MICHAPO kama kawaida mingi sana katika Tanzania. Juzi nimefarijika kukutana na ndugu ambao nimeachana nao siku nyingi.
Kama kawaida majadiliano yetu yakabaki kuzungumzia habari kavu. Sipendi mijadala ya mambo mazito kila mara. Natamani nikutanapo na rafiki watambue hili lakini wao ndio kama kwao kumepambazuka!
Ukifika tu baada ya salamu, kinachofuata ni mambo mazito. Mijadala kuhusu mustakhbari wa Tanzania. Mijadala kuhusu madini na vinginevyo.
Binafsi naamua kuwahamishia katika hoja ya kilimo. Natamani kila mmoja azungumzie kilimo maana ndicho kinachoweza kuleta tija hapa Tanzania.
Kilimo kikiwekewa mkakati wa dhati ni wazi tutarejea katika harakati za kusaidia nchi kujikwamua katika tatizo la kukosa chakula. Kilimo pia chaweza kutusaidia kama taifa kurejesha mkakati wa kuhamasisha chakula bora.
Faida za chakula bora kwa wananchi ni pamoja na kujenga afya zao, huku pia kukiwa na faida ya kuwezesha akili kuwa tulivu na hivyo mtu kuwa makini katika utendaji wa mambo anayotakiwa kufanya.
Wakati nikiwa na tafakari za kilimo nakutana na mwanafunzi mmoja wa Chuo Kikuu Mlimani. Huyu msomaji wa safu hii na ananipachika swali kuhusu hali ya wanafunzi kwa wakati huo.
Anachokieleza ni kuwa nchi haiongozwi tena vema. Nchi imebakia mfano wa kundi la wajanja wachache ambao wamekutana kunywa kahawa. Namuuliza yeye angetaka iweje?
Ananitazama na kuanza kutoa mada! Sina muda wa kukaa hapo alipo na kubwa ni hili la kuchoka kujadili mada ngumu na mambo mazito mazito kila siku.
Mwaka unaisha, unakuja mwingine na ukifanya tathmini utabaini kuwa kichwa kinahitaji kusikia habari tulivu. Kinahitaji kuchekeshwa maana yaelezwa kucheka ni tiba kwa binadamu.
Kichwa hakitaki kusikia habari za huzuni tu. Kinataka pia kusikia vituko na purukushani zingine za dunia. Kinahitaji kupata taarifa zitakazoweza kukupanga kimkakati ili uzidi kufanikiwa na kuirejeshea jamii.
Kutokana na hilo nimeamua kuvuta hewa, nimeamua kupumzika kiasi, lakini kosa la kazi hii siwezi kukimbia na kuacha kasri hili bila chakula.
Wapo wanaoweza uliza mbona nilikimbia katika Gazeti Tando! Jibu lipo dogo tu, navuta pumzi ili nirejee tena. Siku si nyingi nitakuwa huko pia.
Kama ambavyo sasa naamua kujadili kuhusu utata wa Kamati ya Madini iliyoundwa na Rais Kikwete. Usishangae kunikuta nami najiingiza katika mjadala wa kamati hii.
Sina utaalamu kuhusu madini lakini naweza kujadili kamati. Kamati imeundwa na tayari ukitazama yameanza kuibuka mambo.
Jambo kubwa ni watu waliowekwa katika kamati hiyo. Siku moja baada ya kamati hiyo kusomwa, mmoja wa wajumbe sidhani hata kama alikuwa kapata barua rasmi ya kuwa mjumbe wa kamati, alisikika akikubali kwa moyo mkunjufu uteuzi wake.
Siku mbili baadaye kauli kutoka chama chake zikaanza kukinzana na kukiri kwake. Sasa kunaelezwa kuwepo kwa watu wasiopaswa kuteuliwa katika kamati hiyo. Hii ndiyo Tanzania ambayo kila jambo unalofanya linatakiwa kupindishwa hata kama faida au hasara yake hii wazi.
Wanasiasa wanaishi kimtego mtego. Kazi yao ni kutegana na inapogundulika kuwa mmoja anataka kuzidi kete utaona mwingine akiibuka na kulalamika. Hapa ndipo unapotazama sasa hoja ya kamati ya madini inapoanza kupoteza maana ya kazi yake na sasa kazi inageukia kutazama watu wanaounda kamati hiyo.
Mwisho wa siku kamati itafanya kazi na inavyoonyesha majibu ya kamati hii huenda yasipewe maana, kwa kuwa makundi yamejigawa tayari kusubiri majibu wanayoyapenda!
Wiki iliyopita nilidodosa kiasi kuhusu wajibu wa wajumbe wawili kutoka upinzani. Nilidodosa pia wasifu wao huku nikimuelezea Cheyo John kama mwanasiasa mwenye uwezo wa kuunganisha nguvu za pande zaidi ya chama chake.
Mwingine Zitto Kabwe sikumjadili maana kwa maisha na umri hajaweza kujenga tabia ya jumla ya kumbainisha alivyo katika siasa. Lakini sasa hivi ni maarufu na hasa katika hoja za madini.
Ni humo alimoingizwa huku kukiwa na tetesi mtaani kuwa, kama hakufanya tafiti vema katika hoja zake alizozitoa miezi kadhaa kwa sasa anaweza kuwa katika nafasi ya kulamba matapishi!
Hili linaweza kuwa hofu ya chama chake ambacho kimeanza kuhoji baadhi ya majina katika kamati hiyo. Lakini kwa nini tusisubiri majibu ya kazi hiyo na kuiacha kamati kufanya kazi yake kwanza?
Hofu ya aina hii ina picha ya sura za wanasiasa! Sura zao hugeuka kila mara, leo watataka hili na kesho wakiliona linakuja katika njia nyingine ya kuwaathiri wanakimbia! Huenda Chadema kimeshaona jambo lililojificha na kama ndivyo, chama hiki kinatakiwa kutambua mbinu nzuri kuliko hii ya sasa ya kuanza kuufanya umma utazame wanaounda kamati badala ya kazi ya kamati.
Kinachofanywa sasa ni kuonyesha kuwa kamati hiyo haitafanya kazi, ama itafanya kazi lakini kwa upande ule ule wa kuvutia kwa serikali. Lakini si kuna wajumbe wa upinzania ndani ya kamati hii? Kama ndivyo, tuamini kuwa Tanzania kuna wapinzani wa majina tu?
Kama kawaida jamii inaanza kuchanganywa hali itakayofanya mwisho wa siku tusibaini kama kulikuwa na ulazima wa kuiunda kamati hiyo, kufuatia pia kuwepo kwa kamati za madini zaidi ya tatu huko nyuma. Hofu hii inatoka wapi na nani anatakiwa kunufaika na hofu hii? Wanasiasa wana maisha magumu na yasiyotabirika! Naamini wanaweza hata kutoa majibu ya hofu yao ila la msingi tunataka ukweli kuhusu utata huu wa mambo ya madini nchini.