Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Monday, December 05, 2005
MOJA KWA MOJA NA RAIS, KISHA WAZIRI MKUU
NIMEKUJA na furaha leo kukufahamisha Mwanablogu mwenzangu yaliyojiri jana. Furaha yangu ilitiwa simanzi kidogo na maoni niliyoyapata katika ukumbi wa barua zangu mtandaoni ambao nimeamua kuibandika hiyo katika makala hapo chini.

Enewei sasa nianze japo harakaharaka. Jana nikapata fursa ya kuzungumza moja kwa moja na huyu waziri mkuu cheo hiki nimemtunuku mimi nitafurahi kama nawe utabariki mapendekezo yangu. Ni waziri mkuu wa Blogu za Tanzania. Nilikuwa na namba yake ya simu maana Mawaziri wakuu watu simpo tu ndio maana hata namba ya Bwana Fredrick Sumaye ninayo...sijui nikuwekee kwenye kiunganishi hapa lakini hapana siku zake zimeisha huyo subiri nitabandika ya Lowassa siku si nyingi.

Basi mazungumzo na mheshimiwa Waziri Mkuu yalikuwa safi sana na tukaeleweshana kero tunazozikabiri sisi wananchi wa chini na mheshimiwa akazungumzia umuhimu wa kuongeza majimbo ya Blogu zaidi ili nchi yetu iweze kufikisha ajenda ya kuwabadilisha fikra Wanazuoni. Mazungumzo yale matamu yalikatishwa baada ya kilongalonga changu kukaukiwa mafuta, sina maana ya dola bali kiliishiwa umeme.

Nikiwa nimetua simu huku sitaki kupokea simu kabisa ghafla ikaita tena. Sikujua tena huyu nani lakini kwanza nianze na kisa hiki katika "Mzimu wa Watu wa Kale." Mohamed Said Abdulla humtumia mhusika "MSA" katika kazi zake. Huyo MSA ni kifupisho cha majina yake.

Basi bwana Msa ukimuuliza juu ya umuhimu wa Mwanga atakwambia nenda gizani...ukisema maana ya elimu atatoa jibu la kukutaka kutazama yule asiyesoma! Basi kuna huyu mheshimiwa Rais katika Blogu za Watanzania. Bawana huyu ukimuuliza swali la kutaka kufanya hivi hukaa kimya na kukujibu jingine. Siwezi kubandika aina ya majibu yake maana cheo chake huyu kikubwa.

Sasa huyu jamaa akaanza kupiga simu huku akihoji mimi bado nafanya nini Marekani. Nikahisi kuanza kutumiwa watu kunifatilia maisha yangu...maana siku hizi nimechoka na kauli za vitisho na nimejizatiti sana kutozijali. Jamaa huyu ameniweka katika kona utadhani FBI kisha ndipo akajitambulisha hali iliyonihemsha furaha na tabasamu usoni.

Sikuwahi kujadiliana naye lakini mazungumzo yangu hayakuwa mbali sana na yale tuliyozungumza na mheshimiwa Jeff Msangi. Naye akanihamasisha kuwatangazia zaidi Watanaznia wengi kuingia katika Blogu. Sina namna wakuu najitahidi kutimiza kazi yenu maana mwaweza kunipa hata kauwaziri ka ulinzi wa Blogu siku zijazo.
 
© boniphace Tarehe 12/05/2005 06:47:00 AM | Permalink |


Comments: 0


   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved