Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Sunday, January 29, 2006
NINI VYANZO VYA AJALI TANZANIA?

Sarah Daudi Mfanyabiashara wa Dar es Salaam (Kulia) akiugulia kwa maumivu kufuatia ajali ya lori lenye namba za usajili T 181 AGT alilokuwa akisafiria kupinduka kulikotokana na tairi moja la upande wa kushoto kupasuka. Lori hilo lilikuwa likitoka Lushoto kuelekea Dar es Salaam mwishoni mwa wiki na ajali hii ilitokea eneo la Maili Tano. Dereva wa Lori hilo ambaye aliumia vibaya alitambuliwa kwa jina moja la Jang'andu. (Picha na Peter Mgongo). (Nimetafsiri hili kwa heshima ya wasomaji wangu wa Kiswahili)

NIMEKAA kipindi kirefu kuangalia vyanzo vya ajali Tanzania. Kwa taarifa yako ajali ni moja ya vyanzo vikubwa vya maafa katika Tanzania inayofatana kabisa na idadi ya wanaokufa kwa malaria na kisha magonjwa kama ukimwi hufuatia.

Katika kufikiri nikagundua haya, kukosekana sheria za kudhibiti leseni za kuendeshea magari, kutokaguliwa magari yanayoendeshwa, kutokuwa na sheria ya kubana unywaji pombe wakati na kabla ya kuendesha na pia kukithiri kwa rushwa katika makosa yanayoambatana na matumizi yasopasa ya barabara. Nchini Tanzania mtembea kwa miguu hana haki ya kutumia barabara na mwenye gari ni Mungu. Leseni za kuendesha utolewa kwa dakika tu bila kupima viwango vya dereva. Kutokana na hilo madereva wengi hawana uwezo wa kuepa ajali na hivyo kama hakutakuwa na mkakati wa kudhibiti leseni za madereva, kukagua magari yanayosafiri basi ajali zitazidi kuongezeka. Hoja hii imekuja baada ya kukuta picha hii katika gazeti la The Express linalohaririwa na rafiki yangu Fatma Bapumia.(Huyu nilisoma naye Chuo cha Uandishi wa Habari TSJ na kisha tukawa wote Chuo Kikuu Dar es Salaam)
 
© boniphace Tarehe 1/29/2006 11:27:00 AM | Permalink | Maoni 3
KUHUSU HATI YA MUUNGANO: MWANASHERIA ZANZIBAR AJICHANGANYA
KAMA ilivyo kawaida ya viongozi wa Tanzania kutokutunza kumbukumbu au kujifanya wako juu ya wengine, ndivyo inavyojionyesha katika habari hii. Hati za Muungano ziliwahi kutamkwa na Mwanasheria huyo kuwa hazipo katika ofisi yake lakini sasa anapoona mambo yanazidi kutanuka anaingia na hoja ya kisiasa isiyoendana kabisa na majukumu ya kazi yake ambayo kwa dhati hayausihani na kutetea upande wowote zaidi ya kutazama mhimili wa sheria. Kutunza matatizo si kuyatatua na kama Zanzibar wanadhani kuwa wakimya katika masuala ya Muungano ni kuunufaisha Muungano wanakosea. Masuala ya Muungano yana haki ya kujadiliwa na kuzungumzwa na yeyote maana athari za Muungano si za kundi moja.

Msimamamo wa Kasri la Mwanazuo katika hoja ya Muungano ni mmoja. Hati ziwekwe wazi na jamii ijadili. Kasri linahitaji kuona Muungano wa Afrika na kuwa taifa lakini linasisitiza juu ya hatua zote kufanyika kwa uwazi, kufutwa kwa hoja za siri na pia kuwepo tashwishi la kufikia maafikiano na Muungano ili waafrika waambae katika Bara lao bila mipaka. Kuungana kwa Afrika hakuna maana kuwa aina nyingine za kuungana kama kwa Tanganyika na Zanzibar kunyamazishwe bila kutafuta mbinu za kuunganisha za kisayansi kama alivyowahi kudokeza Fredrick Taylor.
 
© boniphace Tarehe 1/29/2006 11:01:00 AM | Permalink | Maoni 2
Thursday, January 26, 2006
GAZETI TANDO JIPYA LATANGAZA HATARI TANZANIA
Kama kulewa madaraka, sijui kutafuta namna za kulejesha fedha walizotumia kugawa rushwa ama nini sijui? Haya yametokea na yameanza mapema sana baada ya wanasiasa wa Tanzania katika kipindi hiki ambapo nchi inakabiliwa na janga la njaa, ujambazi ambao hasa unatokana na kutanuka kwa wigo wa walio nacho na wasio nacho, kupanuka kwa matumizi ya serikali n.k, basi kama haitoshi viongozi wapya wanatangaza kutaka kuongezewa mishahara na marupururupu kibao. Hii inatia huruma namna walivyo vipofu hawa, inatia hasira namna wasivyotambua wanaowawakilisha, inaumiza moyo kuna wamesahau sasa hivi tu au ni ulimbukeni kama nilivyowahi kubainisha kwa JEFF pale Toronto. Hivi gari la Milioni 50 na hoteli za kifahari na mavazi ya mbwembwe yanayotengenezwa Marekani na Uingereza ndio Ubunge?

Nisichafue radha ya kumkaribisha Ndugu Mustapha anayekuja kwa kali hiyo na Gazeti Tando lake liitwalo Hotspot. Karibu Mustapha nadhani utashangaa jamii hii inayomiliki Magazeti Tando ilivyo na ukarimu kwa namna itakavyopita kwako leo hii hii kukukaribisha.

Kwa taarifa tu, Blogu hii imefunguliwa na Mustapha jana usiku baada ya mazungumzo yangu na January John akiwa Illinois kwa simu huku yeye January akichati na Mustapha kupitia kisemeo cha Yahoo. Hii kasi inanipa faraja sana kisa cha kuweka kando mjadala wangu na Nyembo kama ulivyoongezwa pia na MKWINDA. Nitarejea kwa hawa baadaye.
 
© boniphace Tarehe 1/26/2006 08:20:00 AM | Permalink | Maoni 3
Tuesday, January 24, 2006
NYEMBO UMEWASHA MOTO
NATUNGA shairi hili kama jadi baada ya NYEMBO ama HUD HUD kunijibu kwa shairi hili katika Gazeti Tando lake. Mjadala huu haujaisha na hautamalizika mapema licha ya shujaa MKWINDA kutangaza kuukimbia huku akiahidi kujiingiza kwa machale. Simuamini Mkwinda asemayo maana ushairi ni sawa na ramli au uchawi fulani. Huweza kumuamsha aliyelala na akaghani tungo bila ridhaa yake. Hiki ndicho kitokeacho sasa maana licha ya majukumu mengine ukikuta tungo zinakujibu unaamua kuingia vitani. Sasa pata tungo hii hapa chini kisha kama jadi changia mawazo yako.

Hudi ya Moshi mabasi, abiria kubebea
Yanitia wasiwasi, malenga kujiitia
Jina hili la ukwasi, uzunguni latokea?
La kwangu liwapi jina, Nyembo hujalijulia?

Nilisema tangu zama, Nakuzerwa itikia
Nilirithi ujima, ngano zangu tangazia
Limenipa kusimama, na mengi kuyafanyia
Hizo ndaro punguzia, nijue navyoitiwa!

Mbingu ilishangilia, na jua likachekea
Nakuzerwa kizaliwa, kando ya ziwa sikia
Dhoruba ikatokea, bila wavuvi ulia
Kulikuwa kuzaliwa, kwa malenga Nakuzerwa!

Kaishi kwa mbili saa, kisha neno kasemea
Ukumbi watu kajaa, Malenga kumsikia
Karatasi kaiomba, na kalamu andikia
Utungo akaugani, mwaka mwema tangazia.

Wazee wakakimbia, tohara kumfanyia
Wakakutwa na udhia, kwa jambo waloonea
Kisu akawaombea, kisha yeye jikatia
Damu iliyotokea, ikapelekwa jangwani.

Sikia kilotokea, jangwani ipomwagiwa
Mafuta yakachimbiwa, Arabuni shangilia
Na tende zikaotea, Islamu shangilia
Ngamia wakafikia, maji yake kujinywea.

Karne ilitokea, Fumo bado kuzaliwa
Inkshafi bado tajwa, Mwanakupona sawia
Saadan nakwambia, ni mwana bado zaliwa
Sasa huyu ndugu Nyembo, pawapi angetokea?

Tafaruku likazuka, shairi badilishia
Akaitwa mtukuka, maamuzi kufikia
Mizani na vyao vina, kundi moja kashikia
Na wengine kawambia, mapingiti kutungia.

Nyembo wapaswa sikia, kilio utajutia
Wa nchi kavu malenga, majini hupotelea
Huwezi mkondo fata, Mkwinda kesha kimbia
Katu sumu simezani, malengani kufiliya.

Musoma amekulia, Bukoba akasomeya
Dar akitembeleya, Ndanda ghani kutungiya
Mkwawa kamjuliya, Na Songea mwamkua
Kisha Mlimani kenda, kutaka kudurusia.

Huyu ndiye Nakuzerwa, malenga aso udhia
Kwa Bush anandikiya, shetani kufukuziya
Blogu kafunguliya, umma upate someya
Kisha rudi kwao piya, jamii badilishiya.

Sikamilishi nasema, hapa naendelezea
Njoo Nyembo nakwambiya, ubazazi kushikiya
Kigoli kakungojeya, kule kwenda mkunjiya
Halafu ujite malenga, kwa fani usojulia?
 
© boniphace Tarehe 1/24/2006 12:20:00 PM | Permalink | Maoni 1
Sunday, January 22, 2006
UCHUNGU KATIKA NCHI YANGU!!!


Good Samaritans trying to rush to hospital a pedestrian who was shot by four robbers suspected to be involved in a robbery that occurred at Eljabri Jewelers shop at Mkunguni/Livingston Streets, Kariakoo, Dar es Salaam on Saturday. Tsh. 300,000, a gun and other property were stolen. Although the bandits were reported killed by the police on the same evening, there is confused information about whether the killed persons were robbers or not . (Photo by Peter Mgongo).
 
© boniphace Tarehe 1/22/2006 01:56:00 PM | Permalink | Maoni 7
HATUIJENGI AFRIKA KWA FIKRA HIZI????
HIZI ni fikra zangu, zimekuwa na kushamiri zaidi tangu nimeishi ughaibuni. Niliweza fikiri chini ya mipaka zamani lakini sasa hapana! Kila ninapoulizwa wapi natoka jibu langu awali lilikuwa Tanzania. Kila nilipogundua kuwa hili si jibu sahihi huku ughaibuni nikabadilika, nikaanza kutangaza kutokea Afrika. Kila nitajapo jina hilo siulizwi wapi inapatikana! Maswali yanayofuata si mada yangu hapa leo.

Najivuna sana sasa kwa kuwa Mwafrika, nafarijika zaidi kwa kuwa natoka huko na maisha yangu yatakuwa huko na siku nikifa nipumzisheni huko. Kila ninapokutana na taarifa za machafuko kati ya Mwafrika na mwafrika naumia, naweweseka naugua moyoni. Kila nisikiapo mipango ya kuwatenga waafrika katika Afrika nauliza hawa wana maana gani? Je ni kukosa kutambua mipaka ya bara hili, ni kutofahamu tunavyounganishwa kila tuwapo nje ya bara hili? Kwa nini mipaka katika Afrika wakati mataifa makubwa yanafungua milango yao ili kutukandamiza na kutunyonya? Kwani Kenya kuwa na wasomi wengi ni kosa? Nigeria kuwa na idadi kubwa ya watu na wasomi pia ni dhambi? Je kuna haja ya kutimuana katika Afrika katika misingi ya kazi, elimu na masuala mengine? Hivi hizi suluba wanazozipata waafrika huku ughaibuni watasuuzika roho zao wapi kama si Afrika! Hivi nani ametuloga, nini maana ya Mungu ibariki Afrika? Mnasema tu hamtendi sio? Naandika maandishi haya kwa uchungu. Machozi yanaweza nitoka hapa lakini sitaki kisima hiki kitazamwe na hawa walionizunguka maana wote weupe. Hawa wanyonyaji wetu na wana sera zinazofanana! Si wote lakini wachache wao wenye nafasi za kiuchuimi na madaeraka hawatupendi kabisa. Wangetamani tuwe vipofu watunywese sumu! Hawatuthamini kabisa ...lakini sasa kwa nini na sisi twabaguana hivi? Hivi Watanzania mmekatazwa kwenda mataifa mengine? Kwanbi mlipokuwa mnanyimana Pasipoti ili mbakie nchini kwenu ndiyo tabu ya ninyi kuishi na wenzenu toka Afrika? Mtanisaidia mlio ughaibuni...siamini katika mipaka aliyoipanga Bismarck kichaa wa Ujerumani aliyekutana na wakora wenzake pale Berlin mwaka 1884-1885.

Hao vichaa wakatenga mipaka katika bara lisilo lao. Sasa tunashupalia mipaka hii na kuumizana wenyewe kwa wenyewe. Kweli tunaweza kuungana na kuwa na Afrika Mashariki kama hali ni hii ya kupandikiza chuki. Misingi ya maandishi yangu ni habari hii kutoka katika gazeti la Chama tawala Tanzania CCM AMBALO LIMEANDIKA HABARI HII.
 
© boniphace Tarehe 1/22/2006 11:56:00 AM | Permalink | Maoni 1
Thursday, January 19, 2006
BLOGU YA FDC

NIMEPITA na kuangukia blogu ya FDC. Hiki ni chama cha siasa Uganda ambapo mgombea wake Urais Kiiza Besigye amekuwa hasimu mkubwa wa Mfalme Yoweri Museveni hadi akatiwa katika hatihati za kusotea segerea. Waweza isoma hapa na kutoa maoni ya vyama vya siasa na wanasiasa wa Tanzania kufungua blogu zao na kuweka maandishi. CHADEMA ni moja ya vyama Tanzania ambacho viongozi wake wana blogu lakini wote hawajawahi kuweka maandishi humo.
 
© boniphace Tarehe 1/19/2006 03:47:00 PM | Permalink | Maoni 1
MIFUKO YA PLASTIKI TANZANIA ITAIGA LINI RWANDA?
KATIKA vitu vinavyochangia uharibifu wa mazingira ni mifuko ya Plastiki. Mifuko hii licha ya madhara yake kwa binadamu imekuwa ikipingwa vita ya chini chini hapo Tanzania. Hakuna jitihada za dhati za kuiondosha. Sasa hivi tunapokumbwa na ukame na majanga kama njaa tunashindwa kukumbuka kuwa ardhi inapofunikwa na mifuko ya plastiki pia huathiri uoto wake. Soma hapa kuona harakati za Rwanda katika kupambana na mifuko hiyo huko.
 
© boniphace Tarehe 1/19/2006 12:52:00 PM | Permalink | Maoni 3
Tuesday, January 17, 2006
NYEMBO KWANI WAITWANI?
KUMEIBUKA mwezi wa ushairi katika Blogu za Kiswahili. Alianza Mkwinda, malenga mkongwe kutoka Pwani ambaye amekuja kuwa tishio katika wanablogu wanaogani tungo za mashairi. Katika pita pita akatokeza MWANDANI naye akaimba hivi. Kama haitoshi Malenga mwingine akazaliwa Zanzibar. Huyu ni MATERU. Mjadala wa MKWINDA ukamkuna NYEMBO, akajibu nami nikachangia kidogo. Sasa NYEMBO kapaa kabisa na utungo katika Blogu yake.
Miongoni wa wanaotajwa na NYEMBO katika majigambo haya ya kishairi tunayotaka yachukue sura mpya katika Blogu ni mimi. Sasa natangaza nami kuingia katika majibizano haya ya kishairi na watani wangu hawa nikianza na NYEMBO. Kumbuka hii si nafasi ya kumfanya HARAKATI asahaulike kwa kuwa aliahidi kukariri shairi moja kwa wiki ahadi ambayo haikutimizwa. Pata sasa shairi hili hapa chini.

Nyembo wewe waitwani, hadi uje malengani
Ni wapi unakeshani, tungo zako karirini
Nani amekunyweshani, sumu tamu mezeani
Waweza huu mchezo, ama waja taniani?

Katu sumu simezani, kitumbua situpani
Siki kwangu asalini, utungo jifunikani
Naweza tupa mpini, kisha jembe limiani
Nambie Malenga Nyembo,waitwani shairini?

Diwani ya Nakuzerwa, itatoka si utani
Hodo hodi ni muswada, DAMBAYA kishirikini
Ewe Malenga Mkwinda, huyu Nyembo atokapi?
Kama naye malengani, jinale anaitwani?

Nahisi kaja kwa tambo, wakongwe kuwatishani
Ushairi ni ulimbo, weledi unaletani
Hauji kama mkumbo, kukukuta ukubwani
Nikali mama tumboni, shairi nililighani!

Tungo tungile zamani, sasa kazi someshani
Mama alinambiani, nilivyoghani tumboni
Huzuni kimtokani, siku hizo kumbukani
Kanileta duniani, njia nachia tambaa.

Nyembo toa masharubu, kama wataka tungani
Utajageuka bubu, ulingoni kimbiani
Tambua huu weajibu, mahoka waulizani
Kama wadhani mchezo, uliza upotokani!

Mwandani nawe changia, uvamizi uwanjani
Beti waweza pangia, Mshairi kuitwani?
Hoja waweza pangia, kisha ngoma alikwani?
Mshairi mtu gani, hoja hii fafanua!

Natoka sasa wagenzi, hoja nimeanikani
Tungo zachie wapenzi, walale wakiliani
Ghani wache wakufunzi, walale wasibaini
Kisha Nyembo rudi tena, kama waweza tungani.
 
© boniphace Tarehe 1/17/2006 03:25:00 PM | Permalink | Maoni 4
NGOMA MTINDO MMOJA, BLOGU NYINGINE TENA!
KAMA nilivyowahi kubaninisha mazungumzo yangu na JEFF pale Toronto wito mmoja ulikuwa kushawishi tunaowafahamu wafungue blogu zao. Kazi hiyo inafanyika kwa kasi sana na matunda yake ni haya...blogu ya IBRAHIM BWIRE ikitokea hapo Bulyanghulu inakuwa ya kwanza kutoka katika anga za migodi ya Tanzania iliyobinafsishwa. Huyu jamaa mwanafikra sana na kama unabisha mtembelee sasa umuone na kumkaribisha. Kwani uongo tazama sasa NURU AKILINI.
 
© boniphace Tarehe 1/17/2006 08:55:00 AM | Permalink | Maoni 0
Thursday, January 12, 2006
HAMKANI SAFARI YAENDELEA KWA KASI, MBUROGU MPYA HIYOOO!
NATUMIA jina Mburogu kutoka kwa mtani wangu mmoja wa Kenya lakini haina maana kuwa nimelihalalisha! Lakini sasa ile kasi ya kuongeza Watanzania katika teknolojia hii inazidi kuchukua picha na hapa ninamtangaza kwenu NDYEMALILA anayeblogu toka Arusha. Mtembeleeni kama ilivyo ada na kumsabahi. Wakati ninapomtangaza huyu nazidi kutoa rai ya waheshimiwa wanablogu kuongeza jitihada ya kusaka wavunaji maana wasomaji ni wengi lakini wanablogu ni wachache.
 
© boniphace Tarehe 1/12/2006 07:28:00 AM | Permalink | Maoni 1
Wednesday, January 11, 2006
RIPOTI YA MWEZI YA MBUROGU ZA KISWAHILI

Rabuka Mola jalia, mwanao kuamkani
Shairi pate tungia, Bloguni somekani
Ahadi nilitolea, hima vema timizani
Ripoti kuandikia, ya mwezi uloishani.

Kazi tulojipatia, njema wewe wasifuni
Watu tunawafunzia, maarifa ongezani
Pamoja twakatalia, maovu kufanyikani
Mola Baba angazia, taifa la bloguni.

Mwezi ulioishia, chache zilianzishwani
MAISHA TAFAKARIA, Musoma ikatokani
KURUNZI kamulikia, kutokea mabondeni
Alabama kasikia, Sauti BARAGUMUNI.

Wito sijasahulia, weledi jitambueni
Tafakari nafanyia, Blogu Kiswahilini
Hoja mlizotolea, ndizo naunganishani
Kisha wote kuonea, kile mchokifanyani.

Pale nilipoishia, Kanada nikaendani
Harakati kakutia, Toronto kusalimuni
Ilikuwa yavutia, gwiji huyu muonani
Ndesanjo kakumbukia, simu kutupigiani.

Sasa wazi naanzia, wote sasa tuliani
KASRI niliishia, siasa shabikiani
MATERU bila julia, naye moto kawashani
Ukweli katupashia, Zanzibar iko motoni.

Hoja ya kuweka picha, JIKOMBOE katoani
Riwaya kushikilia, HARAKATI jikitani
BWAYA yeye katania, nani anayesomani
Majibu akapatia, hoja yake ifutani.

Hotuba ilo sawia, igizo jipya nchini
Blogu zikasemea, lazima kuitunzani
MARK kaitafutia, JEFF kaitundikani
Lengo kuja tazamia, Kikweto alofanyani!

DAMIJA kaendelea, Blogu jina pewani
Wasifu kiandikia, lini wangu tatoani
MWANDANI alopotea, kaleta hoja razini
Katwambia kumbukia, nyumbani bora nchini!

Huko Dodoma nalia, sijui chawakinzani
MIRUKO alikimbia, Polisi tukasemani
MARTHA naye kaamua, kwa mwezi kuja mojani
Simanzi kanachilia, kushindwa kumsomani.

Hawa sasa nasemea, kweli wamekimbiani
FATMA mwanasheria, London kajifichani
NGURUMO wa Tanzania, kajificha gazetini
Kila anapotokea, semina kitangazani!

KAKA PORI
katokea, tathimini angazani
Teknojia yakua, hata huko maporini
Sasa anaandikia, na picha kisha wekani
NYEMBO kamkumbushia, ya Kikwete kuhojini.

Bibie CHEMI nasema, hongera mama semani
Urembo wanafanyia, wanitia walakini
MOTOWAKA nakwambia, picha yako iwekeni
Maana utajulia, KESSY ukimuonani.

Ewe MKWINDA julia, kaziyo twaheshimuni
Tazama wageuzia, wengi ngano kutungani
MKINA mpe gunia, arejeee duniani
PAMBAZUKO tambulia, wajibu kuandikani.

ZAINABU na BAKANJA, hawa ni wa msimuni
BITIDAFFA wa Dodoma, naye amejiungani
KAZONTA anafatia, mgomo kuendeshani
Watwacha kwenye udhia, sisi kutowasomani!

Mwisho wake BANGAIZA, mimi sijaufikani
TERRIE wewe nakwambia, subiri nakufatani
KIVALE namuonea, kimya kakumbatiani
Naomba jibu patiwa, yupi hawa amshani?

Hoja uliyotolea, MSANGI toka nyandani
Hima wazi jadilia, kwani ina utatani
Tumeshaanza onea, madaraka jipeani
Huu utata anzia, wa wanamtandaoni.

MICHUZI sijachelea, picha zako kusifuni
Bongo unaangazia, ughaibuni onani
Nasi sasa twaigia, bila woga anikani
Kumbuka wito natoa, kwa wengine kupitani.

Umoja wetu jalia, twapaswa kuukuzani
Nguvu tukizingatia, wengi itawawashani
Kumbuka ni yetu nia, mpya nyingi funguani
Macho wakishafumbua, Tanzania tachekani.

GAPHIZ unosomea, nawe nakukumbukani
Mwaka mpya kutokea, Heri ukatupeani
Nami sasa nasemea, kazi njema tufanyeni
Vitabu tukifunua, hazina tutapatani.

Kaditama naishia, Texas kuishini
Wito niliutolea, Mellisa kikubalini
Kwangu amenitokea, fikira kufufuani
Simba naweza vamia, bila woga nipatani.
 
© boniphace Tarehe 1/11/2006 11:32:00 AM | Permalink | Maoni 7
Tuesday, January 10, 2006
HERI YA MWAKA MPYA NDESANJO

PICHA hii ni zawadi kwa Ndesanjo. Hapo ni katika Basi kutoka Ottawa kwenda Toronto.
 
© boniphace Tarehe 1/10/2006 01:13:00 PM | Permalink | Maoni 2
MTAA NA MNARA MREFU KULIKO YOTE !


MTAA wa Yonge ndio mrefu kuliko yote duniani na pia Mnara wa CN ndio unaoshika chati ya urefu duniani. Maajabu haya muhimu hupatikana Toronto kama picha zionyeshavyo hapo chini.
 
© boniphace Tarehe 1/10/2006 01:08:00 PM | Permalink | Maoni 0
MREMA YUKO WAPI?

Tunapoamua kuunda wizara sasa ya kushughulikia usalama wa Raia kwani Tanzania iko vitani sasa? Tunaogopa nini kutazama Historia na je kwani Mrema amekufa hadi tuogope kumrejeshea madaraka kama tunaona tumeshindwa kupambana na uhalifu?

Sherehe ya Boxing Day jijini Toronto iliendana na vijana wakora kurushiana risasi na kisha moja ya risasi hizo kumdhuru mpita njia aliyekuwa binti mbichi kabisa...inauma sana Michuzi! Picha hiyo inaonyesha eneo tukio hilo la kinyama lilipotokea. Nilichopendezwa nacho ni moyo wa kuthamini utu ambapo jamii nzima inajitokeza kutoa pole na kuweka mashada ya maua kwenye eneo la tukio. Nchini Tanzania ili upate heshima na huruma ya jamii ni pale unapokuwa kigogo au mtoto wa kigogo lakini jamii ya kawaida maskini wakifa hata kama ni kutokana na ujambazi husindikizwa na ndugu zao na serikali kubaki kimya.
 
© boniphace Tarehe 1/10/2006 01:02:00 PM | Permalink | Maoni 0
BUNGE LA KANADA



HILI ni Bunge la Kanada, kama ilivyo Kongres ya Marekani kuingia humo hakuna masharti magumu kama ilivyo kuingia ikulu na Bunge la Tanzania. Jumba hili liko Ottawa.
 
© boniphace Tarehe 1/10/2006 12:16:00 PM | Permalink | Maoni 0
MWENGE WA KANADA


HAPA mi sehemu ya kuingia katika Bunge la Kanada na huo ni mwenge wao unaowaka licha ya kuwa kuna barafu. Sijui kama elimu hii Mwalimu Nyerere aliipata hapa na kuamua kuweka Mwenge unakaa mlima Kilimanjaro mlima pekee wenye barafu.
 
© boniphace Tarehe 1/10/2006 12:10:00 PM | Permalink | Maoni 0
Sunday, January 08, 2006
FIKRA ZILIZOZAA BARAGUMU!

HAPA ni Baltmore, Maryland anaonekana Mwaipopo John Mkazi wa Baragumuni baada ya kuishiwa kauli juu ya kuanzisha Blogu mpya. Pembeni yake ni Kasrilamwanazuo na mjadala huo ulifanikiwa baada ya miezi miwili baada ya Mwaipopo kufungua Blogu yake akiwa Alabama.
 
© boniphace Tarehe 1/08/2006 01:10:00 PM | Permalink | Maoni 2
Wednesday, January 04, 2006
BARAZA LA KIKWETE
BARAZA LA MAWAZIRI

A. MAWAZIRI

OFISI YA RAIS

Waziri wa Nchi – Menejimenti ya Utumishi wa Umma
1. Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia (Mb)
Wizara ya Nchi – Utawala Bora
2. Mheshimiwa Philip Sang’ka Marmo (Mb)
Wizara ya Nchi – Siasa na Uhusiano wa Jamii
3. Mheshimiwa Kingunge Ngombale Mwiru (Mb)

OFISI YA MAKAMU WA RAIS

Waziri wa Nchi – Muungano
4. Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi (Mb)
Wizara ya Nchi – Mazingira
5. Mheshimiwa Prof. Mark James
Mwandosya (Mb)

OFISI YA WAZIRI MKUU

Waziri wa Nchi – Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa
6. Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda
(Mb)
Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge)
7. Mheshimiwa Juma Jamaldin Akukweti
(Mb)

WIZARA ZINAZOJITEGEMEA

Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
8. Mheshimiwa Dkt. Asha-Rose Mtengeti Migiro (Mb)
Ushirikiano wa Afrika Mashariki
9. Mheshimiwa Andrew John Chenge (Mb)
Fedha
10. Mheshimiwa Zakia Hamdani Meghji (Mb)
Mipango, Uchumi na Uwezeshaji
11. Mheshimiwa Dkt. Juma Alifa Ngasongwa (Mb)
Viwanda, Biashara na Masoko
12. Mheshimiwa Nazir Mustafa Karamagi (Mb)

Kilimo, Chakula na Ushirika
13. Mheshimiwa Joseph James Mungai (Mb)
Maliasili na Utalii
14. Mheshimiwa Anthony Mwandu Diallo (Mb)
Maji
15. Mheshimiwa Stephen Masatu Wassira (Mb)
Nishati na Madini
16. Mheshimiwa Dkt. Ibrahim Said Msabaha (Mb)
Miundombinu
17. Mheshimiwa Basil Pesambili Mramba (Mb)
Afya na Ustawi na Jamii
18. Mheshimiwa Prof. David Homeli Mwakyusa
(Mb)
Elimu na Mafunzo ya Ufundi
19. Mheshimiwa Margareth Simwanza Sitta (Mb)
Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia
20. Mheshimiwa Prof. Peter Mahmoud Msolla
(Mb)
Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana
21. Mheshimiwa Prof. Jumanne Abdallah
Maghembe (Mb)
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
22. Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli
(Mb)
Habari, Utamaduni na Michezo
23. Mheshimiwa Muhammed Seif Khatib (Mb)
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
24. Mheshimiwa Prof. Juma
Athumani Kapuya (Mb)
Usalama wa Raia
25. Mheshimiwa Harith Bakari Mwapachu
(Mb)
Mambo ya Ndani
26.Mheshimiwa Capt. John Zefania Chiligati (Mb)
Katiba na Sheria
27. Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu (Mb)
Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto
28. Mheshimiwa Sofia Mnyambi Simba (Mb)
Maendeleo ya Mifugo
29. Mheshimiwa Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa (Mb)

B. NAIBU MAWAZIRI

OFISI YA WAZIRI MKUU
Maafa na Kampeni Dhidi ya Ukimwi
30. Mheshimiwa Dkt. Luka Jelas Siyame (Mb)
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
31. Mheshimiwa Celina Ompeshi Kombani (Mb)
WIZARA ZINAZOJITEGEMEA
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
32. Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi (Mb)
33. Mheshimiwa Dkt. Cyril August Chami (Mb)
Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki
34. Mheshimiwa Dr. Diodorus Buberwa Kamala (Mb)
Fedha
35. Mheshimiwa Abdisalaam Issa Khatib (Mb)
36. Mheshimiwa Mustafa Haidi Mkulo (Mb)
Mipango, Uchumi na Uwezeshaji
37. Mheshimiwa Salome Joseph Mbatia (Mb)
Viwanda, Biashara na Masoko
38. Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David (Mb)
Kilimo, Chakula na Ushirika
39. Mheshimiwa Christopher Kajoro Chizza (Mb)
40. Mheshimiwa Hezekiah Ndahani Chibulunje (Mb)
Nishati na Madini
41. Mheshimiwa Lawrence Kego Masha (Mb)
Miundombinu
42. Mheshimiwa Dkt. Maua Abeid Daftari (Mb)
43. Mheshimiwa Dkt. Milton Makongoro Mahanga (Mb)
Maji
44. Mheshimiwa Shamsa Selengia Mwangunga (Mb)
Afya na Ustawi wa Jamii
45. Mheshimiwa Dkt. Aisha Omar Kigoda (Mb)
Elimu na Mafunzo ya Ufundi
46. Mheshimiwa Mwantumu Bakari Mahiza (Mb)
47. Mheshimiwa Ludovick John Mwananzila (Mb)
Elimu ya Juu, Sayansi na Tekinolojia
48. Mheshimiwa Gaudensia Mugosi Kabaka (Mb)
Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana
Vijana na Kazi
49. Mheshimiwa Jeremia Solomon Sumari (Mb)
Ajira
50. Mheshimiwa Daniel Nicodem Nsanzungwako (Mb)
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
51. Mheshimiwa Rita Louise Mlaki (Mb)
Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto
52. Mheshimiwa Dkt. Batilda Salha Burian (Mb)
Usalama wa Raia
53. Mheshimiwa Mohamed Aboud (Mb)
Mambo ya Ndani
54. Mheshimiwa Bernard Kamillius Membe (Mb)
Maendeleo ya Mifugo
55. Mheshimiwa Dkt. Charles Ogessa Mlingwa (Mb)1
Maliasili na Utalii
56. Mheshimiwa Zabein Muhaji Mhita (Mb)
Habari, Utamaduni na Michezo
Habari na Utamaduni
57. Mheshimiwa Dkt. Emmanuel John Nchimbi (Mb)
Michezo
58. Mheshimiwa Joel Nkaya Bendera (Mb)
Sheria na Mambo ya Katiba
59. Mheshimiwa Mathias Meinrad Chikawe (Mb)
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
60. Mheshimiwa Omar Yussuf Mzee (Mb)

IKULU, DAR ES SALAAM
4 Januari, 2006
 
© boniphace Tarehe 1/04/2006 07:23:00 AM | Permalink | Maoni 3
Tuesday, January 03, 2006
WANDUNGU NIMEMLETA WAZIRI MKUU MUMTAZAME


MOJA ya matukio nitakayoyakumbuka katuka kuumaliza mwaka na kuanmza huu ni kukutana na mheshimiwa Jeff Msangi na kulishana fikra. Makutano yetu yalianza hivyo na mengi nimeanza kuyaandika na kuyatuma nyumbani ili wasomaji wa huko wanufaike pia. Kumuona Jeff si faraja katika kizazi cha Blogu za Tanzania bali mwamko mpya wa safari kali ya kukuza na kuujengea heshima uwanja huu. Nadhani mwaweza hapo Bongo Miruko kumtembelea Michuzi ama Materu. Kutoka Texas hadi Toronto si mchezo lakini inawezekana kama tutatambua kuwa umoja huu ni sawa na ule tuliozoea wa watuma salamu katika redio na magazeti
 
© boniphace Tarehe 1/03/2006 07:22:00 PM | Permalink | Maoni 7
ZIARA YA CANADA KATIKA PICHA


Hiyo ni Zanzibar kama mnavyoona, wakazi wa Tanzania mtanisamehe maana sitafafanua kazi inayofanyika huko ndani lakikni nimechukua picha hii kuwaonyesha kuwa Zanzibar nayo si hapa hapo Toronto.
 
© boniphace Tarehe 1/03/2006 07:17:00 PM | Permalink | Maoni 2
Sunday, January 01, 2006
MWAKA MPYA 2006, POLENI KWA KUONGEZA MAJUKUMU MAPYA!
POLENI kwa kumudu kuongeza majukumu ya mwaka huu 2006. Kila MWANAZUO hutambua kuwa mwaka mpya uanzapo yeye huwa na jukumu linalofanana na serikali za duniani yaani kulipa kodi. Katika nchi ya KASRI ambapo chakula cha wakazi wake ni FIKRA upo wajibu uliowekwa na Jamhuri hii kuwabainishia Wanazuo wote mbinu muwali za kujaza fikra hizo ili isitokee mbele ya safari Wanazuo wakaishiwa chakula chao bora.

Mwaka huu kunaonekana kuongezeka kwa kasi Wakazi wa nchi mbalimbali wanaohamia nchi ya KASRI baada ya kubaini kuwa maslahi ya nchi hii pamoja na hali yake ya maisha haifanani kabisa nanchi zilizopata kuwepo katika sura ya dunia. Hawa utakutana nao wakionyesha kiu ya kula fikra kwani walizikosa siku nyingi na wanahitaji tani nyingi za fikra hizo kwa mwaka huu ulioanza jana.

Kutokana na jamii ya Wanakasri kugundua hilo wametangaza jukumu rasmi la kila mkazi kusoma kitabu kimoja kila baada ya miezi mitatu. Viongozi katika Kasri watakuwa na jukumu zaidi la kusoma kitabu kimoja kila mwezi ili kuchangia nguvu zao kuwalisha wageni wanaohamia hapa.
Nchi nyingi duniani na hasa Bara la Afrika limekabiliwa na ugonjwa wa Kutosoma na tiba ya ugonjwa huu imekuwa haipatikani huko zaidi ya nchi ya Kasri. Kutokana na hali hii kila mmoja amejiwekea nafasi ya kuongeza juzuu na maarifa zaidi ili tiba za wananchi wa dunia hiyo iweze kupatikana na ikiwezekana kuwafikia huko waliko.

Si malengo ya Jamhuri hii kutangaza mema yanayoizunguka nchi yetu bali kuonyesha umuhimu wa kuchangia rasilimali zetu kusaidia kuondoa upofu wa fikra katika nchi nyingine. Jukumu hili hufanywa kwa upole na unyenyekevu maana wananchi wa nchi hizo wamegeuka dhoofu kufuatia vitisho na suluba zilizowakabili katika miongo mingi. Hapa zuoni huwezi kwenda kwa ari mpya, kasi na hata nguvu! Wananchi watakuuliza ulikuwa wapi siku zote au huko nyuma hukuona njia?

Kinachonifurahisha ni haya maisha ya Wanakasri, walitazama mapema sana wakaishi katika kuwekeana mitego ya fikra, hawa ukiwauliza twaweza kupata wapi maji ya kunywa...watakujibu chukua miti mitano panda pale kweye kilima kisha shuka bondeni na kata lako unywe maji! Ukiwauliza wanapata wapi fikra za kutosha kulisha umati mkubwa unaoongezeka bila kuyumba watakwambia chagua kupenda kuishi au kufa!

Nakukaribisheni sana katika kampeni hii ya wana Kasri. Mwaka huu unatakiwa kuongeza jukumu hili ambalo KASRI limetangaza kuwa kauli mbiu ya mwaka 2006. Poleni sana kwa kuongeza majukumu mapya.
 
© boniphace Tarehe 1/01/2006 09:26:00 AM | Permalink | Maoni 1
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved