Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Wednesday, May 24, 2006
NANI ANAZUNGUMZA UKWELI KUHUSU HABARI ZA AFRIKA? (3)
MIAKA mingi imepita tangu Tanzania ikiwa na chuo kimoja cha Uandishi Habari, chuo ambacho kilitoa elimu iliyoishia kiwango cha stashahada. Siku hizi kuna utitiri wa vyuo vinavyofundisha uandishi wa habari. Vipo vinavyotoa shahada pia lakini bado kuongezeka kwa vyuo hivi hakujaleta mapinduzi katika fani ya uandishi ili kuifikisha sehemu ya kuaminika kama mhimiliwa nne katika nchi.

Kazi za uandishi wa habari zimeongezeka lakini uendeshaji wake umebakia wa kubabaisha kutokana na sababu kadhaa. Kubwa ni kukosekana kwa utashi wa waandishi wenyewe katika kujenga taswira yao, hapa nazungunmzia suala la mwandishi kujijengea uwezo yeye kama yeye katika fani hii. Na pili, vyombo vya habari kutothamini sana ubora wa kazi zaidi ya kutaza faida ya soko badala ya misingi na miiko ya kazi za uandishi wa habari kama taaluma na fani yenye miiko, maadili na sheria zake.

Huku ughaibuni vyombo vya habari vinajitanua zaidi na kuongeza majukumu hali inayotanua wigo wa kazi za waandishi wa habari. Vyombo hivi havimalizii habari katika kuichapa gazetini au kuirusha redioni na kwenye televisheni tu; vinachapa vitabu, vinashiriki kutengeneza filamu na matukio mengine ambayo hutanua mapato ya kampuni, mapato ya waandishi na pia kujenga jamii ya watu wanaothamini kusoma na kutunza kumbukumbu za mambo. Tanzania bado waandishi wetu wamebaki wengi kuandika hotuba au ripoti wanazozisikia zikitolewa na viongozi au watu wenye kutengeneza habari na mara nyingi hawana nafasi hata ya kuhoji aina ya ripoti na hotuba hizo, wanafanya kazi ya kujaza kurasa za magazeti au kutosheleza dakika za redio na televisheni zao kwenda hewani.

Habari nyingi siku hizi zimekosa radha, zimekosa kuonyesha jitihada za mwandishi kuchimbua na zimebakia kushabikia, kupongeza, kusifia na kushutumu! Utasoma habari kwa mfano, rais alisemani mawaziri 33 tu kati ya 60 wanaohitaji nyumba na habari kuwa serikali inatumia mamilioni kuwaweka katika hoteli inapotosha ukweli,” alisema. Mwandishi anaishia hapo na hawezi kufunua kinywa kuhoji ata hao wametumia kiasi gain kuishi mahotelini na nini kiliwafanya kuishi hoteli za anasa huku wamezaliwa katika nchi hii hii ya Tanzania na wanaishi maisha ya chini tu, nini hasa chanzo cha wao kuvaa gwanda jipya la kutamani maisha ya anasa huku wanaongoza nchi maskini.

Bado utakutana na habari kama, serikali imeidhinisha mikopo ya bilioni za shilingi kwa ajili ya Wabunge na kuwataka wanunue magari yatakayoweza kuwafikisha kutembelea wananchi wao jimboni. Waandishi wetu wataishia kuandika hapo bila kuingia ndani zaidi kutaka kujua magari ya aina hiyo yatakayowawezesha wabunge kuwafikia wananchi ni aina ipi na yanahitaji gharama kiasi gani? Tena hutasikia swali kuhusu mikopo hiyo kutolewa wakati nchi ikiwa bado na njaa, au je mikopo ya aina hii itaishia kwa wabunge tu au itatanuliwa na kwa wananchi wengine maana ukilinganisha uwiano wa msamaha wa mikopo hiyo hasa sehemu ile inayolipwa na serikali, hakukuwa na haja tena ya mbunge huyo tena kupewa kiinua mgongo chake cha milioni nyingi za shilingi baada ya miaka 5 na tena kuna haja gani kugawa pesa bure kupewa wabunge wanaolipwa mishahara mikubwa tu huku Bodi ya mikopo ya wanafunzi wa vyuo vya juu ikishindwa kutoa mikopo kulingana na mahitaji ya wanafunzi!

Nafasi ya gazeti ni ndogo mno na kamwe haiwezi kukidhi matakwa ya mwandishi hasa ikifika sehemu ya yeye kutoa maoni yake na namna anavyodhani jambo fulani laweza kubadilishwa na kuleta mafanikio ya nchi. Wajumbe wa Kongresi ya Marekani mara kadhaa wametumia habari za magazeti katika kutetea hoja zao au kuthibitisha kile wanachokizungumza.

Sababu ya hawa kufikia hatua hii ni kutokana na waandishi kuthamini kazi zao na kuzifanya kwa ukamilifu. Waandishi anatambua majukumu yao hasa na wanajivuna pale wanapoweza kuchimbua jambo na kulianika hadharani. Katika nchi zetu bado kuna matatizo yanayoendana na waandishi kuwa katika orodha ya malipo ya baadhi ya wakuu serikalini au kuamua kwa makusudi kushangilia upande mmoja bila kutambua madhara ya ushabiki hasa ufanywapo na waandishi wa habari.

Mbunge wa kipindi cha nyuma wa Temeke, Augustine Mrema aliwahi kutumia nukuu za magazeti kama ushahidi wa hoja zake Bungeni. Katika tuhuma zile hakufanikiwa kushinda na aibu haikuwa kwa Mrema pekee, ilienda hadi kwa vyombo vya habari alivyovipeleka Mrema kama msingi wa ushahidi wake.

Je vyombo vile vilijiuliza kuhusu kudharauliwa kwa taarifa zao ambazo Mrema alizitumia kama ushahidi wa kutetea hoja yake? Havikujali kabisa, lakini kama hoja hizo zingepokelewa na Mrema kuonekana kidedea hakungekuwa na namna vyombo hivyo vingetaka kujikuza kwa wasomaji kuwa vinafanya kazi nzuri ya kuchunguza mambo kwa kina?

Upo ukweli kuhusu hoja hiyo hapo juu na kweli vyombo vya habari vinahitaji sana kulisaidia bara la Afrika kuonekana nje huenda kwa habari ambazo hatuzipendi na pia zile tunazozipenda. Ni namna moja tunaweza kufanya hivi hasa pale tutakapokuwa na habari mbadala kuhusu matukio ya bara letu.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe Darfur nchini Somalia viko Afrika. Kuna vyombo vingapi vya habari nchini Tanzania ambavyo vimepeleka waandishi wake kuchukua habari hizo? Je mbona habari hizo zachapishwa katika magazeti zikitokana na tafsiri ya habari zilizoandikwa na wageni?

Kweli hakuna uwezekano wa waafika wenyewe kwenda huko na kuandika habari hizo na kuwatumia wageni ili waweze kupata taarifa sahihi zisizo na makosa sana, taarifa zinazoweza kusaidia kufikia ufumbuzi wa mgogoro huo haraka? Hii ni sehemu ya hoja yangu na inaonyesha namna vyombo vyetu vinavyobaki kuwa tegemezi hata katika mambo yetu wenyewe!

Mapema mwanzoni mwa mwaka huu tulipata kutembelewa na Bob Woodward, mwandishi mashuhuri katika habari za uchunguzi aliyefanikiwa kuandika habari zilizomng’oa Richard Nixon katika urais wa Marekani mwaka 1974. Bob Woodward licha ya kuwa bado ni mwandishi sasa, anajishughulisha zaidi na uandishi wa vitabu na kampuni yake inamtumia sambamba na waandishi wengine kuandika vitabu vya uchunguzi wa matukio mbalimbali yanayotokea Marekani na nje ya Marekani.

Mauzo ya vitabu huku yapo juu na gharama za vitabu ni kubwa tu. Je nini kinafanya Afrika vitabu visiuzike na nani aliwaambia waafrika wasipende kusoma. Mustapha Puja ni mhariri katika kampuni moja ya uchapaji hapo Tanzania. Nilizungumza naye siku za hivi karibuni kuhusu namna ya kuweza kuchapa kazi yangu katika kampuni hiyo anayofanyia kazi.

Nilipomgusia kuwa kazi yangu ni riwaya, akaniambia kampuni hiyo haiwezi kuchapa kazi hiyo labda iwe imeandikwa na Profesa au mtu mwenye shahada ya Daktari ya Falsafa. Nilicheka kidogo maana nilitazama kuwa Shaaban Robert licha ya kutokuwa na elimu kama hii niliyonayo mimi, ameweza kuwa na maandishi ambayo maprofesa wengi hawatawahi kukaribia hata nusu yake.

Je huyu naye angenyimwa kuchapishiwa kazi na Waingereza tungekwa tunasoma kazi za nani? Kwa nini tusibaini kuwa soko la usomaji huanza pale kunapokuwa na machapisho mapya kwanza?

Vitabu vyetu vingi hata vilivyo katika mtaala wa elimu ni vya kipindi cha nyuma mno. Kwa ujumla haviendani na wakati huu tunaoishi sasa na hakuna mkakati wa kubadili vitabu hivyo kutokana na sababu kadha wa kadha moja ikiwa machapisho finyu na pili kile kinachozungumzwa kuwa utamaduni wa kusoma kutokuwepo.

Kama hatuwezi hata kusoma mambo yetu wenyewe hali inayowakwaza watu kutoandika tutarajie nani aweze kutoa taarifa bora kabisa kuhusu maisha yetu? Narudi katika mada yangu, Afrika yote yafanana kabisa, kutokusoma na kupenda mambo kwa njia za panya kunaathiri sana hata mfumo wetu wa elimu.

Katika muswada wangu wa “Barua kwa Mama” nimejadili ndoto niliyokuwa nayo kabla sijaingia chuo kikuu. Niliamni nikihitimu hapo nitakuwa gwiji wa kutambua maandishi ya juzuu na juzuu, jambo ambalo sikufikia matarajio yake. Sikufikia chembe ya matarajio yangu kutokana na sababu kadha wa kadha na moja kubwa ni hiyo tabia ya kutaka kufanikiwa kupitia njia za panya, kushinda mitihani bila kusoma au kusoma maandishi yale yanayodhaniwa kutoka katika mitihani pekee.

Kuna uandishi mpya wa vitabu nchini Tanzania umeingia ambao unatazama sana suala la kuwawezesha wanafunzi kushinda mitihani. Kuna vitabu vingi siku hizi vyenye maswali na majibu na hivi ndivyo hupata kuchapwa haraka na makampuni ya uchapaji ya nyumbani.

Vitabu hivi hununuliwa sana maana wanafunzi wetu hawana haja na maarifa bali kufaulu mitihani kwa namna yoyote hata kwa kuiiba kabisa ikiwezekana. Kama kizazi hiki kinalelewa hivi utawezaje kukipambanisha na vizazi vya nchi za ulimwengu wa kwanza ambavyo vinafundishwa kwa umakini na kutambua maana ya kusoma na kujenga fikra za kutambua kila jambo?

Je hatuoni kuwa inawezekana kabisa kuwa mtu anayeishi Afrika akasoma katika elimu ya muundo huu, siku akikalishwa kitako na mwingine aliye ughaibuni na kujadili mambo ya Afrika kuwa inawezekana kabisa kuwa mtu wetu akaonekana hana hata taarifa za kutosha kuhusu masuala ya eneo analoishi?

Vyuo mbalimbali Marekani vina idara inayohusu masomo ya Afrika. Sijawahi kusikia masomo hayo yakitolewa huku Afrika na mjadala huu umekuwa ukitanuka sana huku. Kwa nini viongozi wa Afrika wasijenge vyuo vya kutoa masomo haya ili wasomaji kutoka nje wafike Afrika kuchota maarifa ya Afrika. Je hatuoni kuwa kesho ni rahisi kuwa na wataalamu wanaoifahamu Afrika zaidi kuliko sisi wenyewe kama htuna mikakati ya ziada kukabiliana na hili. Unadhani nani atakuwa na habari njema za Afrika kama hawa wanazisoma kabisa na sisi tunaishia kuzitazama, mjadala huu wa nani anafahamu habari za Afrika zaidi ni mpana mno. Hauna mwisho ila unatoa taswra ya nini Afrika ifanye na kuachana na tabia ya kulia na kulalama kwa kila jambo.
 
© boniphace Tarehe 5/24/2006 09:49:00 AM | Permalink |


Comments: 4


 • Tarehe 5/25/2006 2:30 AM, Mtoa Maoni: Blogger zemarcopolo

  umegusa mahali muhimu sana makene.hili tatizo la vyombo vyetu yza habari ni kubwa sana.pamoja na usahihi na utafiti pia kumejitokeza matumizi ya lugha za ajabuajabu katika habari za maana.kwa mfano nilisoma kichwa cha habari SALIM AULA wakimaanisha kuwa amepewa jukumu la kushiriki katika mgogoro wa Darfur.sasa hii ina madhara sana kwa jamii ingawa inaonekana kama ni utani tu,ila kwa lugha nyingine unawaambia watu kuwa cha muhimu ni KULA!!!na ndio maana kijana wa kitanzania sasa hivi anafikiria ulaji tu na ulaji wa kula leo sio kujenga nchi kwa manufaa ya kizazi kijacho na cha sasa.mwandishi wa jkawaida nchini anaandika habari ambayo ameitwa kupewa kwenye semina,mikutano nk.ndio maana hata ukifungua leo ippmedia.com utakuta habari ya mambo aliyosema IGP kwenye mkutano nk.kiini cha yote haya ni umasikini na tatizo kubwa la mtanzania wa leo anafikiri kuwa kuwa masikini ni kigezo cha kuwa na kiwango duni na hii inapelekea watu kufikiria kimasikini.na mtu anayefikiria kimasikini siku yote atabaki masikini mpaka atokee masiah wa kumfungua ubongo.swali,je huyo masiah atatoka wapi?ni lazima miongoni mwetu kuwe na masiah kwa sababu wale wasio miongoni mwetu wanafurahia uzumbukuku wetu.wao kwao ujinga wetu ni biashara nzuri,tena nzuri sana.utani ni pale jinsi mtanzania anapoambiwa ukweli na mtanzania mwenzake......hakubali anaona sio kweli,mtanzania kwa sababu ambazo mimi sizielewi anapenda kusikia kutoka kwa wageni kuliko toka kwa wenzake!!!!!kazi tunayo!!

   
 • Tarehe 5/26/2006 7:16 AM, Mtoa Maoni: Blogger mwandani

  Hii habari ni kweli kabisa, saa nyingine utamaliza kusoma bila kuelewa sababu iliyomfanya mwandishi kuchapa hiyo habari/maelezo/soga hata sijui niyaite vipi.

  Nafikiri pia wakati umefika, wa kuahamasisha umma kubadili mitizamo. Tumepotoka sana kiasi hatuwezi kujitupa kwenye mambo ya uandishi huo unaousema, siyo kwa sababu nyingine yoyote bali bado tuna tongotongo fulani. Kwanza msudani akijua kuwa mwandishi ni mwafrika wa afrika hata kumpa viza ya kwenda huko Dafur itakuwa ngumu.

  makala hii imenifanya nikumbuke habari ya watumishi waliopewa talanta kwenye biblia. Na siye tusipojitahidi kuongeza kutokana na tulichonacho tutazidi kubaki kama tulivyo.

   
 • Tarehe 5/29/2006 10:26 AM, Mtoa Maoni: Blogger Ndesanjo Macha

  Huyu Mustafa Puja aliyekataa kuchapa kazi zako kwakuwa huna PhD amelewa mvinyo ambao unafanya watu wengi kudhani kuwa mtu anayeitwa "msomi" anajua kila kitu na wale ambao sio "wasomi" hawana lolote la kusema. Watu kama Puja wanadhani elimu inapatikana tu darasani. Mtazamo huu una historia yake na ulijengwa kwa nia ya kujenga matabaka na kulimbikiza madaraka mikononi mwa wale wanaotumia miaka nenda rudi kusoma mambo yaliyoko katika vitabu vya wale wanaotutawala kiuchumi, kiutamaduni, kiimani, na kiakili.

  nenda vijijini ukaongee na wazee ambao hawajaenda shule utashangaa mambo wanayojua bila kupitia mfumo wa ujinga (yaani mfumo wa elimu).

  Mtazamo huu kuwa wasomi ni daraja la juu ndio unafanya waandishi kupenda kwenye kuwahoji hao "wasomi" kisha wanakuja na kichwa cha habari kisemacho, "wasomi wamkubali Kikwete." Inakuwa kama vile kauli ya msomi ni kauli ya mola.

  Nadhani blogu zinatupa nafasi ya kuonyesha mapungufu ya vyombo vya uongo ambavyo vinatupa habari ambazo wakati mwingine hujui mwanzo wala mwisho. Vyombo hivi ni kwaya za mapambio. Mapambio ya kuwasifu viongozi (ili waandishi hao waonekana mali kwa hao viongozi) na mapambio ya kuwasifu wanaomiliki vyombo hivyo.

  Tuna kazi kubwa sana mbele yetu. Uzuri ni kuwa kazi yenyewe inafanyika. Haihitaji watu toka sayari za mbali. Ni mimi na wewe. Na tutaifanya. Sio lazima tuimalize, wako wanaokuja nyuma yetu.

   
 • Tarehe 5/30/2006 9:18 AM, Mtoa Maoni: Blogger Jeff Msangi

  Makene,
  Ni dhahiri kwamba umedhamiria kwenda sambasamba na kauli mbiu yako ya ukweli daima,uongo mwiko.Usemayo hapa ni zaidi ya ukweli.Mapinduzi ya kijamii tunayoyaota yanagusa sana nyanja kama hizi.Elimu yetu tunaitafsiri visivyo huku tukikenua meno kama ngiri kwa hisia kwamba tumefika.Nadhani tunaenda vizuri kama tukiwaza pamoja nawe.Makala safi sana hii.

   
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved