Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Friday, May 05, 2006
WAGOMBEA BINAFSI SASA RUKSA! NI USHINDI KWA MTIKILA NA UMMA UNAOPENDA DEMOKRASIA

NCHINI Tanzania kuna mambo yanafanyika na kwa mtu anayetazama na kuchunguza upepo wa mambo utafahamu agenda ya mambo haya. Mwanzo, ni namna ambavyo serikali sasa imeamua kutoa fursa kwa watendaji kufanya kazi zao bila kuingiliwa na tena kuondoshwa kwa mtindo wa kifalme katika madaraka ya dola.

Sasa hivi kila sehemu viongozi wanazotembelea kunafatia wananchi kusema hadharani kero zao jambo ambalo lilikuwa nadra sana huko nyuma. Wananchi wanapaza sauti na hii inakuwa ni hatua ya kwanza katika safari ya kuelekea uhuru wa kujieleza "Freedom of Expression." Vyombo vya habari vya Tanzania vimekuwa vikipewa changamoto ya wazi ili vibadili mfumo wa kuandika barua au ripoti na badala yake vianze kutambua nafasi yake ya kuzungumza mambo makubwa na kuyachambua. Kauli hizi hazikuwapo Tanzania kwa miaka mingi lakini haya yanatokea.

Juzijuzi ilifutwa sheria mahakamani, sheria mbaya iliyoruhusu rushwa na kupitishwa na serikali ya Rais Mkapa. Sheria hii ingeweza kufutwa Bungeni lakini kwa kuwa walioko huko asilimia kubwa waliingia kwa muundo huo, licha ya kuwa Rais Kikwete wakati anazindua Bunge la awamu ya nne, kusema kuwa suala la takrima/rushwa litapaswa kujadiliwa na baraza hilo, lakini utaona kuna mkono ulipitishwa haraka kutokea mahakamani ili maamuzi yafanyike kuiondoa Tanzania katika nchi kongwe kabisa kuruhusu rushwa duniani. Hili lilikuwa tukio la kuweka kwenye kumbukumbu kama hili la hivi karibuni la Bunge la Mexico kuruhusu madawa ya kulevya katika nchi hiyo kwa Lengo la kuikomoa Marekani!

Basi kama uliwahi kupitia mapendekezo ya Tume ya Jaji Nyalali kuhusu ubadilishaji wa sheria na katiba hasa vipengele vilivyokuwa vinakwamisha demokrasia nchini utagundua kuwa sasa jua linaanza kuchomoza baada ya hivi juzi Mahakama tena kukubaliana na madai ya Christopher Mtikila aliyoyafungua tangu mwaka 1994 kuhusu kuruhusu wagombea binafsi. Hili ni tukio muhimu sana kufikiwa katika Tanzania na linatanua demokrasia ya hali ya juu na kufanya suala la nafasi za vyama kugeuzwa miungu ya siasa za Tanzania kufutika ama kuelekea katika bahari ya sahau! Wale waliokuwa wanatishiwa kugombea baada ya kuona vyama vinakuwa na mizengwe sasa wanaweza kuungana na jamii yao na hivyo kuwa moja kwa moja watumishi wa umma na sio vyama na kisha wakafanikisha maendeleo ya jamii badala ya sasa kubakia ushabiki wa vyama vya siasa kwanza kabla ya umma.

Mahakama inaanza kutekeleza matukio haya huku kukiwa na kesi inayofunguliwa jumatatu ijayo kuhusu aliyekuwa Mkuu wa Polisi nchini, Omari Mahita, kuhusu kuvunja haki za binadamu na kukihujumu chama cha CUF. Kwa kasi hii tunaanza kupata majibu kuwa watu waliohusika na maangamizi hata ya Janiari 27, 2001 kule Zanzibar wanaweza kufikishwa mahakamani.

Kuna tukio lingine ambalo nitakosea kama nitalisahau leo kwa sababu ya furaha hii ya kupitishwa mfumo niliowaza kuupigania hivi karibuni wa haki za wagombea binafsi. Hivi Mama Mkapa alipofungua NGO kwa jina la taasisi ya ofisi ya umma aliyoikalia kwa nafasi ya yeye kuwa mke wa rais, ofisi iliyokuwa katika jengo la umma, ikilindwa na askari na ikitumia fedha za umma kuiendesha, anawezaje leo kuiambia Tanzania kuwa ile ni NGO yake aliyoibuni? Hivi Watanzania hawaoni kwa macho yao wizi wa fikra na matumizi mabovu ya ofisi za umma kama huu unaotangazwa na Anna Mkapa kupitia EOTF?

Mada hiyo nitaiandikia tena nikipata muda, sitaiacha kabisa maana haiwezekani ofisi za umma zitumike kuwanufaisha wachache kwa vivuli huku jamii ikidhaniwa imelala na haina macho ya kufanya. Kumbuka unajifunza nini kuhusu kashfa za Siti Mwinyi wakati ule Mrema akiwa waziri wa mambo ya ndani, Tena jadili na jirani yako hapo ulipo kuhusu Anna Mkapa na tetesi za kumiliki majumba na mali nyingi nyingi hapo Tanzania tukiwa hatuna taarifa za nje. Je unaweza kufahamu kuwa mali za Rais wa awamu ya tatu, kwa ubainifu ikiwa ni pamoja na hekalu pale Lushoto ni ndogo kabisa kulingana na hizi tetesi kuhusu mkewe? Tunasubiri nini kuanza kujadili hoja hizi bila woga sasa wakati nchi yetu inapoanza kuonyesha kukomaza sekta nyingine zilizo nje ya dola?

INAWEZEKANA WAUNGWANA, CHEZA KARATA YAKO!
 
© boniphace Tarehe 5/05/2006 11:06:00 AM | Permalink |


Comments: 18


 • Tarehe 5/05/2006 11:21 PM, Mtoa Maoni: Blogger Reginald S. Miruko

  Nafurahia kuwa mtu wa kwanza kuleta maoni hapa. Hii ni kwa sababu hata mimi nilitaka kuandika hoja hii leo, lakini sasa nakuunga tu mkono. Acha tu Mtikila aitwe kichaa, lakini si kichaa, ana akili kuliko wanasiasa wengine. Yeye kaamua kutafuta haki mahakamani kaipata mara ya pili. Kwa kesi hii (hukumu) amewakomboa watu wengi, nikiwemo mimi nisiyependa vyama lakini nataka kushiriki uongozi wa nchi yetu kama mwanasiasa. Kwenye vyama kuna unafiki mreeeefu, na demokrasia fiiiinyu sana. Mfano ndani ya CCM, mwenyekiti ambaye ni Rais akishaamua jambo kila mtu anaogopa dola, anafuata. Mfano, hivi sasa Kikwete anawania pekee uenyekiti wa CCM taifa badala ya Mkapa aliyelazimika kustaafu kabla ya muda wake kumalizika, si kwamba wengine hawataki huo ulaji, bali wamebanwa mbavu. Uhuru!

   
 • Tarehe 5/06/2006 3:28 PM, Mtoa Maoni: Blogger Jeff Msangi

  Huu ni ushindi.Nadhani sasa zile ndoto za ukombozi zinazidi kukaribia kuwa kweli.

   
 • Tarehe 5/07/2006 9:12 AM, Mtoa Maoni: Blogger Ndesanjo Macha

  Nami nimeandika kufurahia hukumu hii. NIliandika kabla ya kuja hapa. Hii ni furaha kubwa na kama unavyopenda kusema: Mtikila kacheza karata yake.

   
 • Tarehe 5/08/2006 7:20 AM, Mtoa Maoni: Blogger charahani

  Haiwezekani kabisa jambo hili mkalifurahia peke yenu tu bila ya mimi kushirikiana nanyi, hili ni suala kubwa sana hivyo nami naungana naynyi katika kusherehekea ukombozi huu unaotuondoa katika makucha ya 'mwenzetu'. ili nasi angalau siku moja Ndesanjo akiamua kugombea kwao kule sijui Kiraracha atarudi tu na kufanya hivyo au Makene kule Bumeirafuru nawe unaweza kugombea safi sana hura bado sheria zingine.

   
 • Tarehe 5/08/2006 9:49 AM, Mtoa Maoni: Blogger Michuzi

  mi nasema hiviiii...endapo watanzania wote tungekuwa wapiganaji kama alivyo mchungaji mtikila tungekuwa mbali. ila taarifa niliyopata punde ni kwamba serikali ina nia ya kukata rufaa dhidi ya hukumu ya kuua 'takrima'

   
 • Tarehe 5/09/2006 3:23 AM, Mtoa Maoni: Blogger Absalom Kibanda

  Uamuzi wa kukubaliwa kwa wagombea binafsi kwa hakika kumefungua zaidi mlango wa ushiriki wa kweli wa Watanzania walio wengi katika demokrasia. Sasa hata akina sisi ambao hatuna ushabiki na vyama vyovyote vya siasa, tutapata fursa ya kugombea uwe ni ubunge hata urais.
  Tanzania sasa inaweza ikashuhudia akina Ross Perot wakigombea urais.

  Mchakato wa kumpata mgombea urais ndani ya CCM mwaka jana ni moja ya ushahidi kwamba kweli tunahitaji ruhusa ya kupata wagombea binafsi. Kwa hakika iwapo kungekuwa na ruhusa ya wagombea binafsi wakati ule, basi yale majungu mabaya ya kisiasa, rushwa za wazi wazi, hujuma dhidi ya vyombo vya habari na mambo mengine yanayofanana na hayo tusingeyaona.

  Huenda na mimi binafsi naamini wangetokea watu wengi tu wa kumuunga mkono Salim Ahmed Salim au Malecela katika urais bila kujali alikuwa akiwasilisha maslahi ya chama gani.

  Naamini pia kwamba, ule 'unabii' wa Mwalimu Nyerere kwamba upinzani wa kweli utawezekana iwapo tu CCM itagawanyika, utatimia kupitia ruhusa hii ya wagombea binafsi, kwani wanasiasa wenye uwezo na wanaokwamishwa ndani ya chama hicho kwa sababu tu ya mizengwe watapata fursa ya kugombea ubunge na hata urais kama wagombea binafsi.

  Lakini pia ugombea binafsi utasaidia sana kuisafisha CCM. Naamini kile ambacho Mwalimu alikiita ukokoro wa CCM hatimaye utakufa. KIla ambaye hakubaliani na sera za CCM hatimaye atapata fursa ya kujiandaa kama mgombea binafsi na hata lazimika kujiunga na vyama vya upinzani ambavyo ni dhaifu. Hali hiyo ingekuwapo mapema, watu kama Njelu Kasaka leo hii wasingekuwa wapinzani kwa sababu tu ya kulazimishwa na mfumo kandamizi.

  Kwa sababu hiyo tutarajie kuiona CCM ikiyumba na pengine kudhoofika kama KANU ya siku za mwisho za Moi (si ya sasa ambayo angalau ina nguvu sasa), tutarajie kuona mfumo wa ruzuku kwa vyama vya kisiasa ukibadilishwa, tutarajie kuona rushwa ikipungua ndani ya CCM, tutarajie kuona udikteta wa vyama ukifa kifo cha mende, tutarajie kuona viongozi shupavu wakishinda, tutarajie kuona wabunge hata wale wanaotokana na vyama kama CCM wakiwa na kifua cha kuipinga serikali bungeni bila kujali athari za kupokonywa uanachama kwani hata wakipokonywa wataendelea kubakia na ubunge wao. Hakika Makene na wana Magazeti-Tando sasa tunaelekea kwenda demokrasia

   
 • Tarehe 5/09/2006 12:35 PM, Mtoa Maoni: Blogger MK

  Mimi hapa nina furahi kwa suala la takrima tu lakini ktk swala la mgombea binafsi naona wamechemsha.

  Wamechemsha kwa sababu:

  a: Watapata wapi Sera (manifestos) za maana, Sababu sio wote watakao jua sheria.

  b: Watapata wapi pesa za kuendesha kampeni na ktk uchaguzi au ndio hasara kwa wananchi na pesa zetu za kodi ndio watapewa wao.

  c: Matajiri wengi kama akina Mengi, Wahindi, Waharabu watatumia pesa zao ktk kugombea nafasi mbali mbali na siasa huru itakuwa hakuna.

  d: Kwa mgombea binafsi, atafuata Sera gani na sisi au Taifa tutafuata Sera gani kama wakishinda?

  e: Ukiangalia Mataifa mengi ya Afrika yenye machafuko, Vurugu yanatokana na kuwa na vyama vingi au makundi mengi sana ndani ya nchi au watu wengi kuwa ktk Siasa sasa ongezeko la wagombea binafsi ni kama kukaribisha yote hayo.

  f: Kwa wakati huu tu mambo sio mazuri sana hapo Zanzibar wakati kuna vyama vichache, je ongezeko la wagombea binafsi na wafuasi wao sio kuongeza matatizo sehemu kama Zanzibar au Tanzania kwa ujumla.

  g: Hii System ya wagombea binafsi sio nzuri kwa Tanzania sababu Tanzania ni nchi changa na hatuja komaa kisiasa labda hapo baadae sana tena sana. System hizi ni nzuri na sawa kwa nchi zilizo endelea.

  Tunabidi tuangalie ni wapi tunaelekea watanzania na tuweze kutetea yaliyo mazuri kwa wote tusije tukaleta machafuko kwa sababu za wagombea binafsi.

  Nasubiri kwa hamu kwa Serikali kukata rufaa kuhusu wagombea binafsi maana kwa kuangalia mbali tu naona moto unatufuata.

  Mwisho, Siungi mkono suala lolote la wagombea binafsi kwasababu nchi yetu bado haipo tayali kwa hilo kwa sababu ni changa kisiasa na changa kwa maendeleo inabidi tuwaze na kuweka misingi sahihi kwa masuala mengine na sio hili.

  Haya yalikuwa ni mawazo yangu binafsi na sio lazima yawe sahii kwa wasomaji wengine.

  Nashukuru,
  ©2006 MK

   
 • Tarehe 5/10/2006 3:28 AM, Mtoa Maoni: Blogger tamba

  Mtikila japo kuwa simfagilii, lakini historia ya nchi itamkumbuka. Mtume hasifiwi kwao, ni mtetezi kweli wa haki za wanyonge na sheria zinazokandamiza

   
 • Tarehe 5/10/2006 11:26 AM, Mtoa Maoni: Blogger Ndesanjo Macha

  Kuna ukurasa wa wikipedia ya kiswahili wa Mtikila. Yeyote anaweza kujazia:
  http://sw.wikipedia.org/wiki/Christopher_mtikila

   
 • Tarehe 5/10/2006 11:29 AM, Mtoa Maoni: Blogger Ndesanjo Macha

  Masuala ya haki za msingi sidhani kama yanahitaji muda. Unajua tukisema kuwa eti hatuwezi kuwa na wagombea binafsi maana nchi yetu bado changa ni sawa na kusema tusiwe na uchaguzi wa wabunge na rais maana nchi yetu haina nguvu kubwa za kiuchumi hivyo hakuna fedha za kugharamia uchaguzi.
  Mahakama ilichofanya ni kutafsiri katiba. Katiba ndio sheria mama, mambo mengine kama sijui nchi yetu ni changa, hatujakomaa kisiasa hayana nguvu za kisheria. Katiba yetu inaruhusu mtu yeyote aliye raia kugombea nafasi yoyote ya uongozi au kuchagua kiongozi.

   
 • Tarehe 5/11/2006 1:33 AM, Mtoa Maoni: Blogger MK

  Vyama vilivyopo sasa vimeshindwa kuleta maendeleo na kuondoa Umasikini wa watanzania karibia Million 33 na hapo hapo kuna baadhi ya hivyo vyama havina misimamo na kuna wakati vina amua kuleta fujo (Vurugu) ndani ya nchi au vingine vinazunguka dunia nzima na kuomba wazamini wetu waweze kutunyima misaada, Je unadhani ya kwamba kuleta hii njia ya wagombea binafsi italeta suluhisho ya hayo matatizo tuliyo nayo? Au ndio kwanza italeta kutokuelewana ndani ya nchi?

  Katika maoni yangu hapo juu nilizungumza ya kwamba sio wote wanao jua sheria sasa je wataweza vipi kutunga sheria zao? Na wakishinda nchi itafuata sheria gani?

  Je watapata wapi pesa za kuendesha kampeni au kulipia gharama zote za chaguzi? Au ndio kodi yetu watanzania watapewa wao kuendesha hizo chaguzi? Auoni ya kwamba wengi wao watajiita wagombea binafsi ili kujitafutia pesa na baadae kushindwa (Kwakua wanajua watashindwa).

  Tunamuita Mtikila kama mkombozi wa watanganyika au vyovyote vile, kama kweli ni mkombozi kwanini alishindwa kupiga kura mwaka jana badala yake alikuwa marekani? Je kwanini akuonesha mfano?

  Ukweli utabaki ya kwamba Tanzania ni nchi changa kwa maendeleo na Kisiasa sasa ni sisi wenyewe kizazi cha sasa kujifanya kwamba Tanzania ni sawa sawa na Marekani kwa maendeleo na ukomavu wa Siasa.

  Kuwa na Wagombea binafsi wengi ni kurudisha nyuma maendeleo yetu maana kutakuwa hakuna siasa ya kweli na ndio mwanzo wa kuleta Vurugu ndani ya nchi. Angalia dunia nzima ambayo ipo machoni mwetu na utaona kwamba nchi zilizo na fujo au matatizo yanatokana na kuwa na idadi kubwa ya vyama au wagombea kama sisi.

  Siku zote waenga walisema mtoto akililia wembe mpatia umkate na atajifunza baadae, Na muombe baadae isiwe mbali sana sababu hiki hiki kizazi kitajuta na maamuzi mnayo yaweka hivi sasa.

  Mlilia vyama vingi na mkaleta vyama visivyo eleweka sasa ona Zanzibar ilivyo, imeshakuwa donda ambalo hakuna wa kulitibu na hapo hapo kuna donda ndani ya Zanzibar yenyewe, Wengine wameshaanza kudai Muungano sio wa haki, Wengine ni Viongozi wakubwa wanataka katiba ibadilishwe wazidi kukaa madarakani.

  Kuweza kuona haya sio lazima uwe na Phd, Degree au Masters bali ni kuweza kuangalia mbali kwa manufaa ya Taifa na wananchi wake.

  Kwa Manufaa ya Taifa na wanchi wake ningeiomba Serikali ipinge hii hukumu (Kukata rufaa) ili kuliweka Taifa mahali salama.

  Mtikila na wengine wote wanao kubali mambo ya mgombea binafsi sio watu wanao itakia Taifa yale yaliyo mema na ndio hao wanataka Serikali Tatu.

  Mwisho, Taifa letu ni Changa sana tena sana kwa mambo ya wagombea Binafsi na tunabidi kuwekeza nguvu ktk kuleta maendeleo na kuondoa umasikini. Kuna mambo mengi tunabidi kufanya mwanzo na ndio tufuate haya ya wagombea binafsi.

  Mtakuja kujibu maswali hapo baadae maishani wakati vizazi vyetu vikija kutuuliza kwa nini tulifanya hivi? Na hapo ndio mtatafuta majibu.

  Haya yalikuwa ni mawazo yangu binafsi na sio lazima yawe sahii kwa wasomaji wengine.

  Naomba niishie hapa nisije kuandika yasiyo takiwa kuandikwa.

  Nadhani sitokuwa nimewaudhi baadhi ya wasomaji wengine, Kama mtakuwa mmeudhika kwa yote nawaomba mniwie radhi.Ukweli utabaki ukweli.

  Nashukuru,
  Copyright 2006 MK. All rights reserved

   
 • Tarehe 5/11/2006 3:21 AM, Mtoa Maoni: Blogger Ndesanjo Macha

  MK: umesema kuwa vyama vilivyopo hivi sasa vimeshindwa kuondoa umasikini. Kumbuka kuwa vyama vingi viliruhusiwa mwaka 1992. Na toka mwaka huo hakuna chama chochote kipya kilichoingia madarakani. Chama kinachotuongoza sasa ndio kimekuwa kikituongoza miaka yote. Kwahiyo kama umasikini haujaondolewa Tanzania hakuna uhusiano wowote na vyama vingi. Kiulize chama ambacho kimekuwa kikituongoza kupitia marais wanne.

  Ni kweli kuwa vyama vingi havina msimamo wa kueleweka. Hatuwezi kutumia sababu hii kusema kuwa hakuna haja ya kuwa na siasa ya vyama vingi. Kwanza vipo vyama vyenye msimamo. Pili, vyama hivi vimeanza majuzi, havina fedha au uzoefu wa kutosha. Ukivitazama baadhi ya vyama utaona kuwa vinapitia kwenye hatua mbalimbali za kukua na kukomaa. Viko ambavyo vitachukua muda mrefu, vingine muda mfupi, vingine vitakufa…yote hii ni moja ya mambo ambayo lazima yatokee kwenye demokrasia inayokua. Haya sio mambo ya kututisha na kutufanya tuseme kuwa vyama vingi ni chanzo cha mgogoro ndani ya nchi.

  Halafu wakati mwingine tunasahau kuwa sio vyama vya upinzani tu ambavyo havina msimamo. Hata chama kinachotawala kuna wakati huwezi kujua msimamo wake. Kwa mfano, hadi leo CCM inatuambia kuwa ujamaa na kujitegemea ndio njia pekee ya kujenga jamii ya watu walio sawa na huru. Huu ni uongo. Lakini pamoja na uongo huu hatuwezi kusema kuwa tusiwe na vyama. Haya ndio mapungufu ambayo tuna jukumu la kuyaondoa. Sio kukimbia.

  Sioni uhusiano wa wagombea binafsi na kutolewana ndani ya nchi. Sababu kubwa ambazo zinachochea na zitaendelea kuchochea kutoelewana ndani ya nchi hazihusiani na wagombea binafsi. Sababu ni kero ambazo hazijapatiwa ufumbuzi. Kwa mfano, tazama suala la Unguja na Pemba. Tazama yanayotokea Zanzibar kila wakati wa uchaguzi.

  Kuna uthibitisho gani kuwa nchi ikiwa na wagombea binafsi (KAMA KATIBA YA NCHI INAVYORUHUSU) kutakuwa na fujo nchini?

  Umeuliza:
  Katika maoni yangu hapo juu nilizungumza ya kwamba sio wote wanao jua sheria sasa je wataweza vipi kutunga sheria zao? Na wakishinda nchi itafuata sheria gani?

  Sijaelewa vizuri swali lako. Ninachojua ni kwamba wabunge ni watunga sheria ingawa sio lazima wajue sheria au wawe wanasheria. Swali la pili umeuliza wagombea binafsi wakishinda nchi itafuta sheria gani. Jibu ni rahisi: katiba ndio sheria mama ya nchi (haijali aliyechaguliwa ni mgombea binafsi au la). Sio kazi ya rais au mbunge kuamua kuwa sheria gani zitafuatwa. Katiba tayari inatoa maelekezo juu ya sheria za kufuata na iwapo kuna sheria za kubadilishwa, katiba hiyo inatupa mwongozo wa jinsi ya kubadilisha au kutunga mpya. Kwahiyo suala la sheria ya kufuatwa sio maamuzi ya mtu binafsi.



  Umeuliza wagombea binafsi watapata wapi fedha za kampeni? Jibu litapatikana tukiweza kujibu, je wagombea wenye kofia za vyama wanapata wapi fedha za kampeni?

  Umeonyesha kuwa na wasiwasi kuwa wagombea binafsi wanaweza kutumia mwanya huo kujinufaisha binafsi kifedha. Mbona kuna wagombea wenye kofia za vyama ambao wanatumia ugombea wao au uongozi wao kama mwanya wa kujinufaisha? Tamaa ya kujinufaisha na kuiba mali ya umma anaweza kuwa nayo mtu yeyote. Awe wa chama cha upinzani, chama tawala, au awe mgombea binafsi. Jibu la wasiwasi wako ni kuwa sheria na sera vinaweza kutumika kuzuia wagombea kutumia fedha za kampeni vibaya. Dawa sio kuadhibu wagombea binafsi kwa makosa ambayo “tunadhani” kuwa watayafanya wakati makosa hayo tayari yanafanywa na wagombea wa vyama.

  Ningependa ufafanuzi zaidi na mifano kuhusu hoja yako kuwa fujo na matatizo katika nchi nyingi duniani yanatokana na idadi kubwa ya vyama. Tazama Somalia. Somalia nchi ile wanaongea lugha moja, wana dini moja, na wakati wa Siad Barre walikuwa na chama kimoja. Ningependa kujua ni vipi matatizo, vita, na fujo katika nchi kama Indonesia, Cambodia, Iraki, Chechnya, Bosnia, Ireland ya Kaskazini, Hispania, Liberia, Sierra Leone, Nepal, n.k. yametokana na idadi kubwa ya vyama.


  Kuhusu donda la Zanzibar. Nitasema kwa kifupi tu: donda lile halitokani na vyama vingi. Tukisema kuwa chanzo cha matatizo ya Zanzibar ni idadi ya vyama tutakuwa tumerahisisha sana uchambuzi wa mgogoro ule. Hivi unadhani kuwa chanzo cha mgogoro ule ni vyama vingi? Sio. Kama vyama vingi ndio chanzo, Bara nako si kuna vyama vingi? Mbona hakuna aina ya migongano tunayoiyona Zanzibar?

  Mwisho, sidhani kama kuna haja ya kuomba msamaha kwa kutoa mawazo yako. Kama mtu anaudhika kwakuwa mtu mwingine katoa mawazo yake, tatizo sio lako bali ni la yule aliyeudhika. Yeye ndiye aombe msahama!

   
 • Tarehe 5/11/2006 4:38 AM, Mtoa Maoni: Blogger MK

  Naheshimu mawazo yako, Hayo yalikuwa mawazo yangu tu na sio lazima yaendane na ya kwako.

  Nadhani sitokuwa nimewaudhi baadhi ya wasomaji wengine, Kama mtakuwa mmeudhika kwa yote nawaomba mniwie radhi.Ukweli utabaki ukweli.

  Nashukuru,
  Copyright 2006 MK

   
 • Tarehe 5/11/2006 6:57 AM, Mtoa Maoni: Blogger Ndesanjo Macha

  Sidhani kuwa kuna ulazima mawazo ya watu yote yaendane. Huu ndio msingi wa mijadala. Maana kama mawazo yetu wote lazima yafanane basi kunakuwa hakuna haja ya mijadala wala hakutakuwa na haja ya watu kutoa mawazo. Kitendo cha mawazo yetu kutofanana ndio hasa kinaleta umuhimu wa kujadiliana, kuelimishana, na kutafuta ukweli.

  Njia mojawapo ya kupata ukweli na kuelimishana ndio hii ya kutoa hoja na mawazo yetu bila wasiwasi kuwa kuna watu wengine hawatapenda mawazo yako au hawatakubaliana nawe. Tunaweza kujadili na kuweza kufikia hatua ya kukubaliana au kukubali kutokukubaliana.

  Kama kuna watu ambao wanaudhika kwakuwa umetoa mawazo wasiyokubaliana nayo, watu hao watakuwa wanataka wawe na haki ya kuwa na mawazo na fikra fulani ila hawataki haki za wengine kuwa na mawazo na fikra tofauti na zao. Hawa tunaweza kuwasaidia pia kwa mijadala.

  Mjadala huu naaamini kuwa una faida kubwa kwetu kama taifa na wanablogu. Ningependa wanablogu tuuendeleze. Makene: umesema kuwa ukipata muda utauendeleza. Tunasubiri.

   
 • Tarehe 5/12/2006 11:53 AM, Mtoa Maoni: Blogger Michuzi

  nafuatilia mjadala kwa makini, japosijachangia. naomba kuuliza wenzangu kuhuhusu minong'ono inayodai ati mtikila anatumiwa; kwa mfano katika hii hoja yake mpya ya kupeleka mahakamani taasisi za mifuko ya jamii kwa kukiuka katiba. sina nia ya kupindisha mjadala, ila ni kutaka semi zenu juu ya hizo tetesi zinazoambatana na maswali ya ni wapi mtikila anapata pesa za kuweza yote hayo. naomba kuwasilisha

   
 • Tarehe 5/14/2006 3:18 AM, Mtoa Maoni: Blogger Indya Nkya

  Kwamba Mtikila anatumiwa na nani sijuhi. Kam anatumiwa na kisha kuleta mabadiliko mazuri si mbaya. Lakini kama anatumiwa halafu tena kesho Serikali itafute sababu ya kuzima maamuzi ya mahakama basi itakuwa kasheshe. Tungoje tuone hawa watu wasio na aibu watakapopinga sheria ya takrima.

   
 • Tarehe 5/19/2006 4:59 AM, Mtoa Maoni: Blogger Rashid Mkwinda

  Pamoja na mchango wa wachangiaji wengi katika blogu hii juu ya ushindi wa Mtikila, binafsi naona ni sawa na kutiwa mchanga wa macho tu kwani kuwepo kwa wagombea binafsi, mgombea mmoja, chama kimoja ama vyama 100 sioni mabadiliko yoyote, awali tulidhani uwepo wa mfumo wa vyama vingi utakuwa ni ukombozi kwa wanyonge na walalahoi, lakini kinyume chake ikawa ni kizungumkuti cha kubadilisha misemo ya kiswahili, Rushwa kuitwa TAKRIMA ili mradi waliopo katika mfumo wabalki pale walipo hadi Nabii Issa(Yesu) arudi.

  Wadanganyika hatuwezi kudanganyika kwa kupewa pipi kama watoto wadogo, hii yote ni michakato isiyo manufaa yoyote kwa mtu wa hali ya chini ambaye hajui atakula nini, atamsomeshaje mtoto wake hadi kiwango cha juu,atamudu vipi angalau apate kibanda cha kujihifadhi,huu ni ubabaishaji.

  Angalia ardhi tuliyonayo inauzwa kwa wawekezaji wa nje ilhali, wadanganyika wanaitwa ni wachimbaji wadogo wadogo huko Mererani, Chunya, Nyarugusu, Geita, Mwadui na kwingineko.

  Mie naona kuwepo kwa mgombea binafsi, wagombea wa ndani ya vyama vya siasa hata wakiwa 101 hawana maslahi na wadanganyika walio wengi,kinachoendelea ni mchezo fulani wa SIHASA chini ya anga la nchi ya Wadanganyika tutaghilibiwa weee!!!!! hadi tukome.

  Mbona basi hatubadiliki?tukabadilisha mfumo wa uongozi ili kama kweli tunakerwa na ukiritimba wa ubabaishaji uliopo ndani ya mfumo wa chama kimoja?

  Ngoja niishie hapa naona kama vile sijafungwa luku natiririka bila breki.

  WAKATABAHU

   
 • Tarehe 5/19/2006 6:44 AM, Mtoa Maoni: Blogger Absalom Kibanda

  Nimerudi kidogo katika hoja hususan mchango wa ndugu yangu Michuzi. Ni kweli kuna maneno ya chini chini yanasema kwamba huyu Mtikila anatumiwa tu. Hilo laweza likawa la kweli au la uongo, lakini sisi la msingi ni hoja na si mtu.

  Kuna mtu mmoja alipoambiwa kuhusu kutumiwa kwa Mtikila alisema hapana, Mtikila hatumiwi ila anatumwa au anawakilisha maoni ya watu wenye wenye mtazamo kama wake.

  Kinachoonekana hapa ni kwamba, Mtikila awe anatumwa au anajituma au hata kutumiwa, lakini ukweli ni kwamba wako watu wengi ambao wanaunga mkono hoja yake. Kumbuka kwamba hata mwana CCM nambari Moja, Mwalimu Nyerere alikuwa akiunga mkono hoja ya mgombea binafsi na kwa sababu hiyo basi isingekuwa ajabu iwapo angesikia kwamba kuna mtu amefungua kesi ya namna hiyo mahakamani basi angemuunga mkono na pengine kuchangia.

  Naamini kuna watu wengi wanaounga mkono hoja ya Mtikila na hao ndiyo wanaokuwa tayari kuchangia kiasi chochote cha fedha kwa ajili ya kufanikisha kesi za namna hiyo na usije shangaa kusikia kwamba miongoni mwa wanaomuunga mkono wako ndani ya CCM.

   
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved