Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Thursday, July 13, 2006
BARUA YA PROFESA SHIVJI KUMUAGA PROFESA CHACHAGE
RAFIKI na ndugu yangu mmoja kaona na mimi nafaa kupata liwazo la barua hii. Nikaona na wewe msomaji unapaswa kupata pia liwazo hili kalba sijabandika na mimi makala yangu baadaye jumapili hii kumuaga shujaa aliyetukimbia hivi wiki hii. Nisizungumze sana soma barua hii ya Shivji.

Ndugu yangu
Rafiki yangu
Kamaradi Chachage:
Nani kasema umetuacha?

Eti umefariki!
Kwani mwili ndiyo maisha?
Maisha ni fikra.
Maisha ni vitendo.

Maisha ni ubinadamu.
Fikra zako,
vitendo vyako,
ubinadamu wako,
utadumu.

leo, kesho, keshokutwa na milele.
Vitendo vyako tutavienzi,
ubinadamu wako tutauiga,
fikra zako tutazieneza.
Msomi wa Afrika,

mteTEzi wa wanyonge,
mshabiki wa fikra za kitabaka,
tabaka la wavujajasho.
nimetumwa.
Nimetumwa na Wasomi wenzako wa Afrika kupitia CODESRIA nikuletee Salaamu zao.
Wameniambia, nikuage.
Nimekataa.

Sikuagi.
Nitakusindikiza tu.
uwaone Wazee Wako,
majirani zako,
watu wema wa Njombe.

Uchanganyike na viumbe wa ardhi na bahari,
viumbe visivyo na ubaguzi,
mipaka,
unyonyaji,
ukandamizaji.
Uwashawishi, wafundishe wanadamu maana ya ukombozi. Kama ulivyokuwa unatufundisha sisi daima.

‘Ewe Issa, kwani, Shivji siyo mwana wa adamu?’,
Ukanitania,
Ukichota kutoka hazina ya ucheshi wakO bila uchoyo.
"Umejipachikia majina haya yote ya Miungu!
MLIMBIKAZI, WE ISSA!’

"Mungu wa Waislamu na Mungu wa Wakristo,
Mungu wa Wahindu na Mungu wa Wasambaa.
unataka wapigane?
wachinjane.
Eti moja ni –a,
mwingine ni –ji!’

"Futilieni mbali ushenzi wenu wa kubaguabagua!’, ukakasirika.
"Unganeni kujikomboa", umetusihi,
"kutoka kwa makucha ya ubeberu na ubepari, unyonge na udhalilishaji.’

Buriani ndugu yangu,
Buriani rafiki yangu,
Buriani Kamaradi Chachage.
Ufikesalama.
Upumzike na Viumbe visivyonyumbishwa na vituko vya Wanaadamu.


Nakuahidi.
Nitaufikisha ujumbe wa maisha yako.
Kwa WanaUdasa,
Kwa WanaCodersia.
Kwa Wana wa Tanzania,
Kwa Wana wa Afrika………………….Buriani………..
 
© boniphace Tarehe 7/13/2006 10:51:00 PM | Permalink |


Comments: 2


 • Tarehe 7/14/2006 3:02 AM, Mtoa Maoni: Blogger mwandani

  Mungu amuweke pema.

  Hili shairi la Shivji linatoa mwangaza mzuri wa nafsi ya marehemu. Kweli, utu wake, na kazi zake zitaendelea kunufaisha.

  Ahsante Makene kwa kutuwekea shairi.

   
 • Tarehe 7/17/2006 4:09 AM, Mtoa Maoni: Blogger Bwaya

  Sikudhani kama ingekuwa rahisi liwe blogini, Makene nashukuru. Nililiona kwenye Rai ya wiki jana. Kweli Tanzania imetokwa na mtu muhimu kama inavyoonekana kwenye shairi la Shivji na hata katika makal yako ya mwananchi, ambayo bahati nzuri imeiweka kwenye blog hapo juu. Kazi ya kuziba hili pengo si mchezo. Marfehemu hakuwa kama wasomi wengine tulionao.

   
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved