Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Sunday, October 01, 2006
Bodi ya mikopo imesahau sheria iliyoiunda?
MWAKA 2005 Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya
Juu iliunmda tume ya kuchunguza vyanzo vya migomo
katika Vyuo vya Elimu ya juu nchini. Tume hiyo
ilifanya kazi ila inaonyesha kuwa ripoti ya tume hiyo
haikuweza kusomwa na hata watendaji wa Wizara hiyo!

Hawakuisoma ripoti hiyo ambayo pia haikuibua masuala
mapya! Kama ilitokea waliisoma, basi waliipuuza na
huenda waliitupa na kuikanyaga! Hawajaisoma hawa,
najua kabisa maana nadhani tume hii iliundwa tu kwa
lengo la kutafutiana ulaji!

Tume nyingi zimeumdwa ili kuwapa ndugu fulani
ulaji na hili linatokana na kudharauliwa ripoti zake
baada ya kukamilisha kazi ya kuzikusanya. Awamu ya
tatu ni mafano tosha kuhusu matumizi hasi ya
kapendekezo ya tume zlizowahi kuundwa katika awamu
hiyo, Tume ya Migomo Vyuo vya Juu ikiwa mojawapo.

Tume ya kuchunguza vyanzo vya migomo katika vyuo vya
elimu ya juu nchini ilitoa pendekezo la kuwataka
wanafunzi katika vyuo vya elimu ya juu kutojiusisha na
siasa. Ilielezwa kuwa vyama vya siasa vinatumiwa
kuhamasisha migomo katika vyuo vya elimu ya juu na
kwamba kama wanafunzi hawataruhusiwa kujiunga na vyama
vya siasa na kutumia haki yao ya kidemokrasia basi
migomo itaingia katika bahari ya sahau.

Tume hii haikutaja wazi kuwa ni chama tawala
kinachosajili wanachama kila kukicha katika vyuo vya
elimu ya juu huku kikiwa na matawi yake na makada wake
kila chuo. Ukitazama sana hoja hii unagundua madhara
ya tume zinazoanza kazi zikiwa na majibu mezani maana
suala hili lilifikishwa na waziri wa wizara hiyo
Bungeni likitakiwa kuundiwa sheria lakini masuala
muhimu kama;

Posho za wanafunzi, sifa za kukopeshwa, wakati wa
kupokea mikopo, hali mbaya na duni ya mazingira ya
wanafunzi vyuoni, idadi kubwa ya wanafunzi katika
madarasa, upungufu wa wahadhir, upungufu wa vitabu,
mitaala iliyopitwa na wakati na mengine kemkem
hayakupatwa kupewa kipaumbele sana hali inayosababisha
matatizo ya migomo kuendelea!

Kuundwa kwa Bodi ya mikopo kulionekana kuwa ni
suluhisho la kuwaondolea anafunzi dhana ya kusomeshwa
na serikali ili wasiwe na kigezo cha kuibana serikali
pale wanapokosa au kuchelerweshewa fedha. Tume ya
mikopo ililenga pia kuwabana wanafunzi/ wakopaji
kutojihusisha na utumiaji wa nguvu au migomo katika
kuomba mikopo hiyo hata pale inapopatikana kwa tabu
kama ilivyo sasa.

Kuundwa kwa Bodi hii hakukuzingatia tatizo la moto
mkali uliowashwa baada ya sasa wanafunzi wote wa vyuo
vya elimu ya juu ambao zamani walitengwa kutokana na
wengine kutopata udhamini wa serikali, kuwa
wanaunganishwa na hivyo kuwa na adui mmoja yaani
serikali pale wanapocheleweshewa fedha zao au webzao
wanaponyimwa fedha hizo!

Kwa ujumla kuundwa kwa Bodi ya Mikopo kulitakiwa
kuambatana na mikakati makini ili kuwafanya waombaji
wapate wanachohitaji bila kuwepo malalamiko ya
kukosekana kwa mikopo hiyo na pia kuwafikia wakopaji
kwa wakati.

Katika mapendekezo ya tume ya iliyokuwa ikichunguza
vyanzo vya migomo katika vyuo vya elimu ya juu,
ilielezwa kuwa tatizo la ucheleweshaji wa posho au
kutotolewa kwa posho (sasa mikopo) kwa baadhi ya
wanafunzi lilikuwa ni tatizo kubwa la migomo. Bodi ya
Mikopo ilionekana kuwa suluhu la tatizo hili baada ya
wafanyakazi wa Wizara kuonekana kuwa na majukumu zaidi
ya kusghughulikia posho za wanafunzi.

Ni wazi kuwa mapendekezo ya tume hiyo hayakufanyiwa
kazi. Kutiokana na sababu hii bado keron za vijana
wetu wanaosoma katika vyuo vya elimu ya juu ziko pale
pale.

Inachosha, inasikitisha na inaumiza kuona vijana hawa
wakiacha jukumu lao la msingi la kusoma na badala yake
kuanza kuandamana kudai posho. Hili ni tatizo
linalotokana na uzembe wa pande nyingi na kuu ni
tawala za vyuo, wizara na Bodi yenyewe.

Tatizo la wanafunzi ni dogo na lingeweza kutatuliwa
kwa kutoa taarifa mapema kwa wanafunzi wanaofikia
vigezo vya kupata mikopo na wale wasiofikia vigezo.
Bodi ingetamka siku baada ya kupokea maombi kuhusu
kutoa majibu kwa muombaji kama amekubaliwa au la!

Ikumbukwe kuwa waombaji wanalipa fedha za kupelekea
maombi yao. Fedha hizi si mradi wa Bodi bali
zilitakiwa kutumika kwa ajili pia ya mawasiliano kati
ya muombaji na Bodi kabla hata waombaji hawajaanza
safari ya kwenda katika vyuo walivyochaguliwa.

Migomo ukiongezea na mazingira magumu yanayowakabili
wanafunzi hapa nchini ni sababu nyingine inayochangia
kuipua wahitimu chapwa! Ni sababu nyingine ya kuandaa
wapenda rushwa na wezi kutokana na wahitimu wengi
kuamini kuwa, hali ngumu inayowakabili katika vyuo
inatatuliwa pale wanapohitimu na kisha kupata nafasi
katika sekta mbalimbali, na hivyo tena kutumia nafasi
zao kwa manufaa yao baada ya kutaabika sana wakati wa
kusoma.

Tabu mpya inayoambatana na shaka kwa wanafunzi sasa
inatokana na kauli ya Waziri Peter Msola. Waziri huyu
alikiuka sheria iliyopitishwa na Bunge inayotoa
mamlaka ya kuanzishwa kwa Bodi ya Mikopo nchini.

Kukiuka kwa waziri huyu kunatokana na yeye kuweka
vigezo vyake vilivyo kinyume na katiba ya nchi hasa
kipengele cha haki ya elimu na pia sheria yenyewe
isiyofafanua kuhusu kigezo cha madaraja ya mhitimu
kutumika wakati wa kuomba mikopo.

Kama nchi yetu ingekuwa na mfumo mzuri wa sheria
sambamba na watu wake kutambua umuhimu wa kutumia
mahakama kupata haki zao; basi waziri Msola angekuwa
keshabuluzwa kortini na wanafunzi wenye sifa za kupata
mikopo hiyo kama ilivyobainishwa na sheria ya Bunge
lakini wakakosa kutokana na kukosa madaraja ya kwanza
na ya pili kwa wasichana.

Sifa kubwa zinazobainishwa na sheria ya Mikopo ni;
mwombaji awe raia wa Tanzania, awe amedahiliwa katika
chuo chochote na asiwe na uwezo wa kujitoleza
kujisomesha.Sifa hizo hazibagui aina ya taaluma
anayotaka mkopaji wala chuo anachojiunga.

Suala la Chuo na aina ya masomo kama ambavyo
linatumiwa sasa na Waziri Msola ni kigezo kingine
kinachopingana na sheria ya mikopo. Ni kigezo pia
kinachokiuka misingi ya Katiba na kinaweza kuhojiwa
mahakamani na kupata tafsiri nzuri tu itakayobainisha
uduni wa kuielewa sheria hiyo kunakotumiwa na waziri
Msola.

Kazi ya muhimu ya Bodi ni kutathimini maombi ya
mwanafunzi na kutazama kama ana sifa za kupewa mkopo.
Suala la mwanafunzi huyo aliombaje udahili katika chuo
si suala la Bodi. Bodi haina mahusiano na vyuo kuhusu
sifa za wanafunzi wapi wajiunge na vyuo hivyo.

Bodi ina kazi ya kupokea maombi ya mikopo na kutoa
mikopo huku ikizingatia wahitaji kuwa hawatoki katika
familia zenye uwezo wa kuwasomesha,(hiki ni kigezo cha
kwanza) na pili wamepata udahili katika chuo husika!

Mwenyekiti wa Bodi ya Mikopo na Mbunge wa Musoma
Vijijini, Nilmud Mkono; naye licha ya kuwa Mwanasheria
amejiingiza katika kuongeza utata wa kutotambua
majukumu ya Bodi anayoiongoza. Ameshindwa kufahamu
kuwa kila mwananchi ana haki ya kukopa katika Bodi
hiyo ilimradi atimize vigezo!

Kitendo cha Bodi kuanza kubagua nani akopeshwe na nani
aachwe kinapingana na sababu ya msingi ya kuanzishwa
kwa Bodi ya Mikopo. Sababu ilikuwa kutafuta usawa kwa
wanafunzi wa vyuo vya serikali na wale wa vyuo vya
binafasi maana wote ni wananchi wa Tanzania na
wanapohitimu hutoa ujuzi wao kwa nchi bila kubagua.

Kigezo hicho kilitazama pia aina ya wanafunzi
wanaodahiliwa katika vyuo vya binafsi hasa kigezo cha
sifa za kujiunga. Vyuo vya serikali havikuweza kumudu
kuchukua wanafunzi wote. Kutokana na hali hii
wanafunzi wengi walikosa nafasi na hii ikawa
changamoto ya vyuo binafsi kuongeza udahili ili
kupunguza idadi ya wanafunzi wanaokosa nafasi katika
vyuo vya serikali.

Kauli ya Mkono kusuhu wanafunzi waliogoma katika Chuo
Kikuu Mlimani kuwa ni wahuni inatia wasiwasi kuhusu
yeye kufahamu watu anaosimamia kuwatumikia katika Bodi
hiyo. Ni kauli hii inayombaini Mkono kuwa naye hajui
vema kuhusu yupi mwenye sifa ya kuwa mteja wake.

Kuna mengi yanaweza kujadiliwa hapa lakini hasa suala
la Bodi kuingilia udahili wa aina ya wanafunzi badala
ya kuishia kutoa mikopo kutokana na mahitaji
linatakiwa kutazamwa kwa upana sana. Si busara
wanafunzi kuandamana na kugoma kila mara na mogomo
kamwe haiwezi kuwa suluhisho la matatizo ya wanafunzi.

Migomo mingi inatokana na uzembe au kutotambua
majukumu na wajibu wa baadhi ya watendaji wa umma.
Bodi ya mikopo kabla haijaanza kupambana na mtihani wa
kufatilia urejeshaji wa mikopo itazame utatuzi wa
tatizo hili kwanza. Kama kuna udhaifu unaotokana na
serikali kuchelewa kuidhinisha fedha uelezwe kuliko
kuwaumiza wanafunzi ambao wanakopa huku wakitarajia
kurejesha mikopo hiyo baadaye.

Athari ya migomo ni kubwa na kwa taifa kama Tanzania
inachukua miaka mingi kuipooza athari hiyo hata kama
haitazamiki. Bodi ya Mikopo na Wizara nionavyo
hazitambui majukumu yake au haziko makini kujua nini
kizungumzike wapi na namna ipi itumike kutatua
matatizo ya ugawaji fungu kidogo lilolopo ikiwa
wahitaji ni wengi. Mbinu maridhawa ni kukaa na wadau
wa elimu na hawa walengwa (wanafunzi) ili kujiwekea
vigezo na utaratibu wa uendeshaji wa Bodi hii la sivyo
tusubiri migomo ya wanafunzi wa vyuo vyote vya elimu
ya juu nchini.
 
© boniphace Tarehe 10/01/2006 09:17:00 AM | Permalink |


Comments: 0


   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved