Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Friday, May 26, 2006
KIKWETE SUALA SI KUTOUZA TENA NYUMBA BALI KUREJESHA ZILIZOUZWA!
NAKUANDIKIA waraka huu ikiwa ni moja ya kazi nilizojiwekea. Nakuandikia ikiwa ni kuongeza msisitizo wa imani yangu na msimamo wangu kuhusu suala la kuuzwa kwa nyumba za serikali, suala nililolipa nafasi katika Muswada wa Kitabu changu pia. Nakuandikia kuwa na wewe ulisema ulijigawia nyumba ya serikali na sasa nakukumbusha kuwa suala si kutouza hizi zinazojengwa sasa, nakukumbusha kuwa zinatakiwa nyumba zote kurejea na huu ni msimamo wangu na watanzania maelfu wanaothamini haki ya mali za nchi yao. Hivi juzi umetoa kauli na ikaandikwa kwenye vyombo vya habari. Hii ni kauli inayowaumiza vichwa kundi la akina Pombe Magufuri na mwengine waliokuwa katika serikali ya Mfalme Benjamin Mkapa. Na wewe ulikuwa katika serikali hiyo, na makamu wako alikuwa makamu wako huko pia. Waziri mkuu wako alikuwa waziri mwenzako huko pia na mawaziri wako lukuki wametokea katika serikali hiyo iliyojigawia nyumba za umma baada ya ninyi wenzetu kutuzidi kete kwa kutumia madaraka yetu kama dhamana ya matakwa yenu.

Suala la nyumba hizi sidhani kama litakuja kuachwa liishe hivi hivi katika Tanzania ya leo ambapo watoto maskini wanaosoma vyuo vya juu wanatakiwa kulipa gharama zao za mikopo huku ninyi mkigawiana mali za umma bure tena mchana kabisa! Nakukumbusha kuwa utawala hautadumu kwako milele na kuwa hatuwezi kuona huko kesho ni kipi kitadaiwa na wananchi! Ili kuepusha leo kujenga kesho chafu ni bora kufanya yanayowezekana sasa ikiwa ni moja, kutangaza gharama za kila nyumba iliyouzwa, pili kutangaza minada ya nyumba hizo ilivyofanyika na tatu kuwaomba wananchi kurejesha fedha za hao waliojigawia nyumba zetu sasa ili wakajenge zao kwingine na kisha nyumba hizo kurejea serikalini na kutumiwa na mimi na wewe na wengine watakaopata nafasi ya kutumikia umma wetu.

Hatutishani kabisa katika suala hili na wala Kasri hapa siandiki kwa jazba. Msimamo wangu kuhusu nyumba hizi sikuuanza leo nimekuwa nao siku nyingi na hakuna atakayenibadilisha kabisa. Kama mnamuenzi kweli Nyerere basi lazima mjikane na kurejesha nyumba za umma na kisha kuanza kujenga zenu na watoto wenu popote mpendapo. Si dhamana ya madaraka haya tuliyowapa ni ya muda mfupi tu, je mnadhani mtaishi nayo milele, kumbukeni hukumu yenu kesho kama nanyi mnashiriki kunywa kikombe hiki cha damu ya watanzania.

Nyumba za serikali zatakiwa kurejeshwa kwa kuwa zilikiuka misingi ya uuzwaji au ugawanjwi wake. Mlijigawia na hilo ni kosa. Natafuta kifungu cha sheria ili niende mahakamani siku moja lakini kabla hatujatumia mbinu hizi za kuaibishana ni bora mkaona kuwa maandishi haya nayaandika sasa jambo ambalo huko nyuma nisingeweza kufanya. Mnadhani ni nini kinanisukuma kuandika hivi? Mnadhani ni wangapi wanaweza kuandika haya na kuayasimamia zaidi yangu kwa sasa, mnangoja nini kuwaodosha wote katika nyumba zetu sasa na kuwarejeshea vijisenti vyao ili nyumba za umma zibaki za umma? Kikwete nakamilisha kwa kukumbusha kuwa hii ilikuwa sifa yako mojawapo wakati wa uteuzi. Uliaminika kuwa hukununua nyumba na ulipotangaza kununua pia ilitamkwa kuwa ni siasa ya kutaka kuunganisha wezi na wadhambi pamoja na wema ili safari ya kushinda madaraka ikamilike! Umeshashinda na raia maskini wanakuona kama ngao yao sasa, unangoja nini kutumia nguvu ya umma badala ya kuwatazama mafisadi waliotumia nafasi zao kujinemesha wakihema na kucheka huku umma ukitazama kwa husuda! Unadhani umma huu utatazama hadi lini, kadri siku zinavyokwenda ndipo na wewe tunakuingiza katika makundi haya hata kama una nia njema na nchi hii sasa. Kumbuka wanaokuzunguka tunawafahamu na hila zao zinajulikana. Kama huchukui hatua maridhawa itatupa nafasi ya kuota masiha mwingine na wewe kukuingiza katika kundi hili hili la wale waliopita baada ya Nyerere kiongozi wetu tunayemthamini na kumuenzi sana. Je wataka lipi baada ya kushinda dola sasa? Jikane na chukua msalaba wako safisha nchi bila woga, hao wanakuzunguka ni wachache mno ukilinganisha na bahari ya watanzania inayotaabika kutokana na tabia ya hao kuwa na matumbo yasiyo kinai.
 
© boniphace Tarehe 5/26/2006 02:15:00 PM | Permalink |


Comments: 9


 • Tarehe 5/27/2006 12:59 AM, Mtoa Maoni: Blogger Mija Shija Sayi

  Kaka yangu Makene leo ya Musoma yametibuka!!...haya jitahidi lakini kwenda pole pole ili wasipate sababu ya kusema tunawakosea adabu. Nao wanaudhi mno wakati mwingine.

   
 • Tarehe 5/27/2006 2:10 AM, Mtoa Maoni: Blogger charahani

  Kaka haya mambo ni magumu na yanatia hasira mno, haiwezekani eti wewe nyumba ijengwe kwa kodi za wananchi tena kwa bei mbaya halafu wauziane wajanja kwa bei poa. Huu ni unyonyaji hatuwezi kuchekelea eti tu kwa kuwa hazitauzwa zinazojengwa sasa kwani zile zilizouzwa si hawa hawa walibadilisha maamuzi. Tunataka nyumba zote za serikali zirudishwe serikalini ni kodi za babu zetu na ni stahili ya kila Mtanzania anayefikia madaraka ya kiasi hicho.

   
 • Tarehe 5/27/2006 5:49 AM, Mtoa Maoni: Blogger Indya Nkya

  Tabu, tabu, taaaaabu. Kwa kweli Makene safari ni ndefu ya kutembea. Watu hujisahau sana kana kwamba historia huwa haipo wala haiandikwi. Hizi nyumba zilitolewa kwa hesabu fulani. Kila mhimili unazimiliki. Wabunge, majaji na waserikali. Kila unapopiga utaona ni ngumu kupenya. Lakini mambo yatakuwa sawa miaka siyo mingi. Nguvu ya umma inahitajika kudai kilicho chetu.

   
 • Tarehe 5/29/2006 10:04 AM, Mtoa Maoni: Blogger Ndesanjo Macha

  Makene, ni siku nyingi zimepita toka nikutane na maneno makala namna hii kwenye blogu zetu. Sababu iliyokufanya ukaandika kwa ukali (bila kutukana) ninaielewa. Na watanzania wengi wanaielewa. Ingekuwa nyumba zile sio mali yetu ningeshangaa kwanini umekuwa mkali namna hii. Ila nyumba zile ni zetu. Sasa hawa wafisadi wanaojifanya kuwa eti ari mpya huku wakiwa ni wale wale ambao kwa miaka nenda rudi wamekuwa wakipora mali zetu bila aibu wanakuja leo hii na matamko yao ya hapa na pale yanayoshangiliwa na vyombo vya uongo. Tukijenga nchi inayoridhishwa na matamko tutakuwa tunajidanganya.

  Umesema vizuri sana pale ulipomkumbusha kuwa waliomzunguka ndio wale wale walikuwa mafisadi wakati wa mfalume Mkapa. Leo hii wanajifanya eti wao ni kiboko ile mbaya. Tukiwa na Makene wengine mia moja watajua kuwa janja yao tunaitambua.

  Swali lako la msingi ninaliunga mkono: suala sio kutouza, suala ni kurejesha mali ya umma. Kituo!

  Je umeipanua hii iwe makala kwenye safy yako kule nyumbani? Inafaa kusomwa na wengi.

   
 • Tarehe 5/29/2006 12:08 PM, Mtoa Maoni: Blogger Boniphace Makene

  Ndesanjo hewara kaka, niliwaza hivyo nami pia, nitajitahidi kutoa sentensi moja na kutanua katikati hapo ili ieendelee kusimamia msimamo wangu na wenzangu mnaoamini kama mimi kuhusu suala la nyumba zetu. Asanteni kwa maoni yenu nitawanukuu pia nanyi ambao mmeweza kuchangia katika makala hiyo ya nyumbani.

   
 • Tarehe 5/29/2006 2:55 PM, Mtoa Maoni: Blogger zemarcopolo

  hii makala inaamsha uzalendo.ni vyema tena vyema sana isomwe na watanzania wengi iwezekanavyo.iwapo utafanya hivyo makene tafadhali katika paragraph ya kwanza nna mchango huu .....huu ni msimamo wangu na watanzania MAMILIONI(badala ya maelfu) wanaothamini haki ya mali za nchi yao.

   
 • Tarehe 5/30/2006 9:05 AM, Mtoa Maoni: Blogger Jeff Msangi

  Makene,
  Barua hii ni ilani ya kutosha ambayo raisi wetu anaweza kabisa kuitumia ili utendaji wake uwe kama wanavyotarajia watanzania wengi.Hakuna jinsi mtu yeyote anaweza kujustify dhuluma ile ambayo wananchi wametendewa.Hoja ni hiyo ya kurudisha tu.Na mtu asikuambie kwamba hilo haliwezekani kwa sababu linawezekana kabisa.Uhuru na haki daima.

   
 • Tarehe 5/30/2006 10:22 PM, Mtoa Maoni: Blogger KIDUME

  Hili suala la nyumba kuuziana hawa viongozi ambao tumewapa dhamana ya kuongoza nchi sio haki kabisa,Mimi naunga mkono kabisa makala yako ndugu Makene kwani hii inaonyesha ni kiasi gani CCM na serikali zake walivyo walafi!Tunataka nyumba zilizouzwa zirudishwe na pia itugwe sheria kabisa kuwa ni marufuku kuuza mali yeyote ya umma,kwani ingawa rais anadai kuwa hizi nyumba mpya hazitouzwa hii haitoshi kwani walafi waliomzunguka wanaweza kubadili uwamuzi huo muda wowote endapo watafanikiwa kurithiswa madaraka hapo mbeleni.Ndugu Kikwete najua hii ni moja ya mitihani mikubwa kwako baada ya kutwaa madaraka kuhakikisha kuwa unasikiliza kilio cha wananchi na si kuendelea kukumbatia wabadhirifu na wabinafsi kama awamu ya mfalme Mkapa!

   
 • Tarehe 6/30/2006 1:53 AM, Mtoa Maoni: Blogger kasuku

  Hili suala la nyumba mimi pia limenikera sana. Japo na mimi nitafungua mjadala kwenye blog yangu ya gersonmsigwa.blogspot.com, lakini naomba niseme watanzania wana kila haki ya kudai nyumba hizo. Zipo ambazo zilijengwa kwa milioni 120 na sasa zimeuzwa kwa milioni 7, na hata nyingine chini ya hapo.

  Nionavyo mimi kunyang'anya zote sio rahisi sana. Ila Kikwete anaweza kuamua vibosile wote wa wenye nyumba mbili au zaidi iwe zote wamenunua serikalini au mojawapo wamejenga wenyewe, waachiwe moja na zingine zirudi serikali ili waishi watumishi wapya na wenye mishahara midogo. Manaake kwa sasa mtu ana mshahara milioni 1.5 bada anauziwa nyumba ya serikali na yeye bado anaishi nyumba ya serikali sasa huyu mtumishi analipwa kima cha chini 60,000 ataishi vipi bila nyumba walal gari?

   
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved