Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Sunday, July 16, 2006
NI CHACHAGE YUPI ALIYETUTOKA?
NI MWEZI Julai sasa; hiki ni kipindi cha joto kali
sehemu mbalimbali nchini Tanzania. Jijini Dar es
Salaam hali inatisha zaidi lakini baadhi ya
wakazi wa jiji hili tumejipa uhalali wa kumudu ghasia
za joto hili kutokana na mavazi tunayovalia!

Mimi ni miongoni mwao, nimevalia shati maridadi na tai
imeibana shingo yangu. Shida ya joto siioni kabisa,
naongeza na koti juu ili niweze kuwahi miadi ya
kukutana na Profesa huyu!

Napita kutoka ofisi za Mwananchi hapa Tabata relini na
safari yangu ni kuelekea Chuo Kikuu Dar es Salaam.
Huko nitakutana na Mwenyekiti wa Chama cha Wahadhiri
wa Chuo hicho na pia Mkuu wa Idara ya Sosholojia.

Mavazi niliyovaa yananipa hadhi ya juu sana na
yananitofautisha na msimamo wa mwenyeji
ninayemtembelea. Profesa Seth Chachage leo pia kavalia
shati lake la bluu hivi lenye rangi inayoonyesha
kupauka na suruali ya kaki. Chini kavalia viatu vya
wazi ambavyo pia ukivitazama ni vya gharama nafuu
kabisa! Najiuliza moyoni, hivi huyu si ni Profesa
mwenye heshima kubwa tu nchini; nini siri ya maisha
haya! Huyu ndiye Chachage mbegu ya watanzania walioiva
katika misingi ya Kimaksi na wakatambua maana ya
ujamaa na kisha wakauishi kwa dhati!

Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mlimani wenye mtazamo wa
kusoma ili kupata fedha na kuishi maisha ya juu
wanamuona Chcahge kama profesa asiyefaa kuigwa!
Hawatambui kabisa maana ya fikra za elimu, hawajui
utajiri wa ubongo na usomi. Kubwa ni kuwa, hawajui
thamani ya uanazuo! Wanamtazama huyu kama priofesa
aliyepoteza njia na kuwasifia wale wanaodhalilisha
usomi na uanazuo wao kwa kushabikia hata mambo
yanayoudhalilisha usomi na taaluma zao ili tu
wajipatie fedha!

Ninapofika ofisi hii iliyo katika gorofa lefu kabisa
katika kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii, nafuta
kwanza jasho. Kutembea ngazi kupanda ghorofa kama si
ya sita hivi...sikumbuki vema, ni jambo gumu. Lifti ya
jengo hili siiamini kabisa maana wanafunzi
wameongezeka na ubora wa majengo hautazamwi! Inaweza
siku moja kuleta zahama na mafundi kwa Tanzania
unafahamu!

Ofisi ya Chachage imepambwa na karatasi na vitabu kila
kona. Kuna meza kubwa na viti viwili vya wageni. Kisha
nyuma kuna ubao ambao nao umjaa maandishi. Inaonyesha
amekuwa katika mikutano isiyoisha kila siku na hapa
muda huu yu dhaifu kiasi fulani.

Ni siku chache zimepita tangu idara ya Sosholojia
ikutane na mabadiliko yaliyolenga kuboresha tabia ya
usomaji wa wanafunzi. Huko nyuma masomo hayo yalikuwa
mchekea na tangu Chachge ateuliwe kuwa Mkuu wa Idara
hiyo amekuja na mkakati maridhawa hali iliyowafanya
wanafunzi zaidi ya 150 kufeli somo moja huku wakiwa
mwaka wa mwisho!

Profesa huyu ni mzuri katika kujenga hoja na
kuzisimamia. Ana mtazamo wake na kamwe hayumbishwi
kirahisi. Huwezi kumuambia chochote kuhusu George Bush
na vita vyake vya Irak! Inapotokea suala la kusimamia
misingi ya kazi, hana mzaha na hili nimeweza
kulishuhudia katika vikao mbalimbali vya maamuzi
katika Chuo hicho enzi za uanafunzi wangu hapo.

"Samahani Makene, ninameza madawa na yananichanganya
kichwa hapa. Hizi dawa ni kali sana sijui
unazifahamu?" Ananiuliza na mimi najidai kutingisha
kichwa kuashiria kukubali huku ukweli ukiwa sijawahi
kuzitia kopeni dawa hizo!

Chachage anazungumzia namna elimu ya juu inavyopuuzwa
nchini Tanzania. Ananitazama na kuniambia, "wewe
umetoka hapa unatakiwa kutamka ukweli huu maana kuna
watu hapa hawataki kabisa kusikia haya tunayoyasema,"
anasema na kuongeza;

"Tafuta mazingira ya kutoniweka jina katika maelezo
yako maana wakisoma hawakawii kusema ni hawa hawa
akina Chachage." Kauli hii anaitoa ikiwa ni siku
chache tangu kuwepo mkwaruzano kati ya watawala wa
Chuo hicho na uongozi wa UDASA kuhusiana na maamuzi ya
kufukuza wanafunzi chuoni hapo bila kuhusisha upande
wa wahadhiri na pia kupitisha maamuzi ya kuongeza
idadi ya wanafunzi bila kutazama nafasi za wahadhiri
sambamba na mishahara yao!

Nilifika katika ofisi hii kuzungumzia namna wahadhiri
wa Tanzania wanavyokimbilia nchi za nje kutafuta
malisho bora. Hoja nyingine ilikuwa kulinganisha
vipato kati ya wahadhiri wa vyuo vya Tanzania na nchi
nyingine za Kusini wa Afrika.

Chachage ananipa makabrasha baada ya kupekua karatasi
lukuki ofisini kwake. Anaonyesha namna kazi ya ualimu
inavyodhalilishwa licha ya kuwa wahadhiri hao hukaa
miaka na miaka shule na kuumia kusoma. Hoja yake
inatazama namna ambavyo wanyonge wa fikra
wanapoukimbia uhadhiri na kwenda kwenye siasa ili
kutafuta malisho jambo ambalo yeye hakulipa
kipaumbele!


Chachage anapunguza idadi ya maprofesa walioamua
kutumikia umma licha ya kazi zao za kitaaluma. Mchango
wake katika majukumu ya kumzungumzia maskini ulikuwa
thabiti mno na kweli alifanikisha lengo la kauli ya
Mwalimu Nyerere kwa wasomi wa Tanzania, hasa
linapokuja suala la kuwazungumzia wananchi maskini
pale wanaposahauliwa na serikali zao.

"Makuwadi wa Soko Huria" ni riwaya kati ya mpya za
Kiswahili ambazo zinazungumzia maudhui ya wizi na
uuzaji wa nchi. Kazi hii ya Chachage inatoa picha ya
maisha yake hata baada ya kuanguka kwa usoshalisti
huko Urusi.

Ameishi maisha ya bila kujiunga na chama chochote cha
siasa licha ya kuwa aliweza kushiriki katika mapambano
ya kujenga demokrasia na utetezi wa wanyonge dhidi ya
tabala la wanyanyasaji.

Maisha ya Chachge yanabaki kuwakumbusha wasomi wa
Tanzania hsa suala la kuwakimbia maskini na kujijali
zaidi wao. Mchango wake katika kutatua matatizo ya
migogoro katika Chuo Kikuu iliyohusu wanafunzi na
utawala wa Chuo au na serikali ni suala lingine la
kulikumbuka.

Waliowahi kukabiliana na mikono ya sheria zisizo na
miguu na maamuzi yasiyotazama busara katika Chuo hicho
watafahamu umuhimu na nafasi ya Chachage. Huenda wengi
wasingalihitimu masomo yao hapo kama ambavyo waliokuwa
wakihusika na masuala ya kukiuka misingi ya kusoma kwa
haki watabaki wakimuona kama mti mkavu usiokatika
kutokana na namna ambavyo hakupenda udanganyifu katika
mitihani.

Huyu ndiye profesa hasa, aliyekuwa msemaji wa umma,
mwandishi wa vitabu, mhadhiri hasa na jabali
lisiloyumbishwa kwa misingi ya mali. Maisha yake
yatakumbusha vijana wengi wanaotamani simku moja
Tanznaia kurejea katika enzi za ujamaa ambapo matajiri
waliojiuzia nchi watakapopinduliwa chini na kuleta
uruhu wa kiuchumi wa raia masikini.

Mola mlaze pema Profesa Seth Chachage maana vita
ulivyomtuma kupigana amepigana vema na imani yako
ameilinda.
 
© boniphace Tarehe 7/16/2006 09:43:00 AM | Permalink |


Comments: 1


  • Tarehe 7/19/2006 4:57 PM, Mtoa Maoni: Blogger Ndesanjo Macha

    Asante sana Makene kwa heshima uliyotoa kwa Prof. Chachage kwa kuandika mistari hii iliyokaakaa kiriwayariwaya. Mchango wa huyu bwana ni vigumu kuweza kuelezea mwanzo hadi mwisho. Umefanya jambo la maana kuweka katika kumbukumbu ya kasri hili maneno haya machache kuhusu huyu ndugu yetu.

     
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved