Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Saturday, December 24, 2005
MSEKWA ANATAKA NINI?
FIKRA Thabiti alituma bomu kwangu na Ndesanjo jana. Alitaka tuseme, nilichangia na kuahidi kutuma uchambuzi katika gazei la Mwananchi ili kiu yangu ifike kwa wapiga kura wa CCM wajue nini kinachowakabiri.

Materu
nimeandika na makala yangu mwaweza pia kuisoma hapa chini.

Msekwa anataka nini bungeni?

MAISHA ya wanasiasa matamu sana, hayafai kuigwa hata kidogo na kikubwa yamejisimika katika sifa moja kuu uongo. Ni katika sifa hiyo hiyo ambapo Mwanasiasa hugeuka kuwa kigeugeu.

Niombe radhi kwa mifano hii ninayoitumia leo, imekuwa karibu kwangu na hivyo nadhani itachangia kusimamisha hoja yangu. Waziri wa Afya serikali ya Benjamin Mkapa alitangaza mapema mwaka uliopita mkoani Tanga kuwa hatagombea tena ubunge.

Wengi tulifurahi maana tulitambua kukua na kuthamini nafasi ya wakati katika kuongoza. Tulijua sasa Tanzania inaanza kupata watu wanaobaini kuwa madaraka ya kisiasa si ajira bali utumishi.

Nimekatishwa tamaa kusikia huyu huyu sasa ni mbunge wa viti maalum kupitia CCM. Kumbe kutangaza kule kulikuwa geresha, alikuwa keshapata mlango mororo wa kuingilia madarakani, na kwa kuwa alikuwa karibu sana na kampeni za mgombea urais wa CCM, Rais Jakaya Kikwete sina swali kuhusu kuteuliwa kwake kuwa waziri tena.

Haya ndiyo maisha ya wanasiasa, geugeu sana, wanadhani jamii imelala haiwatazami, wanaamini kuwa nchi bila wao haiendi. Kauli za hivi karibuni za Rais Kikwete kurejea kutaja majina ya waliokuwa wakiwania urais naye kupitia CCM kuwa bado anawahitaji inatia maswali kadhaa. Mosi inaonyesha kuwa ukigombea unakuwa muhimu kuliko wengine au unapata nafasi ya kuwa na kura inayohesabika zaidi kuliko sisi akina kalubandika!

Mbona Rais hasemi kumtegemea Mbowe, Lipumba au Senkoro? Mbona hamtaji Mrema, Kyara na au Mvungi? Utajua kuwa siasa za Tanzania sasa zimekuwa sawa na maji ya mtungi mmoja. Wenye nguvu ya kuyanywa ni wale waliokaribu na mtungi huo. Na hapa ni chama cha Mapinduzi.

Moja ya masuala yaliyozungumzwa wakati wa mchakato wa kupata mgombea wa CCM ilikuwa utata wa John Malecera kutolewa mapema. Utafiti usio rasmi ulifafanua hoja ya umri maana kwa umri wake tayari ilishatosha kustaafu na kupumzika. Kwa kuwa siasa ni ajira Tanzania hakuna aliyekubali na sasa familia yake iko bungeni yale yale ambayo kama utachunguza utayakuta yalitawala katika bune lililopita.

Mwanasiasa mimi...sikumbuki ninalozungumza sasa. Nakumbuka ninalosema baadaye. Mwanasiasa mimi...mtalaamu wa hekaya za uongo na uzandiki. Mwanasiasa mimi....mtaalamu wa kulamba matapishi.

Mwezi uliopita nchini Marekani kulikuwa na taarifa ya Ikulu ikipinga kauli za Rais George Bush alizowahi kutoa kipindi cha nyuma. Bush kama muumini wa mfumo wa Kikonsevativu, aliwahi kukaririwa akimtumia Mungu kuwa, "alimtuma kuivamia Iraki jambo ambalo alifanya na sasa anasikia kuwa anamwambia kuingilia mgogoro wa Palestina na Islaeli na yuko radhi kufanya hivyo."

Nch za Mashariki ya mbali ziliogopa kauli hii maana wanamjua Bush kwa vita. Al jazeera ikatangaza na kuonyesha hofu ya mataifa hayo. Ikulu ya Marekani ikapinga na kusema Bush hakuwahi kutamka maneno yanayofanana na hayo. Kumbuka kuna mikanda ya video lakini hii nimeitumia kukupa tu picha ya maisha ya wanasiasa!

Kushindwa kupiga hatamu ya maendeleo kunachangiwa na uongozi wa kubebana. Kuchaguliwa kwa Kikwete kumekuja kama adhabu baada ya kuonekana kuwa Rais huyu anaweza kupambana na tabia za kupinga kubebana katika madaraka. Kama alivyowahi kusema Mkapa, ukitaka kumjua mtu mpe madaraka, sasa Kikwete ni Rais na tunasubiri kumpima baada ya kuchagua baraza lake la mawaziri kama atafuata mfumo ule ule wa funika kombe!

Hakuna chuo cha kuongoza, maarifa ya uongozi hupatikana kutokana na mazingira na hatab kizazi na kizazi. Hoja ya kuundaa watu kujitawala ilikuwapo wakati Tanganyika ikisubiri Uingereza ikubali ijitawale. Mtakumbuka tulivyokabiliana na hoja hii huku tukionyesha ari ya kutaka kujitawala.

Tulifanikiwa lakini sasa kuna wajanja wamegeuza kabisa madaraka ya kisiasa kuwa ajira zao. Inawezekana wamefanya mengi mabaya na sasa wanaogopa watajificha wapi na wanajuan utawala hata kama utabadilishwa hakuna atakayewagusa...lakini wasiombe nafasi ya wakati ikawapitia.

Maneno yangu yote huko juu ni kupuliza tarumbeta tu. Nimesoma maoni ya Watanzania wengi katika mtandao ambao wameonmyesha dukuduku lao kuhusu spika wa Bunge lililopita kuamua tena kugombea. Anasema, mosi ni haki yake kikatiba, je hatambui kwa kukalia kiti hicho kwa miongo mingi amevunja haki za wangapi waliokuwa na uwezo wa kukikalia?

Anasema, ameombwa na wabunge kuwa asisitaafu? Ni wabunge wapi, awataje sasa...nani hajuin kuwa alivunja bunge siku ile Mkapa alipotoa hotuba yake ya mwisho? Nani hajui kuwa tukio hilo liliambatana na Msekwa huyu kufuta uwakilishi wa Wabunge wa Tanzania katika mabunge mengine?

Nani hakumbuki sakata lake na Balozi Mongella, Rais wa Bunge la Afrika na ambaye inawezekana akawa Waziri mkuu ajaye wa Tanzania? Mmemsahau Msekwa inaonekana...alikutana na wabunge wapi maana hawa wapya wamechaguliwa juzi na hana madaraka ya kukutana nao ili hadi wamuombe kuwa spika wao?

Amesahau Msekwa kuwa moja ya hoja katika kampeni zake miaka mitano iliyopita na iliyomrahisishia kushinda ni kuwa alitangaza kuwa hicho ni kipindi chake cha mwisho? Alishinda na sasa amesahau, amekuja na kauli za wanasiasa zilizopitwa na zama za kutaka kuomba ridhaa ya kumalizia kazi walizozianza, kazi zipi hizo Msekwa ambazo zimekushinda kwa muongo sasa wataka kuzimalizia hapa na zama hizi za kasi, ari na nguvu?

Mila za kiafrika hazinipi fursa kutamka mengi, namuonea huruma babu yangu Msekwa lakini naomba kumkumbusha kuwa kwa mila hizo hizo, vijana wa kiafrika tumepewa jukumu la kuwatunza wazazi wetu. Msekwa aseme kama anataka kutunzwa tujue moja na hilo litafanyika.


Ukifatilia mbali utatambua kuwa kipindi cha utawala wa Msekwa kama Spika Tanzania imepitisha sheria mbalimbali na kwa sasa tunahitaji Rais wetu Mpendwa Kikwete kuzifuta. Moja ni hii iliyoidhinisha matumizi ya rushwa. Sheria hii imeipatia Tanzania rekodi ya kuwa nchi pekee inayoruhusu rushwa kwa kupatia sheria muwali iitwayo Takrima.

Haya ni matunda ya Msekwa na bunge lake, wabunge wapenda rushwa wamemuomba kugombea tena...amewaitikia na sasa amechukua fomu. Katika kinyang'anyiri hicho yupo Jamadin Akukweti, Naibu Spika wa Msekwa! Tazama hapa kituko kingine, yaani hawa walikuwa hawawezi kuketi na kuambiana kuwa mzee imetosha na sasa mimi naibu wako nipande kuchota maarifa zaidi?

Au Msekwa haoni kuna lojiki kwa Akukweti kugombea na yeye kwenda kumnadi. Antamani nini...au haamini kuwa Akukweti mgombea ubunge aliyepata pia kuzomewa mbele ya Kikwete, kuwa ameiva na anaweza kusimamia pale aliposhindwa Msekwa?

Katika kinyang'anyiro hiki pia yupo Phillip Marmo, huyu aliwahi pia kushika madaraka ya Akukweti na sasa ni mbunge. Amerudi na anaataka tena. Sina haja sana na mwanamama ambaye amejitokeza wala huyu kijana Elias Mnyeti.

Kwa zama hizi nadhani UVCCM ilipaswa kutangaza kabisa kuwa iko upande wa Mnyeti. Hili lilitakiwa kufanywa wazi na kutangaza kuwa haitatoa mchango wa wagombea ambao wametawala vya kutosha. Najua hili haliwezi kufanyika lakini hata kisirisiri tu.

Hkuna haja ya kukubaliana na wagombea wanaogeuza ofisi za serikali kuwa sawa na taasisi zao. Utakumbuka Waziri Mkuu aliyemaliza muda wake, Fredirick Sumaye aliwahi kutangaza wakati ule alimuachia jimbo mtu wake wa karibu, Marry Nagu tena katika kipindi kigumu baada ya kudondoshwa katika kuwania urais.

Kauli za Sumaye ziliwagusa pia akina Msekwa, ziliwagusa mawaziri wa serikali ya Mkapa ambao sasa wanabipu simu ya Kikwete kutafuta kuitwa tena kikosini. Ziliwagusa wengi wanaoamini madaraka ya umma ni ajira zaoi za maisha.

Huenda watanzania haawajui madaraka ya spika. Spika ni moja ya vyeo vinne vikubwa katika Tanzania. Kinaweza kuwa cha tatu au cha nne. Katika nchi yenye mgawanyo huru wa madaraka cheo hiki nadhani ni cha pili kutoka kwa Rais kufuatia madaraka ya Makamu wa Rais kubakia kama picha isiyo nakazi maalum hadi Rais asiwepo.

Msekwa amekalia kiti hicho kitambo, ameyaona matamu na hataki kung'atuka. Anasubiri aibu ya kushindwa na kwa kuwa ameshajua kuwa ni miongoni mwa vigogo vya CCM anaamini kuwa atapitishwa, na tena bunge kwa kuwa ni la CCM pekee atatangazwa mshindi kisha atatuambia akina mimi tunaoandika makala hizi tuache wivu wa kike?

Siku hizi nimekuwa muumini mzuri wa ahadi za TANU. Ni katika ahadi hizo nakumbuka hii ya kusema kweli daima na kuweka kando fitina. Msekwa anapaswa kuishi kauli zake, anatakiwa kuambiwa na watanzania wamseme...maana si yeye tu mwenye uwezo.

Wazee wasiojenga tabia ya kuamini kuwa kuna watoto wao wanaweza kutunza familia kama wao wanapata taabu sana katika siku za maisha yao. Msekwa anaweza kuwa katika kundi hili, yeye anaamini kuwa Uspika ni Msekwa na Msekwa ni Spika milele. Nadhani wakati muwali sasa akumbuke kuwa madaraka ya umma ni mali ya umma na aukishapewa kumbuka kuwa ni haki ya wengine nao kucheza karata zao ili apatikane manju bora ngoma iweze chezwa usiku kucha. Wasalaam Msekwa...jaribu karata yako!
 
© boniphace Tarehe 12/24/2005 05:58:00 PM | Permalink |


Comments: 6


 • Tarehe 12/26/2005 11:02 PM, Mtoa Maoni: Blogger Fikrathabiti

  Mheshimiwa makene!
  Nimesoma makala yako nakupata hamasa ya kuirudia mara kadhaa hasa katika sababu anazotoa MSEKWA juu ya nia yake ya kugombea tena kiti hicho.

  Inasikitisha kuona mheshimiwa kama yeye anashindwa kua na tafsiri sahihi pale watu wanapoambiwa "TUTAKUMISS"!!!!!

  Mwaka 2000 wakati akitoa msimamo wake wa kutogombea tena kiti hicho wabunge kadhaa walisema kwa utani "MZEE TUTAKUMISS" kauli ambayo bwana mkubwa ameitafsiri kua ya yeye kuendelea kuhitajika!!!

  Jambo ambalo bwana Makene unapaswa kujiuliza ni kwamba inawezekana vipi katika makubaliano yaliyofikiwa miongoni mwao kutokee mgawanyiko kama si mpasuko wa watu wanaounga mkono sura zilizojitokeza kuwania kiti hicho.Angejitokeza vipi bwana Akukweti ambaye alikua naibu wake kuwania kiti hicho,Angerudije bwana Mamo katiko ulingo wa kukodolea macho kiti hicho,Jee huyu Mh. Sitta katokea wapi kama kulikua na makubaliano?

  Kaka makene hali inazidi kumwendea kombo babu yetu huyu kutokana na ule mtandao uliokua ukimpigia debe Kikwete kugawanyika na kutofautiana wazi wazi juu ya uamuzi wa msekwa na kauli yake inayotafsiriwa kama ni ya kujidhalilisha kwa kusema uongo.Nilicheka sana pale wiki iliyopita Babu msekwa alipoomba appointment na Rais kumuuliza kama yeye alikua na chaguo lake katika kinyang'anyiro hicho.KWELI MAJI YAMEMFIKA SHINGONI!!!!

   
 • Tarehe 12/27/2005 2:07 AM, Mtoa Maoni: Blogger Bwaya

  Mkuu Makene,
  Hongera kwa makala nzuri ya kwenye Mwananchi Jumapili. Umenikumbusha kisa fulani kilichotokea darsani kwetu mwaka 2004 nikiwa kidato cha 5. Kuna mwalimu moja Mmarekani (yeye anajiiita Volunteer) alikuwa akitufundisha Biology. Kila siku alikuwa haachi kuikuza nchi yake na tamaduni zake kwa kutulazimisha hata kusherehekea sikukuu ambazo hazina kichwa wala miguu. Mfano Halloween, ujinga fulani hivi. Kilichokuwa kinakera zaidi ni yeye kuonyesha dharau za wazi wazi kwa nchi yetu,kujaribu kutufanya tujidharau na kuwatukuza wao wenye pua ndefu.
  Ukweli ni kwamba aliopnyesha wazi wazi tabia za Wamerakani kujiona kuwa wao ndio bora kuliko viumbe wengine katika dunia hii. Nashukuru kwa sababu wapo Watanzania wengi hawakubaliani na kiburi cha watu hawa wanataka kututawala kwa kila kitu.
  Juzi Jumapili tukiwa kanisani, alikuwapo mmoja wao ambaye kwa hisia hizo hizo akataka kuingilia mipango ya kanisa pia kufuata utaratibu, waumini wakamsuta vibaya.
  Nadhani huu ni wakati wa kupambana nao, kuanzia hatua ya mmoja moja na hata taifa kwa ujumla. Wanachosha kwa kiburi chao wakati hawana lolote hawa.
  Nikupe pole kwa yaliyokupata katika safari yako.
  Uliniuliza nasoma wapi, Niko Education nataka kuwa Mwalimu fani ambayo hata hivyo haina umaarufu nchini. Lakini naamini ina mchnago mkubwa sana kwa maendeleo ya nchi hii, au unasemaje?
  Kuhusu Msekwa, usishangae ndio mtindo wetu.

   
 • Tarehe 12/27/2005 2:09 PM, Mtoa Maoni: Blogger Boniphace Makene

  Bwaya huyu unayezungumza naye katika Kasri yapaswa umite kwanza Mwalimu. Ni mwalimu wa kusomea na kuhitimu Chuo Kikuu Dar es Salaam. Ualimu sifa ndugu yangu, ni heshima ambayo wengi hawaipati lakini kama tutaudharau hesghima hiyo itapotea. Mwalimu Boniphace Makene ameweza kuwa hivin alivyo kutokana na yeye kubaini maarifa ya walimu. Sasa afunza na kusomesha pia. Usijali Bwaya haya ndiyo maisha na tunu ya ualimu.

  Materu nafurahi sasa umeamua kuwa unachangia na mijadala. Kuhusu neno langu sioni sababu ya kulipunguza maana hii ndiyo tofauti ya Blog na magazeti yanayosajiliwa pale Maelezo.

   
 • Tarehe 12/27/2005 10:25 PM, Mtoa Maoni: Blogger Fikrathabiti

  Heshima ifike kwako bwana CN!

  Imenibidi nichukue japo sekunde chache kukujulia hali wewe mwanaharakati uliye katika ardhi ya tanganyika na kukutia moyo katia kile unachosoma kwa sasa.

  Nashukuru pia kama ulitambua ualimu ni fani yenye mchango mkubwa sana kwa maendeleo ya nchi yeyote iwayo na mimi siamini kua haina umaarufu!!!!

  Vita iliyo mbele yetu ni kukomboa wadogo na ndugu zetu kifikra ili wawe chachu ya fikra chambuzi zinazojali maslahi ya bara letu hili.

  Nafasi uliyonayo kama mwalimu mtarajiwa naichukulia kama uwanja wa kuandaa wanamapambano wa kifikra.Nikipata fursa nitakuja mlimani tuongee na kujuana zaidi kwani kwasasa nipo zanzibar.

   
 • Tarehe 12/28/2005 4:47 AM, Mtoa Maoni: Blogger Ndesanjo Macha

  Makene, ningependa kusoma makala hiyo anayozungumzia Bwaya.

   
 • Tarehe 12/28/2005 9:07 AM, Mtoa Maoni: Blogger Boniphace Makene

  ndesanjo nikifanikiwa kupata makala hii haraka kwenye shubaka langu nitaibandika. Nikichelewa naomba niwie radhi maana visafari sasa vinazidi lakini fahamu kuwa kumbukumbu ya kuibandika inabaki palepale.

   
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved