Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Thursday, September 07, 2006
Mikopo elimu ya Juu na falsafa ya aliyenacho!
LEO hii nimepata fursa ya kupitia picha zangu za
zamani. Mkononi nimeifikia hii niliyoipiga Bungeni
Dodoma mwaka 2005. Tumekaa katika mgahawa wa Bunge
sehemu hii ya ukumbi wa zamani ambao wiki hii
umebatizwa jina jipya. Unaitwa ukumbi wa Msekwa ikiwa
ni heshima ya Spika huyu aliyekalia kiti hiki kwa
miaka na kisha kubwagwa katika uchaguzi uliofanyika
mapema mwaka huu.

Inawezekana Msekwa amepakwa mafuta kwa mgongo wa bia.
Siamini kama heshima ya ukumbi huu ilipaswa kwenda
kwake kabla ya Spika mtangulizi Adam Sapi Mkwawa.
Ukitazama sana utagundua geresha na kebehi hasa kwa
wabunge hawa ambao waliamua kwa dhati kumuweka
kandobaada ya yeye kung'ang'ania kutokustaafu kama
alivyowahi kuahidi.

Picha niliyoishika inanipa hasira, inanitia huzuni na
tena inaninifungua fikra. Nakumbuka msemo wa Kiswahili
ninaoupinga sana lakini hapa nitautumia, "mtumikie
kafiri upate mradi wako!"

Msemo huu nimeupinga mara nyingi kutokana na kuwa
unawaathiri maskini na wasio na uwezo kwa kuwafanya
kujijazia fikra za unyonge dhidi ya tabaka tajiri na
tawala. Msemo huu una walakini hasa ukizingatia kuwa
hauzungumzi kuhusu muda utakaotumika katika
kumtumikia kafiri.

Ubaya mwingine unaojiibua katika msemo huu ni
kuwa,unawafanya maskini watumwa wa matajiri na unatoa
fikra kuwa ni haki kunyanyaswa kwa kuwa tu unatafuta
maisha bora! Misemo mingi ya Kiswahili inaleta hali
dunishi ukiitumia bila kuitathimni. Profesa Zakaria
Mochiwa (mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Tanzania)
aliwahi kuandika kitabu na kukipa jina la "Mvumilivu
hula mbovu" akipingana na msemo mwingine usemao kuhusu
mvumilivu kula mbivu.

Ndugu msomaji nikurejeshe katika picha hii iliyopo
mkononi kwangu. Nikuonyeshe waliopo hapa; tazama vema
maana yupo Dk. Pius Ng'wandu (Waziri wa Sayansi,
Teknolojia na Elimu ya Juu awamu ya tatu), yupo Aziza
Sleyum Ally (Mbunge wa viti maalum CCM, Vijana na sasa
Viti Maalum Tabora), kuna binti huyu anaitwa Annet
Sisya, yupo Kiomoni Kibamba, namuona Andendekisye
Christopher na mimi. (watatu sisi wawakilishi wa
serikali ya wanafunzi Chuo Kikuu Dar es Salaam).

Tumefika hapa Bungeni kukutana na waziri Ng'wandu ili
kutoa mtazamo wetu kuhusu utata wa inayoitwa sasa Bodi
ya Mikopo. Hiki ni kipindi kabla sheria ya kuundwa kwa
Bodi haijapitishwa ambapo ilipitishwa baadaye siku
mbili zilizofuata baada ya siku tuliyopiga picha hii.
Tumejipanga hasa na hoja lakini Ng'wandu anazipangua
nyingine ambazo wakati huo naona zina mantiki lakini
umma niliouwakilisha wakati huo usingependa
kuzisikiliza.

Tunamweleza Ng'wandu kuwa mikopo hii isiwe na urasimu
na badala yake itolewe tu kwa kila mwanafunzi
aliyefaulu vizuri. Nchini kwetu hapa unapozungumzia
kufaulu vizuri mara kwa mara unazungumzia wanafunzi
wanaojiunga na Chuo Kikuu Dar es Salaam. Tunaona
tumefikisha ujumbe safi lakini Ng'wandu anatoa hoja
nzito hasa kuhusu namna na nani anayeweza kufaulu
vema.

Ng'wandu anasema; "katika Tanzania ya sasa ni watoto
wetu sisi (anamaanisha yeye na watu wa daraja
lake)wanaoweza kufaulu vizuri. Ukitazama sasa hivi
wanafunzi wanaotoka shule za binafsi wanafaulu vizuri
mitihani yao ya taifa kuliko wanaotokea shule za
serikali.

"Kama tutatoa mikopo kwa kutazama kufaulu basi lengo
la kuwasaidia wenye shida halitafikiwa. Tutakuwa
tumempatia tajiri fedha na kumtupa maskini anayehitaji
msaada," anasema Ng'wandu.

Mfumo wa elimu yetu umemtenga mototo wa maskinina
umejenga mazingira magumu kwake kuweza kufaulu. Nafasi
za mtoto huyu kuweza kupenya na kupata maisha ya
ahueni zimepungua, hakuna ajira kama zamani zilizoweza
kuwachukua watoto wanaofaulu madaraja ya tatu na ne
ambao wengi ni hawa wa maskini wanaoshindwa kufaulu
kutiokana na mazingira yaliyo nje ya uwezo wao.

Shule anazosoma mtoto huyu hazina walimu na kama wapo
hawafundishi vema. Mtoto huyu hukatiza masomo kutokana
na kukosa karo ama kutofaulu kutokana na kukosa uwezo
wa kulipia masomo ya ziada maarifu kama Tuisheni. Pia
huduma nyingine kama chakula, mavazi na vitabu ni
vikwazo kwa jamii ya maskini hali inayodunisha kundi
hili pia.

Mtoto wa tajiri au atokaye katika familia yenye kipato
cha kati anayo nafasi kubwa ya kufaulu na kupata
daraja zuri. Ni huyu ambaye sasa Rais wake
aliyemchagua hivi karibuni anayemzungumzia na kumapa
nafasi nzuri ya kubakia kileleni hasa baada ya kupata
elimu hadi ya juu. Ni huyu ambaye sasa atapata mkopo
wa kusoma kwani atakuwa amevuka sifa za serikali
badala ya sifa za vyuo ambavyo ndivyo vinafahamu nani
mwenye haki ya kujiunga na chuo na yupi hafai.

Kwa mara nyingine tena serikali inajionyesha namna
inavyoweza kuingilia na kuathiri teuzi za wanafunzi
katika vyuo maana kuna vyuo vingi vitakaa kuwapa
nafasi wasiopata madaraja haya ya kwanza kwa kuwa
vinatambua maisha ya watanznaia wengi kuwa hawataweza
kuwasomesha watoto wao bila msaada wa serikali.

Ni mara nyingine tena katika kipindi cha mwezi mmoja
ambapo rais Kikwete anaonyesha kusahau wananchi
anaowawakilisha au kukosa kutambua na kuthamini kuwa
kioa jambo lina wataalam wake ambao wanaweza
kulizungumzia vema kuliko yeye. Kuwa rais si maana ya
kuzungumzia kila jambo, suala la mikopo lingeweza
kuzungumzwa vema na bodi ya mikopo kuliko serikali. Ni
bodi hii inayoweza kufahamu nani mhitaji na nani
asaidiwe vipi. Ni bodi hii inayotambua nani ana unafuu
na inaweza kuweka mikakati ya kusaidia kulingana na
mahitaji hata kama kiasi kilichopo cha fedha ni
kidogo.

Kauli ya Rais inafuatana na muendelezo wa Waziri wa
Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu ambaye pia amepata
kukaa na wanafunzi akiwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha
Kilimo Sokoine, Profesa Peter Msola. Hata Waziri huyu
naye anashindwa kufahamu maisha ya wanafunzi wa aina
ipi wasaidiwe na badala yake anatumia mbinu ya kitoto
ya kutangaza madaraja ya kufaulu bila kuzingatia
ukweli wa maana ya kuwepo kwa Bodi ya Mikopo. Bodi hii
ipo kwa kuzingatia wasionacho kukopesha na kubana
watoto wanaotokea katika familia zenye uwezo wa
kujilipia gharama za shule kutokopeshwa ili wanafunzi
wengi waliokuwa wakikosa nafasi na huku wakihitaji
msaada wa serikali wapate pa kukimbilia.

Msola anaonyesha upofu wa uprofesa wake hali
inayotuonyesha wazi kuwa naye keshatumbukia katika
kundi linalothamini nafasi yao maana watoto wa Msola
wako katika daraja lile alilolizungumza Ng'wandu,
daraja linaloweza kuwapatia watoto wao kila kitu na
hivyo kuwakuta wakifaulu madaraja mazuri.

Mawazo ya Ng'wandu niliyoaibua hapo juu yanaweza
kumuweka waziri huyu wa zamani katika kundi
linalopingana na tabia za watawala kujipendelea zaidi
na kusahau wananchi wenye shida. Mawazo haya hata
akiyatoa sasa kwa waziri mwenye dhamana ya wizara hiyo
yanaweza kuonekana kama uchonganishi tu na kiasi
kikubwa hayatasikilizwa maana yanachoma tabia ya
tabaka tawala!

Mazingira ya kufaulu nchini kwetu yanaambatana na
tabia chafu zikiwemo wizi wa mitihani na kubadili
matokeo kabla hayajatangazwa na Baraza la Mitihani.
Jiulize maswali haya; ni nani anaweza kuiba mitihani
au kununua mitihani ya taifa? Ni nani anaweza kubadili
matokeo yake kabla hayajatolewa au kutangazwa na
baraza la Mitihani?

Nafahamu maswali haya yatanihitaji kutoa uthibitisho!
Hata siku moja hiyo si kazi yangu kama Mwandishi!
Nabakia kutoa kidokezo kwani hoja hizo zinafanyika na
wahusika mara zote wamekuwa watoto wa familia zenye
uwezo au wanatokea familia zenye madaraka.

Swali lingine ni hili; ni nani anaweza kulipia masomo
ya ziada maarufu kama tuisheni kwa watoto wake? Si
mkulima anayeishi Nyangao! Hata kidogo haiwezekani
kabisa mtoto yatima au wa mfugaji aweze kupata fedha
za kutosha kutunza familia na kisha kulipia mwanaye
masomo ya tuisheni. Ni watoto wa wakubwa na hasa
wanaokaa mijini wanaonufaika na unafuu wa familia zao
na hivyo kujikita katika kupata elimu inayofaa na
inayoendana na mitihani ya taifa.

Mtoto wa kijijini na hasa wa shule za wananchi ambazo
hazina walimu na vifaa atabakia kutofaulu. Akifanikiwa
atapata daraja za kati, lakini hiki ni kigezo cha yeye
kutokopeshwa ili asome zaidi?

Ni nani tunahitaji kumkomboa. Mheshimiwa Komredi Rais
Kikwete naona unawatazama watu wa kaida yako. Safari
hii pia unaitazama Tanzania kutokea Oyterbay au
Regent! Huioni Tanzania kabisa kutokea familia ya
mkulima anayeshindwa kumpeleka mwanaye shule kisa
kutomudu kununua sare.

Naona humuoni kabisa mtanzania anayeshindwa kulipia
karo ya shule ya kutwa. Humuoni kabisa mtanzania
anayekosa fedha ya kununua kalamu na penseli na
daftari ya mwanaye. Sasa mtoto anayetoka familia hii
unatarajia apate daraja la kwanza katika mitihani ya
taifa inayotungwa na kusahihishwa kwa kutazama majina
ya shule?

Mitihani isiyotazama mazingira magumu ya shule nyingi
bali inayoridhisha na kunufaisha shule zilizo katika
mazingira ya upendeleo na nyingi zikiwa mijini?
Mitihani isiyopima uelewa wa mtu bali iliyotungwa kwa
lengo tu la kupunguza kundi fulani lisipande na kwenda
elimu ya juu?

Tanznaia inahitaji kundi la kati. Kuongezeka kwa
wanafunzi wengi katika vyuo vikuu hakujengi tabaka la
kati. Tabaka la kati linatakiwa kujengwa kwa kuongeza
shule za sekondari na kuifanya elimu hiyo ifanane na
maisha ya watanznaia.

Kunatakiwa kupanuliwa ajira za kundi hili ili wazazi
wanaoona elimu ya muhimu ni vyuo vikuu wapunguze fikra
hiyo. Tazama zamani kazi mbalimbali za viwandani,
majeshini na kwingineko zilivyoweza kujenga kundi la
tabaka la kati. Kuna mikakati gani sasa hasa
ukizingatia kuwa ubinafsishaji umekwapua kila kitu na
kufanya kuongezeka kundi kubwa lisilo na ajira?

Wazazi wengi wanapeleka watoto wao vyuo vikuu kwa
sababu tu wanadhani wakimaliza huko watapata ajira
safi. Wengi wanaamini wazi kuwa watoto wao wakimaliza
vyuo vikuu bila kujali aina ya taaluma wanazosoma huko
watafanikiwa!

Hii si kweli maana sasa tumeshaona kundi hili
likizagaa mitaani bila kazi za kufanya. Kama
litaongezeka kundi hili huku kukiwa hakuna tabaka la
kati tunaathari nyingi hasa katika uadilifu wa kazi
mbalimbali chache zilizopo.

Tathimni ya elimu yetu inapaswa kufanyika haraka hata
kabla hatujajadili mabadiliko ya katiba. Tunatakiwa
kutazama namna ya kujenga tabaka la kati maana hili
ndilo la watendaji kuliko sasa ambapo tunazalisha
maofisa wa kukaa maofisini.

Tunatakiwa kutazama nani wa kusaidiwa na namna ya
kufanya hivyo inawezekana kwa kutazama rekodi za
wanafunzi waliposoma kabla kutaka kujiunga na vyuo.
Tena tunaweza kutazama kiasi cha kodi za wazazi wa
watoto wanacholipa na hivyo kugundua yupi anafaa
kukopesha na yupi asikopeshwe.

Ubaguzi katika suala la elimu na hasa kwa fedha ya
umma ni dhambi. Ni dhambi isiyosamehewa hasa
inapoonekana kuwa watu wenye nafasi hutumia nafasi zao
kusomesha watoto wao nje ya nchi ambako huko hulipa
gharama kubwa zaidi kwa elimu inayoweza pia kupatikana
nyumbani.
 
© boniphace Tarehe 9/07/2006 11:44:00 AM | Permalink |


Comments: 4


  • Tarehe 9/20/2006 3:20 AM, Mtoa Maoni: Blogger mloyi

    Mikopo kwa wanafunzi imekuwa ubaguzi kwa wanafunzi! Mwenye nacho anaongezewa zaidi na asiyenacho anaachwa palepale!
    Serikali inatambua wazi kuwa mfumo wake wa elimu ni duni kulinganisha na mifumo ya elimu ya shule binafsi za wachache! lakini bado wanawapambanisha watoto wa shule hizo na za serikali katika uteuzi mbalimbali. Hawaangalii kwamba hawa wasiposomeshwa na serikali elimu yao itaishia hapohapo walipofikia lakini kundi lingine haliitaji msaada wa serikali wanauchukua sababu upo na uendelezo wa tabia za wazazi wao za kuwakandamiza walio chini yao.
    Iwapo serikali imeweka kota kwa wasichana, sinauhakika na kigezo chake, kwanini isiweke kota na kwa wenye kipato cha chini ili umasikini na ujinga usiwe matatizo ya kurithi na kuwapa matumaini watanzania wote.
    wameweka vigezo, sijui wana maana gani, kwanza nilizani itakuwa njia ya kuwafanya wawajibike na kusiwe na malalmiko juu yao, lakini cha kushangaza mfumo huo kuanza tu, Mlimani mgomo, tunangojea kusikia yaa vyuo vingine, kwa kulalamikia kutowajibika kwao na wao wanajibu kwa kuwashambulia wanafunzi kwa "wapiga kura wao" ambao huwa na masikio makubwa sana kusikiliza uwongo wa viongozi wao na kuukubali.
    Kuna mahali nilikaa nikaogopa kuonyesha mpande wangu, nikauliza ni lini Mlimani kutatulia watu wasome bila malalamiko? wakanijibu labda aondoke Professa Luhanga Kwanza! Inaonyesha jinsi alivyochokwa kwa tabia yake ya kutekeleza wanafunzi na kufikia maamuzi ya ajabu! Anajidai chuo hakihusuki na masuala ya mikopo, bila kuunganisha kwamba bila mikopo chuo hakitafikia malengo yake- wanafunzi watakosekana kwa kiasi kukubwa sana- anaacha kuwasaidia wanafunzi wake kwa ajili ya kiburi! Inaonekana haunganishi masuala vizuri na badi ya mikopo ili wanafunzi wakiripoti tuu chuoni wakute mikopo imeshaandaliwa na waendelee naratiba za masomo kama zilivyopangwa.
    Mambo ni mengi ya kusuluhisha kabla hali hazijakaa sawa na kila mmoja afanye wajibu wake.

     
  • Tarehe 9/20/2006 8:57 AM, Mtoa Maoni: Blogger NDABULI

    Safari ni ndefu

     
  • Tarehe 9/21/2006 1:01 PM, Mtoa Maoni: Blogger MTANZANIA.

    Mathayo na uongozi wa taasisi kubwa kama ile wapi na wapi ndugu zangu?Ni kweli maana hata mienilikuwa pale na nakumbuka siku ya kuuaga mwili wa Bomani pale Nkurumah kulikuwa na mbinu za kumshushua VC,lakini kwa vile ulikuwa msiba basi akatunziwa heshima.Ninachomaanisha ni kweli VC haunganishi vema ili kupunguza matatizo ya mikopo.

     
  • Tarehe 9/23/2006 7:05 AM, Mtoa Maoni: Blogger mwandani

    Nahisi watu wanaotetea mikopo walisoma wakati wa elimu bure. UDSM ilisifika miaka ya nyuma - waulize akina M7.

    Haidhuru, Jitihada zote za kuongeza elimu zilifanikiwa kwenye mambo ya ngumbaro na elimu ya chini kwa wote, kwa idadi ya waliojiunga na mashule. Lakini tatizo la vitabu, madawati na mishahara ... tatizo la elimu nusu nusu limekuwepo na sijui litaisha lini.

    Ukiangalia takwimu utabaini wanaoendelea baada ya shule ya msingi wanapungua sana, siyo leo tu hata miaka ya elimu bure.

    Kikwete anaendelea kufanya udalali, mara marekani, mara kaalikwa huyu au kiongozi yule aje kuwekeza.

    Jumuiya ya Afrika Mashariki ndiyo hiyo nayo inakuja, tunalia lia wakenya wanachukua kazi zetu... sasa watumishi walioelimika watatosha vipi kama mikopo inakuwa kigezo chenye kipaumbele kupata elimu?

    Panatakiwa pawe na affirmative action fulani.

     
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved