Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Tuesday, January 24, 2006
NYEMBO UMEWASHA MOTO
NATUNGA shairi hili kama jadi baada ya NYEMBO ama HUD HUD kunijibu kwa shairi hili katika Gazeti Tando lake. Mjadala huu haujaisha na hautamalizika mapema licha ya shujaa MKWINDA kutangaza kuukimbia huku akiahidi kujiingiza kwa machale. Simuamini Mkwinda asemayo maana ushairi ni sawa na ramli au uchawi fulani. Huweza kumuamsha aliyelala na akaghani tungo bila ridhaa yake. Hiki ndicho kitokeacho sasa maana licha ya majukumu mengine ukikuta tungo zinakujibu unaamua kuingia vitani. Sasa pata tungo hii hapa chini kisha kama jadi changia mawazo yako.

Hudi ya Moshi mabasi, abiria kubebea
Yanitia wasiwasi, malenga kujiitia
Jina hili la ukwasi, uzunguni latokea?
La kwangu liwapi jina, Nyembo hujalijulia?

Nilisema tangu zama, Nakuzerwa itikia
Nilirithi ujima, ngano zangu tangazia
Limenipa kusimama, na mengi kuyafanyia
Hizo ndaro punguzia, nijue navyoitiwa!

Mbingu ilishangilia, na jua likachekea
Nakuzerwa kizaliwa, kando ya ziwa sikia
Dhoruba ikatokea, bila wavuvi ulia
Kulikuwa kuzaliwa, kwa malenga Nakuzerwa!

Kaishi kwa mbili saa, kisha neno kasemea
Ukumbi watu kajaa, Malenga kumsikia
Karatasi kaiomba, na kalamu andikia
Utungo akaugani, mwaka mwema tangazia.

Wazee wakakimbia, tohara kumfanyia
Wakakutwa na udhia, kwa jambo waloonea
Kisu akawaombea, kisha yeye jikatia
Damu iliyotokea, ikapelekwa jangwani.

Sikia kilotokea, jangwani ipomwagiwa
Mafuta yakachimbiwa, Arabuni shangilia
Na tende zikaotea, Islamu shangilia
Ngamia wakafikia, maji yake kujinywea.

Karne ilitokea, Fumo bado kuzaliwa
Inkshafi bado tajwa, Mwanakupona sawia
Saadan nakwambia, ni mwana bado zaliwa
Sasa huyu ndugu Nyembo, pawapi angetokea?

Tafaruku likazuka, shairi badilishia
Akaitwa mtukuka, maamuzi kufikia
Mizani na vyao vina, kundi moja kashikia
Na wengine kawambia, mapingiti kutungia.

Nyembo wapaswa sikia, kilio utajutia
Wa nchi kavu malenga, majini hupotelea
Huwezi mkondo fata, Mkwinda kesha kimbia
Katu sumu simezani, malengani kufiliya.

Musoma amekulia, Bukoba akasomeya
Dar akitembeleya, Ndanda ghani kutungiya
Mkwawa kamjuliya, Na Songea mwamkua
Kisha Mlimani kenda, kutaka kudurusia.

Huyu ndiye Nakuzerwa, malenga aso udhia
Kwa Bush anandikiya, shetani kufukuziya
Blogu kafunguliya, umma upate someya
Kisha rudi kwao piya, jamii badilishiya.

Sikamilishi nasema, hapa naendelezea
Njoo Nyembo nakwambiya, ubazazi kushikiya
Kigoli kakungojeya, kule kwenda mkunjiya
Halafu ujite malenga, kwa fani usojulia?
 
© boniphace Tarehe 1/24/2006 12:20:00 PM | Permalink |


Comments: 1


  • Tarehe 1/26/2006 6:13 AM, Mtoa Maoni: Blogger Rashid Mkwinda

    Nyembo wewe'takufunga,lugha ukiibananga,Makene nitakupunga, fikira zikikuchenga,
    Tusiwe kama kipanga, mkwapua vifaranga,Bakora tawacharanga,mkianza kuboronga.

    Hii ni dondoo panda katika post yangu usome zaidi....

    Wasomaji wa Blogu hii ni burudani tu ya ushairi yenye lengo la kujiongezea masamiati kwa minajili ya kukuza lugha ya Kiswahili.

    Hakuna uadui wowote kati yetu kwa njia ya malumbano aina hii washairi wengi watajitokeza....BLOGU yetu itapendeza!!! we acha tu au vipi Ndesanjo natania????

    Wakatabahu

     
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved