Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Saturday, February 17, 2007
Sakata la madiwani Arusha na dhana ya cheo ni dhamana
SIJAWA nyuma ya wakati hata kidogo! Nisamehe na niruhusu nikukumbushe wewe mpiga kura wa Arusha! Ulichagua madiwani ambao chama chao kimewahukumu kuwa, wametumia vyeo vyao kama dhamana ya matakwa yao.

Chama kimewahukumu baada ya kubaini kuwa wametafuta utajiri kupitia nafasi ya uwakilishi uliowapa wewe mpiga kura. Hili si jambo la kushangaza tena katika Tanzania ya sasa. Matumizi ya madaraka kwa faida binafsi ni jambo linalosifiwa siku hizi.

Nchi imegeuka kabisa maana hapa nchini siku hizi mwizi anapendwa. Anaimbiwa nyimbo za ushujaa kwa kuwa tu ameweza kuiba bila kushikwa. Misingi ya utendaji kazi kwa uadilifu imetangazwa kuwa ushamba hali inayofanya kila kiongozi na watu wengi, kuhaha kusaka nafasi za uwakilishi ili waweze kuchota, kuiba na kisha kutukuzwa kama wazalendo halisi wa nchi hii.

Shaaban Robert aliwahi kuandika shairi la 'Tanga' katika kitabu chake cha Sanaa ya Ushairi. Ndani ya shairi hilo akafananisha nchi iliyosahau maadili kuwa mithili ya jangwa ambalo ni miujiza kuotesha mazao.

Nimekuwa nikijiuliza kuhusu uhusiano kati ya waliowahukumu madiwani wa Arusha, kama wana maisha tofauti yanayoweza kuwafanya wao kuwa safi kabisa ili kutoa hukumu hiyo. Nadhani hili ndilo hasa jambo la kujadiliwa maana inawezekana pia kuwa mtego huu haukulenga kunasa wanaoathiri taifa bali kukomoa wasio na nguvu lakini pia wamo katika mfumo.

Vita hivi vya makundi katika mfumo havina maana kuwa vinaonyesha mabadiliko katika utumishi. Ni muendelezo wa adhabu kwa aliye duni na dhaifu na haiwezekani kabisa haki ikafanikiwa. Tazama, baada ya tukio hilo la Arusha, wananchi wa Manispaa ya Moshi nao wakalalamika kuhusu vigogo katika manispaa hiyo pia kufanya matukio ya kujichukulia viwanja, wakaitaka CCM ifike huko lakini hadi sasa ipo kimya.

Zoezi hili kwa nini liishie hapa Arusha na lisitazame pia namna viongozi wa umma wanavyoingia madarakani? Kweli, kama kuna kutazama eneo hili la namna ya upatikanaji wa madaraka, ni viongozi wapi wanaoweza kusimama na kudai kuwa waliingia katika ofisi za umma bila kutumia mbinu chafu zinazopingana na maadili ya utawala wa umma? Je, huu si msingi mwingine wa TANU ambao unavunjwa?

Sitawatetea madiwani wa Arusha hata kidogo, lakini macho yangu yanataka kuona tukio kama hili likivuka mipaka. Si kweli wizi ni sifa na wala tamaa si jambo la kuabudiwa. Simpendi mwizi, awe wa kuku au huyu aliyejihusisha na kamisheni ya ununuzi wa rada. Ninachokitazama ni uwiano katika wizi na athari ya tukio hilo kwa jamii.

Mwizi katika kamisheni ya ununuzi wa rada anahitajika kufahamika mapema na kisha kukatolewa maamuzi na hukumu yake haraka kuliko ya hawa madiwani! Kwa nini kesi ya mwizi wa kuku itolewe majibu mapema lakini ile ya rushwa imalizwe kichinichini au polepole? Huu ndio mtindo wa maamuzi katika vyama, nambieni kama kuna mtindo mpya wa kuyapoza mambo kwa kungoja jamii ikumbwe na jambo jingine jipya, kisha ijisahau na kuacha jambo la awali kupoa.

Kuna swali laweza kukuumiza sana, hasa unapokuwa njiani na ukakutana na mtu asiyeona akawa anasisitiza kumuonyesha mwenzake njia! Hapa ndipo unapopata picha ya Tembo iliyotolewa katika hadithi za zamani, hasa siku ile wasioona watano walipoamua kutembelea mzoga wa Tembo na kila mmoja akatoka na picha yake ya kusimulia. Je, tunatakiwa maisha yetu yaongozwe kwa mtindo huu?

Je, ni muhimu kukimbilia majibu rahisi siku zote bila kujiuliza siku yatakapokuja magumu tutayakabilije? Jamii inayotaka maisha mepesi huishia kufanya mambo dhaifu, hukosa maadili na hujaa kero zisizoisha.

Madiwani wa Arusha wanasemwa walisigina amri kumi za mwana TANU. Waliivunja hasa hii ya kutotambua kuwa, cheo ni dhamana na kwamba, hawakutakiwa kutumia vyeo vyao au vya wengine katika kufanikisha mambo yao binafsi! Hili ni kosa, ni kosa kubwa na athari yake ni mithili ya sumu ya bafe inaposambaa katika mwili wa binadamu.

Hayati Justin Kalikawe hunikumbusha sana kila nikifikiri chanzo cha yeye kuimba wimbo wa 'Mv Bukoba.' Wimbo huu unanikumbusha rafiki na ndugu zangu niliowapoteza katika ajali hiyo! Tena nakumbuka pia ajali ya treni iliyotokea nje kidogo ya Dodoma mwaka 2002.

Maudhui ya wimbo wa Kalikawe hayakusikilizwa kabisa! Kama yangesikilizwa ni dhahiri kuwa ajali ya treni isingetokea. Si ajali hiyo tu bali zipo nyingine nyingi zinazozidi kutamalaki. Vyombo vya usafiri wa maji na hata ndege za hapa Tanzania hununuliwa zilizo chakavu ughaibuni.

Nani anafanya manunuzi haya? Jibu hapa rahisi sana; ni huyu anayetumia cheo chake kama dhamana ya matakwa yake. Kalikawe analia katika wimbo huo; "usitumie cheo chako kama dhamana ya matakwa yako, utasababisha ajali kama ile ya Mv Bukoba," anaimba na kurudia kiitikio hiki.

Kalikawe Mola akupe usingizi mororo huko uliko juu ya haki. Tungo zako ni utajiri tosha uliotuachia na kweli tunasikitika kukukosa. Bado tunazisikiliza na kutumia mashairi yako kujenga hoja.

Katibu Mkuu wa CCM, Mbunge na zamani Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuf Makamba aliwahi kukaririwa na vyombo vya habari mwaka 2005 akilalamikia kuhusu hatua ya serikali kwenda kasi kudai malipo ya nyumba za serikali walizouziwa viongozi wa juu.

Zoezi la uuzwaji wa Nyumba za serikali ni moja ya mambo yanayoambatanishwa na utumiaji wa madaraka kwa dhamana ya watawala. Nimemtumia Makamba hapa kufuatia yeye kutumia muda mwingi kunihamasisha kuandika kuhusu madiwani wa Arusha kuwa walitumia madaraka yao vibaya na kwamba chama kilifanya maamuzi sahihi dhidi yao kama jambo la kawaida na lililozoeleka ndani ya CCM.

Makamba anawakilisha kundi la taasisi za serikali ambazo zimebadili utawala kuwa ufalme. Mfalme hakosei na siku zote afanyalo ni jema. Utawala kama huu nasikia upo katika majeshi yetu maana huko nako kuna kauli ya mkubwa kutokupingwa.

Ni kweli adhabu ya madiwani wa CCM Arusha ililenga kusafisha uozo wa kutumia vibaya madaraka? Jibu la wazi ni kuwa, si kweli! Adhabu ile haikulenga kufanya hivyo, maana kama ingefuata na sehemu nyingine ambazo zina utata wa matumizi mabaya ya madaraka zingetazamwa na kisha kupewa hukumu inayostahili.

Mkakati wa viongozi kujigawia majumba ya serikali kwa kupotosha ukweli kuwa wanajiuzia kwa gharama nafuu huku jamii ya watu wengi ikibaki bila makazi bora ni kutumia vyeo kama dhamana ya matakwa binafsi.

Makamba ni mmoja wa waliokwisha kutumia vyeo vyao kama dhamana ya matakwa yao ukitumia mfano wa huu wa nyumba za serikali. Pia atakuwemo na Mwenyekiti wa CCM aliyemteua Makamba na ambaye pia ni Rais wa Tanzania, awamu ya nne.

Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete, alitangaza naye kujichukulia nyumba ya umma. Nini aibu kama hii, hasa kufanywa na viongozi waliolelewa ndani ya misingi ya chama kama TANU kilichozaa CCM. Chama cha TANU wanachozungumza sasa kutumia ahadi zake kuadhibu wengine ndani ya CCM?

Je, TANU haikujadili kuhusu mali za umma na tena kukawepo msisitizo wa namna ya kuzitunza katika Azimio la Arusha? Azimio la Arusha halikutaifisha mali na kuanzisha msako wa wahujumu uchumi nchini? Ni kweli kuwa tendo hili tukufu limesahaulika katika nchi na halina nafasi ya kurejea tena?

Kizazi cha sasa hakina kumbukumbu sana kuhusu harakati za kusaka wahujumu uchumi na namna zoezi hilo lilivyoweza kuineemesha Tanzania. Zoezi hilo lilisaidia kupunguza ufa kati ya matajiri dhidi ya maskini. Lilijenga uwezo na maadili kwa wananchi kwa kuwataka kusaka fedha safi na sio chafu. Lilijenga nidhamu katika madaraka ya umma na likasaidia umma kubaini kuwa majukumu ni wajibu na sio lazima yaendane na malipo ya ziada.

Moja ya sababu ya mafanikio ya Azimio la Arusha na hasa vita dhidi ya wahujumu uchumi na utaifishaji wa mali na kuzifanya za umma, ilikuwa kuwepo viongozi wenye moyo wa kufanya kazi hiyo. Kulikuwa na viongozi waliokubali kuzikana nafsi zao na kisha kubeba msalaba wa azimio hilo.

Majina yanayobakia na heshima kabisa katika kufanikisha harakati hizi ni Waziri Mkuu atakayebakia na heshima ya pekee kabisa kuliko Waziri Mkuu yeyote kupatikana hadi sasa nchini, Edward Moringe Sokoine. Inasemekana kuwa marais waliofuatia wamekuwa wakimkumbuka na kusaka mawaziri wakuu kutoka mkoani Arusha, dhana yao ni kupatikana Moringe mwingine!

Ukiacha Waziri Mkuu Moringe, Tanzania ilikuwa na Rais wa umma, Hayati Julius Nyerere. Huyu alikuwa na nia ya kuifanya Tanzania nchi isiyo na matabaka.

Ni jambo linaoonekana wazi kuwa, viongozi hawa mahiri wakirejea leo nchini watabaki katika simanzi. Hatutakuwa na nyumba za umma za kuwakalisha, labda tutawapeleka katika mahoteli ya kifahari ambayo pia vigogo kadhaa wana hisa nayo au walishayabinafsisha.

Wataumia kukuta waliowaachia urithi waliridhika kuuza kila walichozalishiwa. Wataumia sana kuona namna waliowaacha walivyosahau historia ya namna nchi ilipotokea.

Itakuwa huzuni kwao kutazama kuwa viongozi vijana waliowaamini ndio walioamua kujigawia na kisha wakazikarabati kwa gharama kubwa nyumba za umma. Ni vigumu kubaini nini kitajiandika katika ramani ya mioyo ya viongozi hawa wanaotangazwa kuhenziwa kwa maneno huku wakiwa walishatupwa kapuni katika matendo!

Kimsingi wataumia sana na hasa tabia hii ya viongozi wa umma kuamua kwa makusudi kuwataifisha mali wananchi maskini. Wataumia sana maana wanaofanya hivi ni wale waliodhani wangeendeleza mapambano ya kupigania haki ya wananchi maskini.

Ni aibu kabisa kwa viongozi wa Tanzania kukumbatia ubinafsishaji katika mambo yaliyotakiwa kubaki ya umma. Nchini Marekani, Rais mstaafu Bill Clinton aliwahi kulalamikia Kongresi ya nchi hiyo wakati ikitawaliwa na chama cha Republican, hasa ilipokuwa ikipitisha miswada mbalimbali iliyohitaji kubinafsisha mambo kadha wa kadha yahususyo huduma za jamii.

Lengo la Republican lilikuwa kukata matumizi kutoka kwa serikali lakini kuyatanua katika matumbo ya wachache. Kwa kufanya hivi kungenufaisha wanachama wengi wa Republican ambao ni wafanyabiashara.

Ni kweli serikali inatakiwa kukimbia baadhi ya majukumu kwa hofu za wanasiasa kusimamia shughuli hizo au kutumia nafasi zao kuharibu sekta mbalimbali zilizo chini ya serikali? Jibu la swali hili linaweza kupatikana kwa kila kiongozi wa umma, hasa anayetambua kuwa, kukimbia wajibu kwa hofu ya kashfa si tu inasaidia kuchaguliwa wakati wa uchaguzi unaofuata, bali pia unachangia kukwamisha mipango ya serikali kufuatia serikali kukabidhi watu wachache nguvu zake za uchumi.

Hii kwa namna nyingine ni sawa na kuifanya serikali kuwa ombaomba wa mali zilizokuwa zake. Mali ilizoamua kuziacha zinufaishe wachache au wale waliohusika na zoezi hilo au vinginevyo!

Nchi imefikia hatua ya kuwepo utaifishaji mpya! Tofauti na ule wa wakati wa Azimio la Arusha, wa sasa ni wa viongozi wanaochukua mali ya maskini.

Mfano wa Arusha unatoa mwanya tu wa namna viongozi wanavyoweza kujineemesha kupitia migongo ya wananchi. Ipo mifano kama hii ya kuihenzi kampuni ya Richmond, kuiruhusu ibadili jina ili kutafuta kupoteza lengo miongini mwa wananchi, na pia kutumia nguvu za madaraka kuhakikisha kuwa wabunge hawaijadili kabisa hoja hiyo bungeni.

Nani ananufaika na usiri wa mikataba inayowekwa na serikali. Vipi kuhusu manunuzi yenye utata ambayo serikali inayashangilia kwa kauli moja bila kuogopa kuwa yanachangia kudunisha maisha ya wananchi wengi maskini?

Kama adhabu ya madiwani wa Arusha imezingatia kuvunjwa kwa nguzo za ahadi za mwana TANU, vipi viongozi wetu wanavyoendesha nchi hii na hasa zoezi hili la kuiba mali za umma mchana kweupe kwa kutumia mbinu za kupitisha agenda za mali hizo, wao kujiuzia au kujigawia?

Hamkumbuki tena kuwa azimio hilo lilipinga kujikabidhi mali na likapinga hata kuwa na nyumba za kupangisha? Jiulize tena kuhusu matumizi ya milioni 100 kujadili hoja za watu binafsi na kisha baada ya kupoteza fedha hizo kazi inaishia kuitana katika ofisi za Spika kunywa kahawa!

Hii si mifano ya matumizi mabaya ya madaraka na fedha za umma kwa matakwa binafsi? Vipi kuhusu udanganyifu wa kuwapa wananchi wote elimu na kisha ikafatia kutangazwa asilimia 40 za kuichangia tena?

Kuna maswali mengi ya kujiuliza, kama kweli uongozi wa umma wa Tanzania ulilenga kuyafanya madaraka mali ya umma, kungelikuwa na ushikishaji wa umma katika kufikia maamuzi. Kusingekuwa na matumizi ya magari na maisha ya kifahari kwa viongozi wa umma wakati wanaowaongoza wanazidi kuwa maskini.

Ukweli unabaki kuwa, maamuzi yaliyowafikia madiwani wa Arusha yalitokea ili kudhibiti wasio na nguvu ndani ya mfumo ulioharibika. Je, jamii yapaswa kushangilia maamuzi haya badala ya kutaka kuona mabadiliko makubwa yanafanyika na hasa udhibiti wa viongozi wakubwa ambao inaonyesha wanatumia nao madaraka yao vibaya kutetea uovu, kuufanya au kujihusisha nao kwa usiri?

Profesa Euphrase Kezilahabi aliandika shairi la 'Sisi kwa sisi' katika Diwani yake ya Karibu Ndani na akabainisha kuwa; "sisi kwa sisi tukilana je safari lazima iendelee?" Tuko safarini lazima twende tuendako hata kama dereva wetu hataki kutufikisha.
 
© boniphace Tarehe 2/17/2007 11:44:00 PM | Permalink |


Comments: 0


   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved