Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Wednesday, January 11, 2006
RIPOTI YA MWEZI YA MBUROGU ZA KISWAHILI

Rabuka Mola jalia, mwanao kuamkani
Shairi pate tungia, Bloguni somekani
Ahadi nilitolea, hima vema timizani
Ripoti kuandikia, ya mwezi uloishani.

Kazi tulojipatia, njema wewe wasifuni
Watu tunawafunzia, maarifa ongezani
Pamoja twakatalia, maovu kufanyikani
Mola Baba angazia, taifa la bloguni.

Mwezi ulioishia, chache zilianzishwani
MAISHA TAFAKARIA, Musoma ikatokani
KURUNZI kamulikia, kutokea mabondeni
Alabama kasikia, Sauti BARAGUMUNI.

Wito sijasahulia, weledi jitambueni
Tafakari nafanyia, Blogu Kiswahilini
Hoja mlizotolea, ndizo naunganishani
Kisha wote kuonea, kile mchokifanyani.

Pale nilipoishia, Kanada nikaendani
Harakati kakutia, Toronto kusalimuni
Ilikuwa yavutia, gwiji huyu muonani
Ndesanjo kakumbukia, simu kutupigiani.

Sasa wazi naanzia, wote sasa tuliani
KASRI niliishia, siasa shabikiani
MATERU bila julia, naye moto kawashani
Ukweli katupashia, Zanzibar iko motoni.

Hoja ya kuweka picha, JIKOMBOE katoani
Riwaya kushikilia, HARAKATI jikitani
BWAYA yeye katania, nani anayesomani
Majibu akapatia, hoja yake ifutani.

Hotuba ilo sawia, igizo jipya nchini
Blogu zikasemea, lazima kuitunzani
MARK kaitafutia, JEFF kaitundikani
Lengo kuja tazamia, Kikweto alofanyani!

DAMIJA kaendelea, Blogu jina pewani
Wasifu kiandikia, lini wangu tatoani
MWANDANI alopotea, kaleta hoja razini
Katwambia kumbukia, nyumbani bora nchini!

Huko Dodoma nalia, sijui chawakinzani
MIRUKO alikimbia, Polisi tukasemani
MARTHA naye kaamua, kwa mwezi kuja mojani
Simanzi kanachilia, kushindwa kumsomani.

Hawa sasa nasemea, kweli wamekimbiani
FATMA mwanasheria, London kajifichani
NGURUMO wa Tanzania, kajificha gazetini
Kila anapotokea, semina kitangazani!

KAKA PORI
katokea, tathimini angazani
Teknojia yakua, hata huko maporini
Sasa anaandikia, na picha kisha wekani
NYEMBO kamkumbushia, ya Kikwete kuhojini.

Bibie CHEMI nasema, hongera mama semani
Urembo wanafanyia, wanitia walakini
MOTOWAKA nakwambia, picha yako iwekeni
Maana utajulia, KESSY ukimuonani.

Ewe MKWINDA julia, kaziyo twaheshimuni
Tazama wageuzia, wengi ngano kutungani
MKINA mpe gunia, arejeee duniani
PAMBAZUKO tambulia, wajibu kuandikani.

ZAINABU na BAKANJA, hawa ni wa msimuni
BITIDAFFA wa Dodoma, naye amejiungani
KAZONTA anafatia, mgomo kuendeshani
Watwacha kwenye udhia, sisi kutowasomani!

Mwisho wake BANGAIZA, mimi sijaufikani
TERRIE wewe nakwambia, subiri nakufatani
KIVALE namuonea, kimya kakumbatiani
Naomba jibu patiwa, yupi hawa amshani?

Hoja uliyotolea, MSANGI toka nyandani
Hima wazi jadilia, kwani ina utatani
Tumeshaanza onea, madaraka jipeani
Huu utata anzia, wa wanamtandaoni.

MICHUZI sijachelea, picha zako kusifuni
Bongo unaangazia, ughaibuni onani
Nasi sasa twaigia, bila woga anikani
Kumbuka wito natoa, kwa wengine kupitani.

Umoja wetu jalia, twapaswa kuukuzani
Nguvu tukizingatia, wengi itawawashani
Kumbuka ni yetu nia, mpya nyingi funguani
Macho wakishafumbua, Tanzania tachekani.

GAPHIZ unosomea, nawe nakukumbukani
Mwaka mpya kutokea, Heri ukatupeani
Nami sasa nasemea, kazi njema tufanyeni
Vitabu tukifunua, hazina tutapatani.

Kaditama naishia, Texas kuishini
Wito niliutolea, Mellisa kikubalini
Kwangu amenitokea, fikira kufufuani
Simba naweza vamia, bila woga nipatani.
 
© boniphace Tarehe 1/11/2006 11:32:00 AM | Permalink |


Comments: 8


 • Tarehe 1/11/2006 4:09 PM, Mtoa Maoni: Blogger Jeff Msangi

  Ahsante Makene,
  Leo sijui hata kichwa changu kinaongea lugha gani.Maisha ya ughaibuni lah,kama mnavyojua.Lakini baada ya kusoma ripoti kama hii basi tabasamu linajongea.Ahsante Makene

   
 • Tarehe 1/12/2006 2:04 AM, Mtoa Maoni: Blogger mwandani

  Swadakta! ripoti kinamna hii, inaniwacha hoi (kwa utamu wa tungo)

   
 • Tarehe 1/12/2006 5:04 AM, Mtoa Maoni: Blogger Phabian

  Naam!! kaka naona tunakumbushana wajibu na kupeana majukumu kinamna safi sana ujumbe umefika.

   
 • Tarehe 1/12/2006 11:41 PM, Mtoa Maoni: Blogger Fikrathabiti

  Bwana makene tujalie heri ya binti huyo wa kando yako.Hakika shairi hili atakua kalitia nakshi huyo mrembo wa pembeniyo a.k.a THE UNKNOWN.

   
 • Tarehe 1/16/2006 4:13 AM, Mtoa Maoni: Anonymous Anonymous

  Hala hala hiyo picha isijezua utata nyumbani bongo.

   
 • Tarehe 1/17/2006 4:49 AM, Mtoa Maoni: Blogger mloyi

  Kasirini latoka neno
  Motowaka alipata
  Pichaye iko mferejini
  Yatiririka pamoja maji


  Wazi macho yako weka
  uwe na uvumilivu
  mimba ishatungwa
  mtoto yu njiani


  Motowaka utamwona
  Technolojia yake hafifi
  Aenda iboresha usiku huu
  aweze onekana.

  Kesho ni ya manyani
  kwa motowaka itafika
  mburoguni ajitokeze
  wote kumwona.

   
 • Tarehe 1/23/2006 9:59 PM, Mtoa Maoni: Blogger nyembo

  Ahsante kaka!
  furaha yangu kwako imefikia upeo,siwezi kuilezea katika kazi yako hii...
  nashukuru kutupa moyo ni kazi ya kishujaa sana!

   
 • Tarehe 1/24/2006 8:06 AM, Mtoa Maoni: Blogger Rashid Mkwinda

  Kweli moyo inatia, kwa kazi tunofanyia, Makene ameanzia,salamu kutuletea,ni muhimu shukuria, kwa kazi ulofanyia, hongera nakupatia, mola atakujalia.

  Sote tukatika jahazi,bahari twatembelea,Kwetu hii iwe kazi, wengine hamasishia, ujumbe wetu u-wazi, wasomaji waujua, twendelee kuuenzi, hatima tutafikia.

  Makene kwa hii kazi, ni kweli umepania, mkono wako u-wazi, kwa njia kuoneshea, hatutofanya ubazazi, hima tutakufatia.

  Wakatabahu.

   
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved