Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Sunday, January 01, 2006
MWAKA MPYA 2006, POLENI KWA KUONGEZA MAJUKUMU MAPYA!
POLENI kwa kumudu kuongeza majukumu ya mwaka huu 2006. Kila MWANAZUO hutambua kuwa mwaka mpya uanzapo yeye huwa na jukumu linalofanana na serikali za duniani yaani kulipa kodi. Katika nchi ya KASRI ambapo chakula cha wakazi wake ni FIKRA upo wajibu uliowekwa na Jamhuri hii kuwabainishia Wanazuo wote mbinu muwali za kujaza fikra hizo ili isitokee mbele ya safari Wanazuo wakaishiwa chakula chao bora.

Mwaka huu kunaonekana kuongezeka kwa kasi Wakazi wa nchi mbalimbali wanaohamia nchi ya KASRI baada ya kubaini kuwa maslahi ya nchi hii pamoja na hali yake ya maisha haifanani kabisa nanchi zilizopata kuwepo katika sura ya dunia. Hawa utakutana nao wakionyesha kiu ya kula fikra kwani walizikosa siku nyingi na wanahitaji tani nyingi za fikra hizo kwa mwaka huu ulioanza jana.

Kutokana na jamii ya Wanakasri kugundua hilo wametangaza jukumu rasmi la kila mkazi kusoma kitabu kimoja kila baada ya miezi mitatu. Viongozi katika Kasri watakuwa na jukumu zaidi la kusoma kitabu kimoja kila mwezi ili kuchangia nguvu zao kuwalisha wageni wanaohamia hapa.
Nchi nyingi duniani na hasa Bara la Afrika limekabiliwa na ugonjwa wa Kutosoma na tiba ya ugonjwa huu imekuwa haipatikani huko zaidi ya nchi ya Kasri. Kutokana na hali hii kila mmoja amejiwekea nafasi ya kuongeza juzuu na maarifa zaidi ili tiba za wananchi wa dunia hiyo iweze kupatikana na ikiwezekana kuwafikia huko waliko.

Si malengo ya Jamhuri hii kutangaza mema yanayoizunguka nchi yetu bali kuonyesha umuhimu wa kuchangia rasilimali zetu kusaidia kuondoa upofu wa fikra katika nchi nyingine. Jukumu hili hufanywa kwa upole na unyenyekevu maana wananchi wa nchi hizo wamegeuka dhoofu kufuatia vitisho na suluba zilizowakabili katika miongo mingi. Hapa zuoni huwezi kwenda kwa ari mpya, kasi na hata nguvu! Wananchi watakuuliza ulikuwa wapi siku zote au huko nyuma hukuona njia?

Kinachonifurahisha ni haya maisha ya Wanakasri, walitazama mapema sana wakaishi katika kuwekeana mitego ya fikra, hawa ukiwauliza twaweza kupata wapi maji ya kunywa...watakujibu chukua miti mitano panda pale kweye kilima kisha shuka bondeni na kata lako unywe maji! Ukiwauliza wanapata wapi fikra za kutosha kulisha umati mkubwa unaoongezeka bila kuyumba watakwambia chagua kupenda kuishi au kufa!

Nakukaribisheni sana katika kampeni hii ya wana Kasri. Mwaka huu unatakiwa kuongeza jukumu hili ambalo KASRI limetangaza kuwa kauli mbiu ya mwaka 2006. Poleni sana kwa kuongeza majukumu mapya.
 
© boniphace Tarehe 1/01/2006 09:26:00 AM | Permalink |


Comments: 1


   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved