Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Wednesday, December 28, 2005
UKO WAPI MHESHIMIWA MBUNGE?
WIKI hii nimekuwa katika wakati mgumu sana. Sifahamu kama miaka inaenda hivi kama kweli nitakuja kukomboka na hali hii. Mawazo, fikra na kuchoka akili kumeniandama...sijui nifanyeje na kila nitazamapo sura ya mke wangu na baadaye wanangu nashindwa kuyapeleka macho yangu kukabiliana nao kama zamani.

Nilijiita mzazi bora miaka ya nyuma, nilikuwa nikijitapa sana mtaani hali hii ilitokana na ubingwa wa kujua mbinu za kupanga uzazi. Sikutaka itokee hatari ya mimi kuwa na watoto lukuki hivyo nilimpeleka mama Sikujua kuchukua dawa za kuzuia uzazi mapema baada ya kupata mtoto wa tatu. Maamuzi haya niliyafanya baada ya kumpata Mawazo kidume changu cha kulinda jina la ukoo wangu.

Tangu azaliwe Mawazo na hasa baada ya Mama Sikujua kuchukua dawa za kupanga uzazi, ameondokea kuwa na magonjwa yasiyoisha ya tumbo. Afya yake imekuwa ikizorota na kunipa simanzi. Furaha hapa nyumbani imegeuka taswira hasi, mkondo wa giza na kusudio lisilotazamika.

Wanangu ambao umri bado huu chini wamekuwa na kibarua cha kuambatana nami shambani na siku nyingine kwenda wao peke ya hasa siku ninazompeleka mama yao zahanati. Kila nikirudi hukuta vilio vya watoto hawa ambazo ukiwatazama nyuso zao utabaini kuwa walisahau bashasha karne nyingi zilizopita. Masha huyu mtoto wa pili ndiye hasa ambaye hakauki dimbwi la machozi. Analilia vyakula vitamu ambavyo siku hizi siwezi tena kujibana kuwanunulia hawa wanangu.

Wanatamani mboga iliyoungwa, hakuna mafuta ya kupikia hapa nadhani muongo unaelekea. Nilishasahau kuwa kuna nyama na samaki licha ya kuwa wanangu wanalitazama ziwa na mara kadhaa wameenda huko kuchota maji kila kisima chetu kinapokauka. Mwaka huu msimu wa mavuno umeambatana na kilio, hatukuweza kupata pamba kufuatia ukame, na hii ndogo iliyopo haina soko. Makampuni yanayonunua pamba yamegoma kuja kijijini kwetu kwakuwa hakuna mavuno mengi.

Inatubidi kutembea mwendo wa siku mbili kwa miguu ili kulifikia gari linalonunua pamba. Gharama za kusafiri kwa basi nadhani ni kubwa kuliko mauzo ya pamba yangu. Hakuna chakula cha akiba maana mahindi nayo yalikataa kuvunwa mwaka huu.

Sherehe za Krismasi nashukuru zimepita, ilikuwa ni wakati mgumu sana hapa nyumbani. Mama Sikujua mgonjwa huku watoto wakililia nguo mpya. Sasa nasikia kuna hizi za mwaka mpya. Kijijini kwetu kutakuwa na hotuba ya Mbunge tuliyemchagua ikisomwa na Mwenyekiti wa Kijiji. Ngoma ya mgambo imepigwa kuwa lazima tuwe katikia mti wa mikutano na familia zetu kusikiliza hotuba hiyo.

Nawaza siku hizo itakuwaje maana Mbunge huyo hatakuwepo ...amekwenda kusikiliza Bunge jipya. Nasikia tutaweza kumuona akizungumza Bungeni kupitia Tivii aliyoiweka hapa kijijini. Haka kachombo kalichangia sana mheshimiwa huyu kupigiwa kura. Baada ya kushinda ametuachia hapa kijijini lakini tangu atuachie hatujawahi kutazama picha kufuatia kijiji hiki kuwa kimojawapo katika vijiji vilivyowekwa katika ndoto ya kupata umeme. Wanasema haka kativii hakatumii betrii hizi za Matisushta ama zile za National. Kazi ipo na wanangu wanataka kuwa nadhifu siku hiyo ili wasichekwe na wenzao pale watakapokuwa mbele wakitazama picha za mheshimiwa mkombozi wa jimbo letu.

Wakati fikra hizi zinaujaza moyo wangu, namuona mwanangu Masha anakuja kashika kijibarua. Hapa nakitazama kinaonyesha kutoka shuleni. Hii ni michango mipya ya mavazi ya kumpokelea Mkuu wa Mkoa mara shule itakapofunguliwa. Nasikia Masha atakuwa miongoni mwa Chipukizi na hivyo natakiwa kununua sarawili jeusi na shati la kijani kwa ajili ya Masha. Nashika kichwa sijui nitapata wapi fedha za kutimiza matakwa ya Masha.

Ghafla nasikia kilio ndani, ni mama Sikujua anatoa kauli ya kuhitaji msaada, tumbo linamkata na sijui nitamfikishaje hospitalini. Mara ya mwisho tulijitahidi kufika na kuishia kuandikiwa karatasi ambalo siwezi kulisoma zaidi ya hizi herufi sijui ASP. Tuliambiwa twende na karatasi hilo katika duka la dawa la Daktari Nonino lililopo nje ya Hospitali ya mkoa. Kufika huko nilitajiwa fedha ambayo sikuwahi kuota kuisikia katika maisha yangu miaka hii kumi ya Rais Mkapa.

Tukaamua kurudi huku mama Sikujua akilia lakini tufanyeje. Akarudi nyumbani mwendo wa miguu siku mbili akijikokota na kilio cha maumivu. Safari ile ilimuweka kitandani wiki mbili na ni jana tu alipopata nafuu ya kutoa salamu kwangu. Najuta kwa nini nilimpeleka huko maana ilikuwa kumdhoofisha zaidi. Mama Sikujua analia na ninamtazama anatoa macho huku akionyesha kuniomba kitu. Namtazama na kumkaribia huku wanawe wakiwa karibu na machozi yanamtoka...

Nami nalilia moyoni huku nikiona mke wangu akiugulia mauti. Analia...analia,,,maumivu yanazidi kuwa makali. Nakumbuka ahadi za Mbunge wangu kuhusu afya bure kwa kila raia. Natamani awepo hapa atoe haki hii kwa mke wangu. Nakumbuka kukimbia kwa Mzee Matambala ili anipatie vijimizizi ili nimtulize mke wangu. Kabla sijaondosha mguu nagundua kuwa ananidai dawa alizotoa tiba zaidi ya mara tatu. Nashawishika kuchukua huyu kuku tuliyekuwa tumembakiza hapa ili aweze kuwa hazina yetu ya mwisho.

Ninapomfukuza kuku huyu ghafla inatokea pikipiki barabarani na kumgonga...kuku wangu anakufa na hapo nashangaa kuwa napaza sauti ya kulilia kuku huyu na kusahau maumivu na uchungu wa mke wangu! Mwenye pikipiki katimka na siwezi kumpata...nashia machungu machungu makali na sauti inanitoka ...uko wapi mheshimiwa Mbungeeeeee? Naanguka na kulia huku nikimkumbatia kuku huyu! Ninapoamka nakutana na sura za Sikujua, Masha na Mawazo wote wananitazama huku wakilia...wananionyesha kwa kidole kuwa niingie katika banda langu. Ninapoingia huko nakaukiwa na nguvu naanguka chini na kujikuta keshoye nimezingirwa na wanakijiji!

Nawauliza yuko wapi mheshimiwa Mbunge? Naona mwenyekiti wetu anaelekeza uso wake pembeni yangu...hapa machale yananicheza, kuna mtu kalala kafunikwa shuka jeupe...natoa kelele za uchungu bila kutazama kisha naishiwa nguvu na kuzirahi tena!
 
© boniphace Tarehe 12/28/2005 04:21:00 PM | Permalink |


Comments: 0


   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved