Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Saturday, October 14, 2006
NAMKE NDIPO NISEME?
NAMKE ndipo niseme
Nishike jembe nilime
Mdomo nisiachame
Na macho yasitazame?

Nilie nikichekea
Watu wasijejulia
Nicheke nikililia
Umati furahishia?

Nandike bila somea
Nikopi walosemea
Nisome walofutia
Ukweli taupatia?

Nikue bila julia
Nilale bila otea
Nisene bila wazia
Hayawani niitiya?

Utoto lini achia
Ukubwa lini fikia
Kumbukumbu kujulia
Muhimu kwa walofia?

Ni mwaka naukatia
Langu tando fungulia
Mwadhani litadumia
Mawimbi kuyashindia?

Sitaki kujisifia
Mtoto sijatembea
Ni lini nitasemea
Siku nitapofilia?

Nyamongo kalizaliwa
Mwisenge akapitia
Mabui akaishia
Na Nyasho kitembeleya!

Kienda Ihungo Piya
Matoke kutafuniya
Nadanda akatimkiya
Mkwawa akihamiya.

Kikafika Dasalama
Tiesijii someya
Kalamu kikashikiya
Mlimani kupandiya!

Kisha hitimu ilimu
Na kupata unajimu
Amerikani jihimu
Mataifa jifyunziya!

Huko kikaanzishiya
Gazeti Tando la umma
Kasri kaliitiya
Mwaka moja wapitiya!

Nini anachotakiya
Kama si kulaliya
Siku ajapo filiya
Mwili tu poteleya!
 
© boniphace Tarehe 10/14/2006 02:32:00 AM | Permalink |


Comments: 5


  • Tarehe 10/14/2006 8:41 AM, Mtoa Maoni: Blogger Jeff Msangi

    Makene,
    Nimekubali.Ushairi mzuri sana huu,maneno haya wanayasikia?

     
  • Tarehe 10/15/2006 1:28 AM, Mtoa Maoni: Blogger Sultan Tamba

    Hongera mshairi! Ujumbe una njia nyingi za kuufikisha. Hata hivyo watu wako masikio wazi na macho mita mia moja kuangalia! Usishangae kesho ukasikia shairi lako watu wanaliimbia taarabu!!! Hongera! Nimelipenda na ujumbe wake.

     
  • Tarehe 10/16/2006 6:11 AM, Mtoa Maoni: Blogger mzee wa mshitu

    KAKA HII BETI YA USHAIRI INANIKUMBUSHA SANA HAYATI PEPE KALE ALIVYOJIIMBIA MWIMBO WA KUJIAGA: Nini anachotakiya
    Kama si kulaliya
    Siku ajapo filiya
    Mwili tu poteleya!

     
  • Tarehe 10/23/2006 4:51 AM, Mtoa Maoni: Blogger Rashid Mkwinda

    Sema ulojifunzia, kwa kalamu kushikia,wafunze wenzio pia,ukumbukwe kijifia, hazina uloachia, vilembwe kunakiria, kazizo nafurahia, zaduru bara baharia.

     
  • Tarehe 10/23/2006 4:59 AM, Mtoa Maoni: Blogger Rashid Mkwinda

    Nini kuimbia taarabu amenikumbusha Bw.Tamba hawa vijana wa kizazi kipya ndio haswa watakuwa wa kwanza kunakiri kikubwa ni kwamba hawataki kuketi chini kujifunza ngano hizi kwa malenga walobobea watu wa aina hii wakijififia na hazina itapotea kama walivyojifia akina Shaaban Robert na hazina zao kuhondhiwa sidhani kama familia inanufaika? labda tumuulize Ikbal Shaaban Robert mwana wa mwisho wa mzee Shaaban ambaye nilikuwa namuona akiibuka na baadhi ya mashairi ya babaye magazetini zijui ndio urithi aliopewa wa kunakiri kazi za babaye bila kunoa ubongo wake hilo mie sijui msije kunisuta.

    Kazi nzuri sana hii imetulia muala wake vina na mizani vimejipanga vyema huku ujumbe ukisawiri mandhari ya shairi lako.

    Marhabaa ndugu yangu kaza msuli safari ni ndefu kuelekea kujikomboa katika fani ya fasihi simulizi na andishi

    Wakatabahu

     
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved