Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Monday, November 28, 2005
SAFARI YA MASHUA SEHEMU YA KWANZA
Kwa wasomaji wapya! SAFARI YA MASHUA ILIYOTAKIWA KUWA MCHEZO WA KUIGIZA IMEGEUKA HASA RIWAYA. KUNA SABABU LAKINI SASA ENDELEA NA UHONDO WA SEHEMU YA PILI.

Waweza anza na sehemu ya kwanza hapa
Safari ya kichaa yule haikufahamika mwisho wake. Inasemekana alitoweka katika upwa wa Bahari ya Hindi na kukimbilia visiwa vya Ngazija. Alipofika huko hakuthamini tena kazi ya ukichaa, akaanza kujigubika lebasi na kila ulimbende.

Kazi ikikamilika ni jukumu la moyo kupata furaha, huo unakuwa wakati muwali wa kujenga liwazo jipya. Kuna mioyo ambayo inasemwa ilikataa kupata liwazo jipta na baadaye ikajikuta ikiwa katika mikono ya hayawani.

Kichaa yule inaelezwa kuwa alibadili jina na sasa hafahamiki tena. Jina lake la awali hata nami sikuweza kulitambua nilichokumbuka ni ile sura yake ya ukichaa. Sura aliyojibandika baada ya kuja Bara na baadaye Visiwani kwenye karafuu kutimiza shughuli yake.

Miaka ilipozidi kuyoyoma kichaa yule alinyofoa hata sura yake ya bandia na kutumia ile iliyokuwa halisi. Sasa hakumbukiki tena na wale walioweza kumtazama zamani. Kosa alilofanya ni kutoa sura yake ya dhati kipindi cha uzee! Sijui kwa nini hakukumbuka kufanya hivi mapema, yamemkuta makubwa maana hakuna anayemkumbuka na hata huduma za matibabu anazotakiwa kupata hapa hospitalini zimekuwa za malalamiko.

Kufika kwake hospitali kulitokana na ajali ya kipigo baada ya kugonganisha mabibi wawili. Kazi hii inaelezwa kuwa maarufu sana kwa wanasiasa wa Afrika lakini haikuwahi kufafanuliwa kuhusu nafasi ya vichaa katika suala la mapenzi. Kuna wakati nimekuwa nikikutana na vichaa waliozaa na kushindwa kutambua kuwa nani anawazalisha.

Mzee Masakubila aliwahi kunipa taarifa fulani baada ya tukio moja lililotokea pale Rwagasore. Siku hiyo tulikuwa tukipita mitaa ya Makoroboi na kukutana na kundi la omba omba waliohitaji msaada wetu. Wakati akinifahamisha nami kumsikiliza mmoja wa watoto wa ombaomba hao alirukia mkufu na kudhuru kidevu cha Mzee Masakubila.

Mzee wa watu akaanza kutoa kilio cha maumivu. Hakuamini kuwa masharubu yake aliyogharamia kuyalinda kwa miaka mingi yamekupatwa na kimbunga baada ya mtoto huyo kumtolea uvivu. Sifa mojawapo ya Masakubila ilikuwa kufuga hayo masharubu na kisha kila azungumzapo kuyashikashika ili afahamike kuwa dume la mbegu katika mtaa wake.

Ilimbidi kulia na kilio hicho alinambia baadaye kuwa kilikuwa na taarifa mbili, mosi ikiwa kupotea heshima yake maana kwa umri alionao ingekuwa vigumu kuyakuza tena masharubu hayo kabla ya kufa. Na pili alizungumzia tambiko alilolifanya kwa mganga wa kienyeji jirani na Gamboshi ya Magu ili kujiwekea mazingira ya kupata mali mengi.

Mganga yule alimueleza siku alipokuwa akimfanyia mitishamba kuwa, kama kutatokea siku akapaswa kunyoa masharubu yale basi atambue kuwa huo ndio mwisho wa miliki ya mali mengi aliyokuwa nayo. Mzee huyu alikuwa akilia hasa akiwazia suala hili la pili.

Siku hazikupita kukasikika kuwepo vichaa zaidi katika mtaa ule. Mmoja aliwahi kututoa kicheko aliposikika akibwatuka kutafuta masalio ya masharubu. Sikufahamu mapema maana halisi ya masharubu lakini kurejea kwake mara kwa mara kuhusu kutaka masalio hayo kukanipa fikra juu ya mzee Masakubila ambaye kwa kipindi hicho alishalazwa kuzimu yapata miezi sita!

Kuongezeka kwa vichaa katika mtaa wa Makoroboi kuliambatana na adha mbalimbali kwa wafanyabiashara ndogo ndogo. Adha kubwa ilikuwa kufungiwa kwao kabisa na kisa cha kufanya hivi ni kuwa kuna kabinti ka kidato cha sita katika shule moja hapo katikakati ya jiji kaliporwa simu aliyonunua mzee mmoja mwenye madaraka katika jiji. Inasikika kuwa mzee huyo naye alikuwa akishika pembe tu maana kuna mzito mmoja ambaye wakati huo alikuwa katika harakati za kupigania kiti kikubwa cha kuendesha mashua hii iliyochoka!

Hiyo ndiyo hasara ya kuwakwapua watu wasiofahamika, lakini hawa vibaka wangejuaje kuwa kabinti kale kanachukuliwa na kibopa? Swali hilo halina jibu lakini laweza kufananishwa na tukio lililotokea baada ya mke wa kingunge mmoja kusikika akitishia kufutwa taaluma moja ya utamaduni katika nchi ya Wanazuo. Kilichofanyika kilikuwa mwanamama huyo kukaidi majukumu ya kiongozi wa chini katika serikali ya Wanazuo aliyemtaka kuchangisha michango ya kuendesha mashindano ya utamaduni.

Utamaduni lilikuwa suala lenye kupewa kipaumbele sana katika nchi ya Wanazuo. Wakazi wa nchi hiyo waliamini kuwa kwa kuthamini utamaduni kuna siku moja watabainika kuwa wao ni bora zaidi ulimwenguni. Walikosea, hawakujua kuwa kuna Waziri mmoja angeweza kufuta utamaduni kisa mkewe kushindwa kukusanya michango.

Mambo kama haya yameidunisha sana nchi ya Wanazuo na siku hizi hakuna tena kuwapambanisha vijana wao katika michezo na utamaduni. Wajanja wachache waliojichimbia katika Kasri la Fikra, jimbo la chini kabisa katika nchi hiyo wamebaki kupiga mayowe lakini hakuna aliyewasikia. Kinachosikika ni kimoja tu kuwa jamaa huyo aliyefuta utamaduni anasifiwa na mfalme wa Wanazuo na anaweza kurejeshwa madarakani tena.

Haya ndiyo maisha, maisha ya kumbukumbu yanayomjia kichaa yule sasa huko Ngazija. Sura yake ya zamani ingeweza kumsaidia kupata matibabu maana ilifahamika sana. Kibaya ni hiki cha kuwa haikuwa sura yake halisi na sasa anatakiwa kufanyiwa upasuaji wa sura hiyo baada ya mkong'oto huo mkali. Nini hasa kilimfanya kuficha sura wakati huo wote?

Zoezi la kuvizia hati zile lilikuwa na maana kweli kweli. Alikabidhiwa kichaa huyu kwa vile alifahamika katika nchi nzima kuwa anaweza kutumia kila hila kubadilisha maandishi na kila Mwanazuo akakubaliana naye. Kichaa huyu alifanikiwa, kumtia kichaa kiungo muhimu katika ujenzi wa taifa la Kasri la Wanazuo. Taifa lilijengwa baada ya pande moja kuona umuhimu wa kutafuta nguvu za upande wa pili ili matakwa ya madaraka ya huyu jamaa kufikiwa.

Aliwaza sana...siku zikazidi kwenda na kwenda. Akabaki akiwaza huku mkuu wa nchi hii iliyoitwa Zuoni akipanga namna ya kubatilisha mambo. Alishafanikiwa na kazi ilishakamilika ila jukumu moja kubwa. Wakati kichaa huyu ambaye pia alikuwa kiongozi wa Kasri kabla ya kuliunganisha na nchi ya Zuo, akipanga namna njema ya kufanikisha matakwa yake ghafla mambo yakabadilika.

Endelea Sehemu ya pili
 
© boniphace Tarehe 11/28/2005 12:00:00 PM | Permalink |


Comments: 0


   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved