KUMEIBUKA mwezi wa ushairi katika
Blogu za Kiswahili. Alianza
Mkwinda, malenga mkongwe kutoka Pwani ambaye amekuja kuwa tishio katika wanablogu wanaogani tungo za mashairi. Katika pita pita akatokeza
MWANDANI naye akaimba hivi. Kama haitoshi Malenga mwingine akazaliwa Zanzibar. Huyu ni
MATERU. Mjadala wa
MKWINDA ukamkuna
NYEMBO, akajibu nami nikachangia kidogo. Sasa
NYEMBO kapaa kabisa na utungo katika Blogu yake.
Miongoni wa wanaotajwa na
NYEMBO katika majigambo haya ya kishairi tunayotaka yachukue sura mpya katika Blogu ni mimi. Sasa natangaza nami kuingia katika majibizano haya ya kishairi na watani wangu hawa nikianza na NYEMBO. Kumbuka hii si nafasi ya kumfanya
HARAKATI asahaulike kwa kuwa aliahidi kukariri shairi moja kwa wiki ahadi ambayo haikutimizwa. Pata sasa shairi hili hapa chini.
Nyembo wewe waitwani, hadi uje malengani
Ni wapi unakeshani, tungo zako karirini
Nani amekunyweshani, sumu tamu mezeani
Waweza huu mchezo, ama waja taniani?
Katu sumu simezani, kitumbua situpani
Siki kwangu asalini, utungo jifunikani
Naweza tupa mpini, kisha jembe limiani
Nambie Malenga Nyembo,waitwani shairini?
Diwani ya Nakuzerwa, itatoka si utani
Hodo hodi ni muswada, DAMBAYA kishirikini
Ewe Malenga Mkwinda, huyu Nyembo atokapi?
Kama naye malengani, jinale anaitwani?
Nahisi kaja kwa tambo, wakongwe kuwatishani
Ushairi ni ulimbo, weledi unaletani
Hauji kama mkumbo, kukukuta ukubwani
Nikali mama tumboni, shairi nililighani!
Tungo tungile zamani, sasa kazi someshani
Mama alinambiani, nilivyoghani tumboni
Huzuni kimtokani, siku hizo kumbukani
Kanileta duniani, njia nachia tambaa.
Nyembo toa masharubu, kama wataka tungani
Utajageuka bubu, ulingoni kimbiani
Tambua huu weajibu, mahoka waulizani
Kama wadhani mchezo, uliza upotokani!
Mwandani nawe changia, uvamizi uwanjani
Beti waweza pangia, Mshairi kuitwani?
Hoja waweza pangia, kisha ngoma alikwani?
Mshairi mtu gani, hoja hii fafanua!
Natoka sasa wagenzi, hoja nimeanikani
Tungo zachie wapenzi, walale wakiliani
Ghani wache wakufunzi, walale wasibaini
Kisha Nyembo rudi tena, kama waweza tungani.
Msinisahau,nimeinama kama kobe vile,natunga sheria za maapisho.Nikirudi nitakuwa nimebeba bohora ili sote tukasheheni kuliko na sayari wasiyoenda wanadamu.Ushairi mzuri Makene,nasubiri majibu ya watani wako.