Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Friday, May 12, 2006
WAGOMBEA BINAFSI NA KASISI WANAOTAFUNA KONDOO WAO
MADA ya wagombea binafsi inatanuka na wengi wamechangia hapo chini mara baada ya Mchungaji Mtikila kutangazwa mshindi mapema wiki zilizopita. Ilianza mwaka 1994 na mwaka huu mahakama ikaamuru wagombea binafsi wapatiwe haki yao ya kikatiba, yaani kuwapanulia nafasi ya kugombea pia badala ya kuishia kuwa wapiga kura pekee.

Mchangiaji Kibanda alifafanua mafanikio ya hoja hii huku akieleza mazingira ya rushwa zilizokuwa zikitolewa wakati wa mchakato wa uchaguzi wa mgombea urais kupitia CCM mwaka jana ambapo Jakaya Kikwete aliibuka kidedea. Rushwa ya kununua madaraka ilianza kuwa haki mara baada ya uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi, na sheria za kuidhibiti zikapindishwa baada ya CCM kama chama tawala kuona ndiyo njia nafuu ya kukiwezesha kuweza kushikilia viti vingi vya uwakilishi.

Baadaye rushwa hii ikaundiwa sheria na kubalikiwa na Bunge la CCM na kisha kutimika hadi ilipopigwa mweleka juzi na mahakama kuu. Nini faida za kuwa mgombea binafsi? Hili ni swali muhimu sana na Ndesanjo katika mchango wake amefafanua wazi kuwa ni fursa pekee anayopatiwa mtu asiyependa kujigeuza mtumwa. Hoja hii inakubaliwa na Kibanda na Miruko.

Lakini pia kuna mawazo ya MK ambaye anafafanua kuwa hoja ya wagombea binafsi ina taswira ya kuleta vurugu huku akitumia mfano wa siasa za Zanzibar kushikilia hoja yake. Hata hivyo serikali ya Zaizibar ilishapinga mapema kuwa sheria hii haitatambulika huko visiwani huku pia kukiwa na harakati za mwanasheria wa serikali kurejea tena mahakamani kupinga maamuzi haya ya mahakama.

Nimedonoa kidogo tu, lakini furaha yangu ni kuwa mijadala hii sasa inapata taswira mpya na inajadiliwa kweli kweli na kwa umakini kwa hoja bin hoja. Huko gazeti tando la Pambazuka kuna habari ya makasisi kutafuna kondoo wake ambayo imetanua mjadala na kwa mara ya kwanza kupatikana kwa wachangiaji zaidi ya 100. Hii ni picha namna tunavyokua na kilichonivutia zaidi ni aina ya hoja zinazotolewa huku, hazina bezo sana wala matusi ila kila mmoja anajitahidi kuonyesha mwenzake kuwa hoja yake ndivyo ina nguvu. Tuendelee kujadili hasa nafasi ya mwanasheria katika kupinga sheria hii ya wagombea binafsi, je anatumwa na nani, anatumia fedha ya nani, na anamuwakilisha nani kupinga maamuzi hayo?
 
© boniphace Tarehe 5/12/2006 02:16:00 PM | Permalink |


Comments: 7


  • Tarehe 5/13/2006 3:36 AM, Mtoa Maoni: Blogger Vempin Media Tanzania

    Makene,

    Kwani huyu mwanasheria anateuliwa na nani vile halafu analinda maslahi ya nani? bila shaka jibu linajulikana anateuliwa na rais ana analinda maslahi ya watawala, na fedha atakazotumia ni kodi zetu hakuna zingine hana ujanja ingawa atajitetea kuwa anatetea haki za raia wa taifa hili, lakini Makene mi na kamtazamo kengine hivi kweli haya mambo ya ugombea binafsi kwa hapa kwetu, siyo tunafuata mambo ideal, hivi kama hapa tu tuko na mfumo wa vyama vingi lakini bado tunaendelea na fikra na matendo ya chama kimoja mgombea binafsi hatakuwa ideal tu!

     
  • Tarehe 5/13/2006 8:49 AM, Mtoa Maoni: Blogger Rashid Mkwinda

    Mie nadhani huu ni Uhuru bila kuwepo kwa uhuru huria wa kujichagulia cha kufanya, kwani iwapo wagombea waliojitokeza katika vyama tunashuhudia wafuasi wao wakipigwa mabomu wengine wake zao wakibakwa wengine wakikimbia nchi na wengine kuuawa ilhalai wengine tunawaona wakiwa vilema kwa sababu za kugombea, Uwakilishi Ubunge na Urahisi itakuwaje huyu mgombea asiyekuwa na wafuasi wala chama aliyepachikwa jina la mgombea binafsi, nadhani itakayo muunga mkono ni aila yake tu ambayo pia nadhani inaweza kuhofia kupigwa mabomu, kubakwa na mara nyingine kuuawa kwa sababu ya SIHASA za hapa nchini Bongo.
    Naomba nimalizie hapa kwani inatia uchungu kuona Wadanganyika tunaendelea kudanganyika ilhali tunayo macho ya kuonea, masikio ya kusikia, mikono ya kukamatia na miguu ya kutembelea, akili za kufikiria na midomo ya kusemea.
    Tufike mahali tusikubali kuburuzwa katika nchi tuliyozaliwa na kukulia.

    Aaa ngoja niishie hapa hii mada inanitia uchungu sana mambo ya SIHASA tuwaachie wana SIHASA wenyewe sisi akina yakhe washika kalamu tunaambiwa ni wanoko ilhali tunaeleza kile kilichopo.

    Wakatabahu

    Jambo jingine narudi kwako Makene hivi hii Kasri mbona ina mandhari ya Kiulaya ulaya ndio kusema na wewe umekuwa Muulaya kwanini usiweke angalau mandhari ya kule Kanyigo,Karagwe na kwingineko tukaona migomba na Kahawa za kwenu?
    Mie nina wasi wasi huenda umekuwa na wewe ni Muulaya kwani nakumbuka kuna kajipicha ulikapandisha ukiwa na Demu wa kizungu hii kutuonesha kwamba waUlaya ndio wamekuteka kabisa.

     
  • Tarehe 5/13/2006 12:44 PM, Mtoa Maoni: Blogger boniphace

    Charahani, hii ni hatua na kama unafatilia kwa ukaribu siasa zetu suala la mgombea binafsi ndio fimbo ya CCM sasa subiri utaona utabiri wangu utatimia 2015 BAADA YA MAKOSA FULANI YAKIFANYIKA!

    Mkwinda kaka yangu, kasri limejengwa na MK na nimeshindwa kabisa kuingiza vionjo vyangu kutokana na mimi kutokuwa na uwezo wa kujenga maana MK nanambia kuwa kuna masuala ya mahesabu na mimi nilikimbia somo hilo tangu sekondari. Tena suala la picha za weupe na weusi zinaashiria msimamo wangu kuhusu rangi ambazo mimi sioni kuwa ni tatizo maana nimegundua kuwa sisi wanyonyaji na wanyanyasaji zaidi kuliko hata hawa weupe, kama unapitia Barua kwa mama utapata majibu ya mtazamo wangu huu. Unaweza kuwa Ulaya au Afrika lakini utu kwanza kaka!

     
  • Tarehe 5/15/2006 3:03 AM, Mtoa Maoni: Blogger Vempin Media Tanzania

    Ulichokisema Makene ni cha kweli, hivi CCM unadhani inaweza kuchukua kisu ijichinje yenyewe, umenikumbusha suala la wanaoshindwa kura za maoni hawa wakigombea binafsi mama yangu CCM imekufa. Ideally hii kitu ni safi lakini practically Makene bado nina mashaka.

     
  • Tarehe 5/18/2006 3:03 AM, Mtoa Maoni: Blogger Reggy's

    Nafanya utafiti mfupi kwa kuzingatia hoja za watu mbalimbali. Nitaingia tena kuleta maoni hapa. Hodi.

     
  • Tarehe 5/24/2006 3:05 AM, Mtoa Maoni: Blogger nyembo

    nafikiri, kuna mambo mengi sana zaidi ya hili la Mchungaji Mtikila na sheria zilizopindishwa,

    nafikiri ni muda wana blog kuanza kufuatilia hasa masuala ya kisheria zaidi,sio lelemama tu humu!

    tena Bwana Kibanda ajue tutanzisha postmotamu humu, na tunahitaji misimamo imara katika kutetea hoja husika!

     
  • Tarehe 5/24/2006 2:14 PM, Mtoa Maoni: Blogger boniphace

    Mheshimiwa Zemarcopolo, samahani kama nitakosea nomino yako! Unatakiwa kugoogle "Azimio la Dodoma" kwenye sehemu ya tafuta katika Gazeti Tando hili na kisha utalisoma hapo. Huu ni muongozo wa kwanza kabisa unaoongoza jumuiya ya wamiliki wa Mgazeti Tando wa Tanzania.

     
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved