Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Sunday, December 17, 2006
UTATA WA RICHMOND KATIKA MATUKIO
KAMA uliwahi kusoma ripoti ya Trasparency International kuhusu mkataba wa IPTL basi waweza kupata majibu kadhaa katika tukio la kampuni ya Richmond iliyoingia Tanzania kuwekeza katika umeme. Kampuni hii ina mkono wa nani hadi ishindwe kutimiza makubaliano lakini iendelee kutazamwa tu? Je, hii ni IPTL nyingine iliyowekwa na viongozi wa serikali hii ukihusisha kuwa wapo waliokuwemo katika IPTL?

TAZAMA SASA MATUKIO HAYA HAPA CHINI

Februali 28, 2006: Rais Jakaya Kikwete anatangaza mkakati wa kupata megawati 105 kutoka katika mitambo ya kukodi ya Ubungo na Tegeta.

Machi 31, 2006: Rais anaeleza utaratibu wa kupata mitambo ya kukodisha umekamilika na uingizaji wa mitambo hiyo ungefanyika wiki chache zilizofuata baada ya kukamilisha taratibu za manunuzi.

Machi 31, 2006: Rais anasema mitambo hii ya kutumia gesi ingefungwa baada ya miezi miwili hadi mitatu.

Jumanne Juni 7, 2006: TANESCO inatoa taarifa kwa umma kuhusu kuanza mgawo wa umeme. Wateja wanatangaziwa kukatiwa umeme kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa. Bwawa la Mtera siku hiyo lina mita 689.01 juu ya usawa wa bahari huku kina cha juu kikiwa 698.50. Kina hiki hakijawahi kutokea tangu kujengwa kwa bwawa hili.

Juni 23, 2006: Mkataba kati ya Serikali/Tanesco na kampuni ya Richmond Development unasainiwa.

Jumatatu Agosti 8, 2006: Bunge linachachamaa kuhusu utata wa mradi wa kuzalisha umeme wa gesi wa Mchuchuma kwa kumhusisha Waziri wa Viwanda na Bishara wakati huo, Nazir Karamagi kuwa ana mahusiano na mmiliki wa kampuni ya MMI inayomilikiwa na Shubash Patel na hivyo uhusiano wao kuathiri utendaji wa mradi huo.

Ijumaa Agosti 25, 2006: Mtambo wa kuzalisha umeme Songas unaharibika na hivyo kuongeza makali zaidi ya umeme kufuatia kushindwa kuzalisha megawati 40. Mgawo unaongeza saa kuanzia saa 1.00 asubuhi hadi saa 5.00 usiku.

Jumanne Agosti 29, 2006: Umeme unatangazwa kuwa hautakuwapo mchana tena kwa siku za Jumamosi na Jumapili.

Jumatano Agosti 31, 2006: Serikali inasaini mkataba wa kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe Kiwira na kampuni binafsi ya Kiwira Coal & Power (KPC), kuzalisha megawati 200.

Septemba 14, 2006: Mgawo wa umeme uliokuwa siku tano sasa unakuwa wiki nzima.

Septemba 15, 2006: Tanesco inahusisha mgawo kwa sekta ya viwanda. Sasa viwanda vinakosa nishati hiyo kwa siku tatu kwa wiki.

Septemba 29, 2006: Waziri wa Nishati na Madini, Ibrahim Msabaha anatangaza kuwa kampuni ya Richmond kutoka Marekani itazalisha megawati 22.

Septemba 30, 2006: Waziri wa Nishati na Madini, Ibrahim Msabaha anaeleza kuwa kampuni ya Richmond ingewasilisha mitambo yake na kuanza uzalishaji mwezi Oktoba.

Oktoba 4, 2006: Inatangazwa kuwa Richmond ingeanza kuzalisha umeme Oktoba 20.

Oktoba 8, 2006: Jenereta za Richmond zinatangazwa kuwasili, lakini hakuna mafanikio ya jenereta hizo kufika.

Oktoba 10, 2006: Gazeti la "The Citizen" linaandika kuhusu utata wa kampuni ya Richmond kufuatia kutofahamika huko Texas Marekani ambako inaelezwa ndipo makao yake makuu.

Oktoba 15, 2006: Wakati utata kuhusu Richmond unaendelea, Rais Kikwete anapangua baraza lake la Mawaziri na kumuondoa Msabaha katika wizara ya Nishati na Madini na kumungiza Nizar Karamagi.

Oktoba 20, 2006: Richmond inakana kuvunja vipengele vya mkataba na Tanesco kufuatia kushindwa kuanza uzalishaji wa umeme. Hata hivyo taarifa inatolewa kuwa mitambo yake bado iko njiani.

Oktoba 21, 2006: Mitambo ya awali ya kuzalisha umeme ya kampuni ya Richmond inawasili uwanja wa JK Nyerere, Dar es Salaam.

Oktoba 27, 2006: Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinahoji juu ya usiri wa gharama za umeme wa kukodi utakaozalishwa na makampuni ya Richmond na Aggreko.

Oktoba 30, 2006: Waziri Mkuu Edward Lowassa anawaomba wabunge wa CCM wasiibue hoja ya Richmond bungeni. Wabunge hao wanaitikia wito na kuliacha suala la Richmond katika utata usio na maelezo.

Jioni Oktoba 30, 2006: Awamu ya pili ya mitambo ya kuzalisha umeme ya kampuni ya Richmond inawasili uwanja wa JK Nyerere, Dar es Salaam.

Novemba 19, 2006:
Wananchi wanalalama kuhusu utata wa uzalishaji umeme kutoka kampuni ya Richmond.

Novemba 23, 2006: Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi anaeleza waandishi wa habari kuwa umeme wa Richmond ndio rahisi kuliko makampuni yote yanayozalisha umeme nchini. Hata hivyo haelezi kuhusu maana ya urahisi huo.

Novemba 24, 2006: Waziri Karamagi anakana Richmond kuwa na mkono wa mtoto wa kigogo. Hata hivyo haelezi taarifa za kuwepo kwa mtoto wa kigogo katika umiliki wa Richmond amezipata wapi.

Desemba 1, 2006: Rais Kikwete anakwepa kuzungumzia uzembe wa kampuni ya Richmond licha ya kuwa taarifa za awali zinaonyesha kuwa hoja hiyo imo katka hotuba yake aliyotakiwa kuitoa siku ya maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani, kitaifa ikiadhimishwa mjini Musoma.

Desemba 10, 2006: Richmond bado inazidi kushindwa kuingiza umeme katika gridi ya taifa licha ya Waziri Karamagi kuahidi kuwa ingefanya hivyo mwanzoni mwa mwezi Desemba.

Desemba 11, 2006: Richmond inalalama kuwa Tanesco inawahujumu kwa kuwapatia gesi iliyochanganyikana na mchanga.

Desemba 12, 2006: Richmond na Tanesco zinamuhusisha Mkemia Mkuu kuchunguza gesi iliyotolewa na Tanesco kwenda Richmond.

Desemba 15, 2006: Bado umeme megawati 20 hazijazalishwa na magazeti ya Mwananchi na The Citizen yanaandika waliohusika kuandaa mkataba wa Richmond huku Rais akishauriwa kuingilia kati kuufuta lakini haonyeshio kufanya hivyo.
 
© boniphace Tarehe 12/17/2006 01:48:00 AM | Permalink |


Comments: 5


 • Tarehe 12/19/2006 3:14 AM, Mtoa Maoni: Blogger mwandani

  miyeyusho hao

   
 • Tarehe 12/19/2006 5:27 AM, Mtoa Maoni: Blogger mloyi

  Hayo ni mambo makubwa, sijui wakubwa wa nchi hii kama huwa wanashaurika, wao wamekalia uongo juu ya uongo! Wanasema serikali hii haina ubabaishaji, hata hatujasahau tulivyopiga kura wao wameshaanza uongo! uleule wa mkapa.
  Mkapa alikuwa anajisifia kila siku, nchi hii sasa inakopesheka, madeni yake yamepungua kiasi kikubwa, mbona hakutumia uwezo huo wa kukopa kutatua tatizo la umeme? Anakuja huyu wa sasa naye analake, atatatua tatizo la umeme huku anazidisha matatizo, sasa Richmond wako mitambo wamefunga lakini kila siku kuna jambo jipya, umeme bado tatizo!. Hawaoni suluhisho ni kuwekeza Mchuchuma, ili tupate ufumbuzi wa kudumu wao wanahangaika na kuzima moto, bila kufungia vizuri petroli!
  Wakati mwingine nadhani huwa hawana uchungu na pesa za walipa kodi wao, au walipakodi nao hawanauchungu na pesa zao! Ndiyo maana huu mchezo mwa kudang,anyana hauishi.

   
 • Tarehe 12/19/2006 11:33 PM, Mtoa Maoni: Blogger John Mwaipopo

  Is Richmond another IPTL?

   
 • Tarehe 1/08/2007 2:44 PM, Mtoa Maoni: Blogger Michuzi

  HAPPY NEW YEAR!

   
 • Tarehe 1/24/2007 9:21 PM, Mtoa Maoni: Blogger SaHaRa

  Watafanya hivyo - kutudanganya na kuvuja na kuiba pesa ya walipa kodi - mpaka siku ambayo na sisi wananchi tukiamua kufanya kitu. Watanzania hatuna tamaduni ya kulalamika kabisa. Wenzetu wangekuwa wameshagoma.

  Nani ameshawahi kufukuzwa kazi kwa sababu ya uzembe Tanzania? Wote huko juu are watching each others back. Simply, they are untouchable.

  Tumeshasikia madhambi yao mengi mno, tunpigwa promises kemkem za kudhibitiwa hawa wadhambi, lakini baada ya muda tukizubaa tu, madhambi yanafagiliwa chini ya zulia - kama kawaida. Sisi tutazidi kuumia tu.

   
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved