Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Sunday, January 21, 2007
MBIO ZA SHIRIKISHO AFRIKA MASHARIKI ZIMEFICHA SIRI GANI?
AGENDA ILIYOPO

NCHI za Tanzania, Kenya na Uganda kwa sasa zina kamati maalum kwa kila nchi zinazokusanya maoni. Lengo la maoni haya kutoka kwa wananchi ni kupata ruhusa yao kama wanahitaji kuwepo kwa Shirikisho la Afrika Mashariki au hapana.

Kitendo hiki cha ukusanyaji maoni ni cha muhimu sana kwani kinatoa fursa kwa wananchi ambao ndio wamiliki wa mataifa yao kukubaliana ama kuongeza sifa za utaifa au kubakia na huo walionao. Ni kitendo pia cha kukubali kuongeza watumiaji wa rasilimali za taifa lao na vile vile kujitanulia mianya ya kuishi.

Dhana rahisi ya ubepari ni kujitanua zaidi za mipaka yako. Dhana hii hii humsaidia bepari kuweza kupata vile ambavyo hana ndani ya mipaka yake na pia kumuwezesha kutumia uwezo wa wengine kuendeleza vile alivyo navyo ndani yake. Dhana hii inaweza pia kutumika kuthibitisha agenda ya umuhimu wa shirikisho na pia ikatumika kulipinga. Ulimwengu wa sasa unatawaliwa na ubepari. Mfumo huu haukufuatwa na mataifa mengi ya Afrika baada ya uhuru lakini baada ya kuanguka kwa USSR sasa nchi nyingi zimelazimika kusahau mfumo wa kisoshalisti au ukomunisti. Yamebaki mataifa kama Venezuela na Cuba yanayokumbatia sera hizi na kuanzisha vita mpya ya kupandikiza itikadi za kisoshalisti.

MABADILIKO YA AGENDA

Tangu kuvunjika kwa jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977, hakukuwahi kuwa na majibu ya wazi kuhusu nini kilisababisha sana hadi jumuiya hiyo ivunjike. Je, ulikuwa ulafi wa madaraka, uchu wa mali, hofu ya kumezwa na mataifa ya magharibi, hujuma au nini hasa? Majibu yaliyopo katika vitabu vya historia yanaweza kuzua maswali yasiyo na majibu. Je, vipi sasa tumeshapata majibu ya kuridhisha hadi tukubali kuwa na jumuiya hii mpya na nini malengo baada ya kuwepo kwake?

Wajanja wa sasa wamekuja na mtindo wa kubadilisha majina. Wanajua wananchi wa nchi hizi sio wazuri kutunza kumbukumbu. Kutokana na hali hii badala ya kuita Jumuiya ya Afrika Mashariki wakaibuka na Shirikisho la Afrika Mashariki, ubadilishaji wa maneno huku lengo likibakia lile lile la muungano na utanuzi wa utaifa kwa nchi zilizopo ukanda huu.

Kabla wazo la kuunda upya jumuiya au shirikisho jipya kulipaswa hoja ya awali kutoka kwa wananchi. Hili ni kosa la kwanza lililofanywa na Rais Benjamin Mkapa, Daniel Arap Moi na Yoweri Museveni; wakati walipoibuka na wazo hili upya hasa pale waliposaini mkataba wa kuanzishwa tena Jumuiya hii Julai 2000 na kisha kuizindua rasmi Januari 2001. Viongozi hawa walitakiwa kabla ya kuanza mikakati ya aina yoyote kuwashirikisha wananchi katika nchi zao ili watoe maoni. Ni kipindi hiki ambapo kungewezekana kuulizwa maswali ya nini kilisababisha jumuiya ya kwanza kufa na kwa nini tuhitaji jumuiya nyingine.

Baada ya hapo kungekuwa na elimu ya umuhimu wa muungano kama huu sasa na namna dunia ilivyo na mwanya wa kuweza kuiruhusu iwepo kuliko ilivyokuwa wakati ule wa kabla ya 1977. Kutokufanya hivi, ilikuwa ni kudharau wapiga kura, kudharau wananchi na kweli ilikuwa kushindwa kwa utawala unaojali watu katika kufikia maamuzi makubwa yanayohusu maisha na mataifa yao.

Hata kabla ya kuanza zoezi hili la ukusanyaji maoni, agenda ilikuwa kama wananchi wanakubaliana na nchi hizi kuunda shirikisho au la! Kabla hata agenda hii haijaanza kujadiliwa huku kukiwa na maswali kutoka kwa wananchi kuhusu maana ya ukusanywaji wa maoni kuhusu kutaka au kukataa shirikisho, hakukuwepo maoni kutoka kwa wananchi kabla ya kufikia hatua kama; upitishwaji wa sheria ya Umoja wa bandari 2005, uanzishwaji wa Bunge la Afrika Mashariki, namna ya upatikanaji wa uwakilishi katika Bunge hilo na mengine kadhaa, kukawa na kuingizwa kwa Rwanda na Burundi katika jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hapa ikaanza kutambulika mchezo wa msamiati. Maneno mawili tofauti yakaanza kutumika lakini yakiashiria kuelekea maana ile ile. Jumuiya na shirikisho na ikafafanuliwa kuwa Rwanda na Burundi zinaingizwa katika jumuiya ikiwa ni hatua ya kufikia shirikisho. Shirikisho ambalo halijaundwa na ambalo halijapata ridhaa ya wananchi wa nchi zote achilia mbali kukusanywa kwa maoni kutoka kwa wananchi hao.

Mambo yakiendelea hivi kukaanza kukusanywa maoni na agenda ikawa; uharakishaji wa shirikisho au upingwaji wake! Nini maana ya uharakishwaji kama shirikisho hilo halijakubaliwa? Maana rahisi ni kuwa haja ya jumuiya ilishapitishwa na umuhimu wa shirikisho maridhawa na sasa ni uamuzi wa lini shirikisho hilo lianze, huku wakubwa wakiwataka wananchi wao kuharakisha shirikisho hilo na sio vinginevyo.

KAULI TATA NA MASWALI ZAIDI

UGANDA

Mwaka 2006 kabla ya Kombe la Dunia Rais Yoweri Kaguta Museveni aliwahi kukutana na waandishi wa habari wa nchini kwake na kuwalaumu kujisahau kuandika kuhusu masuala ya Afrika Mashariki wakati wako mbele sana kuandika mambo yanayoyahusu mataifa ya Ulaya na Marekani.

Museveni akawaambia kuwa rasimu ya nchi hizi kuungana ilikuwapo kwa siku nyingi lakini hakukuwa na waandishi wa habari waliokuwa wakiiulizia na kuiandika kwa wasomaji wao. Swali hili la Museveni linatoa picha mbili; moja ni hii ya kuonyesha kuwa waandishi wa habari hushabikia sana mambo ya nje na kunyima nafasi kwa mambo ya ndani na pili ni, usiri wa rasimu yenyewe uliokuwepo kati ya viongozi wa nchi hizi hali iliyotokana na wao kuanzisha agenda bila kuchukua mawazo kutoka ngazi za nchini kabisa za uwakilishi wa wananchi. Kubwa hapa ni kuwa, viongozi waliamini kuwa wao ndio mwisho, wao ndio vinara wa maamuzi na wao ndio kauli ya kukubalika na sio kupingwa!

Museveni anabakia kuwa kinara na mwelewa wa juu kabisa kuhusiana na namna ya uendeshaji mambo hapa Afrika Mashariki na inawezekana sasa agenda nyingi akawa anazipa nguvu yake kufuatia ujanja wake na uelewa kuliko marais wenzake ambao; mosi ni wageni madarakani na pili hawakupitia misukosuko mikubwa katika nchi zao kama alivyo yeye.

Ni kiongozi anayesifika katika kupigania kupandisha uchumi wa nchi, uchumi uliokuwa umeshuka kwa kiasi kikubwa, kuweza kuleta chembe ya amani katika nchi iliyokuwa haitulii na pia harakati zake dhidi ya madhara ya ukimwi, ugonjwa uliokuwa na athari kubwa nchini kwake hadi kuupunguza na kufikia hatua ya kuifanya Uganda kupata taswira mpya, heshima dhidi ya mapambano ya ugonjwa huo hatari duniani.

Kwa kutumia ujanja wake, akashawishi mabadiliko ya katiba ili apate muda zaidi wa kutawala. Alishagundua kuwa Kenya kuna kiongozi mgeni, Mwai Kibaki na Tanzania ilikuwa katika kubadili awamu toka ya tatu kwenda ya nne, hivyo kungekuwa na rais mpya, Jakaya Kikwete.

Akafanikiwa kuongezewa muda na kisha akaibuka na agenda mpya, akatangaza nia yake ya kuwa Rais wa kwanza wa Shirikisho la Afrika Mashariki. Uamuzi huu akautangaza kabla hata shirikisho hilo halijapitishwa, halijakubaliwa na wala hakujawa na mkakati wa kuunda kamati za kukusanya maoni kutokwa kwa wananchi wa nchi hizi.

Kukatokea hoja ya kuharakisha shirikisho la Afrika Mashariki. Hii ikawa hoja mbadala ya ile ya ukusanyaji maoni kuhusu kuwepo au kutokuwepo kwa shirikisho hilo. Hoja hii ikaja na sasa inajadiliwa kila nchi huku ikionyesha wazi kuwa; kuna siri katika serikali za nchi hizi, siri isiyofahamika kwa wananchi.

Ni siri hii inayowafanya viongozi wa nchi hizi kudhani kuwa wananchi wao hawana uelewa wala nguvu ya kukataa shirikisho. Ni hoja hii inayowafanya viongozi hao sasa kuwaweka katika upande wa kuwalazimisha kukubaliana na kuharakishwa kwa shirikisho badala ya kujadili kuhusu kukubali shirikisho hilo au kulikataa.

Hata hivyo ujanja wa mtu kama Mseveni kwa waganda ni rahisi kushinda mathalani anapotumia mfano wa nchi yake kukosa bandari na hivyo kuwahamasisha wananchi kukubaliana na jumuiya hii kwani watanufaika na uingizaji wa bidhaa zao kwa gharama nafuu. Hoja hii kwa waganda ina nguvu mno kiuchumi lakini inaweza kubeba agenda ya siri ya Museveni kutaka kuwa rais wa shirikisho na kisha akafanikiwa kupata anachokitaka.

KENYA

Nchini Kenya juma lililopita kumeibuka hoja nyingine kutoka kwa Waziri wa Umoja wa Kanda ya Afrika Mashariki John Koech. Hoja hii inafanana na ile ya Museveni dhidi ya waandishi wa habari wa Uganda.

Koech anasema kuwa; waandishi wa habari wa Kenya ni maadui wakubwa wa umoja wa Afrika Mashariki na wanaonyesha uadui huu kwa kuchapa habari nyingi zinazoonyesha ubaya wa jumuiya hii kuliko mafanikio yake.

Kauli nyingine kutoka Kenya ni ile iliyotolewa na Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Afrika Mashariki (EABC) Arun Devan inayosema kuwa ni vyombo vya habari vinavyoweza kuunganisha shirikisho hili au kulivunja. Sababu zaidi kutoka Kenya ni kuwa kuna uelewa mdogo kutoka kwa waandishi wa habari jambo linalowafanya kuandika kufuatia kampeni badala ya kusifia jitihada hizi.

Kenya pia imewahi kulalamikiwa kutokana na viongozi wake kuonesha kuwahamasisha watanzania kutokuwa na hofu dhidi ya nchi hiyo kuhusu shirikisho hili. Ni wazi kuwa, hofu ya Tanzania kuingia katika shirikisho inatokana na uoga wake katika kujilinganisha na Kenya katika masuala ya viwanda, uchumi kwa ujumla na huduma nyingine za jamii.

Kielimu, Kenya ina wasomi wengi kulinganisha na Tanzania na Uganda na pia nchi hii inaongoza kwa kuwa na wananchi wake wengi nje, wananchi ambao wanaweza kuitumia fursa hii ya Afrika Mashariki kwa mafanikio yao kibiashara na kiutanuzi wa uchumi. Kwa ujumla kuna unafuu mkubwa kwa Kenya sasa kuliko hata ilivyokuwa huko nyuma kunufaika katika shirikisho hili, mosi kwa kupata ajira zilizo wazi katika Uganda na Tanzania na pia kupata ardhi nchini Tanzania kufuatia Kenya kujaa.

Jumuiya ya kwanza ilivunjika kukiwa na lawama zaidi kwa Kenya kujiunga na kambi ya mabepari wa Uingereza na Marekani. Safari hii Kenya ndiyo inayopigania sana kuingia katika jumuiya hii baada ya kubaini kuwa, itasadia kutatua kero za wananchi wake. Hata hivyo nchi hii bado ina sifa kubwa ya ufisadi kutoka kwa viongozi wake na inatambulika duniani kutokana na kutoweza kabisa kupambana na rushwa hasa inayohusu mikataba ya manunuzi ya vifaa hewa vya serikali.

Hata hivyo ukabila uliopo Kenya na mfumo wao wa siasa unaweza kuwakwaza watanzania ambao wamezoea maisha ya kuziba midomo hata wanapoumizwa. Kwa Kenya kila raia anaweza kupiga kelele na ndio maana maandamano ya siasa hayaishi Kenya na tabaka la kati lipo na linafanya kazi yake tofauti na Tanzania ambapo hakuna sasa tabaka la kati linaloweza kusimamia mambo yake vema. Asilimia kubwa ya wananchi wa Tanzania ni tabaka la chini, wasiokuwa na elimu ya kutosha na waishio maisha duni.

TANZANIA

Awamu ya nne inaingia madarakani mwaka 2006 na kisha inaanzisha wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Wizara hii inatoa picha wazi kuwa kuna makubaliano yamefikiwa na kwamba Tanzania iko tayari kuingia katika shirikisho la Afrika Mashariki. Tatizo ni kuwa, nchi hii haijawahusishwa wananchi wake katika kutoa idhini ya mchakato huu. Kama zilivyo Kenya na Uganda, Tanzania nayo imebariki usiri wa kuingia katika shirikisho hili huku ikiamini kuwa nguvu za serikali zinatosha hata kama wananchi wake hawatakuwa na dhamira ya wazi ya kukubali uamuzi huu.

Hali inabadilika na kisha wazo la kukusanya maoni ya kufikia shirikisho yanapenyezwa kwenye mkutano wa wakuu wa nchi hizi lakini yakiwa na nguvu zaidi kutoka Tanzania. Wachunguzi wa masuala ya siasa wanaona tukio hili ni njia ya Rais Kikwete kusimamisha harakati za mtangulizi wake Mkapa katika kuwakimbiza watanzania katika jumuiya ambayo wanafahamu kuwa watabakia wasindikizaji.

Lakini kinyume na matarajio ya wengi, Tanzania nayo inajiunga katika utata wa agenda na kukubali kutojadili kukubali shirikisho au la na badala yake nayo inaanzisha kampeni ya kuharakisha shirikisho.

Huku nyuma, Tanzania kupitia wizara yake ya Afrika Mashariki imewahi kutoa matamko ya kutoitaka Kenya kuingilia maamuzi ya Tanzania kuhusu kama wananchi wa nchi hii wanakubali kujiunga na shirikisho au la. Kauli hii inaonesha kuwa kuna ugumu kutoka Tanzania na pia kuwa nchi hii inaonyesha wazi kuwa inataka kuwahusisha wananchi wake watoe maamuzi.

Waziri wa wizara hiyo anadaiwa pia kususia vikao vya nchi hizo vilivyofanyika Arusha mwaka jana na baadaye anahamishwa katika wizara hiyo. Lakini baadaye kidogo wizara hiyo inayofanya ziara nchi nzima inaonekana ikipingana na dhana ya kuelimisha wananchi na kukusanya mawazo yao kuhusu kama weanataka shirikisho na badala yake inaanza kutoa majibu ya hofu za wananchi. Inafikia hatua inajadili hata suala tata la Zanzibar na kuwataka wazanzibar kutohofu licha ya kuwa uchumi wao unaduni na kukiwa na hoja ya Tanzania Bara kufidia uchumi huo wakati huu wa muungano wa nchi hizi.

Naibu Katibu Mkuu wa Ushirikiano wa kisiasa wa Afrika Mashariki wiki iliyopita anasema; wananchi wakisema ni mapema mno kuanzisha shirikisho wanapaswa watuambie tuanzishe lini, lakini hapa suala si tuanzishe au tusianzishe." Kauli hii inaonyesha tayari maamuzi yaliyopitishwa, wajibu waliojikabidhi viongozi bila kuchukua ridhaa ya wananchi wao. Kama yatatokea yaliyofanyika 1977 basi hukumu wakati huu inao wa kuwaendea.

Kama anavyozungumza Mbunge wa Afrika Mashariki Dk George Nangale, wananchi wengi wa Tanzania hawafahamu chochote kuhusu jumuiya au shirikisho la Afrika Mashariki. Kutofahamu huku kunaweza kuwa ndiko kulikochukuliwa na viongozi wa juu na kuamua kupitisha maamuzi bila kupata ridhaa.

Kimsingi kuna mchezo wa kisanii hapa kama inavyoonyeshwa pia na kamati ya kukusanya maoni kuhusu kukubali shirikisho au la. Kamati hii nayo imebadili agenda na kuwa, kuharakisha shirikisho au la. Tena kamati hii hapa Tanzania inafanya pia kazi ya kushawishi wananchi kuhusu kukubali hatua hiyo badala ya kufanya kazi iliyopewa na kuishia kukusanya maoni tu.

Tayari vyombo mbalimbali vya habari vimeandika kuhusu kujiongezea huku kwa majukumu kunakofanywa na kamati hii ya Tanzania inayoongozwa na Profesa Wangwe. Kauli za viongozi wa juu wa serikali zote za Kenya Uganda na Tanzania zinaonyesha kuwa kuna mchezo wa haraka unaoburuzwa na huenda nguvu za nje ya mataifa haya ili kufikiwa shirikisho hili. Kuingizwa kwa Rwanda na Burundi nayo ni hoja nyingine inayobariki uvamizi huu wa kiuchumi unaotakiwa kuchukuliwa na mataifa makubwa yanyoongozwa na uchu wa kibepari.

Kama ilivyo kwa Kenya na Uganda; kukosa kwa uelewa wa siri hizi au kutofahamu kabisa maana ya kuwa na shirikisho hili kwa sasa kunatafuna watu wa kada zote. Nchini Tanzania mapema wiki hii gazeti moja la kila wiki lilitoa tahariri iliyoitaka serikali kupitia wizara yake ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kutenga fedha zitakazosaidia kuelimisha waandishi wa habari. Lengo la kufanya hivi ni baada ya kuona ziara za Naibu waziri wa wizara hiyo kutembea nchi nzima akihamasisha uundwaji na uharakishwaji wa shirikisho kutozaa matunda.

Wizara hiyo kabla wiki haijaisha ikaitisha warsha katika hoteli moja kubwa jijini Dar es Salaam, warsha hii iliwahusisha wamiliki wa vyombo vya habari na wahariri. Uharaka wa warsha hii unatoa picha kuwa, wizara ina fedha nyingi kwa ajili ya jukumu hili lakini inaacha swali nini siri iliyojificha kuhusu umuhimu wa shirikisho hili ambayo wanayo viongozi huku wananchi hawaifahamu?

Je siri hiyo inaweza kutajwa na kisha kuwashawishi wananchi kuwa sasa maisha yao yatakuwa bora baada ya kushindwa kufanikishwa kwa kuwa huru kwa miaka 45? Ni kweli ukanda huu wa Afrika utaweza kutotumika kama soko la bidhaa za nje na hivyo kuwanufaisha wageni kama ilivyo sasa?

Yapo maswali mengi yasiyo na majibu. Kuna baadhi ya wachunguzi wa masuala ya siasa wanaozungumzia kuhusu kutokuwepo viongozi wenye dira na welewa wa kuweza kubeba jambo hili zito sasa. Kundi hili linatazama vichwa kama Mwalimu Nyerere, Mzee Kenyatta na Obote wakati ule na kisha kwa uwezo ule waliokuwa nao bado jumuiya ikaanguka mwaka 1977. Je. hawa wa sasa wanaweza kuvaa viatu vya viongozi hao japo robo ili kuzifanya nchi hizi zifike huko watakako?

Yapo mengi, na yanajionyesha katika hofu ya wananchi kukosa maendeleo. Yanajionyesha kutokana na uchu wa viongozi kujilimbikizia mali. Yanajionyesha katika kutojali maendeleo ya wananchi maskini hali inayotoa picha kama utanuzi wa utaifa utatokea inawezekana kabisa kuwa wananchi wengi wakabakia kusahaulika au kuwa mtaji wa kura za wakubwa ili wafikie utukufu wa juu kabisa kisiasa. Inawezekana pia kuwa, shirikisho hili likabakia asali ya kundi fulani litakalonufaika kupitia makampuni ya kigeni na sio wananchi wa kawaida.

Hofu hizi zinazidi kukua hasa inapoonekana masuala madogo madogo ya kukuza uchumi na maendeleo ya nchi hizi yanaposhindwa kufanywa na viongozi waliopo. Nini kifanyike baada ya hapa, inawezekana waandishi wa habari wakabaki kuwa kundi la kwanza kulaumiwa kutokana na wao kuhoji usiri uliojificha katika suala hili huku kukiwa hakuna watu wenye dira madhubuti ya kuijenga Afrika Mashariki.
 
© boniphace Tarehe 1/21/2007 05:05:00 AM | Permalink |


Comments: 6


  • Tarehe 1/23/2007 5:14 AM, Mtoa Maoni: Blogger Unknown

    Tanzania haihitaji jumuiya wala shirikisho la afrika mashariki.mpaka sasa tanzania ina underutilize resources zilizopo na nyingine kuzimisuse.cha msingi kwa sasa ni kuwa na matumizi mazuri ya hizo resources.jinsi ninavyoona mimi ni kwamba rais Kikwete ingawa hajatamka hadharani,lakini hapendezwi na kuwepo kwa shirikisho.mawazo ya wananchi thamani yake ni ya kisiasa tu,hii ni kwa sababu kiwango cha elimu ni cha chini mno.mtu akitembelea vijiji vya tanzania wakati wa uchaguzi atashuhudia jinsi sugestibility ya wananchi wa tanzania ilivyo juu.nadhani cha msingi ni serikali kuheshimu mawazo ya wanataalamu wa international relations,political affairs and economists.mpaka sasa sijui msimamo wa wanataaluma hao juu ya suala hili.

     
  • Tarehe 1/25/2007 10:30 PM, Mtoa Maoni: Blogger Sayyed M. Nusura "Baba Jamaal/Jimaya

    Sina mengi ya kuchangia kuhusu hili "SHIRIKISHO",kwani mengi yamekwishazungumzwa na mwandishi wa makala hii pia Dr. Imaan Kondo(Zemarcopolo).
    Kifupi kujiingiza katika mtego huu ni sawa na ile hadithi ya mbwa amwonapo chatu!!
    Tanzania ama watanzania na hasa hawa WANAOITWA AMA KUJIITA VIONGOZI waangalie kwanza hali ya maisha ya mtanzania wa kawaida kuanzia Mmachinga alioyefukuzwa Kariakoo hadi kule vijijini ambako asilimia kubwa ya watanzania ndiko waliko!
    Je, kama mtanzania huyu anashindwa kuwa na NAFASI katika Tanzania , hivi atawezaje kuwa nayo katika SHIRIKISHO!!
    Je, tumemwandaaje Mmachinga wa kitanzania kushindana na mwenzake wa kutoka Kenya,Uganda ama Rwanda na Burundi??
    Je hivi kweli mtanzania wa kawaida ama pengine hata yule ANAYEJIITA MSOMI ana jeuri ya KUJIUZA KENYA ama UGANDA na akauzika??
    Kwa mtazamo wangu jibu ni hapana na ukweli ni kinyume cha hayo niliyoyazungumza.
    Hivyo utafiti wa kina inabidi ufanyike na pia binafsi nasema Tanzania isiendelee kuwa kichwa cha mwendawazimu kama ambavyo siku zote imekuwa! ni wakati wa watanzania kuamka na kuchukua nchi yao

     
  • Tarehe 1/27/2007 5:59 AM, Mtoa Maoni: Blogger MTANZANIA.

    "It is too early to catch the train". Kwa Tanzania yetu huu waweza kuwa mzigo mkubwa kwa taifa. Ni vema nchi yetu ingejikita kutatua matatizo ya ndani kwanza kabla ya kuangalia uwezekano wa kujiunga na hii jumuiya.

     
  • Tarehe 1/30/2007 1:48 AM, Mtoa Maoni: Blogger Unknown

    hawa jamaa utadhani walisoma hii blog kabla ya majadiliano na waandishi wa habari. http://www.ippmedia.com/ipp/nipashe/2007/01/30/83374.html

     
  • Tarehe 1/30/2007 1:49 AM, Mtoa Maoni: Blogger Unknown

    This comment has been removed by a blog administrator.

     
  • Tarehe 1/30/2007 3:55 AM, Mtoa Maoni: Blogger boniphace

    zemarcopolo na wadau wengine shukrani sana jkupita katika kasri lenu. Mawazo yenu yananipa hamu ya kuandika na kubandika zaidi. Shirikisho nililipenda sana kabla ya kuja huku, lakini ninavyotazama hali iliyopo nchini, huu si muda muwali wa sisi kulikimbilia. Tunahitaji tafakari zaidi

     
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved