Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Tuesday, March 27, 2007
Dowans kama Richmond
INAWEZEKANA msemo wa Kiswahili wa 'sikio la kufa halisikii dawa' ukawa kiashirio cha kushindwa kufua umeme kwa Kampuni ya Dowans, zamani Richmond Development Co-operation (RDC). Dowans ilipewa muda wa mwisho wa kuzalisha nishati hiyo kwa megawati 80 kufikia katikati ya mwezi huu na imeshindwa.

Agizo hilo lilitolewa kwa pamoja na Wizara ya Nishati na Madini, Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Biashara kwa maofisa wa kampuni wakiwamo waandamizi wa Tanesco.

Hadi jana, Mwananchi Jumapili iliwakuta wafanyakazi wa kampuni hiyo wakichora michoro, kama walivyokutwa Februari wakati Kamati ya Bunge ilipozuru eneo hilo kwa kushtukiza.

Mitambo ya kampuni hiyo inayotakiwa kufungwa pia bado iko katika makontena yaliyobebwa katika magari.

Kutokana na hali hiyo, ni wazi kuwa zoezi la kuunganisha mitambo hiyo ambalo limekuwa likienda kwa mwendo wa kinyonga, linaashiria kukwama kwa Dowans kwa mara nyingine katika kutoa nishati hiyo.

Ingawa inawezekana nishati hiyo isiwe yenye kuhitajika kwa haraka hasa katika kipindi hiki ambacho mabwawa ya maji yamejaa, lakini kampuni hiyo inahitajika kuekeleza yaliyomo katika makubaliano ambapo ilitakiwa kuwa imeshasimika mitambo Alhamisi ya wiki ijayo.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa Mwananchi Jumapili, ufuaji wa umeme sasa unaweza kuonekana zaidi kama maajabu. Itakuwa ajabu kwa Dowans ndani ya siku mbili kumudu kuzalisha walau megawati 80 za awali ifikapo Machi 15.

Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Biashara, ikiwa chini ya Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na maofisa kadhaa wa Tanesco, waliitembelea Dowans Februari 12, 2007.

Ziara hiyo ilielezwa kuwa ya kushtukiza na Mwananchi Jumapili lilipata fursa ya kufika katika eneo hilo kabla ya ziara.

Kilichofuata kilikuwa agizo la wajumbe wa kamati hiyo sambamba na maafisa wa Dowans kuhakikisha kuwa mpiga picha na mwandishi wa gazeti hili wanafukuzwa na kuondolewa katika eneo hilo.

Hatua yao ya kuondolewa ilifuatana na kukabidhiwa askari aliyekuwa na silaha kuwasindikiza nje kabisa ya eneo la mitambo ya Dowans.

Hata hivyo, ilibainika baadaye kuwa, Dowans iliifahamisha kamati hiyo kuwa ingeanza kufua umeme kiasi cha megawati 80 ifikapo mwishoni mwa Februari 2007.

Kamati hiyo iliridhika na maelezo ya Dowans na kisha ikakubali bila kuombwa, kuiongezea muda zaidi kampuni hiyo kuweza kujiandaa. Muda huo uliongezwa kutoka mwisho wa Februari 2007 hadi Machi 15.

Kwa hali iliyoonekana baada ya gazeti hili kufika katika maeneo ilipo mitambo ya Dowans mapema wiki hii, ni vigumu kwa kampuni hiyo kumudu kufua umeme huo ndani ya muda ilioongezewa, ambao unaishia Alhamisi wiki ijayo.

Dowans Holdings, ilinunua mkataba wa kuzalisha megawati 100 kutoka kwa RDC, hii ilitokea wakati RDC ikiwa imeshindwa kuzalisha umeme huo katika muda uliokubaliwa katika mkataba.

Zoezi hili la kushindwa kuzalisha umeme huo ndani ya mkataba limeikumba pia Dowans, hali inayozua maswali zaidi kutoka kwa Watanzania , hasa kuhusu nini maana ya serikali kuendelea kuibeba kampuni hiyo.

Dowans ilikabidhiwa rasmi mkataba wa Richmond Desemba 21, 2006 ikiwa imenunua makubaliano yote katika mkataba wa Tanesco na Richmond uliosainiwa Juni 23.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Jumapili, mitambo ya megawati 80 ya Dowans, ilishaingizwa nchini na kufikishwa katika eneo lililopangiwa na Kampuni ya Umeme nchini TANESCO.

Hata hivyo, mitambo hiyo iko katika hali ile ile kama ilivyofikishwa pale. Hali hiyo inaonyesha kuna maandalizi madogo na yasiyoridhisha yanayoendelea katika kuunganisha mitambo, hali inayofafanua kuwa, ufuaji wa umeme kufanywa na kampuni hiyo ni ngumu mno kufikiwa katika siku zilizobakia.
 
© boniphace Tarehe 3/27/2007 09:47:00 AM | Permalink |


Comments: 4


  • Tarehe 3/29/2007 2:16 AM, Mtoa Maoni: Blogger Sultan Tamba

    Mikataba mingi mikubwa iliyosainiwa na serikali ya Tanzania ina walakini wa hali ya juu na dalili za ten pacent au twenty, zimetanda kwenye karibu kila mkataba! Hata mkataba huu ukiupiga tochi ndani yake utakuta haya haya! angalau vyombo vya habari vinasaidia!

     
  • Tarehe 4/12/2007 7:48 PM, Mtoa Maoni: Blogger Simon Kitururu

    Naona imegeuka kuwa radha ya kupeana vijiti.Sitashanga nikisikia kampuni nyingine ikanunua mkataba na kushikilia kijiti mpaka itakapojitokeza nyingine.Lakini hakuna sheria ziwezazo kuchukuliwa kuwachukulia hatua hawa jamaa?

     
  • Tarehe 5/18/2007 5:58 AM, Mtoa Maoni: Blogger Fikrathabiti

    KAULI YA JAJI MKUU SAMATA IWE CHANGAMOTO KWA WADAU WA SHERIA NCHINI

    Katika mamabo ambayo watanzania tumekua tukijigamba na kutembea vifua mbele ni AMANI iliyotawala nchini tangu tulipopata uhuru karibu miongo minne na nusu iliyopita..Nchi yetu imetokea kua kimbilio la wageni kutoka nchi majirani ambapo hapakaliki kutokana na kutoelewana na vita vya wenyewe kwa wenyewe na vita vya kimakundi au kimatabaka kati ya watawala na wananchi wao.

    Sina haja ya kuingia kwa undani katika hali tete inayoendelea kwa majirani zetu ila kwa kuanzia mada iliyobeba kichwa cha habari hapo juu niliona ni busara kugusua kwa uchache maswahibu yanayowakumba wenzetu katika siasa zao na mifumo ya utawala na ya kutetetea haki zao.

    Jana Mheshimiwa jaji mkuu Barnabas Samatta aligusia juu ya umuhimu wa vyombo vya sheria hasa mahakama katika kudumisha amani ya nchi husika kwa kuweka bayana kua...nanukuu "Iwapo jamii itapoteza imani kwa mahakama zetu ndio itakua mwanzo wa kupoteza amani nchini" Inawezekana ikaonekana ni sentensi fupi na iliyozoeleka lakini suala linabaki kua ni jitihada zipi zimefanyika katika kunusuru hali hiyo isitokee???Tunafanya nini ili kuhakikisha wananchi wetu hasa wale waliokata tamaa hawapotezi imani kwa vyombo vyetu hivi ambavyo ni mhimili muhimu katika utawala wa kidemokrasia na wenye kuheshimu haki za binadamu????

    Kauli hii imekuja wakati muafaka wakati kukiwa na malalamiko mengi juu ya ubabaishaji unaofanywa na vyombo hivi katika kutetea haki za wanyonge.....Kumekua na ucheleweshaji wa kesi katika kiwango cha kukatisha tamaa na hata mara nyingine kutolewa maamuzi ambayo wakati mwingine yamekua yakizua mjadala juu ya umakini wa vyombo vyetu hivi..Sina nia ya kubeza kila jema linalofanywa na na mahakama zetu ila ni katika kuleta changamoto kwenye mchakato wa wadau kuelekea kwenye ujenzi wa jamii wenye kuheshimu haki za wananchi wenzetu..

    Kumekua na migogoro mingi kati ya mtu na mtu,jamii na jamii,wananchi na serikali,wafanyakazi na waajiri wao,wanafunzi na uongozi wao lakini je "nii hatma ya kelele na tofauti zitokanazo na misuguano ya makundi hayo"?? Siku zote binadamu amekua na tabia ya kujaribu njia mbadala pale anapoona nia na mitazamo yao haiendi sawa na kama walivyotaraji....vitendo vya kuchoma vibaka moto ni kielelezo kirahisi cha kuelezea kuchoshwa na ufanisi wa baadhi ya taasisi au asasi zilizokabidhiwa majukumu ya kusimamia mambo kama hayo....Kwanini raia ambaye amechoshwa na tabia ya jambazi sugu au vibaka wazoefu asiamue kuchukua sheria mkononi wakati kila wanapopoleka malalamiko yao kwenye vyombo husika,hakuna maamuzi ambayo yataonekana kukidhi kero za walalamikaji!!!!!!

    Kuna kesi nyingi katika sekta ya madini kati ya wachimbaji wadogo wadogo na wamiliki wa makampuni ya kigeni,kuna kesi nyingi kati ya wafanyakazi na waajiri wao ambazo bado mwisho wake haujulikani,wastaafu kila siku wanatanga na njia katika kufuatilia haki zao lakini bila matumaini yoyote katika yale mambo wanayodai ambayo asilimia 90% ni ya msingi!!!!!! Siku za karibuni kumekua na zoezi la bomoa bomoa katika jiji la Dar Es Salaam na asilimia kubwa ya wahanga wa tatizo hilo ni machinga.....vibanda vyao vingi vilipitiwa na sulubu hiyo...Sina nia ya kubeza zoezi hilo kwani mantiki yake iko wazi kabisa 'Kupendezesha mandhari ya jiji' hili ni jambo jema na linapaswa kupongezwa na kila mtu lakini swali la msingi ambalo linastaajabisha kila watu makini ni "Kwanini baadhi ya vibanda viachwe" Katika gazeti tando la michuzi alipiga picha ya moja ya vibanda hivyo na kuhoji uhalali wa kuwepo kwake????Watu wengi walichangia na kusema pengine ni cha mkubwa flani!!!je wakubwa hawapaswi kuguswa na sheria????je hao ndo wanapaswa kua juu ya sheria????

    Iko mifano mingi ambayo inatia kichefuchefu katika utekelezaji wa mambo ambayo ni ya manufaa kwa wananchi...Nani hajui kua karibu asilimia 60 ya vituo vya mafuta vilivyopo katika jiji la Dar Es Salaam vipo kinyume na sheria???Je wasimamizi wa sheria hizo wako wapi??? au tunataka wananchi waanze kuamini kua hizo ni miradi ya watunga sera na sheria ambao pia wamepewa ruhusa ya kuzivunja???Ni kwanini majibu ya maswali haya yasipatiwe ufumbuzi wa haraka katika kurudisha imani ya wananchi kwa watawala wao?????

    Kwa kumalizia napenda kutoa tu changamoto kwa serikali yetu kua makini katika kusimamia na kutatua kero za wananchi wake ili waendelee kua tayari katika kushiriki kikamilifu utekelezaji wa mipango ya maendeleo yao....Naamini kubwa na serikali ya mheshimiwa baba JK kwahiyo chondechonde watendaji msimwangushe katika nia yake njema ya kujenga nchi moja inayoheshimu haki na yenye kuweka mazingira ya kila mmoja kufaidi matunda ya uhuru...Ubabe wa baadhi ya watendaji hayana nafasi kwasasa kwani mwisho wake hautupi matumaini yoyote mazuri.....Mfano mzuri tunao kwa migomo inayoendelea kwa wanafunzi wa elimu ya juu....hii kwangu ni ishara ya kuchoshwa na ubabaishaji wa baadhi ya watendaji.....Nadhani itabidi tuanze kujadili nia ya mtu kama Proffessor msola katika kutumikia wananchi wa jamuhuri yetu hii.....Inatia hasira pale unaposikia WAZIRI flani msomi anawakatia simu wananchi wake eti kwasababu amechoshwa na kero zao!!!!!!!Hili naomba niliongelee siku nyingine...

    Naomba kuwasilisha..
    http://fikrathabiti.blogspot.com/

     
  • Tarehe 5/27/2007 1:27 PM, Mtoa Maoni: Blogger Mija Shija Sayi

    Makene naona umepotea siku hizi. Nakupa taarifa kwamba unahitajika hapo chini.

    http://www.blogutanzania.blogspot.com/

     
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved