Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Sunday, January 22, 2006
HATUIJENGI AFRIKA KWA FIKRA HIZI????
HIZI ni fikra zangu, zimekuwa na kushamiri zaidi tangu nimeishi ughaibuni. Niliweza fikiri chini ya mipaka zamani lakini sasa hapana! Kila ninapoulizwa wapi natoka jibu langu awali lilikuwa Tanzania. Kila nilipogundua kuwa hili si jibu sahihi huku ughaibuni nikabadilika, nikaanza kutangaza kutokea Afrika. Kila nitajapo jina hilo siulizwi wapi inapatikana! Maswali yanayofuata si mada yangu hapa leo.

Najivuna sana sasa kwa kuwa Mwafrika, nafarijika zaidi kwa kuwa natoka huko na maisha yangu yatakuwa huko na siku nikifa nipumzisheni huko. Kila ninapokutana na taarifa za machafuko kati ya Mwafrika na mwafrika naumia, naweweseka naugua moyoni. Kila nisikiapo mipango ya kuwatenga waafrika katika Afrika nauliza hawa wana maana gani? Je ni kukosa kutambua mipaka ya bara hili, ni kutofahamu tunavyounganishwa kila tuwapo nje ya bara hili? Kwa nini mipaka katika Afrika wakati mataifa makubwa yanafungua milango yao ili kutukandamiza na kutunyonya? Kwani Kenya kuwa na wasomi wengi ni kosa? Nigeria kuwa na idadi kubwa ya watu na wasomi pia ni dhambi? Je kuna haja ya kutimuana katika Afrika katika misingi ya kazi, elimu na masuala mengine? Hivi hizi suluba wanazozipata waafrika huku ughaibuni watasuuzika roho zao wapi kama si Afrika! Hivi nani ametuloga, nini maana ya Mungu ibariki Afrika? Mnasema tu hamtendi sio? Naandika maandishi haya kwa uchungu. Machozi yanaweza nitoka hapa lakini sitaki kisima hiki kitazamwe na hawa walionizunguka maana wote weupe. Hawa wanyonyaji wetu na wana sera zinazofanana! Si wote lakini wachache wao wenye nafasi za kiuchuimi na madaeraka hawatupendi kabisa. Wangetamani tuwe vipofu watunywese sumu! Hawatuthamini kabisa ...lakini sasa kwa nini na sisi twabaguana hivi? Hivi Watanzania mmekatazwa kwenda mataifa mengine? Kwanbi mlipokuwa mnanyimana Pasipoti ili mbakie nchini kwenu ndiyo tabu ya ninyi kuishi na wenzenu toka Afrika? Mtanisaidia mlio ughaibuni...siamini katika mipaka aliyoipanga Bismarck kichaa wa Ujerumani aliyekutana na wakora wenzake pale Berlin mwaka 1884-1885.

Hao vichaa wakatenga mipaka katika bara lisilo lao. Sasa tunashupalia mipaka hii na kuumizana wenyewe kwa wenyewe. Kweli tunaweza kuungana na kuwa na Afrika Mashariki kama hali ni hii ya kupandikiza chuki. Misingi ya maandishi yangu ni habari hii kutoka katika gazeti la Chama tawala Tanzania CCM AMBALO LIMEANDIKA HABARI HII.
 
© boniphace Tarehe 1/22/2006 11:56:00 AM | Permalink |


Comments: 1


  • Tarehe 1/23/2006 5:23 AM, Mtoa Maoni: Blogger mwandani

    Na gazeti la jana limeandika kuwa majambazi yanayotokea nchi jirani yakamatwa! kumbe hata kazi za ujambazi zinachukuliwa na watu kutoka nchi jirani! masihara mbali,sioni haki ya mtu kufanya kazi bila kibali wakati kuna watu waliofuzu wengi tu wanaambaa bila ajira - sina shida kama watakuja kwa haki kama wengi wetu wanavyokwenda kufanya kazi ughaibuni kwa vibali maalum, Kuingia kinyemela siyo vyema.

    halafu hiyo habari ya machina kuua mbogo waliyemfunga kamba mie imenisikitisha. Wamempiga kwa nondo, ikesha wakamfunga, isitoshe wakamgonga na gari! Dharau kubwa sana - kisa wamemshutumu kwa wizi!

     
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved