Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Tuesday, August 15, 2006
Vya nje safi kwa Mkapa, kwa Kikwete vichungu?
NILIANDIKA makala tatu mfululizo kuhusu nani anasema
kuhusu Afrika kupitia kona hii huko nyuma. (Gazeti la Mwanannchi) Maswali
niliyoyaibua yanapata majibu mapya kila siku.

Maswali mapya yanatokeza na safari hii tunapata pia
picha mpya tuliyoizoea ya viongozi wa Afrika. Viongozi
wasiotaka kuambiwa au kutazama ukweli ukitangazwa nje
ya mipaka na matakwa yao.

Viongozi wanaopinga shida zinazowaathiri wanaanchi wao
kwa kuwa tu wao hawaziishi. Viongozi wanaotawala kwa
usanii wa kubadili sura, mara leo watu wa watu kweli
kweli na kesho wakijificha katika matumizi makubwa
yasiyothamini hata utu wa watu hao hao wanaodai
kusimamia shida zao.

Nakumbuka tena niliwahi kutunga shairi mwaka 1995.
Kichwa cha shairi hili kilikuwa, "Iweje yeye acheke
sisi tubaki kuguna?" Niliandika shairi hilo maana
sikuamini kama nguvu za Benjamin Mkapa wakati ule
zilimtosha kushinda urais.

Nilimuandikia shairi hilo Mwalimu Julius Nyerere maana
ndiye aliyeonekana kucheka baada ya kijana wake
aliyeamua kumpigia kampeni kushinda na kisha baada ya
ushindi watanzania wakaibuka na maisha ya ukapa!

Ukawa ukapa kweli kweli lakini katika sura ya wananchi
wa kundi duni na ukwasi hasa kwa wananchi wa tabaka la
juu na wageni. Zama za Mkapa zimeisha na hakuna
lililobadili ukapa huo kwa maskini huku ubinafsishaji
ukipata ramani kuwa kazi halisi ya masitrika ya wageni
na wenyeji kubaki watazamaji.

Miaka kumi iliyopita tumeshuhudia mengi ambayo sasa
hivi yanajadiliwa. Mengi ni machafu hali inayoninyima
fursa ya kutamani kutafuta mazuri. Sera za kificho na
usiri zilikithiri na zilipata rubani wa kuzisimamia
hasa.

Hakukuwezekana kuzilaumu sana sera za wakati huo.
Mazingira yaliweka mambo mengi tata. Hata sasa
kuyasafisha kunakuwa kugumu na wakati tunapotazama
namna nzuri ya kusafisha, mambo mapya yanaingia
yanayokosesha mtazamo mwema kwa wanaokubali kufunua
macho yao kuona.

Shaaban Robert katika "Kusadikika" anamtumia Karama
kama mhusika wa tabaka la chini anayefanikiwa kuleta
mabadiliko. Karama anakumbana na vikwazo vinavyotishia
uhai wake. Ananusurika tu bila hata kuamini na kisha
anafanywa kuwa Waziri Mkuu wa nchi na kisha kuibadili
na kuifanya yenye neema tele.

Karama anatokea tabaka la wanaokandamizwa. Kutokana na
tabia ya nchi ya Kusadikika, raia wa aina ya Karama
hakupaswa kuwa na majukumu mengine zaidi ya kutazama
maisha yake tu. Busara na fikra njema hazikuweza
kuingia katika maisha ya watu wa kundi la Karama maana
ugumu wa maisha yao ulitosha kuwafanya waishie
kufikiria kero zao za kila siku na hivyo kuacha
masuala magumu kama utawala kwa walijaliwa kuwa katika
koo za mfalme!

Nafurahi kuwa fikra hizi za Shaaban Robert bado
zinaishi na zinachomoza hapa Tanzania sasa. Natazama
kundi la watawala na namna wasivyotambua maisha ya
wanaowatawala, naliona kundi hili linavyodhani lina
madaraka ya kupindisha hata ukweli wa maisha ya watu
wa chini kwa kuwa linaamini tu, watu wa kundi hili
wananunulika kama nilivyozungumzia katika makala mbili
zilizopita!

Kundi la chini limenyimwa nafasi hata ya kuzungumzia
maisha yao wenyewe. Haliwezi kusema na halina msemaji
kama Karama wa ndani ya Kusadikika. Wanajitangaza kuwa
wasemaji wa kundi la chini na wale wasiotokea katika
kundi hilo au wasioishi maisha ya kundi hilo.

Kizuri tena katika Tanzania ni hiki kuwa, wanajifanya
kuwawakilisha watu wa tabaka la chini wengi ni hawa
wanaowatumia watu hawa kujitengenezea maisha yao.
Mifano katika uhalisia wa hoja hii isitazamwe katika
wawakilishi wa serikali tu bali hata hizi zinazoitwa
NGO ambazo kila kukicha zimekithiri katika kuandika
makala za maombi ya fedha sehemu na sehemu na kisha
kuzitumia katika mahoteli ya kifaharai jijini Dar es
Salaanm au maeneo mengine yenye hadhi ya kitalii.

Utawala wa Rais Mkapa ulikithiri sana kuthamini
waandishi na vyombo vya nje. Huko ndiko Mkapa alitaka
kujenga taswira yake maana ndani hakuona kama kuna
jambo la muhimu kwake kulifanya akishirikiana na
waandishi na vyombo vya ndani.

Waandishi wa ndani mara kadhaa walizungumzwa kuwa
haafahamu kazi yao zaidi ya kupandikiza maneno katika
hoja ambazo hazikuzungumzwa. Utawala uliopo sasa uko
kinyume na fikra hii ya Mkapa kuhusu vyombo vya ndani.

Utawala huu unafahamu kuwa ni vyombo hivi
vilivyoufanya uwepo baada ya kubomoa wale ambao
havikuwahitaji. Utawala huu unafahamu kuwa bado vyombo
vya habari vya nyumbani licha ya kuwa uchaguzi kuisha,
vimeendelea kubakia katika kampeni.

Ni kampeni hii ya kusifia kila kukicha bila kutazama
upande mwingine wa sarafu kulikoibua mada hii
ninayoiandika leo. Je tumuamini Mkapa kuwa vyombo
vyetu vya nyumbani havina uwezo hata wa kutazsama
matatizo yetu bali vya nje ndivyo makini katika kuibua
hoja zinazowakabili wananchi wetu?

Je, tumezoea kero za wananchi hadi tumeona ni mambo ya
kawaida kabisa yasiyoweza kuwa habari? Lakini kama
tumezoea hivyo vipi wakubwa wetu waibuke na kupambana
na filamu?

Nilipozungumzia kuhusu nanin anaandika ukweli kuhusu
Afrika nilitumia mfano wa habari za Afrika Darfur na
kwingineko kuliko na machafuko. Vyombo vyetu vya
Tanzania pia hutunmia habari hizi lakini havijawahi
kupeleka waandishi wake huko ili kupata taarifa zaidi
ya kutafsiri zilizoandikwa na waandishi wa kigeni!

Tunapata picha gani hapa? Jibu rahisi litabakia kuwa
vyombo vya Afrika havina uwezo wa kifedha wa
kuwagharamia waandishi wao ili kuwafikisha kila lilipo
tukio muhimu.

Vyombo vya Afrika pia havijajitanua na kuongeza
shughuli nyingine zinazoendana na habari. Vyombo vya
nje sambamba na waandishi wao hujihusisha na aundika
filamu, uandishi na uchapaji vitabu na vyote hivi
huvifanya vyombo kujipatia fedha nyingi huku malipo
kwa waandishi wakiweza pia kupandishiwa kipato chao.

Mwaka 1986 tulihama kutoka Musoma Mjini na kwenda
kuishi Musoma Vijijini. Tulipofika huko, tulikuta bado
ziwa likiwa na samaki ambao wavuvi hawakuona hasara
kuwagawa bure kwa watu waliopo pale ziwani.

Miaka miwili baadaye viwanda vikaingia na samaki
wakawa wakipotelea ziwani huko huko na wavuvi kurejea
wakiwa na mitumbwi mitupu baada ya kufanya mauzo ndani
ya ziwa.
Ni tangu kipindi hicho misafara katika kiwanda cha
Mazara wakati huo hapo Musoma mjini ilipoongezeka
ambapo akina mama walikuwa wakijpanga kusaka kitoweo
maarufu kama mapanki!

Ukweli huu kupindishwa na hata rais wa nchi inatoa
picha mbili. Moja, rais anapenda kusifiwa tu au
anapenda kuwaona watu wa tabaka la juu tu hadi
hafahamu shida za wananchi wa chini na pia, raia
anaongoza watu asiotambua hata kero zao au anazifahamu
ila anataka zisitamkwe maana zilishabadilika na
kutokuwa kero tena!

Muswada wangu wa Kitabu, "Barua kwa Mama" nina maelezo
mengi kuhusu biashara ya ngono. Eneo langu la mjadala
ni Dar es Salaam lakini naweza pia kurejea kabla ya
mwaka 1986 eneo la Rutiginga mini Musoma ambapo
palikuwa maarufu kwa bniahara hiyo!

Siwezi kuiita biashara ya ngono ukahaba maana kufanya
hivyo ni kupindisha ukweli kuhusu nafasi ya mnunuzi na
muuzaji. Bishara ya ngono imekuwepo na inatanuka, sina
uzoefu wa Mwanza lakini Mwanza si kisiwa hasa ukitilia
maanani kuwa bishara ya samaki imeibua kundi fulani
kuwa na fedha na mara nyingi wavuvi baada ya kumaliza
shughuli zao hujiwekea fursa ya kujiburudisha na eneo
muhimu kwao likiwa pia hili la kununua huduma ya
kujamiiana!

Ukitafuta uongo wa filamu ya Darwin Nightmare kama
amabvyo baadhi ya wanaofuata bendera fata upepo
walioonekana kuandamana kuipinga, utatambua kuwa nchi
yetu ina makundi yasiyothamini hata anayeyathamini!

Mtunzi huyu anatoa picha ya pili ambayo vyombo vyetu
vya nyumbani vilipaswa kufanya ili kuwa na uwezo
halisi wa kuwabana wawakilishi ili wapunguze matumzi
yasiyokuwa na maana na fedha chache zilizopo ziwaguse
wananchi wanaohitaji.

Biashara ya ngono haifanywi na wanaume maskini. La
hasha, ni ukweli usiopinda kuwa, wateja wakubwa ni
watu wenye nafasi wakiwemo watoa maamuzi makubwa kwa
nchi. Hawa wanatofautiana kutokana na daraja za
ununuzi na ujihusishaji katika biashara hii!

Kwa nini hawa hawa wasitazame kero za wananchi na
kuzitatua ili dada zetu wanajihusisha na biashara hii
bila kutaka waiache na kuendesha maisha yao kwa namna
nyingine! Je jambo hili likizungumzwa na vyombo vya
nje basi limekuwa kero, uongo na uzandiki?

Kuna haja ya viongozi wetu kukubali kujifunza katika
masuala hasi maana ni haya yaliyofanya nchi nyingi
kuendelea. Ukweli ni kuwa huwezi kugeuza jambo likawa
uongo kwa kuwa tu anayelizungumza ni mtu wa nje!
Tunatakiwa kutazama upya na kupiga vita tabia za
kushabikia na kushangilia hata sehemu ambapo hatuna
mafanikio.
 
© boniphace Tarehe 8/15/2006 01:54:00 AM | Permalink |


Comments: 4


  • Tarehe 8/16/2006 5:49 AM, Mtoa Maoni: Blogger mwandani

    Katika familia kama kuna mtoto mwizi, kuna dada mwepesi wa kutoa ngono, kuna baba mlevi... au kukiwa na lolote baya, atakaponena jirani juu ya familia hiyo mtaa utakuwa haukaliki, familia nzima itanyanyuka macho yamewatoka wakitaka kwenda kumsuta jirani... japo yote kweli

    Nafikiri familia yetu inabidi ikae makini, itazame matatizo hayo ya jinamizi la Darwin. Wanaohusika wafuatilie.

    nilitumaini JK angekuwa anaongea na sare zake kama kina Bush na Chirac na Tony Blair. Hao ndio marais wenzake, halafu katibu fulani wa utamaduni au mahusiano ya nje angesema na huyo mtengeneza filamu. sasa JK kaenda kusutana na mpiga filamu. haya!

    Katika habari hii uliyoandika hapo juu umegusia jambo muhimu - umoja wa raia - ama waandishi au watu wenye madai yoyote. hatuna civil society ya kweli inayowakilisha mawazo ya watu, hiyo ni nguzo ya demokrasia inayolenga kutatua matatizo... tunazo NGO nyingi tu.
    nikiangalia hata upinzani kwa hivi sasa sidhani kama wanaweza ku-mobilise watu wakaenda kutia presha juu ya mapanki au lolote jengine. wanaweza kufanya mikutano ya wanachama - 600 au 700 - lakini sijapata kusikia wamekusanya watu wa kawaida wenye madai muhimu au wanaodhurika na jambo fulani na kutia presha - kwa petition, maandamano au vyenginevyo.

    Serikali itaendelea kupeta, viongozi wataendelea kusuta watu mpaka hapo watu watakapoanza kuwa makini kwa dhati.

     
  • Tarehe 8/16/2006 6:38 AM, Mtoa Maoni: Blogger mloyi

    Nafurahi leo umejitokeza, habari yako ni ndefu kidogo sasa siwezi kuisoma vizuri, nimeichukua nitaisoma nyumbani, kama nitakuwa na cha kuchangia utaniona tena.
    Usiende tena ukakawia kama mwaipopo kaingia mbeya na kutokomea. Msalimie sana ukimuona muulize vipi tena akajikata kimoja?

     
  • Tarehe 8/18/2006 8:47 AM, Mtoa Maoni: Blogger Rashid Mkwinda

    Kinachotaka kujitokeza hapa ni uelewa wa fikra binafsi za mtunzi ambaye amejikita katika uhalisi wa kilichopo ndani ya jamii yetu nashangaa kuona fikra hizi halisi zinataka kupindishwa tena zikiungwa mkono na watu lukuki bila kujali kwamba kufanya hivyo ni kufuata mkumbo.

    Hebu jamani na tufakari uhalisi wa maisha ya Mdanganyika yalivyo yanatifauti gani na fikra za Hubert Sauper?au kwa kuwa waheshimiwa sana hutembelea magari ya kifahari ilhali wapiga kura wakiendelea kuishi katika vibanda vya mbavu za mbwa wakitafakari mlo wa siku moja na kula Mapanki ilhali minofu ikisafirisha nje ya nchi?

    Jamani kwa nini tunavaa miwani ya mbao huku tukilalia masikio tusione na kusikia yamayojiri chini ya anga hili lililojaa kero,kedi, kejeli na adha lukuki?

    Hapana mie nadhani akili zetu hazitutoshi kutafakari yanayojiri hebu na niishie hapa wasije kuniSAUPER bure nikaviacha vitegemezi vyangu vikihanja kisa eti nimeandika kitu cha ukweli?

    Wakatabahu Makene kazi kwako mie simo!!!!

     
  • Tarehe 8/18/2006 11:39 PM, Mtoa Maoni: Blogger Mija Shija Sayi

    Mbona mambo yako wazi kabisa! mara nyingi nimekuwa nikitafakari juu ya hali ya maisha ya wananchi waliozungukwa na Ziwa Viktoria, kwa kweli hakuna uwiano kabisa wa hali yao ya maisha na rasilimali waliyonayo. Hii njaa iwapatayo mara kwa mara hutokea wapi??.. Lipo tatizo mahala. Bahati mbaya sana siku hizi kila mtu amekuwa akiangalia maisha yake binafsi kuanzia kiongozi hadi raia wa kawaida kitu ambacho kimepelekea kutokugundua mwenzio anaishije, hatujaliani tena na ndiyo sababu tunakuwa hatujui kama jirani siku zake zinakwenda kwa kula mapanki tu katika milo yake yote mitatu. Sasa katika hali kama hii anapotokea mtu wa nje na kuja kutushtua kwamba jirani yako anakula mapanki kwa sababu kazidiwa ujanja na walaghai fulani, mimi nilifikiri mtu yule angekuwa ni wa kushukuriwa maana anainusuru hali ya jirani, lakini badala yake ndiyo anaonekana ni muongo na mzandiki, hivi kwa hali hii kweli ya kutokutaka kuukubali ukweli tutafika?

    Halafu kuna haja gani ya kutengeneza filamu nyingine ya kuisafisha sura ya nchi? na kama itatengenezwa basi atafutwe msema kweli na mwenye machungu na wananchi aisimamie. Mchungaji Mtikila angefaa sana.

     
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved