Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Wednesday, May 20, 2009
NIMETIMIZA WAJIBU WANGU

Mwaka sasa umepita tangu nianze safari hii ya kusaka elimu niliyoamini ni muhimu sana kuipata kuliko kuikosa. Nashukuru katika mwaka huu nimekabiliana na mengi na kutokana na hayo naweza sasa kusimama kuwa nimebadilika.

Maisha ya binadamu yana fasili nyingi, yaweza kuwa yale ya kukumbatia sifa mbazo hazikujengi ama kukumbatia watu walio na sumu ya kukuua. Maisha haya haya yaweza kuwa yale ya kuwa na wasiokuthamini ama kuwa na wanaokuthamini. Yote haya ni maisha na ni vigumu kwa mtu kufahamu nani ni nani katika maisha yake.

Ni katika njia hii sasa naweza kutambua maumivu yangu yamepoozwa na nani na akina nani walitegemea kufurahia mimi kubakia katika maumivu! Pia naweza kutegua kitendawili kuhusu nani waliweza kukaa name wakati nikihitaji kuw anao zaidi.

Kwa ujumla kazi niliyofanya nafahamu baadhi hawakupenda kuona nikiifanya lakini wapo walionipa nguvu siku zote kwa kile kisemwacho: “binadamu wengi hupenda kuona ukishindwa jambo ili waibuke na kusema, tulijua tu ataanguka.” Katika wanaoamini katika falsafa ya kushindwa kwangu wamekosa nafasi!

Maisha mapya yanakuja baada ya safari hii. Ndugu zangu akina Materu na Msangi kama sio Mwaipopo watafahamu pia namna nilivyokimbiza mpira huu hadi kuuweka katika penati. Nimepiga penati hii leo japokuwa huwezi kubaini ni lini gori litaingia lakini hadi sasa mpira upo katikati ya gori na kipa namuona anaelekea kushindwa kuuzuia.

Kikubwa ni kuwa, hakuna atakayekushika mkono kuingia darasani katika ulimwengu wa leo. Hakuna atakayekuhamasisha kusoma kwa kuwa anafahamu kwa kufanya hivyo unakaribisha uhuru na ukombozi wako. Adui mkubwa wa maisha ya mtu ni yeye mwenyewe hasa anapokubaliana na hali dhaifu na kuikumbatia kwa kusema, 'nitafanyaje'!

Mwisho nimshukuru Jalia kwa nguvu zake nyingi na majaribio mengi aliyoyapitisha shetani katika kipindi hiki cha mwaka mmoja. Ni kweli navunja rekodi katika Chuo hiki kwa kuwa mwanafunzi wa kwanza kukamilisha masomo haya katika Shule ya Serikali kwa muda wa mwaka mmoja. Hii ni faraja kwangu, nimeandika historia katika uwanja mwingine. Nafahamu njia inayonikabili kuanzia kesho ni ngumu lakini nimejiandaa vema kukabiliana nayo kuliko unavyodhani.
 
© boniphace Tarehe 5/20/2009 12:58:00 AM | Permalink |


Comments: 8


   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved