Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Monday, December 05, 2005
MAKALA YANGU YA MWANANCHI JUMAPILI (TANZANIA) NA MAJIBU YA MTANZANIA MZUNGU!
NINA kibaraza cha kurushia dukuduku zangu katika gazeti la Mwananchi Jumapili nchini Tanzania. Wenzangu ninaorusha nao hekaya ni Freddy Macha, Ndesanjo Macha hawa wakiwa ughaibuni kama mimi sasa. Makala yangu Jumapili hii ilihusu mgomo wa madaktari uliofanyika Tanzania. Nisichokonoe niibandike kama ilivyokuwa hapa.

Mgomo wa madaktari ni darubini ya mengi yajayo

Na Boniphace Makene, EDINBURG, TEXAS

“NITASEMA kweli daima fitina kwangu ni mwiko.” Nimeanza na nukuu ya ahadi za Mwana TANU. Chama hiki kilikuwa chama cha Tanganyika kilishoshirikiana na vingine katika harakati za kupambania uhuru.

Kilifanikiwa na baadaye kukawa na somo la siasa katika shule za msingi hadin sekondari. Ni katika somo hilo nakumbuka wakati ule nikikaa katika darasa lenye vumbi kali la udongo chini ya tofali kasha mwalimu wangu akipita na kupiga wanafunzi vichwani kwa kifimbo chake akiashiria utaje ahadi kumi za mwana TANU.

Sikuwa mmojawao wa hao wana TANU, nililazimishwa tu kuimba ahadi hizi na kubahatika kuipenda hii ambayo sasa sikumbuki ilikuwa ya ngapi. TANU nasikia ilikuja kuungana na ASP ya huko visiwani na kuundwa Chama cha Mapinduzi.

Hadi sasa sijui ni mapinduzi yapi yaliyosababisha kuundwa chama hicho. Nimewahi kusikia kuwa kuliwahi kufanyika kile kiitwacho Mapinduzi huko Zanzibar. Hii si mada yangu leo lakini sijawahi kusikia kuwa Tanganyika na Zanzibar ziliwahi kufanya Mapinduzi yaliyosababisha kuundwa kwa chama kilichoitwa CCM.

Swali hili limejikuta likirejea kila mara kichwani kwangu. Naanza kupata jibu la mapinduzi kuhusu sera za ugawaji wa mali za umma na kuzitia katika mifuko ya mabwanyenye. Neno bwanyenye laweza kuwa geni kwa vijana wa sasa, hili tulilitumia miaka hiyo kuashiria hawa mnaowaita wezi wa mali za umma wenye matumbo yasiyo kinai huku wakigubikwa na bahari za uchu.

Tunao wengi katika Tanzania, wengi wako madarakani na kazi ya kukusanya kila walichokiona machoni mwao waliifanya kikamilifu. Siku si nyingi sasa tutawaona hawa waliojificha katika kivuli cha Ufalme wa awamu ya nne wakibainisha wazi mali zao.

Tutawakuta huko pale tutakapohitaji huduma katika viwekezo vyao. Namkumbuka mmoja huyo sioni hofu kumsema anaitwa Fredrick Sumaye! Yeye nasikia kamiliki mashamba mengi. Siku si nyingi atakuwa na Ranchi kama ninazoziona huku Texas.

Nawaza nikifika Tanzania kumtembelea ili naye anifundishe namna ya kupata mashamba hayo kama inawezekana ili nami nianzishe ranchi. Sijui kama itakuwa kazi nyepesi maana nakumbuka kuwa sitoki katika familia za wafalme na hivyo changu na chako mwenzangu na mimi ni hiki tulichowagawawia hawa mabwanyenyena unaowapigia kura siku si nyingi wiki ijayo.

Vita kati ya mabwanyenye na raia imekuwa ile isiyo kuwa na usawa. Ni kutokana na ukandamizaji huo napata mada ya kuandika baada ya kupokea mawazo mengi kutoka Tanzania yakinihasa kuzungumzia suala la mgomo wa madaktari.

Sitaki kukupasua mbavu ya wivu wa madaktari na mishahra yao hapa Marekani-lakini naomba niseme na wala sitakubaliana na hoja ya kwamba kwa nini nalinganisha Marekani na Tanzania! Kwani huku kunaishi Nguruwe, si wanaishi hawa akina George Bush.

Nani aliwapa uwezo kama si kwamba waliamua kupambana na Mfalme wa Uingereza kama tulivyomchachafya sisi wakati ule tukiwa na kiongozi mwananchi mwenzetu Mwalimu Julius Nyerere! Nani atambui kuwa baada ya kiongozi huyo mwananchi kuondoka tumegeuza mfumo na kuweka madarakani wafalme wasiohitaji kusikia shida za wananchi bali kila siku kujigamba na kukomoa wale wanaodai haki zao?

Mgomo wa madaktari katika Tanzania umesababisha madaktari kufukuzwa na badala yake mameneja kuingia wodini kutibu. Tazama tunavyochezea afya za watu, yaani mtu kasomea umeneja katika afya leo hii anachukuliwa kutibu watu! Aibu…nimekumbuka kuwa katika Tanzania kila mmoja anaweza kufanya lolote ndio maana madaktari wetu bingwa ni mawaziri wa Ulinzi na wahandisi ni viongozi wa juu katika Chuo Kikuu Mlimani na kwingine sijui.

Sifahamu vema taaluma ya waziri wa afya wa Tanzania sasa, nafahamu taaluma ya Naibu wake hapo pia kuna utata ambao sitaujadili leo. Madaktari katika Marekani wanalipwa kwa siku pesa zaidi ya hiyo waliyoomba wenzao wa Tanzania ili walipwe kwa mwezi.

Kitabu cha udaktari katika Tanzania ni kigumu kufuatia kukosekana zana bora za kufunzia. Ili uhitimu unahitaji kuwa gwiji wa kukariri jambo lililonikimbiza kabisa kutamani masomo hayo tangu nikiwa mdogo. Huku Marekani naweza soma udaktari nikafanikiwa kuhitimu na nikatibu vema.

Kufukuzwa kwa madaktari Tanzania ni aibu nyingine inayoonyesha namna wafalme wa Tanzania wanavyojipambanua katika gwanda la demokrasia. Unajua mshahara wa Waziri na hata rais katika Tanzania? Kuna usiri gani katika hilo na wanafanya kazi gani kama si ile ya kutumia mkasi kukata vitambaa kuashiria kufungua barabara au kushikana mikono na wageni?

Madaktari wengi katika Tanzania wamekimbilia nchi za nje hali inayodumaza afya za watanzania. Nakumbuka kuwa tangu uhuru maradhi alikuwa adui mkubwa. Ili kumshinda tulihitajika kuwa na madaktari imara na shupavu katika kazi hiyo. Kufuatia siasa za kifalme katika Tanzania, sasa hivi daktari hana sauti hata ya kuzungumzia shida zake kwani akifanya hivyo anafukuzwa katika nyumba na kasha kuachishwa kazi.

Nadhani bado namkumbusha mgombea fulani juu ya suala la nyumba za serikali. Nimepata jibu ni kwa nini Mawaziri na Rais wao waliuziana nyumba mapema. Walitambua kuwa wanaweza nao kugoma? Hapana kwa nini sasa madaktari hawa hawakuuziwa hizo nyumba pia na badala yake wakaviziwa ili waabishwe katika nchi yao?

Wapo madaktari waliofutiwa udhamini hapo Muhimbili. Asante serikali, lakini wananchi wanafahamu taifa linazalisha madaktari wangapi kwa mwaka na kupoteza daktari mmoja kuna hasara gani? Hii ni tabia ya wafalme, kubomoa wanapojenga…kamwe huwezi pata ukuta bora kwa kila mara kubadili pale ulipoanza kujenga!

Tanzania inaweza kujengwa na kuwa bora kama tutaacha haya! Mosi ubinafsi na mkubwa kabisa ni huu unaofanywa na viongozi wa serikali kwa kupenda kujineemesha wao na familia zao ili kujenga himaya za kifalme! Pili ni suala la kuthamini mawazo ya kujenga ili kila kiungo cha mwili kiweze kutumika na kufahamika ubora wake.

Kuna suala la kuamini kuwa sisi sio bora kuliko wengine. Waliopata bahati ya kujua wasidhani kuwa wengine hawawezi kujua pia. Siku zote katika maisha ni majadiliano na mstaarabu hukubali ukweli na huweza kubashiri hatari kabla ya wakati!

Kuna kosa la madaktari limetendeka, hawa sio malaika najua walipeleka tarumbeta pale Muhimbili. Hilo ni kosa kubwa, madai ya msingi kama waliyokuwa nayo hayawezi kamwe kuandamanishwa na tarumbeta.

Tarumbeta katika Afrika huashiria furaha, harusi na madai ya madaktari yalikuwa mithili ya huzuni zilizoujaza moyo. Huzuni hii ni kebehi kuisindikiza na tarumbeta. Lakini bado kuna haja ya kujadili matumizi ya nyumba za serikali na inatakiwa sasa kuandaa maandamano makubwa ya kuhoji kuzirejesha ili zitumike kwa mafanikio ya umma na sio kundi la wachache walio madarakani!

Kufukuzwa kwa madaktari katika nyumba hizo ni picha mpya ya namna makundi yalivyojengwa katika Tanzania. Iweje huyu aliyejiuzia nyumba leo amfukuze mwenzake aliyekaa katika nyumba ambazo hakuruhusiwa kuuziwa?

Kazi ipo awamu ijayo…watanzania twapaswa kukesha maana hatujui siku wala saa yatakapolipuka mabomu tuliyoyapandikiza kwa miaka mingi. Tumejitahidi kutengana na hakuna mkakati wa kuunganishana kama tunavyojidanganya kuhubiri.

Tazama mgawanyo wa wazi ulioko Zanzibar, hapa sitaandika sana leo maana mada hii inatosha kabisa kuiandika wiki ijayo. Nafasi finyu za kujifunza nje zimebakia za watoto wa wakubwa na huku tuna mifano wazi ya kutaja. Kwa nini watoto wenu wakae na kusoma Ulaya wakati ile Bodi ya mikopo mkiitumia kutaabisha watoto wa maskini wa Tanzania?

Kuna sababu ya madaktari waliogoma na walioghilibiwa kutambua kuwa wote ni madaktari. Sekta ya afya kama itazidi kudhalilishwa hivi tutarajie kuwa na hospitali zitakazoendeshwa kwa mkakati kama wa MEWATA.

Serikali imesahau kabisa majukumu yake na badala yake gharama kubwa zimewekezwa katika mambo yasiyo na msingi. Hivi gharama hizi anazotumia Rais kuaga katika nchi zilipitishwa na nani? Je watanzania wanatambua kuwa hizo zatokana na kodi zao?

Mbona waliomchangua rais huyo hawapati nafasi ya kumuuliza namna alivyoshindwa kuwatatulia kero lakini unasikia leo yuko nchi hii na kesho nchi ile? Huu ni mfano mdogo tu wa maeneo yanakotumika matumizi ambayo yangeweza kusaidia kulipa madaktari.

Vipi kuhusu madini yetu yaliyogawiwa kwa mabwanyenye, menejimenti feki kama Net Group Problem, hizi TanRoads na kule kwenye makusanyo ya kodi hatusikii kelele? Ni kweli haziwezi kutumika kuongeza nguvu ya malipo kwa madaktari wa Tanzania? Tujue kutunza matatizo si sifa…siku zimesalia chache na uongo wa wafalme wa Bongo utawekwa wazi na hapo ndipo kutakapofanyika mapinduzi ya dhati yaliyotarajiwa na CCM wakati wa kuundwa kwake.


Baada ya makala hayo nimepokea ujumbe toka kwa huyu ninayemuita mzungu. Kisa anajua Kiswahili, amesoma makala ya Kiswahili kisha ananijibu kwa kizungu huku akinituhumu kutopenda nchi yangu. Makala ya huyu ndugu ambaye hakuweka jina lake yasema hivi:

You dont love your country:

Hello there!

I have read your article at one of the local news papers here in Tanzania! I can only say that you are Mkimbizi and you don't love your country and your people otherwise you should have being living here and re-build your county - not the US economy!

What if the teachers will ALL decide to Strike! Who made you being there and happily work! Teaches! but do you know how much they get paid ? aaaaha you don't care about that - however the same country with under the shade of the misleading government educated you well until you are now in Texas now having a terrific time!

All I can just try to tell you is that - Our government is strong enough and 90% of citizens agree with the government being strong enough not to allow anyone to decide to do things the way they want, then there is no meaning of having the government then. How about the poor Police can now deicide to strike as there are the one who are working on the difficult and dangerous circumstances!

The economy of Tanzania is boosting up my dear ! We only do not have few things to complain, but every thing at a time! Try and visit home soon and see bwana! Tusizifagilie nchi za wenzetu tuuu! Hebu uje cheki maendeleo yamefikiwa wapi - kwakweli Mkapa na viongozi walio Tangulia wamejitaidi kaka Mpendwa!

We are actually enjoying living home !

 
© boniphace Tarehe 12/05/2005 06:27:00 AM | Permalink |


Comments: 3


  • Tarehe 12/06/2005 8:10 AM, Mtoa Maoni: Blogger boniphace

    Nashukuru mliojitahidi kutaka kuweka maoni hapa. Nami nilipata tabu kuanzia jana lakini naona sasa yanakubali.

     
  • Tarehe 12/10/2005 8:39 PM, Mtoa Maoni: Blogger Ndesanjo Macha

    Unajua hata mimi nimekuwa najiuliza kuhusu hiki chama cha "mapinduzi." Mapinduzi yapi?

    Umenipeleka mbali ulipotaja kauli ya "nitasema kweli daima..."

    Nadhani Makene ungetumia pia :www.ripway.com kuhifadhia makala zako na kisha kuweka kiungo hapa kwenye blogu.

    Halafu, nakuonya acha kabisa kumkejeli Sumaye. Huyu bwana unajua, kutokana na kauli yake mwenyewe anayopenda kuitoa kila akihutubia (huku akikunakuna kitambi), anafanya kazi usiku na mchana. "Serikali yenu inafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kuwa mnapata maendeleo."

     
  • Tarehe 12/11/2005 10:58 AM, Mtoa Maoni: Blogger boniphace

    Ndesanjo nadhani katika hizin kejeli anaweza kutuundisha na sisi tuweze kufanya hizo kazi usiku na mchana kwanza kwa kuzitaja kazi zenyewe na kisha kutueleza aina ya vipato vinavyotokana na kazi hizo. Kwa nini anakuwa na kigugumizi kutuambia hapo ili nasi ndugu zake tufanikiwe au anataka kubaki yeye tu? Kuna kazi anatakiwa kuifanya hasa sasa baada ya kupumua kazi hizo za madaraka makubwa.

     
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved