Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Monday, August 21, 2006
Waandishi tujifunze kutoka kwa wanamuziki wa kizazi
NIMEFIKA hapa Kowak sekondari kufunza. Shule hii ipo
mkoani Mara katika wilaya ya Tarime. Ualimu ni jukumu
gumu na mimi safari hii baada ya uzoefu wa kutosha
hapa jijini Dar es Salaam, naamua kufanya mazoezi
yangu ya vitendo sehemu nyingine kabisa na iliyo
kijijini.

Maisha ya vijijini yanahitaji tahadhari maana kuishi
huko ni sawa na kujifungia huduma nyingine muhimu za
maisha. Kwa Kowak ni tofauti maana hiki ni kijiji
kilichoendelezwa na misheni ya Kikatoliki na kina
umeme na maji. Tena simu zinaweza kupatikana ila
kinabaki tu kuwa kijiji.

Walimu wengi bora hawapendi kufundisha vijijini.
Wanasema huko hakuendani na hadhi yao kwani huduma
zilizopo haziwezi kukidhi matarajio yao. Walimu hawa
wanaweza kuwa kweli na kuna wakati wanakosea kujenga
fikra hizo.

Kuna faida za kufundisha vijijini na hasara zake.
Katika Tanzania kupima faida na hasara za kufundisha
vijijini kwa walimu hasa wenye shahada kunatokana na
vigezo vya mwalimu mwenyewe. Kwangu mimi, kijijini
kama Kowak kwafaa sana maana nakutana na walimu na
wanafunzi walio na kiu ya mafunzo yangu! Ni shule
isiyo na walimu wa kutosha maana wengi hufika na
kuondoka. Hapa natamani kukaa zaidi maana ninaweza
kutumikia kwa nguvu zangu na nikafanikisha lengo la
kazi yangu ya ualimu.

Safari hii ya Kowak nimeifanya takribani miaka minne
iliyopita! Ni hapa ninapokutana na Farida Koshuma,
mwanafunzi wa kidato cha nne wakati huu ambaye tayari
alishafahamika nchini Tanzania pale aliposhiriki
mashindano ya kuimba yaliyoitwa "Pop Idle" na kisha
kibao chake cha "Pesa" kuonekana kutamba katika vituo
mbalimbali vya redio nchini.

Namuuliza Farida kisa cha kusoma shule ya kijijini
huku. Anajibu kuwa baba yake ndiye kampeleka huko ili
kumpa fursa ya kutenga muziki na shule. Hili jambo
jema, lakini kwa nini mzazi huyu asingempeleka manaye
katika shule iliyo na masuala ya muziki ambayo
inafunza masomo mengine?

Jibu ni rahisi, shule za aina hii hazipo Tanzania.
Masomo ya darasani nchini kwetu yamefanywa kama ajira
na yamepangiwa miaka. Maliza miaka saba, kisha ongeza
minne, kisha miwili, tena minne au mitatu. Ukimaliza
hapo ongeza miwili na maliza na mingine minne hadi
mitano, hapo unakuwa Dokta Boniphace Makene!

Muundo wa elimu huu ni mbovu maana unapoteza muda na
kisha unawafanya wanaosoma kushindwa kujihusisha na
shughuli nyingine za kimaisha. Ili usome ina maana
uache kazi au usijishughulishe na shughuli nyingine.

Tunasahau kuwa kusoma kuna lengo la kufunua uwezo wa
wanaosoma waweze kumudu shughuli balimbali za
kimaisha. Kuna haja ya kutazama namna mpya ya utoaji
wa elimu yetu na jambo hili ni mada nitakayoizungumzia
kwa upekee siku zijazo.

Nimemtumia Farida kama mfano wa wasanii wa muziki wa
kizazi kipya! Sipendi kutumia majina kama "kizazi
kipya, muziki wa Rapu au Bongo Flava." Nalazimika
kuyatumia maana ndiyo yanayoeleweka zaidi licha ya
kuwa, hawa wasanii si kizazi kipya maana wanachokiimba
ni kikongwe na pili hizo Bongo flava sifahamu maana
yake halisi ni ipi zaidi ya kuimba muziki wa Hip Hop
kwa Kiswahili.

Namuuliza tena Farida aliwezaje kupata fedha ya kwenda
kurekodi. Anacheka na kunambia kuwa alikuwa akipunguza
matumizi yake ya shule na kisha mwishoni akawaona
ndugu na marafiki kumchangia ili arekodi. Anaeleza
kuwa imemchukua miaka kutunza kiasi kidogo kidogo cha
fedha hadi kufanikiwa kupata za kutosha kurekodi wimbo
mmoja.

Wasanii wengi vijana hawa wanatokea katika familia
maskini. Wengi hawajaenda shule na wanatumia sanaa hii
kupatia muhogo wao wa kula kwa siku. Kuna mengi ya
kujifunza kutoka kwa hawa lakini kubwa nililoliibua
huko ni jkuhusu malalamiko yetu tunaohitaji kuchapisha
vitabu!

Gharama za kurekodi wimbo mmoja unaweza kufika hata
shilingi laki sita za kitanzania. Ili msanii atoe
albamu nzima basi tazama kiwango hicho kisha zidisha
kwa wastani wa nyimbo kama nane hadi kumi.

Ukitazama haraka haraka utaona vijana hawa wanatumia
fedha nyingi sana ambayo huenda wewe unayedhani
ufanyalo ni bora zaidi ungependa wajiwekeze katika
biashara fulani.

Fedha hizo wanakozitoa utashangaa sana huku ukifahamu
kuwa vijana hawa wengi si wafanya kazi, wengi hawana
daraja la juu katika jamii yetu na tena ni kundi
linalohitaji kusaidiwa ili hata kupata muhogo wa siku!

Wanawezaje sasa kupata fedha hizi za kurekodi nyimbo
zao hadi tukaweza kuzisikia kila siku katika redio?
Tunafahamu uchungu unaowakuta hasa tunapoamua kuwaibia
nyimbo hizo kwa kuzirekodi kiholela katika kompyuta au
katika tepu zinapopigwa redioni?

Vijana hawa hujichangisha fedha kidogo kidogo. Inaweza
kuchukua hata miaka kadhaa kabla ya kufikia lengo lao.
Jamii yetu haijatazama kabisa umuhimu wa kuwasaidia
hawa ila iko radhi katika michango ya harusi na
sherehe tu!

Kila siku ninawaza kuhusu dawa ya tiba ya kuendekeza
michango ya harusi lakini tukagoma kuchangishana
kupeleka watoto vyuo vikuu au kuchangia shughuli za
kujikwamua kiuchumi kama hizi wanazofanya vijana hawa!

Lakini unapata picha hii ya ujasiri wa vijana hawa.
Hawatetereki na wanafanikiwa baada ya kuamua kutumia
akiba yao ya mwisho ili kupata kile wanachodhani
kinaweza kuwanyanyua katika maisha yao.

Upande wa pili ni sisi waandishi na waandika vitabu.
Wengi wetu tumelalamikia gharama kubwa za kuchapa
vitabu. Tunadhani kuwa ni kazi ya makampuni ya
kuchapisha kuchukua kazi zetu na kuzichapa na kisha
kutulipa.

Tunashindwa kusoma picha nyingine ya vijana hawa wa
kizazi kipya, wanapopambana na wadosi wanaosambaza
kazi zao hali inayowafanya wengine kukataa kutengeneza
albamu.

Lakini ukweli rahisi unabaki kuwa, gharama za kuchapa
kitabu kopi 1000 ni zinakaribiana kabisa na zile za
kurekodi wimbo mmoja. Sasa kwa nini sisi waandishi
tunaozesha miswada yetu vyumbani kwetu?

Je hatuamini kuwa tukiandika kitabu na kuchapwa
kinaweza kutuweka katika ramani nyingine kwa wasomaji
wetu? Je tunapolalamika kuhusu tabia ya watu wetu
kukosa kusoma hatutambui kuwa jamii inahitaji vitu
vipya na kama havipo jamii tunataka isome nini?

Kama wasanii hawa vijana wasio na nafasi ya juu katika
jamii, wasiofanya kazi za malipo kama sisi waandishi
wanaweza kufyatua albamu kwa kujichangisha visenti
wanavyookoteza inakuwaje sisi tusitenge gharama fulani
katika mishahara yetu ili iweze kuhifadhiwa na kisha
kulipa gharama za kuchapisha vitabu vyetu?

Kama unafatilia masuala mbalimbali ya uchumi na hasa
bajeti ya nchi utakuta mara zote kodi ya karatasi
ikipunguzwa kila mwaka. Hii inatokana na waandishi
kuwa na nguvu dhidi ya wanasiasa.

Lakini mara nyingi wanaonufaika na punguzo la kodi
hizi ni wachapa magazeti na upande wa waandika vitabu
hatujakumbuka kutumia nafasi hii. Jamii isiyokuwa na
waandika vitabu ni wazi imekufa.

Ukitazama hata vitabu vya kiada katika shule zetu
vimekuwa katika mitaala kwa miaka mingi. Sababu ya
kutovibadili moja kuu ni kukosekana kwa machapisho
mbadala. Miaka ya nyuma serikali iliweza kutumia fedha
kuhamasisha kuchapa vitabu lakini sasa haiwezekanani
kila jambo likasubiliwa kufanywa na serikali.

Nini nafasi ya waandika vitabu sasa hasa unapotazama
kuwa wasanii wa muziki wa rapu wanaweza kuchangisha
fedha kwa kujinyima na kisha kutoa nyimbo
zinazowasaidia kupata nafasi katika maisha na pia
kutuburudisha na kutufunza. Kuna umuhimu wa waandika
vitabu kuamka na kutambua kuwa tunatumia vibaya
visingizio vya kukosa makampuni yanayoweza kuchapa
kazi zetu huku tungeweza kwenda kwenye makampuni hayo
na kulipa gharama za kuchapa kama wafanyavyo vijana
hawa wanamuziki waendapo kurekodi.

Faida ya hatua hii inaweza hata kupunguza urasimu wa
ukandamizaji wa maudhui ya kazi zetu na pia inaweza
kusaidia kuchochea usomaji sambamba na ununuzi wa kazi
ziandikwazo na waandishi wa nyumbani. Tunapolalamika
kushuka kwa elimu bila kutoa dira ya maandishi kuhusu
aina mbadala basi nasi tunashiriki kubomoa elimu ya
watoto wetu.

Ni ukweli ulio wazi kuwa taifa lisilothamini watu wake
kuelimika ni taifa mfu. Kama hivi ndivyo kundi la
waandika vitabu na wenye uwezo wa kufanya hivyo
tunajifunza nini kutoka kwa wasanii wa kiazazi kipya
na kwa nini tusijifunze kwa hawa na kuamka sasa ili
tuikomboe jamii!
 
© boniphace Tarehe 8/21/2006 09:49:00 AM | Permalink |


Comments: 4


 • Tarehe 8/24/2006 9:42 AM, Mtoa Maoni: Blogger Jeff Msangi

  Makene,
  Huu ni uwezo,huu ni ujasiri,huna budi kujivunia na kuufanya kuwa kitega uchumi chako.Ni wazi kwamba ninaposema najua kuandika sina budi kuangalia kazi kama hizi zako.Umegusa mambo mengi sana ya msingi mno katika kisa hiki.Mwanzoni nilidhani ni kisa cha kutunga tu,lakini kadri nilivyozidi kusonga mbele nikahisi gari moto inaongeza kasi.Kikawa sio kisa tena bali ukweli mtupu,maoni ya nguvu.Kazi nzuri ndugu yangu

   
 • Tarehe 8/26/2006 11:26 PM, Mtoa Maoni: Blogger Mija Shija Sayi

  Makene umesema kweli, halafu kunakitu huwa najiuliza ni kwa nini wasomi wengi huwa si watekelezaji wa mambo ambayo walitakiwa wayafanye, na badala yake nafasi zao huchukuliwa na watu wengine? Hebu nitoe mfano wa sisi wasanii tuliosoma, mbona hatuwiki kama wale wasiosomea?

  Si bure! hapa kuna tatizo. Wanablogu nawaombeni hili suala tulijadili kwa kina.

   
 • Tarehe 8/29/2006 4:05 PM, Mtoa Maoni: Blogger Ndesanjo Macha

  Kuna jambo umesema ambalo nataka kukaa chini kulifikiri vizuri. Yaani kopi 1000 za kitabu ni sawa na gharama za wimbo mmoja? Sikuwahi kutazama suala hili la utoaji vitabu kwa miwani hii.

  Lakini tukija upande wa pili, wimbo huo mmoja na vitabu hivyo 1000 walaji ni wangapi kwa kila kazi?

  Da Mija, umesema kweli kabisa. Ukisikia msanii anakwenda chuo kikuu basi ujue jukwaani hayupo tena. Huyo atakuja kuwa wale wanaojiita "critic" atakuwa anatumia muda wake kuelezea mapungufu ya sanaa za wale ambao hawakwenda shule.

  Nadhani moja ya sababu ya wasanii wanavyozidi kupata elimu ndivyo wanavyopunguza kasi ya kupanda jukwaani ni hadhi. Sitafafanua, mwenye kunielewa afafanue.

   
 • Tarehe 8/30/2006 2:09 AM, Mtoa Maoni: Blogger charahani

  Kaka hata mimi hili nikuwa sijapata kulifikiria ni kazi kuweza kukusanya visenti kuweza kutengeneza albamu na ninafikiri wanaofanya hivi wanafanya kwa ujasiri tu bila ya kuzingatia risk watakazokutana nazo sisi je?

  Nadhani huku kupanga na kupangua risk ndiko kunakotufanya tushindwe kufanya vitu vingine.

   
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved