Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Saturday, May 27, 2006
YA PICHA NYINGINE HII
NIMEFUMA gazeti tando hili la picha mpya mpya kwa Mzee wa Mshitu nikaona nilipachike ili nawe upate habari za picha za leo leo kabisa kupitia hapa. Fungua na kisha salimia au pata uhondo mwenyewe huko.
 
© boniphace Tarehe 5/27/2006 11:43:00 AM | Permalink | Maoni 0
Friday, May 26, 2006
KIKWETE SUALA SI KUTOUZA TENA NYUMBA BALI KUREJESHA ZILIZOUZWA!
NAKUANDIKIA waraka huu ikiwa ni moja ya kazi nilizojiwekea. Nakuandikia ikiwa ni kuongeza msisitizo wa imani yangu na msimamo wangu kuhusu suala la kuuzwa kwa nyumba za serikali, suala nililolipa nafasi katika Muswada wa Kitabu changu pia. Nakuandikia kuwa na wewe ulisema ulijigawia nyumba ya serikali na sasa nakukumbusha kuwa suala si kutouza hizi zinazojengwa sasa, nakukumbusha kuwa zinatakiwa nyumba zote kurejea na huu ni msimamo wangu na watanzania maelfu wanaothamini haki ya mali za nchi yao. Hivi juzi umetoa kauli na ikaandikwa kwenye vyombo vya habari. Hii ni kauli inayowaumiza vichwa kundi la akina Pombe Magufuri na mwengine waliokuwa katika serikali ya Mfalme Benjamin Mkapa. Na wewe ulikuwa katika serikali hiyo, na makamu wako alikuwa makamu wako huko pia. Waziri mkuu wako alikuwa waziri mwenzako huko pia na mawaziri wako lukuki wametokea katika serikali hiyo iliyojigawia nyumba za umma baada ya ninyi wenzetu kutuzidi kete kwa kutumia madaraka yetu kama dhamana ya matakwa yenu.

Suala la nyumba hizi sidhani kama litakuja kuachwa liishe hivi hivi katika Tanzania ya leo ambapo watoto maskini wanaosoma vyuo vya juu wanatakiwa kulipa gharama zao za mikopo huku ninyi mkigawiana mali za umma bure tena mchana kabisa! Nakukumbusha kuwa utawala hautadumu kwako milele na kuwa hatuwezi kuona huko kesho ni kipi kitadaiwa na wananchi! Ili kuepusha leo kujenga kesho chafu ni bora kufanya yanayowezekana sasa ikiwa ni moja, kutangaza gharama za kila nyumba iliyouzwa, pili kutangaza minada ya nyumba hizo ilivyofanyika na tatu kuwaomba wananchi kurejesha fedha za hao waliojigawia nyumba zetu sasa ili wakajenge zao kwingine na kisha nyumba hizo kurejea serikalini na kutumiwa na mimi na wewe na wengine watakaopata nafasi ya kutumikia umma wetu.

Hatutishani kabisa katika suala hili na wala Kasri hapa siandiki kwa jazba. Msimamo wangu kuhusu nyumba hizi sikuuanza leo nimekuwa nao siku nyingi na hakuna atakayenibadilisha kabisa. Kama mnamuenzi kweli Nyerere basi lazima mjikane na kurejesha nyumba za umma na kisha kuanza kujenga zenu na watoto wenu popote mpendapo. Si dhamana ya madaraka haya tuliyowapa ni ya muda mfupi tu, je mnadhani mtaishi nayo milele, kumbukeni hukumu yenu kesho kama nanyi mnashiriki kunywa kikombe hiki cha damu ya watanzania.

Nyumba za serikali zatakiwa kurejeshwa kwa kuwa zilikiuka misingi ya uuzwaji au ugawanjwi wake. Mlijigawia na hilo ni kosa. Natafuta kifungu cha sheria ili niende mahakamani siku moja lakini kabla hatujatumia mbinu hizi za kuaibishana ni bora mkaona kuwa maandishi haya nayaandika sasa jambo ambalo huko nyuma nisingeweza kufanya. Mnadhani ni nini kinanisukuma kuandika hivi? Mnadhani ni wangapi wanaweza kuandika haya na kuayasimamia zaidi yangu kwa sasa, mnangoja nini kuwaodosha wote katika nyumba zetu sasa na kuwarejeshea vijisenti vyao ili nyumba za umma zibaki za umma? Kikwete nakamilisha kwa kukumbusha kuwa hii ilikuwa sifa yako mojawapo wakati wa uteuzi. Uliaminika kuwa hukununua nyumba na ulipotangaza kununua pia ilitamkwa kuwa ni siasa ya kutaka kuunganisha wezi na wadhambi pamoja na wema ili safari ya kushinda madaraka ikamilike! Umeshashinda na raia maskini wanakuona kama ngao yao sasa, unangoja nini kutumia nguvu ya umma badala ya kuwatazama mafisadi waliotumia nafasi zao kujinemesha wakihema na kucheka huku umma ukitazama kwa husuda! Unadhani umma huu utatazama hadi lini, kadri siku zinavyokwenda ndipo na wewe tunakuingiza katika makundi haya hata kama una nia njema na nchi hii sasa. Kumbuka wanaokuzunguka tunawafahamu na hila zao zinajulikana. Kama huchukui hatua maridhawa itatupa nafasi ya kuota masiha mwingine na wewe kukuingiza katika kundi hili hili la wale waliopita baada ya Nyerere kiongozi wetu tunayemthamini na kumuenzi sana. Je wataka lipi baada ya kushinda dola sasa? Jikane na chukua msalaba wako safisha nchi bila woga, hao wanakuzunguka ni wachache mno ukilinganisha na bahari ya watanzania inayotaabika kutokana na tabia ya hao kuwa na matumbo yasiyo kinai.
 
© boniphace Tarehe 5/26/2006 02:15:00 PM | Permalink | Maoni 6
Wednesday, May 24, 2006
NANI ANAZUNGUMZA UKWELI KUHUSU HABARI ZA AFRIKA? (3)
MIAKA mingi imepita tangu Tanzania ikiwa na chuo kimoja cha Uandishi Habari, chuo ambacho kilitoa elimu iliyoishia kiwango cha stashahada. Siku hizi kuna utitiri wa vyuo vinavyofundisha uandishi wa habari. Vipo vinavyotoa shahada pia lakini bado kuongezeka kwa vyuo hivi hakujaleta mapinduzi katika fani ya uandishi ili kuifikisha sehemu ya kuaminika kama mhimiliwa nne katika nchi.

Kazi za uandishi wa habari zimeongezeka lakini uendeshaji wake umebakia wa kubabaisha kutokana na sababu kadhaa. Kubwa ni kukosekana kwa utashi wa waandishi wenyewe katika kujenga taswira yao, hapa nazungunmzia suala la mwandishi kujijengea uwezo yeye kama yeye katika fani hii. Na pili, vyombo vya habari kutothamini sana ubora wa kazi zaidi ya kutaza faida ya soko badala ya misingi na miiko ya kazi za uandishi wa habari kama taaluma na fani yenye miiko, maadili na sheria zake.

Huku ughaibuni vyombo vya habari vinajitanua zaidi na kuongeza majukumu hali inayotanua wigo wa kazi za waandishi wa habari. Vyombo hivi havimalizii habari katika kuichapa gazetini au kuirusha redioni na kwenye televisheni tu; vinachapa vitabu, vinashiriki kutengeneza filamu na matukio mengine ambayo hutanua mapato ya kampuni, mapato ya waandishi na pia kujenga jamii ya watu wanaothamini kusoma na kutunza kumbukumbu za mambo. Tanzania bado waandishi wetu wamebaki wengi kuandika hotuba au ripoti wanazozisikia zikitolewa na viongozi au watu wenye kutengeneza habari na mara nyingi hawana nafasi hata ya kuhoji aina ya ripoti na hotuba hizo, wanafanya kazi ya kujaza kurasa za magazeti au kutosheleza dakika za redio na televisheni zao kwenda hewani.

Habari nyingi siku hizi zimekosa radha, zimekosa kuonyesha jitihada za mwandishi kuchimbua na zimebakia kushabikia, kupongeza, kusifia na kushutumu! Utasoma habari kwa mfano, rais alisemani mawaziri 33 tu kati ya 60 wanaohitaji nyumba na habari kuwa serikali inatumia mamilioni kuwaweka katika hoteli inapotosha ukweli,” alisema. Mwandishi anaishia hapo na hawezi kufunua kinywa kuhoji ata hao wametumia kiasi gain kuishi mahotelini na nini kiliwafanya kuishi hoteli za anasa huku wamezaliwa katika nchi hii hii ya Tanzania na wanaishi maisha ya chini tu, nini hasa chanzo cha wao kuvaa gwanda jipya la kutamani maisha ya anasa huku wanaongoza nchi maskini.

Bado utakutana na habari kama, serikali imeidhinisha mikopo ya bilioni za shilingi kwa ajili ya Wabunge na kuwataka wanunue magari yatakayoweza kuwafikisha kutembelea wananchi wao jimboni. Waandishi wetu wataishia kuandika hapo bila kuingia ndani zaidi kutaka kujua magari ya aina hiyo yatakayowawezesha wabunge kuwafikia wananchi ni aina ipi na yanahitaji gharama kiasi gani? Tena hutasikia swali kuhusu mikopo hiyo kutolewa wakati nchi ikiwa bado na njaa, au je mikopo ya aina hii itaishia kwa wabunge tu au itatanuliwa na kwa wananchi wengine maana ukilinganisha uwiano wa msamaha wa mikopo hiyo hasa sehemu ile inayolipwa na serikali, hakukuwa na haja tena ya mbunge huyo tena kupewa kiinua mgongo chake cha milioni nyingi za shilingi baada ya miaka 5 na tena kuna haja gani kugawa pesa bure kupewa wabunge wanaolipwa mishahara mikubwa tu huku Bodi ya mikopo ya wanafunzi wa vyuo vya juu ikishindwa kutoa mikopo kulingana na mahitaji ya wanafunzi!

Nafasi ya gazeti ni ndogo mno na kamwe haiwezi kukidhi matakwa ya mwandishi hasa ikifika sehemu ya yeye kutoa maoni yake na namna anavyodhani jambo fulani laweza kubadilishwa na kuleta mafanikio ya nchi. Wajumbe wa Kongresi ya Marekani mara kadhaa wametumia habari za magazeti katika kutetea hoja zao au kuthibitisha kile wanachokizungumza.

Sababu ya hawa kufikia hatua hii ni kutokana na waandishi kuthamini kazi zao na kuzifanya kwa ukamilifu. Waandishi anatambua majukumu yao hasa na wanajivuna pale wanapoweza kuchimbua jambo na kulianika hadharani. Katika nchi zetu bado kuna matatizo yanayoendana na waandishi kuwa katika orodha ya malipo ya baadhi ya wakuu serikalini au kuamua kwa makusudi kushangilia upande mmoja bila kutambua madhara ya ushabiki hasa ufanywapo na waandishi wa habari.

Mbunge wa kipindi cha nyuma wa Temeke, Augustine Mrema aliwahi kutumia nukuu za magazeti kama ushahidi wa hoja zake Bungeni. Katika tuhuma zile hakufanikiwa kushinda na aibu haikuwa kwa Mrema pekee, ilienda hadi kwa vyombo vya habari alivyovipeleka Mrema kama msingi wa ushahidi wake.

Je vyombo vile vilijiuliza kuhusu kudharauliwa kwa taarifa zao ambazo Mrema alizitumia kama ushahidi wa kutetea hoja yake? Havikujali kabisa, lakini kama hoja hizo zingepokelewa na Mrema kuonekana kidedea hakungekuwa na namna vyombo hivyo vingetaka kujikuza kwa wasomaji kuwa vinafanya kazi nzuri ya kuchunguza mambo kwa kina?

Upo ukweli kuhusu hoja hiyo hapo juu na kweli vyombo vya habari vinahitaji sana kulisaidia bara la Afrika kuonekana nje huenda kwa habari ambazo hatuzipendi na pia zile tunazozipenda. Ni namna moja tunaweza kufanya hivi hasa pale tutakapokuwa na habari mbadala kuhusu matukio ya bara letu.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe Darfur nchini Somalia viko Afrika. Kuna vyombo vingapi vya habari nchini Tanzania ambavyo vimepeleka waandishi wake kuchukua habari hizo? Je mbona habari hizo zachapishwa katika magazeti zikitokana na tafsiri ya habari zilizoandikwa na wageni?

Kweli hakuna uwezekano wa waafika wenyewe kwenda huko na kuandika habari hizo na kuwatumia wageni ili waweze kupata taarifa sahihi zisizo na makosa sana, taarifa zinazoweza kusaidia kufikia ufumbuzi wa mgogoro huo haraka? Hii ni sehemu ya hoja yangu na inaonyesha namna vyombo vyetu vinavyobaki kuwa tegemezi hata katika mambo yetu wenyewe!

Mapema mwanzoni mwa mwaka huu tulipata kutembelewa na Bob Woodward, mwandishi mashuhuri katika habari za uchunguzi aliyefanikiwa kuandika habari zilizomng’oa Richard Nixon katika urais wa Marekani mwaka 1974. Bob Woodward licha ya kuwa bado ni mwandishi sasa, anajishughulisha zaidi na uandishi wa vitabu na kampuni yake inamtumia sambamba na waandishi wengine kuandika vitabu vya uchunguzi wa matukio mbalimbali yanayotokea Marekani na nje ya Marekani.

Mauzo ya vitabu huku yapo juu na gharama za vitabu ni kubwa tu. Je nini kinafanya Afrika vitabu visiuzike na nani aliwaambia waafrika wasipende kusoma. Mustapha Puja ni mhariri katika kampuni moja ya uchapaji hapo Tanzania. Nilizungumza naye siku za hivi karibuni kuhusu namna ya kuweza kuchapa kazi yangu katika kampuni hiyo anayofanyia kazi.

Nilipomgusia kuwa kazi yangu ni riwaya, akaniambia kampuni hiyo haiwezi kuchapa kazi hiyo labda iwe imeandikwa na Profesa au mtu mwenye shahada ya Daktari ya Falsafa. Nilicheka kidogo maana nilitazama kuwa Shaaban Robert licha ya kutokuwa na elimu kama hii niliyonayo mimi, ameweza kuwa na maandishi ambayo maprofesa wengi hawatawahi kukaribia hata nusu yake.

Je huyu naye angenyimwa kuchapishiwa kazi na Waingereza tungekwa tunasoma kazi za nani? Kwa nini tusibaini kuwa soko la usomaji huanza pale kunapokuwa na machapisho mapya kwanza?

Vitabu vyetu vingi hata vilivyo katika mtaala wa elimu ni vya kipindi cha nyuma mno. Kwa ujumla haviendani na wakati huu tunaoishi sasa na hakuna mkakati wa kubadili vitabu hivyo kutokana na sababu kadha wa kadha moja ikiwa machapisho finyu na pili kile kinachozungumzwa kuwa utamaduni wa kusoma kutokuwepo.

Kama hatuwezi hata kusoma mambo yetu wenyewe hali inayowakwaza watu kutoandika tutarajie nani aweze kutoa taarifa bora kabisa kuhusu maisha yetu? Narudi katika mada yangu, Afrika yote yafanana kabisa, kutokusoma na kupenda mambo kwa njia za panya kunaathiri sana hata mfumo wetu wa elimu.

Katika muswada wangu wa “Barua kwa Mama” nimejadili ndoto niliyokuwa nayo kabla sijaingia chuo kikuu. Niliamni nikihitimu hapo nitakuwa gwiji wa kutambua maandishi ya juzuu na juzuu, jambo ambalo sikufikia matarajio yake. Sikufikia chembe ya matarajio yangu kutokana na sababu kadha wa kadha na moja kubwa ni hiyo tabia ya kutaka kufanikiwa kupitia njia za panya, kushinda mitihani bila kusoma au kusoma maandishi yale yanayodhaniwa kutoka katika mitihani pekee.

Kuna uandishi mpya wa vitabu nchini Tanzania umeingia ambao unatazama sana suala la kuwawezesha wanafunzi kushinda mitihani. Kuna vitabu vingi siku hizi vyenye maswali na majibu na hivi ndivyo hupata kuchapwa haraka na makampuni ya uchapaji ya nyumbani.

Vitabu hivi hununuliwa sana maana wanafunzi wetu hawana haja na maarifa bali kufaulu mitihani kwa namna yoyote hata kwa kuiiba kabisa ikiwezekana. Kama kizazi hiki kinalelewa hivi utawezaje kukipambanisha na vizazi vya nchi za ulimwengu wa kwanza ambavyo vinafundishwa kwa umakini na kutambua maana ya kusoma na kujenga fikra za kutambua kila jambo?

Je hatuoni kuwa inawezekana kabisa kuwa mtu anayeishi Afrika akasoma katika elimu ya muundo huu, siku akikalishwa kitako na mwingine aliye ughaibuni na kujadili mambo ya Afrika kuwa inawezekana kabisa kuwa mtu wetu akaonekana hana hata taarifa za kutosha kuhusu masuala ya eneo analoishi?

Vyuo mbalimbali Marekani vina idara inayohusu masomo ya Afrika. Sijawahi kusikia masomo hayo yakitolewa huku Afrika na mjadala huu umekuwa ukitanuka sana huku. Kwa nini viongozi wa Afrika wasijenge vyuo vya kutoa masomo haya ili wasomaji kutoka nje wafike Afrika kuchota maarifa ya Afrika. Je hatuoni kuwa kesho ni rahisi kuwa na wataalamu wanaoifahamu Afrika zaidi kuliko sisi wenyewe kama htuna mikakati ya ziada kukabiliana na hili. Unadhani nani atakuwa na habari njema za Afrika kama hawa wanazisoma kabisa na sisi tunaishia kuzitazama, mjadala huu wa nani anafahamu habari za Afrika zaidi ni mpana mno. Hauna mwisho ila unatoa taswra ya nini Afrika ifanye na kuachana na tabia ya kulia na kulalama kwa kila jambo.
 
© boniphace Tarehe 5/24/2006 09:49:00 AM | Permalink | Maoni 3
Friday, May 12, 2006
WAGOMBEA BINAFSI NA KASISI WANAOTAFUNA KONDOO WAO
MADA ya wagombea binafsi inatanuka na wengi wamechangia hapo chini mara baada ya Mchungaji Mtikila kutangazwa mshindi mapema wiki zilizopita. Ilianza mwaka 1994 na mwaka huu mahakama ikaamuru wagombea binafsi wapatiwe haki yao ya kikatiba, yaani kuwapanulia nafasi ya kugombea pia badala ya kuishia kuwa wapiga kura pekee.

Mchangiaji Kibanda alifafanua mafanikio ya hoja hii huku akieleza mazingira ya rushwa zilizokuwa zikitolewa wakati wa mchakato wa uchaguzi wa mgombea urais kupitia CCM mwaka jana ambapo Jakaya Kikwete aliibuka kidedea. Rushwa ya kununua madaraka ilianza kuwa haki mara baada ya uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi, na sheria za kuidhibiti zikapindishwa baada ya CCM kama chama tawala kuona ndiyo njia nafuu ya kukiwezesha kuweza kushikilia viti vingi vya uwakilishi.

Baadaye rushwa hii ikaundiwa sheria na kubalikiwa na Bunge la CCM na kisha kutimika hadi ilipopigwa mweleka juzi na mahakama kuu. Nini faida za kuwa mgombea binafsi? Hili ni swali muhimu sana na Ndesanjo katika mchango wake amefafanua wazi kuwa ni fursa pekee anayopatiwa mtu asiyependa kujigeuza mtumwa. Hoja hii inakubaliwa na Kibanda na Miruko.

Lakini pia kuna mawazo ya MK ambaye anafafanua kuwa hoja ya wagombea binafsi ina taswira ya kuleta vurugu huku akitumia mfano wa siasa za Zanzibar kushikilia hoja yake. Hata hivyo serikali ya Zaizibar ilishapinga mapema kuwa sheria hii haitatambulika huko visiwani huku pia kukiwa na harakati za mwanasheria wa serikali kurejea tena mahakamani kupinga maamuzi haya ya mahakama.

Nimedonoa kidogo tu, lakini furaha yangu ni kuwa mijadala hii sasa inapata taswira mpya na inajadiliwa kweli kweli na kwa umakini kwa hoja bin hoja. Huko gazeti tando la Pambazuka kuna habari ya makasisi kutafuna kondoo wake ambayo imetanua mjadala na kwa mara ya kwanza kupatikana kwa wachangiaji zaidi ya 100. Hii ni picha namna tunavyokua na kilichonivutia zaidi ni aina ya hoja zinazotolewa huku, hazina bezo sana wala matusi ila kila mmoja anajitahidi kuonyesha mwenzake kuwa hoja yake ndivyo ina nguvu. Tuendelee kujadili hasa nafasi ya mwanasheria katika kupinga sheria hii ya wagombea binafsi, je anatumwa na nani, anatumia fedha ya nani, na anamuwakilisha nani kupinga maamuzi hayo?
 
© boniphace Tarehe 5/12/2006 02:16:00 PM | Permalink | Maoni 7
Friday, May 05, 2006
WAGOMBEA BINAFSI SASA RUKSA! NI USHINDI KWA MTIKILA NA UMMA UNAOPENDA DEMOKRASIA

NCHINI Tanzania kuna mambo yanafanyika na kwa mtu anayetazama na kuchunguza upepo wa mambo utafahamu agenda ya mambo haya. Mwanzo, ni namna ambavyo serikali sasa imeamua kutoa fursa kwa watendaji kufanya kazi zao bila kuingiliwa na tena kuondoshwa kwa mtindo wa kifalme katika madaraka ya dola.

Sasa hivi kila sehemu viongozi wanazotembelea kunafatia wananchi kusema hadharani kero zao jambo ambalo lilikuwa nadra sana huko nyuma. Wananchi wanapaza sauti na hii inakuwa ni hatua ya kwanza katika safari ya kuelekea uhuru wa kujieleza "Freedom of Expression." Vyombo vya habari vya Tanzania vimekuwa vikipewa changamoto ya wazi ili vibadili mfumo wa kuandika barua au ripoti na badala yake vianze kutambua nafasi yake ya kuzungumza mambo makubwa na kuyachambua. Kauli hizi hazikuwapo Tanzania kwa miaka mingi lakini haya yanatokea.

Juzijuzi ilifutwa sheria mahakamani, sheria mbaya iliyoruhusu rushwa na kupitishwa na serikali ya Rais Mkapa. Sheria hii ingeweza kufutwa Bungeni lakini kwa kuwa walioko huko asilimia kubwa waliingia kwa muundo huo, licha ya kuwa Rais Kikwete wakati anazindua Bunge la awamu ya nne, kusema kuwa suala la takrima/rushwa litapaswa kujadiliwa na baraza hilo, lakini utaona kuna mkono ulipitishwa haraka kutokea mahakamani ili maamuzi yafanyike kuiondoa Tanzania katika nchi kongwe kabisa kuruhusu rushwa duniani. Hili lilikuwa tukio la kuweka kwenye kumbukumbu kama hili la hivi karibuni la Bunge la Mexico kuruhusu madawa ya kulevya katika nchi hiyo kwa Lengo la kuikomoa Marekani!

Basi kama uliwahi kupitia mapendekezo ya Tume ya Jaji Nyalali kuhusu ubadilishaji wa sheria na katiba hasa vipengele vilivyokuwa vinakwamisha demokrasia nchini utagundua kuwa sasa jua linaanza kuchomoza baada ya hivi juzi Mahakama tena kukubaliana na madai ya Christopher Mtikila aliyoyafungua tangu mwaka 1994 kuhusu kuruhusu wagombea binafsi. Hili ni tukio muhimu sana kufikiwa katika Tanzania na linatanua demokrasia ya hali ya juu na kufanya suala la nafasi za vyama kugeuzwa miungu ya siasa za Tanzania kufutika ama kuelekea katika bahari ya sahau! Wale waliokuwa wanatishiwa kugombea baada ya kuona vyama vinakuwa na mizengwe sasa wanaweza kuungana na jamii yao na hivyo kuwa moja kwa moja watumishi wa umma na sio vyama na kisha wakafanikisha maendeleo ya jamii badala ya sasa kubakia ushabiki wa vyama vya siasa kwanza kabla ya umma.

Mahakama inaanza kutekeleza matukio haya huku kukiwa na kesi inayofunguliwa jumatatu ijayo kuhusu aliyekuwa Mkuu wa Polisi nchini, Omari Mahita, kuhusu kuvunja haki za binadamu na kukihujumu chama cha CUF. Kwa kasi hii tunaanza kupata majibu kuwa watu waliohusika na maangamizi hata ya Janiari 27, 2001 kule Zanzibar wanaweza kufikishwa mahakamani.

Kuna tukio lingine ambalo nitakosea kama nitalisahau leo kwa sababu ya furaha hii ya kupitishwa mfumo niliowaza kuupigania hivi karibuni wa haki za wagombea binafsi. Hivi Mama Mkapa alipofungua NGO kwa jina la taasisi ya ofisi ya umma aliyoikalia kwa nafasi ya yeye kuwa mke wa rais, ofisi iliyokuwa katika jengo la umma, ikilindwa na askari na ikitumia fedha za umma kuiendesha, anawezaje leo kuiambia Tanzania kuwa ile ni NGO yake aliyoibuni? Hivi Watanzania hawaoni kwa macho yao wizi wa fikra na matumizi mabovu ya ofisi za umma kama huu unaotangazwa na Anna Mkapa kupitia EOTF?

Mada hiyo nitaiandikia tena nikipata muda, sitaiacha kabisa maana haiwezekani ofisi za umma zitumike kuwanufaisha wachache kwa vivuli huku jamii ikidhaniwa imelala na haina macho ya kufanya. Kumbuka unajifunza nini kuhusu kashfa za Siti Mwinyi wakati ule Mrema akiwa waziri wa mambo ya ndani, Tena jadili na jirani yako hapo ulipo kuhusu Anna Mkapa na tetesi za kumiliki majumba na mali nyingi nyingi hapo Tanzania tukiwa hatuna taarifa za nje. Je unaweza kufahamu kuwa mali za Rais wa awamu ya tatu, kwa ubainifu ikiwa ni pamoja na hekalu pale Lushoto ni ndogo kabisa kulingana na hizi tetesi kuhusu mkewe? Tunasubiri nini kuanza kujadili hoja hizi bila woga sasa wakati nchi yetu inapoanza kuonyesha kukomaza sekta nyingine zilizo nje ya dola?

INAWEZEKANA WAUNGWANA, CHEZA KARATA YAKO!
 
© boniphace Tarehe 5/05/2006 11:06:00 AM | Permalink | Maoni 18
Wednesday, May 03, 2006
SHUKRANI WAZIRI MK
NDUGU zangu mnaotembea hapa msinituhumu kwa wizi wa mali ya umma katika kujenga jengo hili jipya. Ukweli kilichotimia hapa ni kile kiliwahi kuzungumzwa na walii mmoja aliyesema, "mmepewa bure nanyi toeni bure." Komredi waziri wetu wa Teknolojia katika jamii ya wamiliki wa magazeti tando afahamikaye kama MK amejenga nyumba hii bure kabisa. Sijalipa chochote na bado anafanya matengenezo zaidi hivyo haijakamilika.

Kama nawe wapenda kufanyika haya kwa nini usimtafute MK ili aweze kujenga nyumba yako. Kwa kweli Tanzania tuna watu wetu waliojaliwa mengi, MK nakushukuru sana na kukuomba kuboresha nyumba za watanzania ili zitishe kuliko hata hawa wanaotokea mataifa makubwa.
 
© boniphace Tarehe 5/03/2006 05:27:00 PM | Permalink | Maoni 8
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved