Nakumbuka maana kipindi hicho niliweza kukariri barua zangu kwa mashairi. Ni kipindi hicho nilipokuwa shabiki mkubwa wa Ustadhi Andanenga kabla sijakutana naye kwa macho pale Nkrumah Chuo Kikuu Dar es Salaam, katika usiku wa Ushairi nilipokuwa pia msema chochote huku nikighani tungo kama hizi;
Ya Liyongo hutwambia
Siu alikozaliwa
Pate akitembeleya
Na Mwana akafiliya.
Kutoka Utenzi wa Fumo Lyongo: ubeti huo unatangaza maisha yote ya Fumo Lyongo jasiri, shujaa katika upwa wa Afrika Mashariki miaka hiyo. Nakumbuka nilishokuwa nikiyapinga mapingiti ya Euphrase Kezilahabi lakini baadaye ni K. Kahigi aliyeweza kunibadili na kunirejesha kumuamini Kezilahabi na mtindo wao wa mashairi guni.Hiyo ilikuwa chombeza tu lengo ni kumkaribisha malenga mpya huyu, kaja vema sana anapaswa kupongezwa kwa kujenga mhimili wa lugha katika Blogu. Kosa lake katangaza kitu ambacho nakumbuka napingana nacho katika beti alizojibu majibizano yangu na ghani ya maneno ya Ndesanjo.
Mkwinda kaka fikia, keti mwana bloguni
Zamani niliwazia, siku nitapokufani
Nani atashikilia, KASRI langu tunzani
Sasa napata faraja, kijana mpya tokea.
Umekuja kwa makeke, kisa changu kujibuni
Ulinifanya nicheke, machozi kinitokani
Vipi utaje mapene, kwa fani ya malengani
Mkwinda sasa useme, hisa unaziuzani?
Mapene wapi mizani, kitita sikitamani
Natunga nili zuoni, mapene kwangu sumuni
Siwezi kuyatamani, kwani yanageuzani
Utumwa wakumbukani, kisa mapene fatia.
Malenga vina pangia, hoja weka bloguni
Hatutaki majalia, ya pesa kutulipani
Ushairi nashibia, beti nazodondoani
Mkwinda acha makeke, ushairi si mapene.
Kalamu yake Ndesanjo, kali kaka ujuani
Wapaswa kukaa chonjo, Rais mtaniani
Utajatoa mkojo, Segerea laliani
Ndesanjo mtu mwingine, silinganishe na mimi!
Nimegundua kimoja, vina hujavipangani
Sasa niambie hoja, mapingiti watungani?
Kesho utakapokuja, tamka nikujuani
Kalamu ulofungua, wino imeshachojoa.
Tangu juzi nasemea, niko bize masomoni
Mitihani nafanyia, bado sijamalizia
Lakini mwatukania, kisa changu kujibuni
Kalamu nalaza chini, Mkwinda sigange njaa!
Mnanikumbusha mbali kweli. Kumbukumbu tamu sana hizi. Halafu nimefurahi umemtaja Fumo Lyongo. Twahitaji kuandika sana na kwa undani juu ya habari kama hizi maana hivi visa ndio urithi wetu (kama vile wayahudi walivyokusanya visa vyao kwenye torati na manabii). Ziko habari za akina Ngwanamalundi, kwa mfano.
Turudi kwenye ushairi. Unanikumbusha enzi za kusoma gazeti la uhuru kila siku na kusikiliza RTD.