Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Saturday, January 13, 2007
Zanzibar: Kuna mengi usiyoyajua
NAONDOKA mchana hapa ofisi za gazeti la Mwananchi, ofisi hizi zipo Tabata Relini, jijini Dar es Salaam, ninapaswa kukimbia kuwahi huduma za benki maana benki nyingi hufungwa ifikapo saa tisa kasoro robo hivi! Nafika Ubungo na kisha kwa kasi naingia benki ya NBC tawi la hapa.

Nina begi langu mgongoni na ninapoingia ndani nakutana na msururu wa watu ambao siwezi kuuhimili. Kuna joto kali pia humu na hali ya afya ya wateja ni wazi ipo katika hatari. Nakumbuka nimewahi kukutana na misururu ya watu kiasi hiki katika benki za NMB lakini siku hizi hata huduma za NBC hazina ubora wowote.

Mabenki ya Tanzania hayaoni thamani ya kutoa uharaka kwa wateja wao, yanawageuza watumwa na hali hii kama haitabadilika kuna uwezekano kutokea benki moja ya kigeni ikayaua mabenki haya yote bila yenyewe kujijua. Kimsingi hali Wateja ni tabu tupu, kuna hali ya kutotaka kujifunza kurejesha ustaarabu katika huduma hizi.

Anakuja mlinzi wa benki hii ambaye anatoka katika makampuni binafsi! Upatikanaji wa makampuni binafsi katika ulinzi una maswali mengi kuliko majibu. Wengi wao hawana mafunzo, wengine waliwahi kufukuzwa katika majeshi yetu, na wengi ni hawa waliokusanywa kutoka mitaani bila hata kutazama rekodi za maisha yao.

Mlinzi huyu anaanza kuhoji uhalali wa mimi kuwa na begi ndani ya Benki, namtazama kwanza maana hakuna sehemu inapokataza mimi nisiingie na mzigo wangu humu, na pia hakuna sehemu ya kuwekea mizigo hiyo na kuikuta salama! Nashindwa kumjibu maana nilishaona sitapata huduma hapa hivyo naondoka na kusaka ilipo teksi ili niwahi huduma benki hiyo tawi la makao makuu lililopo Posta.

Ninafika Posta na kukuta foleni nyingine kubwa. Najipanga katika foleni hii hadi nachoka! Nina dakika kadhaa tu ili nisichelewe boti ya kuelekea Zanzibar na bado kuna watu kumi mbele yangu. Naamua kuachana na harakati ya kupata huduma za benki baada ya kupoteza muda wa saa moja na nusu hivi.

Nakimbia na kufika gatini na kumkuta mlinzi wa kike kavalia mavazi yake ya bluu. Mimi nimevaa kadeti za kijani; namsalimu na kisha ananifungulia geti niingie. Napita na kisha naambiwa kuweka mzigo wangu kwa ajili ya ukaguzi. Hakuna vifaa vya kuweza kugundua kama kuna vitu hatari katika begi langu. Namuongelesha maneno ya utani mama huyu anayekagua na kisha ananiruhusu kupita bila kunifanyia ukaguzi wa kina.

Naingia katika boti na kukuta wasafiri wenye asili ya Ulaya kuwa ndio wengi kuliko sisi weusi. Nabaini kuna wengi wanatoka Ujerumani na mmoja ninayekaa naye karibu ninapoanza kumzungumzisha ananiambia anatoka Munich. Swali lake la kwanza kwangu ni kutaka kujua kama mimi ni mwanachama wa chama kipi na nini mawazo yangu katika siasa za Zanzibar.

Nakwepa swali lake maana natambua walishalishwa maneno kuhusu utata wa siasa za Zanzibar. Namwambia mimi sishabikii kabisa siasa bali najali uwajibikaji na kujitafutia kipato. Anauliza tena kama naenda kufanya nini Zanzibar; nami namjibu naenda kutalii na kuwa, huu ni utaratibu niliojiwekea kila baada ya miezi sita.

KUSHUKA BANDARINI ZANZIBAR


Mwendo wa saa kama mbili hivi tumetumia katika usafiri na sasa naingia Zanzibar. Nipo na rafiki yangu Gasper Materu anayefanya kazi huku. Namuuliza swali kuhusu nini huwa anawaza kila anapoingia Zanzibar. Yeye ananijibu kuwa ni fikra za kujiona yupo gerezani. Anajiona kafungwa na mipaka ya kisiwa iliyozungukwa na maji. Pia anazungumzia aina ya maisha ya huku kisiwani yalivyo.

Tunatoka na kufika sehemu ya ukaguzi. Namkuta mkaguzi anayenitaka kufungua begi langu. Nafanya hivyo kwa kasi na bila hata kutazama nini ninacho ndani ananiruhusu kuondoka. Natazama hali hii inafanyika hata kwa wageni baada ya kutazama pasi zao za kusafiri sioni wakikaguliwa. Kubwa ni kuwa, kama ilivyo pale bandarini Dar es Salaam, hata hapa hakuna vifaa vya kisasa vya kukagulia.

Tunatoka nje na sitaki kuchukua taxi kwanza. Nataka tukapande daladala za huku. Zamani zikiitwa 'Chai Maharage' na zikiwa na ustaarabu wa mstari mmoja kukaa akina mama na mwingine wanaume.

Naingia katika daladala ambalo urefu wake juu kweli ni adha kwetu warefu. Nakaribishwa kwa kujigonga kichwa juu ya bodi ya gari hili. Kisha nakaa na nagundua kuwa siku hizi hakuna tatizo kwa wanaume na wanawake kuchanganyika katika viti.

Kizuri katika daladala hizi zina idadi maalum ya watu kukaa. Si kama Dar es Salaam ambapo abiria wanaswekwa humo bila kujali hata hali ya afya na usalama wao.

Safari inaanza na ninaanza kuitazama Zanzibar, nchi yenye majumba ya kifahali ufukweni wanakokaa vigogo na yenye vijumba vyenye adha katika maeneo ya watu duni. Kama kuna sehemu duniani unaweza kubaini maana ya matabaka na ukayaona kwa macho ni haya majumba ya Zanzibar, mazuri yanapendeza kweli na ni ya kifahari hasa, lakini ukienda upande wa pili wa kisiwa huko unakutana na picha nyingine.

Makazi ya watu duni yanakatisha tamaa kuyatazama na haya si majengo yaliyoachwa kwa ajili ya kumbukumbu za kitalii bali nyumba za watu duni ambao hawawezi kujenga makasri yenye nakshi!

USIKU WA KWANZA ZANZIBAR
Nimefika hapa ikiwa ni siku ya tatu ya sikukuu ya Idd El Hajj. Huku Zanzibar sherehe hizi hufanyika siku nne na mitaa kadhaa hufungwa kwa ajili ya shamrashamra hizi zinazofanyika hadi usiku wa manane. La kutisha ninalokabiliana nalo ni kukuta watoto wachanga na wa umri mdogo wakishiriki burudani za usiku kama vile hakuna sheria inayowalinda kuhusu kufika kwao katika burudani za watu wazima.

Upo mtaa unaitwa maguniani hapa, ni jirani na viwanja vya gofu na vile vya Gymkhana. Huku kuna kumbi zilizotengwa kwa magunia. Kila ukumbi unapiga aina yake ya muziki na tambua kuwa, kumbi hizi zimeshikana hivi na zipo kama kumi hivi katika eneo hili.

Kuna kelele kali sana, zinaweza kukupasuaa sikio! Shangaa katika kelele hizi nakuta watoto wa miaka mitatu na minne wakiwa wamelala majira haya ya saa nne katika majani nje ya kumbi hizi. Nauliza wenzangu nilioambatana nao, nao wanabaki kushangaa kuona hali hii.

Nazidi kutembea na kisha naamua kuingia katika moja ya kumbi hizi hasa hii inayocheza muziki wa taarabu. Fikra zangu awali ni kuwa humu nitakuta akina mama wazima wakiselebuka muziki huu. Ninayoyakuta ni tofauti na matarajio yangu; nakuta watoto wa miaka kama sita, saba, tisa na mkubwa nadhani humu ni miaka kumi na minane. Hawa wote unawakuta wamekumbatiana wanacheza taarabu.

Nashangaa kumtazama mtoto wa miaka sita akiwa na mwenzake wameshikana na kucheza muziki muda huu. Namtazama namna alivyomkumbatia mwenzake wa kike huku kakivuta kiuno chake katika mtindo mpya uitwao 'mgongo mgongo.' Hili ni jambo ninalolikuta Zanzibar na nadhani litabakia kufanyika hapa hapa Zanzibar maana nchi nyingine hakuna utamaduni huu.

Pembeni kuna vijana kadhaa wanapuliza bangi. Moshi ni mkali sana humu hali inayonifanya kushindwa kuvumilia. Nawaomba rafiki zangu kuondoka humu huku nikibaki na maswali kuhusu; kizazi hiki kijacho kitawezaje kuwa na fikra njema kama kinaachiwa mambo makubwa kuliko umri wao na pili, je Zanzibar haina sheria inayowabana watoto kuingia katika starehe za usiku? Vipi hii mibangi inayovutwa humu bila hata kukatazwa? Ni kweli Zanzibar imehalalisha uvutaji wa bangi? Lakini mbona niliwahi kusikia kuwa pombe ni haramu visiwani huku?

Sheria za Marekani mtoto hawezi kununua pombe achilia mbali kuingia ukumbi wa starehe akiwa chini ya miaka 21. Namuuliza swali hili Jabir Idrissa mwandishi wa habari mwenye makazi yake Zanzibar na ananiambia kuwa, Zanzibar inazo sheria za kudhibiti hali hii lakini wanaopaswa kuzisimamia wameamua kuzisigina. Hata Tanzania Bara sheria hizi zimeanza kupuuzwa hasa Dar es Salaam ambapo siku hizi utakuta wazazi wakielekea katika vilabu vya pombe na watoto wao wadogo.

Madhara ya matukio kama haya ni kutokuwa na kizazi kinachoweza kufikiri vema katika siku za usoni na pia kutokuwa makini shuleni kwa watoto wetu. Zaidi ni kuwa na kizazi kisichotambua mabaya na mazuri. Huku kuporomoka kwa malezi na athari zake ni kubwa ukitazama sasa hivi kuna magonjwa hatari kama ukimwi, matumizi ya dawa za kulevya nk, na vyote hivi vinaacha maswali mengi kuhusu nini utakuwa muonekano wa kizazi kijacho na yapi majaliwa yake!

MADUKANI NA SOKONI


Bei za vitu Zanzibar ziko juu. Hali imebadilika na si kama Zanzibar ya zamani wakati ule kila mfanyabiashara wa bara akielekea huko kufanya manunuzi. Wafanyabiashara wa huku sasa wananunua bara. Zanzibar inaagiza kila zao la chakula kutoka nje.

Kodi za uingizaji vitu Zanzibar zinakuwa juu sasa ukilinganisha na bara kufuatia bidhaa kukabiliwa na kodi za TRA na zile za Zanzibar. Mfano; yai moja sasa lauzwa sh500 huku chakula cha kawaida kama wali na samaki ni sh2500 katika maeneo ya kawaida kabisa yasiyo ya kitalii. Chipsi nusu na robo kuku ni sh2800 na zinaweza kupanda kutegemea na sehemu.

Tatizo la bidhaa kuwa juu linatokana na nchi kushindwa kuzalisha mazao ya chakula ndani. Ardhi inaotesha majani na nimeyakuta yakiwa ya kijani kabisa, lakini jitihada za kilimo ziko katika bahari ya sahau. Kuwepo kwa watalii nako kunachangia bei kuwa juu licha ya kuwa utalii hauwanufaishi moja kwa moja watu duni.

Zanzibar iko katika hatari ya kukosa kabisa namna ya kujiendesha kama anavyozungumza Katibu wa CUF Maalim Seif anaposema kuwa; "magari ya serikali inakuwa vigumu kuyaendesha kufuatia kukosa fedha za mafuta." Uchumi wa nchi hii unategemea sasa mkakati kutoka bara.

Naibu Waziri Kiongozi wa Zanzibar na Waziri wa Habari Ali Juma Shamhuna anatoa hoja tofauti. Yeye anaeleza kuwa uchumi wa Zanzibar licha ya kuyumba lakini hauna athari inayotokana na matatizo ya tofauti za kisiasa kama ambavyo wengi wamekuwa wakisema. Kauli ya Shamhuna ukiichunguza sana utabaini namna isivyo na chembe ya ukweli, ni kauli iliyojikita zaidi katika siasa kuliko ukweli wa maisha na mazingira ya Zanzibar sasa.

UWANJA WA NDEGE

Naamua kutembelea uwanja wa ndege wa hapa Zanzibar baada ya kupata taarifa kuwa kuna ndege nyingi za kimataifa, ndege kubwa zinazotua moja kwa moja hapa kutoka ughaibuni bila kupitia nchi nyingine. Ninapofika nakutana na abiria wengi wageni (watalii) wakichomwa jua kutokana na kukosa sehemu za kukaa wakati wanapotakiwa kujiandaa kuingia katika ndege.

Naamua kutafuta kujua ni ndege za aina ipi zinaingia hapa na mwisho nagundua kuwa kuna ndege za moja kwa moja zinazofanya safari kutoka Ujerumani na kutua hapa, zinazotoka Italia na hata Afrika Kusini. Mfano siku ya Alhamis naambiwa kuna ndege kama sita za kimataifa zinazoingia na kutoka hapa.

Ninapoingia ndani natazama kuwa, hata hapa hakuna vifaa vya kisasa ambavyo vinaweza kutumika kukagulia mizigo. Natafuta mtu anayefanya kazi hapo na kumuuliza kuhusu ndege zinazoingia na abiria wanawezaje kutopoteza muda wao kwa ajili ya ukaguzi wa mizigo; ananiambia kuwa, kuna kipindi wanaweza kupita tu bila kuwatazama sana.

Hapa ninapata swali lingine kuhusu uwezekano wa uwanja huu kuingiza vitu ambavyo havikutarajiwa kuingia nchini. Uwanja huu unalalamikiwa kwa kuwa na njia mbovu ya kuendeshea ndege na pia jengo lake ni chakavu.

Jirani na uwanja huu nakutana na kijimgahawa kisichofanana na hadhi ya uwanja na wageni unaopokea. Nashindwa kufahamu haraka kwa nini serikali isiweze kuwa na hoteli ya hadhi ya kitalii hapa na nini kimefanya kuruhusu mgahawa huu wa hali duni kuwepo.

Katika mgahawa huu nakuta pia watalii wamekaa baada ya kukosa viti katika sehemu ya kukaa kusubiri ndege zao. Uwiano wa mapato, ndege zinazoingia haufanani na hali ya uwanja huu.

Kuna sehemu inaonyesha ulegevu na ulegevu huu unaweza kutokana na kutotambua thamani ya uwanja huu katika kukuza uchumi au mtindo wa utendaji unaojali bora liende! Uwanja huu ni lulu ambayo inachezewa, siku si nyingi mashirika haya ya ndege yatasimamisha safari zake na Zanzibar kukosa watalii hawa.

Yote nayatazama katika fikra huku nikijiuliza swali kuwa, je, lazima safari iendelee kama alivyowahi kuhoji Profesa Euphrase Kezilahabi katika mashairi yake ya "Karibu Ndani?"

KUINGIA KWA MACHINGA
Ninapita maeneo ya Darajani na mwenyeji wangu ambaye pia ni mwandishi wa habari wa gazeti hili anayeishi Zanzibar. Njiani tunakutana na vijana wakiwa wamebeba bidhaa zao kama walivyokuwa pale Kongo jijini Dar es Salaam.

Mwenyeji wangu ananieleza kuwa, sasa hivi kuna kundi kubwa la vijana limeivamia Zanzibar baada ya harakati za kufukuza machinga jijini Dar es Salaam. Wengi wa vijana hawa wanaishi zaidi ya kumi katika nyumba moja na hatari ya kundi hili ni kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu, uvutaji bangi, utumiaji dawa za kulevya mambo ambayo hapo zamani hayakuwepo Zanzibar.

Inawezekana pia kuwa katika siku zijazo utamaduni uliozoeleka hapo Zanzibar, usalama wa raia na wageni hasa watalii kupotea hali inayoweza pia kuchangia kudunisha sekta ya utalii Zanzibar. Kumbuka Zanzibar haina ajira mpya, mji unazidi kuwa duni, lakini hapa panaweza kuwa kweli sehemu bora kwa vijana wa bara kufanya maisha yenye manufaa? Kama wakikosa wanachotafuta, nini majaliwa ya vijana hawa hasa sasa ambapo serikali inawafukuza kufanya biashara bila kupanga nini wafanye?

KUREJEA DAR ES SALAAM
Naamua kurejea sasa Dar es Salaam na jicho langu nalitupa tena katika njia za kuingilia bandarini. Wasiwasi wangu ni kuhusu wepesi wa kupita silaha, dawa za kulevya kutokana na ukweli kuwa Zanzibar haiwezi kabisa kulinda pwani zake na kudhibiti vitu vinavyoingia humo kinyume cha taratibu. Unaweza kuona urahisi huo maana hata sehemu halali za kupitia zina walakini katika ukaguzi na pia ukosefu wa vifaa vya ukaguzi.

Hali mbaya ya kiuchumi Zanzibar inalifanya taifa hili kushindwa kupanga na kujiamulia mambo yake yenyewe. Kuna utegemezi mkubwa kwa Bara na nchi wahisani. Ninapofika sehemu ya kuingilia bandarini ninawaweka wageni weupe kama watano hivi mbele yangu.

Naona wanapigiwa mihuri katika pasi zao lakini kama ilivyo kwangu hakuna ukakaguzi wa mizigo yao kabla hawajaanza safari ya kwenda bara. Naona tunapita tu bila kukaguliwa na kisha tunaingia katika boti kuanza safari ya kuelekea Dar es Salaam.

Inapofika saa 12:00 jioni tunafika Dar es Salaam na hapa kama ilivyokuwa kwa Zanzibar hatukaguliwi mizigo yetu. Tunaingia katika nchi inayojivunia amani, nchi inayotangaza vita dhidi ya rushwa, vita dhidi ya dawa za kulevya; lakini nchi isiyotambua hasara ya kutolinda mipaka yake.

Naanza kukumbuka maana ya Mwalimu Nyerere kutafuta muungano wa Tanganyika na Zanzibar; naona wazi maana ya Bara kuharibikiwa mambo yake mengi kama haitaweza kuisaidia Zanzibar kulinda mipaka yake. Hakuna ukaguzi hapa pia? Najiuliza sana swali hili maana siku hizi kuna mengi, kuna ugaidi na pia kuna kelele hapa zinazoropokwa tu kuhusu athari za dawa za kulevya!

Kuna watu wanafanya semina kuhusu athari za dawa hizi lakini hata siku moja hawazungumzii maeneo yanayoweza kuwa njia ya dawa hizi. Eneo moja sasa ni Zanzibar maana inawezekana kabisa ndege zinazoingia na pia uhuru uliopo katika uwanja wa ndege na bandari vikatumika kama njia za kuingizia visiwani na hata bara. Ninapovuka na kutoka nje ya bandari napumua na kisha nakumbuka kuandika makala hii jambo nililolifanya leo hapa.
 
© boniphace Tarehe 1/13/2007 10:50:00 PM | Permalink |


Comments: 4


 • Tarehe 1/15/2007 9:53 AM, Mtoa Maoni: Blogger Jeff Msangi

  Makene,
  Nimeisoma habari hii na kushindwa kujua niseme nini cha zaidi ya masikini Zanzibar na Tanzania yetu!Tunaambiwa tuna viongozi,tunaambiwa wana dira na muelekeo.Je viko wapi vitu hivyo?

   
 • Tarehe 1/17/2007 3:19 AM, Mtoa Maoni: Blogger SIMON KITURURU

  Inasikitisha!

   
 • Tarehe 1/20/2007 7:18 AM, Mtoa Maoni: Blogger MTANZANIA.

  Nchi yetu inawekwa rehani sasa.Sijui mwisho wake utakuwaje.

   
 • Tarehe 1/21/2007 12:52 PM, Mtoa Maoni: Blogger Ndesanjo Macha

  Kilichonikuna kwenye habari hii sio maudhui yake bali pia mtindo ulioutumia kuiandika. Jamaa zake yule jamaa mwenye madevu anayedhaniwa kuwa anaishi mapangoni wakitaka kufanya unyama nchini kwetu kutakuwa ni kilio tupu. Watu wanakagua mizigo ili kama alama tu. Hakuna wanachokagua. Halafu umetaja kidogo kuhusu makampuni ya "ulinzi" na watu wanaowaajiri. Habari hii ni ndefu sana. Angetokea mtu aandike habari ya kipepelelezi kuhusu hili tungejua mengi sana.

  Tuje kwenye "mteja mfalme." Bado maeneo mengi ya biashara hayajajua kuwa unapomjali mteja unaongeza thamani ya biashara yako. Kama ulivyosema, zikija biashara toka nje zinazojali wateja, basi za kwetu kilichobaki ni kunyoosha mkono wakati tatizo lenyewe ni dogo. Jali mteja. Rahisisha namna ambayo mteja anapata huduma na taarifa mbalimbali za huduma zenu.

   
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved