Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Tuesday, January 30, 2007
NI SIFA HIZI ZILIZOMFANYA JK KUMBAKIZA MRAMBA?
"MU wapi niwatazame
Semeni msiachame
Mawazo yasiwachome
Kwa bezo msilalame.

Hamna jipya mseme
Wajumbe msiwatume
Tazameni mjipime
Majaribu yawakome!"


Sina
shaka huu mzima, nakusalimu mtu duni, nakusalimu mtu bora! Salamu ni muhimu walisema wahenga, lakini haziwezi kulinganishwa na ndoto, hasa ndoto ya maskini inayoweza kupaa hadi mbingu ya saba.

Ndoto ya maskini huchanganywa na vitu vitu vingi mfano; fikra za kuweza kumudu maisha, fikra za kujenga uwezo wa kukabili adui na fikra za kujenga himaya ya kudumu katika mafanikio. Ndoto hizi zaweza kuwa za mchana au usiku na zote zina athari tofauti kufuatia mandhali zinapotokea.

Ninaota sana usiku siku hizi. Nimeota mada hii na naamua kuindika leo. Mwandishi mzembe hulala usiku na kukesha mchana. Nasikia viongozi wetu nao huzungumzwa kuwa wanakesha sana usiku wakiwazia shida zetu. Siamini hilo, maana sijawahi kuona nyumba zao umeme ukiwaka usiku kucha. Kwanza ni vigumu kuchungulia nyumba zao kufuatia kuta zilizowekwa kuzunguka nyumba hizo za vigogo kuwa ndefu. Kuta hizi za nini kama wanakesha? Je, anayekesha naye anaogopa mwizi? Hapana, inaonyesha hawakeshi hawa bali wanalala sana tu usingizi wa pono!

Mwandishi mahiri hupata visa usiku. Kwake usiku ni wakati tulivu kupata visa lakini kwa wavivu wakati huu hupewa sura ya starehe ya kushangilia usingizi. Usiku ni wakati wa tabu pia kwa watu jasiri lakini unatumiwa kama liwazo la unono kwa woga! Waandishi wengi wa ngano wamewahi kusema kuwa, usiku ni kipindi cha mawewe, kipindi kisichotoa muwasho wa kupata na kuandika visa kwa mwandishi.

Rais wetu Jakaya Kikwete anaendelea na safari zake za kila wakati ughaibuni. Wiki hii amekuwa Uswizi na kisha akaenda Ethiopia. Sikupta taarifa mapema kuhusu aina ya timu za michezo zilizopo katika nchi hizo ili niweze kubaini kuhusu kama ataenda kuchukua jezi za timu hizo au la! Nadhani Uswisi kutakuwa na timu za michezo ya kuteleza katika barafu au kriketi!

Sijui na sidhani kama nitajua mapema, lakini safari hizi hata zitetewe vipi; faida yake na uwiano wa hasara havilingani! Ni lini tutaacha wageni waje kwetu na kukutazama kama sisi tutazidi kuwafata huko huko? Watatambuaje matatizo yetu wakati tupo kwao na kufurahia vyao? Hapana waheshimiwa hapa msinizibe mdomo nitaendelea kusema tu!

Leo nimeamua kukusabahi mkuu wa kaya yetu Rais Jakaya Kikwete. Wakubwa kama nyinyi mwahitaji maneno machache ya kuwaeleza maana mna majukumu mengi. Utanihurumia maana sina machache leo, nakuandikia mada hii leo na nitaimalizia juma linalofuata.

Nimekumbuka ulikuwa Uingereza wiki iliyopita. Tunamshukuru Mola kuwa alikurejesha salama nyumbani ili uweze kufanya kazi zako na kisha ukaweza pia kupanga safari nyingine. Habari za safari yako ya Uingereza tulizipata sana na hakukuwa na ukame wa taarifa kama alivyotaka kukuambia mhariri wa habari katika gazeti ulilolianzisha wewe, gazeti linaloendeshwa kwa kodi zetu sisi wana kaya hii.

Ukiwa huko Uingereza ulikumbana na gazeti moja la huko lililokuwa na habari kuhusu nchi yako. Gazeti hili liliitunza habari hiyo hadi ujio wako ufike, ulipofika likaichapisha. Lengo la gazeti hili lilikuwa kutoa tahadhari kwako na kwa raia wa Uingereza kuhusu nchi ya Tanzania. Lengo hili lina sifa hasi na chanya ila hasi ni zaidi kuliko chanya kwetu sisi watanzania.

Habari ile haina hasara kwa Uingereza na sioni maana ya wao kupoteza gharama zao kuichimbua. Tulitakiwa sisi watanzania kufanya hivyo, hatukufanya! Nani rafiki kama huyu anayeona uchungu wa hasara inayobebeshwa kwa raia maskini kufuatia viongozi wa nchi kutokuwa makini hasa wanapofanya manunuzi ya vitu vya gharama kubwa? Uchungu unaotokana na viongozi hao kutokutathmini kwa kina wapi na nani wanamhusisha katika manunuzi hayo, achilia mbali aina ya kitu kinachonunuliwa?

Hii imekuwa kama jadi yenu viongozi wa Tanzania. Mnafanya mambo mengi kwa majaribio hata sasa ambapo nchi ina uhuru wa miaka 45. Na zaidi ni kuwa hamtaki kukubali makosa na kukiri mlipoteleza ili wengine wasirejee makosa yaliyowahi kutokea.

Hali hii ya kutaka kuwa wakamilifu daima inazifanya serikali zinazofuatia kuendelea kubeba matatizo yaliyosababishwa na zile zilizopita. Na kibaya pia ni hiki cha kuendeleza enzi za watawala waliofanya vibaya kuingia katika awamu mpya bila kujipanga na kubadilika. Madhara ya suala hili ni kuendeleza kuboronga katika serikali zinazofuata kama tunavyoendelea kuona!

Usihofu mheshimiwa rais, na sisi waandishi wa Tanzania tutatunza habari za nchi hizo na kuwasubiri siku watakapokuja hapa kwetu. Lakini napatwa swali hapa, watawezaje kuja huku wakati unawafata huko huko na hizi ziara zako za ughaibuni? Inawezekana ikatokea siku moja na hiyo ndiyo tutakayotumia kuwaweka kitimoto ili wapate nao freshi mithili ya vile walivyokukalisha wewe huko Uingereza hadi ukahamaki kidogo!

Lakini jambo la kukumbuka ni kuwa; wao wamezoea kuulizwa maswali ya kushtukiza tofauti na wewe ambaye mara nyingi watu wako wanataka tukuandikie kwanza maswali kisha wakutafutie majibu. Wao wanafahamu sana maana ya vyombo vya habari na huko vina nguvu kuliko hapa, achilia mbali rasimu ya sheria iliyo katika Baraza lako mheshimiwa rais inayotaka kukata uhai wa afya za habari hapa nchini na kutufanya wapiga tarumbeta wa himaya ya watawala.

Rais, kweli suala la manunuzi ya rada ni aibu ya Uingereza? Tanzania inapigana na nani hadi ing'ang'anie kununua rada ya aina hii! Mna mpango wa kuanzisha vita na nani ili wananchi wenu tuanze maandalizi ya kuwa wakimbizi? Kama hakuna nini hasa wasiwasi wenu ambao utawatofautisha na watu mliokuwa mnatumia nafasi zenu kutafuta upenyo wa kujijengea faida?

Rais, Uingereza ione aibu ipi kama imeweza kuibua uozo huu, uozo unaochimbua madhambi ya vigogo ambao kauli zao tu zinathibitisha nia yao mbovu dhidi ya raia maskini wa taifa hili? Nafahamu macho ni yetu mafupi kuona, lakini tunaweza kujenga walau hoja hafifu! Hoja hizi zitaiishi kitambo kabla ya kupatikana majibu maridhawa na siku majibu yakitokea uchafu utawagusa ninyi mlio juu!

Ni kweli rada ilikuwa muhimu hivyo kuliko hata umeme mheshimiwa rais? Kuliko hata njaa iliyotutafuna mwaka jana? Kuliko hata ukosefu wa madarasa na huduma mbovu za afya? Kuliko ujenzi wa barabara na hata madarasa na mikopo ya wanafunzi? Je, ni macho yetu sisi ambayo hayaoni? Kama ndivyo, toeni sababu na sio vitisho kama alivyokuwa akitoa Basil Mramba wakati akitetea manunuzi ya rada na ndege ya rais.

Rais kumbuka kuwa, waziri wa Tanzania wa Mambo ya Nje katika miaka kumi iliyopita ni wewe. Nafasi yako ilikuwa kubwa katika kufahamu jema lolote na baya kuhusu Tanzania. Kuhusu linalokusudiwa, linalofanywa na hata linalotarajiwa kufanywa kwa ajili ya nchi yetu. Nafasi hii ilikupa fursa kuwafahamu adui na rafiki zetu. Uliweza kufahamu nani anatuibia na nani anatusaidia! Ulijua mengi sana na hata haya ya rada na ndege uliyafahamu kwa undani sana, huwezi kuepa hili!

Sisi wa hapa ndani, tuliishia kumsikia Waziri Basil Mramba akizungumza kwa kujiamini wakati alipokuwa akiratibu mkakati wa manunuzi ya dege la rais pamoja na hili rada. Mramba aliwahi kutoa kauli yenye kuongeza maswali kadri siku zinavyoongezeka bila kupata majibu, hasa kuhusu nini kilimfanya kujiamini kiasi hicho wakati huo na kama ilivyo sasa.

Inawezekana Mramba alirithi mfumo wa kauli za viongozi waliopo nchini. Nitumie mfano wa waziri Mkuu wa zamani Cleopa Msuya aliyewahi kusema kuwa; kila mtu atabeba msalaba wake. Kauli hiyo kwa kiasi kikubwa ilikuwa ikitetea kukua kwa ufa kati ya tajiri na maskini katika nchi hii. Kauli hii inazungumzwa kuwa, ilikuwa tathmini ya upanuzi wa nguvu za kiuchumi kwa matajiri na viongozi wa serikali katika Tanzania kulinganisha na watawaliwa. Hali hii ilianza kujiibua kipindi cha awamu ya pili, na ni kipindi hicho hicho ambapo Msuya alitoa kauli hiyo na yeye akiwa Waziri Mkuu.

Mramba akaliambia Bunge kuwa; watanzania wako radhi kula majani lakini rais wao anunuliwe ndege ya kifahari, ndege inayofanana na hadhi yake. Mramba hakutaja wala kufafanua kuhusu hadhi hiyo ya rais hasa pale anapomzungumzia rais ambaye anaweza kuwa ameshindwa, kutumia rasilimali za nchi kunufaisha wazawa badala ya wageni. Pale utawala wa rais huyo, unapokuwa umetumika sana kutanua ufa kati ya tajiri na maskini, umesaini mikataba kwa makampuni ya kigeni na kubinafsisha mashirika ya umma, bila kujali faida kwa nchi na tena bila kuonyesha chembe ya uzalendo kwa nchi na watu wake.

Huyu ndiye Mramba, Waziri wa Fedha (wakati huo) aliyetarajiwa kuwa asingekuwemo kwenye kikosi cha awamu ya nne. Kinyume na fikra hizo za wachambuzi wa masuala ya siasa, Mramba akabakia katika kikosi na safari hii akapewa wizara nyingine nyeti. Wizara ya miundombinu na sasa nyeti nyingine (Viwanda na Biashara), ili aweze kutazama namna njema ya kuiunganisha Tanzania na kuipa miundo mbinu yenye manufaa. Ili aweze kukuza uchumi na kisha kuitanua mapinduzi ya viwanda na biashara katika kipindi hiki cha soko huru.

Kabla hakujacha, Mramba akaibuka na kugawa kiasi kikubwa cha fedha katika ujenzi wa barabara inayopita katika jimbo lake. Wabunge wakambana na kutaka kujua nini hasa kiburi cha yeye kufanya maamuzi kama haya aliyowahi pia kulalamikiwa Msuya na jimbo lake la Mwanga.

Hata hivyo nguvu za chama zikatumika. Mramba akapitishiwa ulaji wa jimbo lake na kuziacha sehemu mbalimbali za nchi zenye kukosa barabara bora zikibakia na adha hiyo huku barabara ya jimboni kwa Mramba ikipitishiwa fedha za ujenzi.

Kitendo hiki cha kupendelea jimbo lake, kilitosha kutoa kauli kutoka kwa rais juu ya Mramba. Lakini pia kulikuwa na hili la upitiaji upya wa mikataba ambayo mingi ilipitishwa wakati Mramba akiwa Waziri wa Fedha. Kama mikataba hiyo ilionyesha utata, basi hakukuwa na haja ya Mramba kubakia katika ngazi za madaraka katika serikali ya awamu ya nne.

Sababu za hoja hiyo ni kuwa; awamu ya nne ilichaguliwa huku kukiwa na imani toka kwa wananchi kwa serikali; mosi, serikali kusafisha kila uchafu uliofanywa na awamu ya tatu sambamba na waliohusika kuufanya na pili, kurejesha haki ya umma kuhusu kila kilichopitishwa bila kujali maslahi ya taifa.

Utetezi wa Kikwete kuhusu umuhimu wa rada, unaonyesha namna anavyokubaliana na taifa maskini kufanya manunuzi makubwa yasiyotazama kipaumbele katika mipango ya kupambana na umaskini. Serikali isiyotazama lipi lianze na lipi lifuate huku pia ikitazama lipi lina athari kubwa kwa wananchi ukilinganisha na lingine.

Kimsingi kauli ya Kikwete inampambanua kuwa, alikaa kimya kipindi cha awamu ya tatu kwa sababu tu alikuwa hataki kuwaudhi wakubwa kufuatia kuwepo lengo lake la kuwania urais. Inawezekana pia alikuwa mshirika wa karibu kabisa hivyo hakutaka kujichafua hali inayomtia hofu kutoa kauli nzito sasa!

Mrambaalikuwa miongoni mwa mawaziri wa kwanza kwanza kutetea safari zisizoisha za rais ughaibuni. Kimsingi naye ananufaika sana na safari hizo maana zinamhusisha pia. Hii pia ni hoja ya kuonyesha umuhimu wa Mramba kuwemo katika kikosi cha Kikwete.

Majibu ya Mramba kwa wabunge pale alipobanwa baada ya kupanga fedha nyingi katika barabara za jimbo lake; hasa liposema kuwa na yeye ni mbunge, haikuwa kauli ya kukata tamaa. Inaonyesha ilikusudia nafasi yake kufahamu inatokea wapi. Ilionyesha uhusiano mkubwa na mteuzi wake na ilikuwa ni angalizo kwa wanaomshutumu.
Kimsingi utetezi wa baraza zima la mawaziri kulikofanywa na Kikwete wakati wa maadhimisho ya mwaka mmoja wa utawala wake ni jibu jingine kuhusu kuwepo kwa Mramba serikalini licha ya yeye kuhusika na kutetea mambo kadhaa yanayotoa maswali kuliko majibu. Mramba ni msafi kwa mujibu wa Kikwete kama walivyo mawaziri wake wote na hii ni sababu kubwa ya JK kubakia naye?
 
© boniphace Tarehe 1/30/2007 12:36:00 AM | Permalink |


Comments: 3


  • Tarehe 1/30/2007 10:18 AM, Mtoa Maoni: Blogger Jeff Msangi

    Nimekusoma Makene,
    Umenena yaliyoko moyoni,umejitwika ushujaa wa aina yake.Tuketi tujiulize,hivi wawekezaji(wezi)watarajiwa wanaangalia tabasamu la raisi au mazingira yatakayowanufaisha wao na biashara zao?Hapo ndipo utagundua kwamba anayekuambia safari za raisi zina faida ana lake jambo.Tusimfumbie macho.

     
  • Tarehe 1/31/2007 6:41 PM, Mtoa Maoni: Blogger mwandani

    Safi sana Makene. Umesema kwa upole na kwa kueleweka. Siku hizi tunajua, hatudanganywi kirahisi. Wanaosifu, wanasifu wakiweka maslahi mbele.

    Habari hii ya kwenye gazeti la Tanzania la leo, kwa mara nyingine tena imekuwa kama limetolewa kwenye ukurasa wako. Endeleza kazi.

    Rada: Sasa ni mshikemshike
    http://www.ippmedia.com/ipp/alasiri/2007/01/31/83482.html

    2007-01-31 17:44:55
    Na Mwandishi Wetu, Jijini
    Wakati uchunguzi kuhusiana na ununuzi wa rada ya `bei mbaya` nchini ukiendelea kufanyika nchini Uingereza, sakata hilo limeendelea kupamba moto siku hadi siku.

    Baadhi ya watu wameshaanza kumnyooshea kidole aliyekuwa Waziri wa Fedha wakati rada hiyo ikinunuliwa, Bw. Basil Mramba na kumtaka ajiuzulu wadhifa alio nao sasa wa Uwaziri wa Viwanda na Biashara katika Serikali ya awamu ya nne.

    Baadhi ya wananchi waliotuma maoni yao kwa kituo cha Utangazaji cha BBC, Idhaa ya Kiswahili leo asubuhi wamesema kuwa Waziri Mramba alitetea kwa nguvu zote ununuzi wa rada hiyo na sasa lazima ajiuzulu.

    ``Waziri Mramba alisema hata Watanzania wakila nyasi, ndege ya rais na rada vitakuja...huyo ndiye anapaswa kuwa wa kwanza kuwajibishwa,`` akasema msikilizaji mmoja wa BBC.

    Na kisa cha baadhi ya wananchi kumuwashia moto Waziri Mramba na kumtaka ajiuzulu ni juu kilifuatia malumbano makali yaliyozuka kwenye kikao cha Bunge huko Uingereza jana kuhusiana na uuzwaji wenye utata wa rada hiyo kwa Tanzania.

    Kwa mujibu wa Shirika la Habari Uingereza, BBC, wabunge nchini humo jana walitumia zaidi ya masaa matatu kujadili uhalali wa manunuzi ya rada hiyo yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 40 za Kibongo, uliofanywa na Serikali ya Tanzania kwa Kampuni ya BAE System.

    Mojawapo ya hoja zilizoibua malumbano ya masaa matatu kuhusiana na rada ya Tanzania katika kikao kilichochukua masaa nane, ni juu ya kutolewa kwa kamisheni ya zaidi ya Dola za Kimarekani Milioni 12.

    Wabunge hao walioongozwa na Msemaji Mkuu wa chama cha upinzani cha Conservative wakasema mauzo hayo ya rada kwa nchi maskini kama Tanzania kamwe hayakubaliki.

    Wabunge hao wakaibana zaidi Serikali ya Waziri Mkuu Tony Blair kuwa Tanzania yenye madeni tele inahitaji zaidi kuboreshewa huduma kama za afya na elimu.

    Wakasema kuiuzia rada hiyo ya bei mbaya ni sawa na kuiongezea mzigo mkubwa wa madeni.

    Msemaji Mkuu wa kambi ya upinzani aliibana Serikali kwa kuitaka iweke bayana kama ingegundua kuwepo kwa kamisheni hiyo ya Dola Milioni 12 za Kimarekani ingezuia utoaji wa leseni ya ununuzi wa rada hiyo au la.

    Katika malumbano hayo, wabunge wa chama tawala cha Labour walikuwa wakiunga mkono mauzo ya rada hiyo kwa Tanzania.

    Wakati wa ufafanuzi, Waziri aliyekuwa akimuwakilisha Tony Blair bungeni alikiri kuwa Serikali yake imepata madai ya kuwepo kwa rushwa katika manunuzi ya rada hiyo.

    Hata hivyo, Waziri huyo akasema hawezi kuzungumzia kiundani suala hilo, kwa madai kuwa bado uchunguzi wake unaendelea.
    • SOURCE: ALASIRI

     
  • Tarehe 2/01/2007 2:23 PM, Mtoa Maoni: Blogger Ndesanjo Macha

    Nimepata habari yako toka kwa Jeff. Kiboko. Moto. Ujasiri na umakini wako ndio silaha tuliyonayo dhidi ya uozo katika viambaza vya utawala.

     
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved