Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Monday, June 12, 2006
YU WAPI MARK MSAKI?
NI kitambo sasa tangu komredi Mark Msaki atoke Afrika kUsini na kuja Dodoma na kisha kuratibu Azimio la Dodoma. Majukumu yale makubwa ya kihistoria yalifanikiwa sana chini ya uongozi wake lakini akatarajiwa kuwa angeweza pia kutoa maono ya safari yake katika Gazeti Tando lake baada ya ama kurejea Afrika Kusini au kuamua kutuama kabisa hapo Dodoma.

Hadi sasa sifahamu yuko wapi huyu jamaa na kweli namtafuta sana nizungumze naye maana kuna mengi ya kujadiliana na kuyawekea dira ili jumuiya yetu iweze kubaki na heshima ya kujiandalia mikakati yake na kuitekeleza! Nisikamilishe kilio changu kwa kuandika riwaya tu hebu niandike shairi japo shairi guni hapa pia maana sijatunga ngano hizi siku nyingi nami pia.

Yu wapi Mark Msaki, semeni tumuoneni
Semeni hamjitaki, gwiji huyu mfichani
Ama mnataka laki, ili kumrudishani
Mark Msaki yu wapi, mbona kimya chazidini?

Miruko katuliani, hasemi kajifichani
Twambie alikulani, kisa kutukiambiani
Wapaswa kutofichani, ukweli bainishani
Twambie apotupwani, Marki Msaki jamani

Sandiki nimechokani, lazima niambiweni
Wote mmenyamazani, na siri mmetunzani
Iweje mumfichani, bila sisi ambiwani
Isiwe mbojo kawani, Mark Msaki jamani.
 
© boniphace Tarehe 6/12/2006 09:57:00 PM | Permalink |


Comments: 3


 • Tarehe 6/13/2006 5:52 AM, Mtoa Maoni: Blogger mloyi

  Umenigusa tena na mashairi yako, umenifanya nimalize "mgomo" wa kutoa maoni kwenye nyumba yako.
  Mark Msaki haonekani, hatijui habari zake zinaendeleaje, Mwaipopo alosema amerudi nyumbani bado tunasubiri tathmini yake ya utofauti aliouona alikokuwa ikilinganishwa na Tanzania ilivyobadilika.

   
 • Tarehe 6/13/2006 7:34 AM, Mtoa Maoni: Blogger Jeff Msangi

  Makene,swali zuri sana hili na ushairi makini pia.Mark kama unasoma habari hii,tuambie wapi umejificha?Wanaharakati tujue kama uko salama.

   
 • Tarehe 6/18/2006 11:46 PM, Mtoa Maoni: Blogger msangimdogo

  Nadhani kina Miruko wanaweza kutuambia huyu jamaa wamemficha wapi, maana mimi aliniahidi kuwa wakati anarejea Afrika Kusini angepitia Mbeya, sasa sijui jamaa wamemnywesha juice za Ubuyu na karanga ameamua kulowea Dodoma au vipi. Au Msonge mpya wa Bunge umemvuta asitake kuondoka? Miruko tueleze mmempeleka wapi Msaki

   
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved