Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Wednesday, December 28, 2005
NINI HATIMA YA UBABE HUU WA MAREKANI?
KUNA msemo wa Kiswahili usemao, "ada ya mja kunena, muungwana ni vitendo" Natumia msemo huu kuonyesha heshima yangu kwa wanaochangia mijadala katika KASRI. Kompyuta ninayotumia inatatizo katika kuweka viunganishi lakini naomba nikidhi ombi la Ndesanjo kwa kuweka makala hii hapa chini kama ilivyochapishwa na gazeti la Mwananchi Jumapili iliyopita. Waweza isoma sasa



NIMEKUWA katika safari wiki iliyopita na wahenga hawakukosea walipotoa msemo wa tembea uone. Niko katika pitapita za kuvuka mageti katika viwanja vya ndege na huko ninakutana na kizaazaa.

Msururu wa kuingia uwanjani katika njia ya wasafiri ni mrefu na inafika nafasi yangu nakutana na bibi huyu anayeonyesha sura ya tabasamu lakini tu na matendo yake ya kinyama kabisa. Haya ndiyo maisha yaliyopo Marekani, kila utakayekutana naye atakuonyesha tabasamu la usoni lakini moyoni si kuwa ana hamu na wewe.

Katika Tanzania sisi si wepesi wa kucheka cheka lakini tufanyavyo hivyo huwa ni kwa dhati kabisa kutoka moyoni. Hapa athari za ubepari zimegueza binadamu kuwa wanyama kabisa. Fikra zao ziko katika kujenga faida tu na utu umewekwa kando.

Napofika kwa huyu bibi ananiambia kukaa katika geti jingine, kauli hii anaitoa akiwa anatabasamu hali inayonipa mkuhisi kuwa huenda kaona nipewe njia bora zaidi. Nadhani unajua kuwa Afrika mgeni hupewa thamani ya kwanza, nadhani kuwa ni hili linalofanyika hapa...baadaye nang'amua kuwa sivyo!

Tangu kumeingia hili suala la ugaidi mataifa ya Afrika nayo mengi yamejumuishwa katika orodha ya nchi za kigaidi. Kisa eti ni umaskini wa nchi hizo. Nini maana ya umaskini wa nchi na ipi faida ya utajiri wa taifa moja ambalo raia wake wa hali ya chini wanalia katika hatari kubwa?

Hii ndiyo taswira ya Mrekani, taifa lenye uchumi bora kulingana na takwimu za Benki ya dunia na IMF lakini nchi yenye ufa mkubwa kati ya maskini na tajiri. Nasikia hii ilikuwa pia sera za awamu ya tatu katika Tanzania. Sera za kukuza uchumi kwa kufuata takwimu za Benki la Dunia na IMF. Vyombo hivyo ni makuwadi sawia wa Marekani na ili taifa liweze kukubalika kuwa linatanua uchumi wake na kuingizwa katikia takwimu zake lazima kuwe na hali ya kukubali magandamizo na manyanyaso ya Marekani.

Tanzania ilikubali, hoja ya kwanza ni huko kubadilishwa kwa Hati za kusafiri kwa lengo zikidhi matakwa ya kusomeka na kompyuta za Marekani. Tukabebeshwa mzigo wananchi bila kupenda na sasa cha moto tunakiona. La pili ni kupitishwa kwa kishindo sheria ya ugaidi. Sijui ugaidi ni nini hapo Tanzania, nadhani ni siasa za CUF na CCM!

Basi kutokana na haya masuala ya kukumbatia sera za Marekani basi nikaanza kupata adha ya kukaguliwa na kila kifaa cha teknolojia. Jamaa hawa hawakutosheka na baada ya kumaliza kuna huyu mjinga akaamua kabisa kuanza kunitomasatomasa, ni wazi alinipa mfadhaiko, sijatomaswa siku nyingi lakini hiin ilikuwa kero nyingine kwangu!

Nikajifanya kusahaun yaliyonikuta hapo San Antonio, nikaanza kusafiri na kufika uwanja wa Ohare, Ottawa, yakawa mengine. Hapo nikaanza kuhojiwa maswali makali na kwa tathmini yangu nikaanza kubaini vita vya wazi kati ya Marekani hata na Canada.

Nikaonekana mimi naheshimu sana sheria za Marekani na kutotilia mkazo hizi za Canada. Nikaonekana naona Marekani ni nchi zaidin kulikom ilivyo Canada na ikaja suala la kutoka Tanzania hapo Canada na Marekani zikawa na hoja sawa. Mimi kutoka Afrika nafata nini katika mataifa haya?

Mizigo yangu ikakaguliwa kwa kutoa kitu kimoja hadi kingine. Ikanikumbusha enzi zile elimu ya sekondari Tanzania ikitawaliwa na ubabe. Kipindi cha shule chache, kipindi cha walimu kuwa wafalme hali iliyowafanya kufukuza wanafunzi walivyopenda. Oma ufukuzwe enzi hizo, begi lako na mizigo yako ilikuwa ikiwekwa hadharani kwa ukaguzi ili wanafunzi wengine watizame kama kuna mali zao unataka kuondoka nazo...nakumbuka chuki hii japokuwa ikupata bahati ya klufukuzwa!

Naiita bahati maana kuna dhana niliyojiwekea katika maisha kuwa jambo baya ni muhimu sana likutokee ili uweze kukamilika. Kama mabaya hayakutokei huwezi kujiita fundi wa utatuzi wa matatizo. Fikra hizi zinanikumbusha tena kitabu cha Nelson Mandela "Long Walk to Freedom."

Ninapopita na kuruhusiwa kuingia sasa Canada, nakutana na swali kutoka Marekani. Marekani imekuwa katika mjadala wa kujenga kuta za kuzunguka mipaka yake. Moja ya sababu kubwa zinazotumiwa na wawakilishi wa Republican ambao ndio chanzo cha mjadala huo kupelekwa katika Kongresi ni kuwa hii itasaidia kupambana na ugaidi na pia kulinda kuingia kwa raia wa kigeni kinyume cha utaratibu.

Marekani chini ya George Bush huyu na si yule aliyewahi kusifiwa na Mandela nyakati za kupambana na ubaguzi wa rangi Afrika Kusini, ameamua kutokumbuka tena historia ya Mareakani. Hakumbuki kuwa majimbo kama Texas, New Mexico na sehemu ya Califonia yalikuwa chini ya Mexico. Hakumbuki kuwa nchi hiyo na majimbo yake yote 50 yaliwahi kuwa nchi huru...na tena hakumbuki kuwa umoja huu wa Marekani hautadumu miongo kadhaa ijayo!

Bush na chama chake kinatangaza kujenga ukuta, na swali hili limewashangaza wengi niliokutana nao hapa Canada. Kila mmoja anahoji ujinga wa serikali ya Marekani. Wanauliza je huu ndio mwisho wa ugaidi ambao chimbuko lake ni Marekani? Wanahoji tena vipi kuhusu mauzo ya madawa ya kulevya ambayo huratibiwa na wafanyabiashara wa Marekani ambayo husambazwa katika mataifa mbalimbali. Na je Bush na Republican hawana kumbukumbu ya Ukuta wa Berlin?

Raia wanatamkika kuwepo Mrekani kinyume na utaratibu wanafikia milioni 11. Hawa wanachangia nguvu zao kwa kasi kubwa sana kunyanyua uchumi wa nchi hii. Marekani haikuwahi kuondokana na mfumo wa kitumwa badala yake iligeuza utumwa na kuupatia majina mengine matamu katika taswira ya ulimwengu.

Mabepari wa Marekani wamejenga himaya za maisha yao kutokana na unyonyaji wa wazi. Mishahara wanayowalipa hao wanaoitwa wakimbizi katika Marekani licha ya kuwa ina unafuu kuliko katika mataifa yao ya awali lakini bado ni ya kiukandamizaji sana. Hali ya mabadiliko katika maisha ya Marekani imekuwa mbaya zaidi hasa kipindi hiki cha uongozi wa Republican.

Analaeuskas, mwandishi wa "Discivering America as it is," alifika Mrekani kutoka Urusi akiwa na ndoto tunazokuwa nazo wengi tukiwa nje ya Marekani. Analaeuskas alikimbia kipindi kile cha serikali za kikomunisti na akadhani kufika kwake Marekani ni kuingia katika mbingu ya dunia. Hakukuta hilo na katika kitabu hicho anachambua hali ya maisha ya Marekani na kuonyesha kuwa mazingira yab Urusi kulikuwa na unafuu mkubwa sana kuliko hali hii anayoitazama Marekani.

Mfumo wa kikomunisti tuliwahi kuuishi hapo Tanzania, bado wananchi tunauthamini lakini viongozi wetu tangu awamu ya pili walitamani ukubwa wa Kimarekani wakakimbia mfumo huo na hiki ndicho chanzo cha kupanuka ufa kati ya tajiri na maskini katika Tanzania.

Ubabe wa Marekani unapatikana katika mazingira mengi, nchi hii ndiyo hasa inayochangia Mexico kutokuendelea kutokana na kunyonya kwa wazi vyanzo vya kiuchumi vya Mexico. Licha ya kupakana na Marekani maisha ya Mexico hayana tofauti sana na Tanzania, rushwa ni mdudu mtamu kuliwa lakini sijapata taarifa kama nchi hii nayo ijna sheria inayohararisha rushwa kama Tanzania na sheria ya Takrima iliyowekewa mkono na rais wa awamu ya tatu!

Harakati za kujenga ukuta zinakuja wakati bado athari zilizosababishwa na kimbunga Katrina na Rita hazijaondoka. Mikakati ya kusaidia maskini hasa wenye ngozi kama yangu ni ndogo na sijui zitaonekana lini.

Hali ya kiusalama kwa vikosi vya Marekani katika Iraki na Afghanistan bado si ya kuridhisha. Mazingira ya kuepusha dunia katika janga la ugaidi hayaonyeshio mafanikio badala yake kunajengwa matukio yanayoweza kuhatarisha zaidi mahusiano katika ulimwengu na hivyo kuchochea ugaidi na matukio mengine ya kujitoa mhanga.

Serikali mpya imeingia madarakani hapo Tanzania. Inaweza nayo kufuata misingi ya kutaka sifa za takwimu za kiuchumi kutoka Benki ya Dunia na IMF. Nchi nyingi zilizopata kusifiwa na mashirika haya ni zile zinazokumbatia uchumi wa Kimarekani, uchumi unaotoa fursa kwa wachache kujigeuza mabwanyenye na kuwanyonya wengi. Haya si matarajio ya wapiga kura wa Tanzania.

Watanzania wanahitaji uchumi shirikishi, uchumi utakawaweka wamoja na sio kuwatenga kama awamu mbili zilizomaliza muda wake zilivyoweza kufanya. Sasa hivi kuna matajiri ambao hawakuwahi kuota shida katika Tanzania huku kukiwa na maskini anayefariki kwa kukosa shilingi mia za kununulia panadol.

Watanzania wanataka kuona usawa unaopatikana katika kupiga kura unaelekezwa katika uchumi pia. Hakuna maana ya kuwa na kura moja mtu mmoja huku ikifika katika kutumia rasilimali za umma kunakuwa na wachache kumiliki zaidi ya wengine.

Haya ni maisha ya kibabe ya Marekani na Tanzania inaweza kujifunza vema. Kukosekana ajira nchini kunatokana na kutokuwa na mikakati ya kujenga ajira mpya. Kukosa elimu bora kunatokana na kugeuza mfumo wa elimu badala ya kuwa haki ya watu sasa ni haki ya wenye mali. Kukosa madawa katika hospitali kunatokana na kukithiri kwa ubinafsi katika mifumo yetu ya afya. Wakubwa kuthamini kutibiwa Ulaya na kutotambua shida zinazowakabili wananchi wa chini.

Kuimarika rushwa nchini kunatokana pia na serikali kuona rushwa ni jambo muhimu kurahisisha utawala. Kama sivyo sitarajii kuona bunge jipya likishindwa kuikataa sheria inayoruhusu rushwa au hata mfumo wa mahakama ambao pia bado ni dhaifu katika Tanzania ukiipinga sheria hiyo kwa kuwa inapingana na haki za binadamu. Htujapata jemedari wa kupambana na rushwa na huyu mpya anaweza kuanza kwa kurejesha nyumba aliyojigawia sawa na wenzake katika awamu ya tatu.

Uongozi wa Tanzania sasa unataka vitendo, hakuna haja ya maneno maana tumezungumza sana zaidi ya miaka 40 na hakuna tulichofanikiwa! Tunahitaji kutooneana haya...tunahitaji mapambano mapya yasiyotazama sura!

Inawezekana wazi Tanzania ikajiendeleza na kujitosheleza kama tutakubali kusimamia misingi ya kujiendeleza na kulijenga taifa letu. Twatakiwa kuachana na kujisifu kuwa sisi ni halali kukopa na kuwa tunajenga heshima ya kukopesheka!Tangu lini mkopeshwaji akajisifu, kuwa mimi maskini safi sana hadi jamaa zangu wanakubali kunikopesha. Huo si ustaarabu wa Afrika, waafrika tangu awali tu waoga wa madeni na ndio maana tukakubali kuanza na siasa za kujitegemea.

Umakini unahitajika sasa kinyume na hivyo tutazidi kudhalilika kila tunapotembea katika uso wa dunia. Haya tunayoyaona tunapoingia katika mipaka ya nchi za wenzetu ni ishara kuwa tunatakiwa kuwaonyesha kuwa sisi nasi tu huru na tuna imani na misingi yetu na kimsingi tunajiongoza na sio kuburuzwa!
 
© boniphace Tarehe 12/28/2005 03:26:00 PM | Permalink |


Comments: 0


   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved