Blogu za Tanzania katika kuleta mabadiliko ya Kiuchumi na Kisiasa Tanzania siku zijazo.

Kazi hii ngumu sana lakini hatupaswi kuiogopa, sasa ni kama wajibu na tunatakiwa kuifanya kwa moyo mmoja. Jukumu lingine ni hili la kuongeya Blogu za Kiswahili na kuzitangaza. Mlioko ughaibuni mnaweza kusaidia zaidi katika hili na kidogo kidogo walioko nyumbani wataongezeka kwa kasi.
 
© boniphace Tarehe 12/16/2005 03:12:00 PM | Permalink | Maoni 1
Thursday, December 15, 2005
SALAMU ZA KRISMASI NA MWAKA MPYA 2006 KWA WANABLOGU WA KISWAHILI

Nimetumia neno Blogu hapa si maana nimelihalalisha. Nipo katika vita ya kulikataa. Nafanya hivi kutokana na mbio za haraka kuweka shairi hili na kuzindua mtindo mpya wa kutoa waraka maana nasikia shairi laingia moyoni kuliko utungo wa aina yoyote uliopata kuwepo katika sura za dunia. Haya hili ni shairi lenu wenzangu. Wananchi wa KASRI mwaweza lisoma maana latungwa na Mwanazuo mwenzenu. Haya nisikuchelewesheni...someni uhondo huu!

Nimeamka salama, namshukuru Manani
Amenijalia mema, haki yangu msifuni
Fikira zimerindima, na kunambia kichwani
Wapaswa shukuru hawa, kwa kazi wazofanyani.

Ilikuwa ni ndotoni, kelele nikapigani
Nikataka nipeweni, kompyuta niandikeni
Vina nikavibaini, na kuiweka mizani
Hulka ikanituma, shairi kulitungani.

Asubuhi ikafika, nikafika KASIRINI
Nikahisi nimechoka, uchaguzi kusomani
Mkono ukatamka, wataka kuandikani
Nikaujibu hewala, shairi ninatungani.

Nikenda Jikomboeni, za jana nikaonani
Harakati kafatani, kichwani nikagusani
Nikarudi kwa Mwandani, Kiswahili katajani
Fikra zikanituma, safari mbele kwendani.

Nikaja kwa Bangaiza, naye kaja kimwandani,
Pambazuko kakataza, CHADEMA na uzunguni
Damija naye kacheza, za kina mama wekani
Mkwinda akafanyani, bora weka shairini.

Nikaja kwa Mtafiti, hewala nikaonani
Yeye amejizatiti, Blogu shabikiani
Huyu mama wa matiti, matako kayaanzani
Nikenda kwa tahayari, hofu yangu Mswahili.

Nikashuka kwa Msangi, kakuta kitangazani
Sijui tapaka rangi, kazi yake kuishani
Wa Kutoka Ugogoni, kwa mwezi huja mojani
Sura kaanza kunjani, Mavitu kutoyonani?

Muwakilishi Vyuoni, muoga namsemani
Mengi yapo najuani, kuleta anahofuni
Bakanja yuko mijini, kisifu ivyojengwani
Nikatambua Ngurumo, ni mtu wa msimuni.

Fatma binti Karama, alikuwa kikaoni
Agenda amezichoma, kashindwa kuripotini
Nyembo nikamtazama, picha leo kawekani
Bwaya naye kang'amua, wanasiasa laghai.

Kazonta kabaki wazi, rushwa anaipingani
Marekani mwafatani, Zainaty kahojini
Beatrice kashikani, wanawake ongozani
Nikafika Furahia, bashasha sikupatani.

U wapi ewe Materu, na Mark ulofikani
Njia ninafunguani, salamu zangu wapani
Huyu aliwaagani, kisa likizo kwendani
Sasa anajivunia, mtori kibololoni.

Nitakuwa safarini, kwa Jeff ninaendani
Nasikia kwagandani, barafu poromokani
Mkina sije ombani, wambie rushwa achani
Salamu za mwaka mpya, hapa wazi nawapeni.

Mpo wengi najuani, wachache nimetajani
Msotajwa samahani, haraka yanishikani
Naweza kuandikani, Ottawa nikifikani
Msamaha nipeweni, iwapo nitashindwani!

Naweza shindwa fikani, kuwalisha fikirani
Nendako sifahamuni, kisa radhi kuwahini
Uzima nikutakeni, Mola nguvu wajazini
Nikirudi KICHAKANI, Januari iwe unono.
 
© boniphace Tarehe 12/15/2005 09:35:00 AM | Permalink | Maoni 8
Tuesday, December 13, 2005
KARIBU MALENGA MKWINDA
SI lengo langu kuhamisha mjadala ulioanzishwa na huyu jamaa baada ya kumtangaza Mwanablogu mpya huyu. Sijashawishika kutomchapa mwanablogu huyu malenga bakora za mashairi maana nimemisi majibizano haya tangu enzi zile nikiwa Ndanda Sekondari, wakati ambapo rafiki ya Shaaban Dammbaya aliweza kunipata hamasa ya kuandaa muswada wangu wa kwanza wa Mashairi ulioitwa "Hodi Hodi Duniani, Diwani ya Dammbaya na Nakuzerwa."

Nakumbuka maana kipindi hicho niliweza kukariri barua zangu kwa mashairi. Ni kipindi hicho nilipokuwa shabiki mkubwa wa Ustadhi Andanenga kabla sijakutana naye kwa macho pale Nkrumah Chuo Kikuu Dar es Salaam, katika usiku wa Ushairi nilipokuwa pia msema chochote huku nikighani tungo kama hizi;
Ya Liyongo hutwambia
Siu alikozaliwa
Pate akitembeleya
Na Mwana akafiliya.
Kutoka Utenzi wa Fumo Lyongo: ubeti huo unatangaza maisha yote ya Fumo Lyongo jasiri, shujaa katika upwa wa Afrika Mashariki miaka hiyo. Nakumbuka nilishokuwa nikiyapinga mapingiti ya Euphrase Kezilahabi lakini baadaye ni K. Kahigi aliyeweza kunibadili na kunirejesha kumuamini Kezilahabi na mtindo wao wa mashairi guni.

Hiyo ilikuwa chombeza tu lengo ni kumkaribisha malenga mpya huyu, kaja vema sana anapaswa kupongezwa kwa kujenga mhimili wa lugha katika Blogu. Kosa lake katangaza kitu ambacho nakumbuka napingana nacho katika beti alizojibu majibizano yangu na ghani ya maneno ya Ndesanjo.

Mkwinda kaka fikia, keti mwana bloguni
Zamani niliwazia, siku nitapokufani
Nani atashikilia, KASRI langu tunzani
Sasa napata faraja, kijana mpya tokea.
Umekuja kwa makeke, kisa changu kujibuni
Ulinifanya nicheke, machozi kinitokani
Vipi utaje mapene, kwa fani ya malengani
Mkwinda sasa useme, hisa unaziuzani?
Mapene wapi mizani, kitita sikitamani
Natunga nili zuoni, mapene kwangu sumuni
Siwezi kuyatamani, kwani yanageuzani
Utumwa wakumbukani, kisa mapene fatia.
Malenga vina pangia, hoja weka bloguni
Hatutaki majalia, ya pesa kutulipani
Ushairi nashibia, beti nazodondoani
Mkwinda acha makeke, ushairi si mapene.
Kalamu yake Ndesanjo, kali kaka ujuani
Wapaswa kukaa chonjo, Rais mtaniani
Utajatoa mkojo, Segerea laliani
Ndesanjo mtu mwingine, silinganishe na mimi!
Nimegundua kimoja, vina hujavipangani
Sasa niambie hoja, mapingiti watungani?
Kesho utakapokuja, tamka nikujuani
Kalamu ulofungua, wino imeshachojoa.
Tangu juzi nasemea, niko bize masomoni
Mitihani nafanyia, bado sijamalizia
Lakini mwatukania, kisa changu kujibuni
Kalamu nalaza chini, Mkwinda sigange njaa!
 
© boniphace Tarehe 12/13/2005 11:03:00 AM | Permalink | Maoni 3
NINI ISHARA YA HAYA

MGOMBEA wa urais na Rais ajaye wa Tanzania baada ya kura za kesho alianguka mapema jana wakati wa kukamilisha zoezi la kuomba kura. Wakati huu si kama ilivyokuwa Mwanza kwa kubebwa na gaidi mmoja lakini kwa sasa ni kile kinachozungumzwa kupungukiwa na nguvu baada ya kusimama wakati mwingi. Vyanzo vya habari hizi kutoka Marekani vilipasha tukio hilo huku vikilifananisha na jingine linalomkabili mgombea pekee Anna Senkoro, aliyefanikiwa kuweka rekodi ya kuwa muwania urais wa kwanza kabisa mwanamke Tanzania, ambaye hata hivyo hajapatwa kutajwa na DaMIJA katika blogu yake, kama alivyofanya katika makala hii na hii, naye tangu ngwe ya pili ya kampeni alikuwa kitandani kutokana na ugonjwa ulioambatana na kutoa hitilafu za mdomo wake na kukosa nguvu za kuzungumza.

Habari zadi za matukio ya aina hii yanatia kumbukumbu ya kifo cha mgombea mwenza wa CHADEMA aliyefariki mapema na kusababisha uchaguzi kuhairishwa. Hata hivyo habari za uchaguzi zinaonyesha hali ya mabadiliko katika nafasi za ubunge huku Kikwete akibaki kuwa Rais wa nne wa Jamhuri ya Muungano anayechukua nafasi katika kipindi kigumu kufuatia wigo kati ya maskini na tajiri kutanuliwa kwa spidi ya kawaida na serikali ya awamu ya pili huku hii ya tatu inayomaliza muda wake ikiwa imeongeza spidi na kufanya ufa huo kutotazamika.

Sera za Kikwete za ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya zaweza kutanua ufa huo kwani yaonesha nguvu zake si kama alizokuwa nazo miaka kumi iliyopita. Pia anakabiliwa na makundi makubwa katika chama chake yanayotarajia fadhila kutoka kwake huku kukiwa na wengi wanaomsubiri kukalia kimya namna walivyojinufaisha kutokana na raslimali za umma.

Maskini wa Tanzania wanamuona Kikwete kama masiha mpya na wanahitaji kumuona akirejesha mali zao zilizobinafsisha kiholela huku sheria za ukandamizaji kama za kujiuzia mali za umma hasa nyumba zikifutwa na nyumba hizo kurejeshwa. Fikra hizi na nyingine nyingi huenda zimechangia kuanguka kwa Kikwete wakati wa ukamilishaji wa zoezi la kumfikisha huku alikoota kwa miaka mingi. Kuna habari nyingine ambazo nimezipata lakini zitaziweka sasa kwa sababu ya kiistaarabu.
 
© boniphace Tarehe 12/13/2005 09:52:00 AM | Permalink | Maoni 4
Sunday, December 11, 2005
NI IKULU AU WHITE HOUSE?


MWANABLOGU wa picha michuzi amebandika picha inayoonyesha mbio zitakapokamilikia baada ya harakati za kisiasa Tanzania wiki hii inayoanza saa chache zijazo. Ikulu ya Tanzania yeye hapo ameiita White House. Nilipokuwa huko Washington D.C nilipata masimulizi juu ya jina la MAKAO MAKUU YA MAREKANI kuitwa White House. Je hii ya Tanzania kwa kuwa nayo yaonekana nyeupe yaifaa kuitwa White House au ndio mwendo wa kukopi kila tunachokiona kwa wenzetu?
 
© boniphace Tarehe 12/11/2005 03:15:00 PM | Permalink | Maoni 2
Saturday, December 10, 2005
MABADILIKO YA KATIBA TANZANIA

NIMEKUWA katika hamu ya kuona Katiba ya Tanganyika inabadilishwa. Katiba iliyopo haikidhi matakwa ya wengi. Imechoka na kubwa zaidi imejaa viraka. Mfumo wa kuunda sheria Tanzania una ukakasi. Sheria zaanzia serikalini na kisha kupelekwa bungeni kupitishwa. Hakuna kwa dhati kile kiitwacho mgawanyo wa madaraka.

Kuna haya madaraka ya Wakuu wa Mikoa na wale wa Wilaya. Vyeo hivi katika ulimwengu wa sasa havina kazi zaidi ya kuongeza mazingira ua ufalme wa watawala wa Tanzania. Kuna haja ya vyeo hivyo kutumika vingine au kuundwa kwa Bunge lenye sehemu mbili yaani lile la wawakilishi wanaotokana na majimbo yaliyopitishwa kwa uwiano wa namba ya wakazi na lile la pili litakalofanana na kuwa na wawakilishi wa aina ya wakuu wa mikoa au mithili ya maseneta ila hawa wanachaguliwa na wanannchi wa sehemu husika. Hii ni hoja ambayo amekuwa nayo mgombea wa CHADEMA, Freeman Mbowe lakini kwa muundo mwingine.

Kama kutakuwa na wawakilishi wa aina hii kunakuwa na uwezekano wa sheria mbovu zinazogandamiza haki za raia kutopitishwa. Tena ni rahisi kuwa na uwiano wa kimaendeleo badala ya sasa Mawaziri kubadilishia miradi ya maendeleo katika majimbo yao ya uchaguzi ili kujijenga kisiasa na kisha kuyadhibiti majimbo ya wapinzani kwa kuyanyima huduma za maendeleo.

Picha hiyo hapo ni Kongresi ya Marekani ambapo tulitembelea hivi karibuni. Marekani ni moja ya nchi zenye Bunge lenye sehemu mbili. Yaana sehemu ya Wawakilishi na Seneti.
 
© boniphace Tarehe 12/10/2005 10:11:00 AM | Permalink | Maoni 2
Friday, December 09, 2005
TUNAKOELEKEA KUBAYA KAMA HIZI NDIZO MAKALA ZA KAMPENI TANZANIA
WANAKASRI, nikusalimu, poleni kwa kunikosa kidogo...ni suala la vimajukumu vinanitinga kwelikweli lakini nimekumbuka kupita kukusalimuni. Katika pita pita yangu nimekutana na makala hii naomba isome mwenyewe kwenye kiunganishi hiki.

Kama hizi ndizo kampeni na lugha za magazeti ya Tanzania nadhani ningeanza kufungia hili kabla sijayatazama mengine. Tazama nyingine hii na isome hadi mwisho. Oooh mbona unaniziba mdomo...samahani sisemi kama ni gazeti la serikali ya CCM. Kama haya ndiyo tunayopanda, siku si nyingi...naomba mnisamehe kutabiri huko tuendako!
 
© boniphace Tarehe 12/09/2005 03:11:00 PM | Permalink | Maoni 2
Monday, December 05, 2005
MOJA KWA MOJA NA RAIS, KISHA WAZIRI MKUU
NIMEKUJA na furaha leo kukufahamisha Mwanablogu mwenzangu yaliyojiri jana. Furaha yangu ilitiwa simanzi kidogo na maoni niliyoyapata katika ukumbi wa barua zangu mtandaoni ambao nimeamua kuibandika hiyo katika makala hapo chini.

Enewei sasa nianze japo harakaharaka. Jana nikapata fursa ya kuzungumza moja kwa moja na huyu waziri mkuu cheo hiki nimemtunuku mimi nitafurahi kama nawe utabariki mapendekezo yangu. Ni waziri mkuu wa Blogu za Tanzania. Nilikuwa na namba yake ya simu maana Mawaziri wakuu watu simpo tu ndio maana hata namba ya Bwana Fredrick Sumaye ninayo...sijui nikuwekee kwenye kiunganishi hapa lakini hapana siku zake zimeisha huyo subiri nitabandika ya Lowassa siku si nyingi.

Basi mazungumzo na mheshimiwa Waziri Mkuu yalikuwa safi sana na tukaeleweshana kero tunazozikabiri sisi wananchi wa chini na mheshimiwa akazungumzia umuhimu wa kuongeza majimbo ya Blogu zaidi ili nchi yetu iweze kufikisha ajenda ya kuwabadilisha fikra Wanazuoni. Mazungumzo yale matamu yalikatishwa baada ya kilongalonga changu kukaukiwa mafuta, sina maana ya dola bali kiliishiwa umeme.

Nikiwa nimetua simu huku sitaki kupokea simu kabisa ghafla ikaita tena. Sikujua tena huyu nani lakini kwanza nianze na kisa hiki katika "Mzimu wa Watu wa Kale." Mohamed Said Abdulla humtumia mhusika "MSA" katika kazi zake. Huyo MSA ni kifupisho cha majina yake.

Basi bwana Msa ukimuuliza juu ya umuhimu wa Mwanga atakwambia nenda gizani...ukisema maana ya elimu atatoa jibu la kukutaka kutazama yule asiyesoma! Basi kuna huyu mheshimiwa Rais katika Blogu za Watanzania. Bawana huyu ukimuuliza swali la kutaka kufanya hivi hukaa kimya na kukujibu jingine. Siwezi kubandika aina ya majibu yake maana cheo chake huyu kikubwa.

Sasa huyu jamaa akaanza kupiga simu huku akihoji mimi bado nafanya nini Marekani. Nikahisi kuanza kutumiwa watu kunifatilia maisha yangu...maana siku hizi nimechoka na kauli za vitisho na nimejizatiti sana kutozijali. Jamaa huyu ameniweka katika kona utadhani FBI kisha ndipo akajitambulisha hali iliyonihemsha furaha na tabasamu usoni.

Sikuwahi kujadiliana naye lakini mazungumzo yangu hayakuwa mbali sana na yale tuliyozungumza na mheshimiwa Jeff Msangi. Naye akanihamasisha kuwatangazia zaidi Watanaznia wengi kuingia katika Blogu. Sina namna wakuu najitahidi kutimiza kazi yenu maana mwaweza kunipa hata kauwaziri ka ulinzi wa Blogu siku zijazo.
 
© boniphace Tarehe 12/05/2005 06:47:00 AM | Permalink | Maoni 0
MAKALA YANGU YA MWANANCHI JUMAPILI (TANZANIA) NA MAJIBU YA MTANZANIA MZUNGU!
NINA kibaraza cha kurushia dukuduku zangu katika gazeti la Mwananchi Jumapili nchini Tanzania. Wenzangu ninaorusha nao hekaya ni Freddy Macha, Ndesanjo Macha hawa wakiwa ughaibuni kama mimi sasa. Makala yangu Jumapili hii ilihusu mgomo wa madaktari uliofanyika Tanzania. Nisichokonoe niibandike kama ilivyokuwa hapa.

Mgomo wa madaktari ni darubini ya mengi yajayo

Na Boniphace Makene, EDINBURG, TEXAS

“NITASEMA kweli daima fitina kwangu ni mwiko.” Nimeanza na nukuu ya ahadi za Mwana TANU. Chama hiki kilikuwa chama cha Tanganyika kilishoshirikiana na vingine katika harakati za kupambania uhuru.

Kilifanikiwa na baadaye kukawa na somo la siasa katika shule za msingi hadin sekondari. Ni katika somo hilo nakumbuka wakati ule nikikaa katika darasa lenye vumbi kali la udongo chini ya tofali kasha mwalimu wangu akipita na kupiga wanafunzi vichwani kwa kifimbo chake akiashiria utaje ahadi kumi za mwana TANU.

Sikuwa mmojawao wa hao wana TANU, nililazimishwa tu kuimba ahadi hizi na kubahatika kuipenda hii ambayo sasa sikumbuki ilikuwa ya ngapi. TANU nasikia ilikuja kuungana na ASP ya huko visiwani na kuundwa Chama cha Mapinduzi.

Hadi sasa sijui ni mapinduzi yapi yaliyosababisha kuundwa chama hicho. Nimewahi kusikia kuwa kuliwahi kufanyika kile kiitwacho Mapinduzi huko Zanzibar. Hii si mada yangu leo lakini sijawahi kusikia kuwa Tanganyika na Zanzibar ziliwahi kufanya Mapinduzi yaliyosababisha kuundwa kwa chama kilichoitwa CCM.

Swali hili limejikuta likirejea kila mara kichwani kwangu. Naanza kupata jibu la mapinduzi kuhusu sera za ugawaji wa mali za umma na kuzitia katika mifuko ya mabwanyenye. Neno bwanyenye laweza kuwa geni kwa vijana wa sasa, hili tulilitumia miaka hiyo kuashiria hawa mnaowaita wezi wa mali za umma wenye matumbo yasiyo kinai huku wakigubikwa na bahari za uchu.

Tunao wengi katika Tanzania, wengi wako madarakani na kazi ya kukusanya kila walichokiona machoni mwao waliifanya kikamilifu. Siku si nyingi sasa tutawaona hawa waliojificha katika kivuli cha Ufalme wa awamu ya nne wakibainisha wazi mali zao.

Tutawakuta huko pale tutakapohitaji huduma katika viwekezo vyao. Namkumbuka mmoja huyo sioni hofu kumsema anaitwa Fredrick Sumaye! Yeye nasikia kamiliki mashamba mengi. Siku si nyingi atakuwa na Ranchi kama ninazoziona huku Texas.

Nawaza nikifika Tanzania kumtembelea ili naye anifundishe namna ya kupata mashamba hayo kama inawezekana ili nami nianzishe ranchi. Sijui kama itakuwa kazi nyepesi maana nakumbuka kuwa sitoki katika familia za wafalme na hivyo changu na chako mwenzangu na mimi ni hiki tulichowagawawia hawa mabwanyenyena unaowapigia kura siku si nyingi wiki ijayo.

Vita kati ya mabwanyenye na raia imekuwa ile isiyo kuwa na usawa. Ni kutokana na ukandamizaji huo napata mada ya kuandika baada ya kupokea mawazo mengi kutoka Tanzania yakinihasa kuzungumzia suala la mgomo wa madaktari.

Sitaki kukupasua mbavu ya wivu wa madaktari na mishahra yao hapa Marekani-lakini naomba niseme na wala sitakubaliana na hoja ya kwamba kwa nini nalinganisha Marekani na Tanzania! Kwani huku kunaishi Nguruwe, si wanaishi hawa akina George Bush.

Nani aliwapa uwezo kama si kwamba waliamua kupambana na Mfalme wa Uingereza kama tulivyomchachafya sisi wakati ule tukiwa na kiongozi mwananchi mwenzetu Mwalimu Julius Nyerere! Nani atambui kuwa baada ya kiongozi huyo mwananchi kuondoka tumegeuza mfumo na kuweka madarakani wafalme wasiohitaji kusikia shida za wananchi bali kila siku kujigamba na kukomoa wale wanaodai haki zao?

Mgomo wa madaktari katika Tanzania umesababisha madaktari kufukuzwa na badala yake mameneja kuingia wodini kutibu. Tazama tunavyochezea afya za watu, yaani mtu kasomea umeneja katika afya leo hii anachukuliwa kutibu watu! Aibu…nimekumbuka kuwa katika Tanzania kila mmoja anaweza kufanya lolote ndio maana madaktari wetu bingwa ni mawaziri wa Ulinzi na wahandisi ni viongozi wa juu katika Chuo Kikuu Mlimani na kwingine sijui.

Sifahamu vema taaluma ya waziri wa afya wa Tanzania sasa, nafahamu taaluma ya Naibu wake hapo pia kuna utata ambao sitaujadili leo. Madaktari katika Marekani wanalipwa kwa siku pesa zaidi ya hiyo waliyoomba wenzao wa Tanzania ili walipwe kwa mwezi.

Kitabu cha udaktari katika Tanzania ni kigumu kufuatia kukosekana zana bora za kufunzia. Ili uhitimu unahitaji kuwa gwiji wa kukariri jambo lililonikimbiza kabisa kutamani masomo hayo tangu nikiwa mdogo. Huku Marekani naweza soma udaktari nikafanikiwa kuhitimu na nikatibu vema.

Kufukuzwa kwa madaktari Tanzania ni aibu nyingine inayoonyesha namna wafalme wa Tanzania wanavyojipambanua katika gwanda la demokrasia. Unajua mshahara wa Waziri na hata rais katika Tanzania? Kuna usiri gani katika hilo na wanafanya kazi gani kama si ile ya kutumia mkasi kukata vitambaa kuashiria kufungua barabara au kushikana mikono na wageni?

Madaktari wengi katika Tanzania wamekimbilia nchi za nje hali inayodumaza afya za watanzania. Nakumbuka kuwa tangu uhuru maradhi alikuwa adui mkubwa. Ili kumshinda tulihitajika kuwa na madaktari imara na shupavu katika kazi hiyo. Kufuatia siasa za kifalme katika Tanzania, sasa hivi daktari hana sauti hata ya kuzungumzia shida zake kwani akifanya hivyo anafukuzwa katika nyumba na kasha kuachishwa kazi.

Nadhani bado namkumbusha mgombea fulani juu ya suala la nyumba za serikali. Nimepata jibu ni kwa nini Mawaziri na Rais wao waliuziana nyumba mapema. Walitambua kuwa wanaweza nao kugoma? Hapana kwa nini sasa madaktari hawa hawakuuziwa hizo nyumba pia na badala yake wakaviziwa ili waabishwe katika nchi yao?

Wapo madaktari waliofutiwa udhamini hapo Muhimbili. Asante serikali, lakini wananchi wanafahamu taifa linazalisha madaktari wangapi kwa mwaka na kupoteza daktari mmoja kuna hasara gani? Hii ni tabia ya wafalme, kubomoa wanapojenga…kamwe huwezi pata ukuta bora kwa kila mara kubadili pale ulipoanza kujenga!

Tanzania inaweza kujengwa na kuwa bora kama tutaacha haya! Mosi ubinafsi na mkubwa kabisa ni huu unaofanywa na viongozi wa serikali kwa kupenda kujineemesha wao na familia zao ili kujenga himaya za kifalme! Pili ni suala la kuthamini mawazo ya kujenga ili kila kiungo cha mwili kiweze kutumika na kufahamika ubora wake.

Kuna suala la kuamini kuwa sisi sio bora kuliko wengine. Waliopata bahati ya kujua wasidhani kuwa wengine hawawezi kujua pia. Siku zote katika maisha ni majadiliano na mstaarabu hukubali ukweli na huweza kubashiri hatari kabla ya wakati!

Kuna kosa la madaktari limetendeka, hawa sio malaika najua walipeleka tarumbeta pale Muhimbili. Hilo ni kosa kubwa, madai ya msingi kama waliyokuwa nayo hayawezi kamwe kuandamanishwa na tarumbeta.

Tarumbeta katika Afrika huashiria furaha, harusi na madai ya madaktari yalikuwa mithili ya huzuni zilizoujaza moyo. Huzuni hii ni kebehi kuisindikiza na tarumbeta. Lakini bado kuna haja ya kujadili matumizi ya nyumba za serikali na inatakiwa sasa kuandaa maandamano makubwa ya kuhoji kuzirejesha ili zitumike kwa mafanikio ya umma na sio kundi la wachache walio madarakani!

Kufukuzwa kwa madaktari katika nyumba hizo ni picha mpya ya namna makundi yalivyojengwa katika Tanzania. Iweje huyu aliyejiuzia nyumba leo amfukuze mwenzake aliyekaa katika nyumba ambazo hakuruhusiwa kuuziwa?

Kazi ipo awamu ijayo…watanzania twapaswa kukesha maana hatujui siku wala saa yatakapolipuka mabomu tuliyoyapandikiza kwa miaka mingi. Tumejitahidi kutengana na hakuna mkakati wa kuunganishana kama tunavyojidanganya kuhubiri.

Tazama mgawanyo wa wazi ulioko Zanzibar, hapa sitaandika sana leo maana mada hii inatosha kabisa kuiandika wiki ijayo. Nafasi finyu za kujifunza nje zimebakia za watoto wa wakubwa na huku tuna mifano wazi ya kutaja. Kwa nini watoto wenu wakae na kusoma Ulaya wakati ile Bodi ya mikopo mkiitumia kutaabisha watoto wa maskini wa Tanzania?

Kuna sababu ya madaktari waliogoma na walioghilibiwa kutambua kuwa wote ni madaktari. Sekta ya afya kama itazidi kudhalilishwa hivi tutarajie kuwa na hospitali zitakazoendeshwa kwa mkakati kama wa MEWATA.

Serikali imesahau kabisa majukumu yake na badala yake gharama kubwa zimewekezwa katika mambo yasiyo na msingi. Hivi gharama hizi anazotumia Rais kuaga katika nchi zilipitishwa na nani? Je watanzania wanatambua kuwa hizo zatokana na kodi zao?

Mbona waliomchangua rais huyo hawapati nafasi ya kumuuliza namna alivyoshindwa kuwatatulia kero lakini unasikia leo yuko nchi hii na kesho nchi ile? Huu ni mfano mdogo tu wa maeneo yanakotumika matumizi ambayo yangeweza kusaidia kulipa madaktari.

Vipi kuhusu madini yetu yaliyogawiwa kwa mabwanyenye, menejimenti feki kama Net Group Problem, hizi TanRoads na kule kwenye makusanyo ya kodi hatusikii kelele? Ni kweli haziwezi kutumika kuongeza nguvu ya malipo kwa madaktari wa Tanzania? Tujue kutunza matatizo si sifa…siku zimesalia chache na uongo wa wafalme wa Bongo utawekwa wazi na hapo ndipo kutakapofanyika mapinduzi ya dhati yaliyotarajiwa na CCM wakati wa kuundwa kwake.


Baada ya makala hayo nimepokea ujumbe toka kwa huyu ninayemuita mzungu. Kisa anajua Kiswahili, amesoma makala ya Kiswahili kisha ananijibu kwa kizungu huku akinituhumu kutopenda nchi yangu. Makala ya huyu ndugu ambaye hakuweka jina lake yasema hivi:

You dont love your country:

Hello there!

I have read your article at one of the local news papers here in Tanzania! I can only say that you are Mkimbizi and you don't love your country and your people otherwise you should have being living here and re-build your county - not the US economy!

What if the teachers will ALL decide to Strike! Who made you being there and happily work! Teaches! but do you know how much they get paid ? aaaaha you don't care about that - however the same country with under the shade of the misleading government educated you well until you are now in Texas now having a terrific time!

All I can just try to tell you is that - Our government is strong enough and 90% of citizens agree with the government being strong enough not to allow anyone to decide to do things the way they want, then there is no meaning of having the government then. How about the poor Police can now deicide to strike as there are the one who are working on the difficult and dangerous circumstances!

The economy of Tanzania is boosting up my dear ! We only do not have few things to complain, but every thing at a time! Try and visit home soon and see bwana! Tusizifagilie nchi za wenzetu tuuu! Hebu uje cheki maendeleo yamefikiwa wapi - kwakweli Mkapa na viongozi walio Tangulia wamejitaidi kaka Mpendwa!

We are actually enjoying living home !

 
© boniphace Tarehe 12/05/2005 06:27:00 AM | Permalink | Maoni 3
Saturday, December 03, 2005
ZI WAPI HATI ZA MUUNGANO? NI MALI YA NANI? ZINAFICHWA KWA SABABU IPI?

MOJA ya matukio niliyoyapenda katika safari yangu Washington Capitol ni kukuta majengo ya kumbukumbu za ujenzi wa taifa la Marekani. Kuna piccha nimeweka kwenye albamu yangu na nyingine nitaziweka baadaye. Jingine ni hili la kukuta maandishi yajulikanayo kama Decoration of Independence. Haya yamechapishwa kabisa na kuwekwa makubwa ukutani.

Maandishi hayo yalikuwa makubaliano ya awali kabisa ya kuunda muungano wa kujenga taifa la Marekani. Tanzania na Unguja zikaungana mwaka 1964 lakini sasa tuko mahakamani kutafuta maandishi ya Muungano huo. Kweli ulifanyika Muungano unaoimbwa kumilikiwa na CCM na kama wanataka kuudumisha nini kisa cha kuficha hati ya Muungano huo.

Kuna yapi yanayofichika katika hati hiyo au Muungano huo ni geresha. Kama wazohili ni sadifu basi inawezekana Tanganyika ikawa sawa na Marekani inalazimisha kuwa na makoloni Afghanistan na Iraki. Kama ni hivyo Zanzibar inahitaji uhuru wake na hili halina siku nyingi. Uongo na usiri umegubika muungano wa mataifa haya. Tatizo hili limejenga hali ya kutokuaminiana. Tazama kufungiwa kwa Tanzania Daima kisa kuchapisha katuni yenye picha ya mfalme wa Tanzania. Haya ni mambo yanayohatarisha amani ya Tanzania. Kunyimwa haki ya kuchambuana na uhuru thabiti wa kuzungumza na kutamka yachomayo moyo.

Kuna wengi waishio katika hatihati kutokana na kusimamia haki zao na kutamka ukweli juu ya Wafalme wa Tanzania wakiongozwa na Mkapa. Kazi ipo kwako nami tunaodhani ni haki yetu kupayuka kila lifanywalo na wafalme wa Bongo. naapa siachi ng'o, bora kumaliza safari hii ya maisha mapema kuliko kudhalilisha mapenzi ya moyo wangu. Nitasema kweli daima fitina kwangu ni mwiko.

Pembeni ni mnara wa kumbukumbu wa moja wa Mababa wa taifa la Marekani na Rais wa Kwanza wa nchi hiyo George Washington. Mnara huu upo Washington D.c.
 
© boniphace Tarehe 12/03/2005 10:21:00 AM | Permalink | Maoni 0
Thursday, December 01, 2005
HII NI ISHARA GANI
NIMEKARIRI shairi hili baada ya mwanablogu Jeff kushindwa kutimiza ahadi yake ya kutukariria shairi kila wiki. Alisema hapa, uongo sitaki tajia. Kisha sasa katokea, kizungu kufungulia. Nimekumbuka sikia, alitaka amshiwa, hivyo nami narejea kwa shairi kutungia.

SIKU ya kwanza kuanza, mwaka mpya kukamata
Macho yangu yanacheza, na tumbo kulia mbwata,
Nimeshindwa kuchomoza, mtihani kukamata
Hii ni ishara gani, kwa mwaka niloanzia?

Mwenyewe nilijapiza, mtiahani kufanyia
Wengine walishajaza, D.C nikitembea
Leo mwayo nimepaza, mlango shindwa fungua
Hii ni ishara gani, kwa mwaka niloanzia?

Nikakimbilia lulu, maktaba tafutia
Huko akaja kaburu, Blogini kunitia
Nikashindwa kumdhuru, hivyo nyumbani rudia
Hii ni ishara gani, kwa mwaka niloanzia?

Njaa ikanitafuna, shibe bora kuwazia
Nikenda viazi tafuna, utamu nikakosea
Nikakumbuka Musoma, mama akivipikia
Hii ni ishara gani, kwa mwaka niloanzia?

Jana ilikuwa jana, kila mtu kuchekea
Majini tulichuana, hakuna aloshindia
Bahari ilijazana, kama Kana tukanywea
Hii ni ishara gani, kwa mwaka niloanzia?

Salamu nikazipa, kwa wengi mpaka mamia
Simu ikawa yalia, kila dakika sawia
Blogu niposomea, salamu nikakutia
Hii ni sihara gani, kwa mwaka niloanzia?

Za intaneti barua, nyingi nimepokelea
Ndugu zangu wa Kanada, hawa napata sifia
Kila moja kakimbia, ujumbe kunandikia
Hii ni ishara gani, kwa mwaka niloanzia?

Melisa akanambia, hii ni ngao sikia
Ni moja inatokea, kwa mwaka hivyo julia
Wapaswa kuitambua, furaha yako wekea
Hii ni ishara gani, kwa mwaka niloanzia?

Najua kamba navuta, kuzimu kuelekea
Sioni mengi matata, kwani sipendi fanyia
Uchungu unonikuta, wafalme kuzidia
Hii ni ishara gani, kwa mwaka niloanzia?

Nimalize tungo tungia, nanyi mpate somea
Blogu yangu sikia, jijaze mwana tulia
Pepo yako pulizia, kila ajaye somea
Ili kesho ikifika, ashindwe kukukimbia.
 
© boniphace Tarehe 12/01/2005 06:12:00 PM | Permalink | Maoni 0
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved