Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Sunday, December 18, 2005
HAPANA NIMEAMKA!
ASUBUHI mapema hivi anaamka mama Makene huyu ambaye ni mama yangu mzazi. Hiyo ni miaka ya huko nyuma wakati bado nasoma shule ya msingi. Anaamka katika nyumba ya shule iliyowekewa vioo kipindi cha ukoloni. Vioo hivi vilivunjika miaka kadhaa kabla hatujaamia nyumba hiyo. Ni nyumba ambayo imekuwa ikipiganiwa na Walimu wa shule ya msingi Mabuimerafuru, wanatamani kuishi katika nyumba yenye flemu za vioo huku wakiziba matundu na karatasi za nailoni.

Upepo unavuma kupitia dirishani, navuta shuka kujifunika zaidi na mama kishaamka anawaamsha sasa dada zangu. Hao nasikia wanatoka na dadangu mkubwa na mama wanaambaa hao kwenda kisimani kuchota maji. Ni mwendo wa kama kilomita mbili hivi na upepo unavuma. Hili linanitia simanzi...siwezi kutoka kitandani kumsaidia mama, maisha ya Afrika ukizaliwa Mwanamme basi umekabidhiwa ufalme.

Napitiwa na kausingizi katamu, simuwazi tena mama na ghafla nasikia mlango wa chumba chetu unagongwa na safari hii kwa nguvu. Mama huyo anakoroma kiasi maana tangu atoke kisimani nusu saa imepita na hatujaamka kwenda shamba. Ninawaza njia ya kufikia huko shambani. Njia hiyo imezungukwa na majani marefu kuzidi kimo changu. Hiki ni kipindi cha masika hivyo kuna umande mkali sana. Ili kufika shambani lazima ulowane na fikiri baridi ya asubuhi. Kuna suala la utelezi hili nalo ni jingine, nimeteleza sana lakini sikuwahi kusikia mama akiniambia waweza rudi nyumbani sasa ukapumzike lazima ufike shmbani na huku kazi ni ngumu, jembe la mkono...usisikie!

Kilimo cha mwaka huu kilikuwa safi, tulijituma sana maana ulikuwav mwaka wa uchaguzi, tumemaliza kumchagua Rais ambaye jina lake likifanana na Marehemu hapana nimesahau Hayati Kaka yangu Benjamin Nakuzerwa. Huyu kaka akawa shabiki mzuri sana wa sera za huyo bwana. Mkapa akapiga kelele kuhusun kufanya kazi kwa masaa mengi na kujenga nidhamu. Tukafuata kauli ya rais, tukalima kwa saa nyingi na kwav kujituma sana,

Sikujua haya na baada ya hapo ikawa hiki kinachonifanya kuchukia siasa za kifalme za Tanzania. Benjamin akatushawishi, familia yangu ikakubali kufanya kazi lakini baada ya msimu pamba yetu ikakosa soko. Tulipata mavuno mengi lakini soko hafifu halikuweza kulipa nguvu na nidhamu yetu. Ni mavuno hayo hayo yaliyotakiwa pia kutumika kumtibu Hayati Benjamin kwa ugonjwa wa Kansa, akamaliza vijisenti vile katika matibabu hafifu na mwisho kauli ikamtoka, akapumzika, akalala, akakimbia, akatutoka, akalalama akisema eloyi eloyi lamasabaktani! Kwa heri kaka nitakukumbuka sana milele!

Baada ya hapo nguvu kazi yetu katika kilimo ikafa, sikuona umuhimu wake lakini nikabaki na kilio cha uboreshaji wa huduma vijijini. Juzi kulikuwa na tatizo la maji Dar es Salaam, Rais mpya akatangaza katika sera zake kuwa hilo limeisha tuisubiri tu kuwa kura zetu zitatatua tatizo hilo. Nasikia watanzania wameamini kuwa kura zao zaweza kuondoa kero hiyo na wamezimpa kwa wingi mno.

Katika pita pita zangu nikaona bora kuwasiliana na mama, nikampata katika kile kijisimu chake alichotumiwa na mmoja wa wanae. Nikalonga naye akanieleza tena kilio cha kukosa maji kwani visima vimekauka hivyo wanatakiwa kutembea kilomita zaidi ya sita kutafuta maji ziwani pale kijijini Chumwi au Murangi. Nashika kichwa tena, nakumbuka nilipata taarifa za mradi mpya wa kupeleka maji Shinyanga na Dodoma kutoka ziwa Viktoria. Mradi huu haupiti kijijini Mabuimerafuru, hakuna kumbukumbu kama kutakuwa na mradi kama huu ili uweze kumnusuru mama yangu katika kilio cha kusaka maji maili nyingi huku akisumbuliwa na miguu kwa miaka mingi. Kipindi anachotoka kwenda kutafuta maji ziwani anakuwa kaacha wanafunzi bila mwalimu. Wanafunzi hao hushangilia tukio hilo maana nao huwa darasani bila kuoga kwa siku kadhaa. Tazama shida ya kukosa sabuni na mafuta ya kujipaka, sasa ongeza na maji ya kuoga na kufua huku darasa la kijijini likiwa bado ni lile lisilo na sakafu.

Nimekaa na kukumbuka kuwa kazi ya kuleta maji Mabuimerafuru, Mikuyu, Seka, Saragana na Nyambono imeshindikana kwa miaka 40 tangu uhuru. Ninatafuta njia ya kumtumia mama baisikeli ya kumsaidia kufika huko ziwani...lakini mama huyu mzee atawezaje kuendesha baiskeli nna uzee wote huo. Naogopa kutuma baiskeli hiyo maana yaweza geuka chanzo cha mauti ya mama yangu. Siwezi kujua nini iwe mbinu njema ila katika uchaguzi uliokamilika walipewa ahadi na mbunge wao kuwa kero zao zitaisha. Mbunge huyo aliahidi pia kujenga barabara ile mbaya kuliko zote nadhani katika Tanzania. Alisema jambo la awali litakuwa kupeleka mitambo ya simu bila kujua huko hakuna umeme. Alisema mitambo hiyo itawaunganisha watanzania walioko vijijini na walio mijini.

Akishakuweka mitambo ya simu, kitafuata kuweka viwanda kadhaa vya samaki. Samaki wote wamekuwa wakiuzwa katika viwanda hivyo huku wakazi wa vijiji vinavyolizunguka ziwa wakitangaza mabadiliko ya tabia za ulaji kuwa wanathamini sana makazi ya samaki hivyo hawataki kuwala kabisa! Wameamua kusaka majani na sasa hayapo kutokana na kiangazi, wananchi wanapigana na ng'ombe kusaka majani. Ni vita kubwa na mbunge nasikia ameshakimbilia Dodoma kuwahi kuapishwa. Hiyo ni sherehe kubwa na hatakiwi kuichelewa, Nasikia pia amewahi maana kuna kazi ya kuzungumza na Rais mpya kama anakumbuka kile kitita alichochangia chama wakati ule wa jkukomboa majimbo. Anataka sasa akumbukwe fadhila zake kwa kupewa walau kauwaziri.

Huyu mbunge hakuwahi kufika kumsabahi mama na hata wapiga kura wengine. Mara ya mwisho walimsikia alipotembelea pale Houston Texas kusalimia kimada wake anayemsomesha pale. Sakata hilo liliripotiwa na gazeti moja la udaku na hii ikachangia gazeti hilo kufungiwa. Mheshimiwa huyo amewahi kabisa Dar es Salaam ili kumnunulia kadi ya pongezi Rais mpya. Nani hajui kuwa alikuwa lazima ashinde lakini ndiyo Tanzania na hiyo ni geresha ya kuomba uwaziri na misamaha ya kodi katika biashara zake.

Nalalama na hasira hapa nasikia Melissa ananiita kumbe nilikuwa naota na katika ndoto hii nimetaja sana hofu ya barafu utelezi katika matope pale Ihungo. Nilikuwa pia nikizungumzia kule bondeni tulikokuwa tukichota maji palivyokuwa na utelezi huku giza totoro likigubika misitu ile ya Ihungo. Siku hizi misitu hii imekatwa kabisa, alikuha Mkuu wa shule mmoja mwenye uchu wa kutengeneza pesa, huyu alianzisha mradi wa kuuza mbao na akatumia msitu wa shule kutimiza haja zake. Sasa ukiwa mjini Bukoba waweza kuiona Ihungo juu ya kilima ikiwa tupu, uchi, si kama zamani ikimelemeta na kuzungukwa na kijani cha miti yenye bashasha. Natulia na kusema nimeamka na kazi imeanza.
 
© boniphace Tarehe 12/18/2005 05:50:00 PM | Permalink |


Comments: 2


  • Tarehe 12/19/2005 12:04 PM, Mtoa Maoni: Blogger Jeff Msangi

    Makene,
    Kazi nzuri sana hii.Unajua tungo za namna hii mimi hupenda kuziita darubini.Zinaeleza ukweli ambao mara chache sana hupewa kipaumbele.Unabakia kuwa mwendo wa bora liende bila kufikiri kwamba haliwezi kwenda bila kupelekwa.Matatizo ya jamii zetu ni magumu kuachiwa wanasiasa wafanye wayatatue,wameshindwa miaka zaidi ya arobaini iliyopita.Lazima tuanze sisi sasa.Tuwawajibishe hao wanaojiita wanasiasa.

     
  • Tarehe 12/20/2005 1:02 AM, Mtoa Maoni: Blogger mloyi

    Wanasiasa ndiyo walivyo? au ni sisi ndiyo tupo tupivyo?Amewahi Dsm Na Dodoma, atafanikiwa na nia yake, hujui kama mwenda bure sio sawa na mkaa bure!. Angalia. Mradi umeanza kujengwa sijui kama watu wa Shinyanga wameanza kuyaota hayo maji, Hapa dsm tumezoea, kila siku tunasikia maji yamepungua sehemu nyingi za jiji kwa juma zima sasa, wakati sisi hatujawahi kupata maji kwa miaka kama mitano, anatusaidia yule mpemba aliyechimba kisima nyumbani kwake lakini akisema anaenda msikitini ina bidi shughuli ya kuchota maji isimame mpaka arudi, tunamsubiri, Sijui hiyo kauli ya kupungua maji inatuhusisha na matatizo ya maji tuliyonayo sisi?
    Kilimo mlilima kwa bidii sana kuliko kipindi cha miezi kumu na nane ya kufunga mikanda, unakumbuka kauli hii?, Soko likawa duni, hamkupata kitu!
    Kaka akaumwa nadhani mlifikiria kuuza kila kitu, hata kama mngebaki watupu,ili apate matibabu ambayo hayapo. Fikiria hali uliyokuwa nayo kipindi hicho, hampo peke yenu wapo wengi sana wenye kupitia hali hiyo lakini hakuna mwenye kujali. Pole sana kwa hili.
    Samaki mmeacha kula siku hizi? mlipenda wenyewe au ili mpate pesa za kununulia dawa na mahindi? Hali halisi hiyo, sijui kama ndesanjo anaikumbuka siku hizi, maana jembe la mkono yeye halioni tena.
    Sherehe hiyo imeanza sijui ni kwa faida ya wapiga kura na wapiga debe wao au kwa ajili ya kuonyesha wao ni wababe huku kazi walifanyiwa.

     
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved