
KASRI LA MWANAZUO limepokea taarifa za kuondoka kwa mmoja wa wanajamii wa Wanazuo wa Tanzania kwa masikitiko. Kama umewahi kusoma "Makuwadi wa Soko Huria" riwaya mpya kabisa inayojadili ubinafsishaji basi utamfahamu Profesa Seth Chachage ambaye kwa taarifa nilizozipata tangu jana amefariki dunia.
Mara ya mwisho KASRI lilipata fursa ya kufanya mahojiano na Profesa huyo na kwa heshima yake mahojiano haya yataandikwa katika safu ya Gazeti la Mwananchi na kisha kuwekwa hapa baadaye wiki ijayo. Nina mengi ya kuandika kuhusu gwiji huyu lakini niishie hapa kuwapa taarifa wanajumuiya ya wamiliki wa Magazeti Tando maana Chachage katika siku za uhai wake amechangia sana kuikuza jamii yetu kwa kuhamasisha msingi wa kumdharau mnyonyaji na kuongeza ujasiri kwa wanaonyanyaswa! Kama unakumbuka sana hili ndilo lengo kuu na msingi wa jumuiya yetu.
Poleni wanazuo wote na nitumie fursa hii pia kutoa pole kwa familia ya Marehemu na jumuiya ya Chuo Kikuu Dar es Salaam. Ni ukweli ulio wazi kuwa Chachge amevipiga vita vilivyo vikali na kwa kiwango kikubwa amevishinda na anapumzika kwa heshima!
Bwana ametwaa na siku zote hakuna anayeweza kuhoji uhalali wa hulka yake njema!
Pichani anaonekana Chachage akiwa katikati katika moja ya makongamano mbalimbali aliyofanya wakati wa uhai wake.
Kweli yametimia.
Niliwahi kukorofishana naye wakati nikiwa rais wa kitivo cha fani na sayansi za jamii na yeye akiwa dean msaidizi wa kitivo hicho.