Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Thursday, June 15, 2006
BAJETI YA TANZANIA 2006/2007
HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA
MHESHIMIWA ZAKIA HAMDANI MEGHJI (MB.),
AKIWASILISHA KATIKA BUNGE MAPENDEKEZO YA SERIKALI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2006/2007
TAREHE 15 JUNI, 2006

UTANGULIZI:

1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge likubali kujadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2006/2007. Pamoja na hotuba hii, vimetayarishwa vitabu vinne vinavyoelezea kwa kina takwimu za bajeti. Kitabu cha Kwanza kinahusu makisio ya mapato. Kitabu cha Pili na cha Tatu vina makisio ya matumizi ya kawaida kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Mikoa na Halmashauri za Miji na Wilaya. Kitabu cha Nne kinaelezea makadirio ya matumizi ya maendeleo kwa Wizara, Idara na Mikoa pamoja na Halmashauri. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2006/2007 ambao ni sehemu ya bajeti hii.

2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuchaguliwa kupitia CCM kwa kura nyingi, kuwa Rais wa nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu nchi yetu kupata Uhuru. Pia, nampongeza Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa kwa kuteuliwa na Rais na baadae kuthibitishwa na Bunge letu kwa kura nyingi kuwa Waziri Mkuu. Nakupongeza wewe Mheshimiwa Spika, na Naibu Spika, kwa kuchaguliwa na Waheshimiwa Wabunge kuongoza Bunge letu. Nawapongeza nyote Waheshimiwa Wabunge kwa kuchaguliwa katika majimbo yenu na wengine kuwakilisha Jumuiya zenu kupitia viti maalum. Napenda pia kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa kuteuliwa kuongoza Wizara zenu. Sote tuna dhamana kubwa ya kuwahudumia wananchi na kukidhi matumaini yao.

3. Mheshimiwa Spika, napenda sasa binafsi kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Rais, kwanza, kwa kuniteua kuwa Mbunge na kisha Waziri wa Fedha wa kwanza mwanamke. Mheshimiwa Rais amenipa heshima kubwa na napenda kumhakikishia yeye, Chama changu na wananchi wote kwa ujumla kuwa nitafanya kazi kwa uwezo wangu wote, na ninamwomba Mwenyezi Mungu anisaidie. Amina.

4. Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa wale wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine kufanikisha matayarisho ya Bajeti hii, ambayo maandalizi yake yamehusisha wadau wengi. Napenda kuishukuru Kamati ya Fedha na Uchumi ya Bunge, chini ya Mwenyekiti wake Mh. Abdallah Omari Kigoda (Mb) kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuchambua makisio yote ya mapato na matumizi. Ushauri wa Kamati hii umesaidia sana kuboresha bajeti ninayowasilisha leo.

5. Mheshimiwa Spika, napenda pia kutoa shukrani zangu kwa Wizara zote, Idara zinazojitegemea, Mikoa, Halmashauri za Miji na Wilaya, taasisi za kitaifa na kimataifa na wawakilishi wa sekta binafsi, kwa michango yao iliyosaidia kufanikisha bajeti hii. Naomba niishukuru kwa namna ya pekee Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutayarisha kwa wakati Muswada wa Sheria ya Fedha na nyaraka mbalimbali za Sheria kama sehemu ya bajeti hii. Aidha, napenda kuwashukuru wafanyakazi wenzangu wa Wizara ya Fedha nikianza na Naibu Mawaziri wa Fedha, Mh. Abdisalaam Issa Khatib (Mb) na Mh. Mustafa Hadin Mkulo (Mb); Katibu Mkuu, Gray Mgonja, Naibu Makatibu Wakuu; Ramadhan Khijjah na Joyce Mapunjo, Wakuu wa Idara, na wafanyakazi wote wa Hazina. Namshukuru Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kwa kuchapisha hotuba hii, vitabu vya bajeti, pamoja na nyaraka nyingine zinazohusu bajeti hii kwa wakati. Mwisho, nawashukuru kipekee wataalam na wale wote waliotoa mapendekezo kuhusu maboresho ya ukusanyaji wa kodi mbalimbali. Mapendekezo na ushauri wao umezingatiwa katika kuandaa bajeti hii.

6. Mheshimiwa Spika, Mkutano huu wa Bajeti ni wa kwanza baada ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika mwezi Desemba, 2005. Katika uchaguzi huo, Chama Cha Mapinduzi kilipata, kwa kishindo kikubwa, ridhaa ya wananchi ya kuendelea kuiongoza nchi yetu. Ushindi huo wa CCM ulidhihirisha siyo tu imani kubwa waliyo nayo wananchi kwa Chama Cha Mapinduzi, bali pia matarajio na kiu yao ya maendeleo kwa Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya.

7. Mheshimiwa Spika, Wakati akifungua Bunge hili tarehe 30 Desemba 2005, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alieleza bayana majukumu ya msingi ya Serikali ya Awamu ya Nne kwamba ni pamoja na, nanukuu: “Kwanza, kuitoa Tanzania kutoka kwenye dimbwi la uchumi ulio nyuma na tegemezi na kuiingiza katika mkondo wa uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegemea; na pili, kuwashirikisha wananchi wote kwa njia ya uwezeshaji katika ukuzaji wa uchumi na kutokomeza umaskini”. mwisho wa kunukuu. Bajeti hii ni mwanzo wa kutekeleza mikakati ya kufikia malengo hayo aliyoyaeleza Mheshimiwa Rais. Katika kutafakari na kuchangia bajeti hii ya mwaka 2006/2007, hatuna budi kuzingatia lengo kuu la kukuza uchumi kwa kasi zaidi, na kuwajumuisha wananchi walio wengi zaidi kushiriki na pia kufaidika na matunda ya uchumi imara.

UTEKELEZAJI WA SERA ZA BAJETI YA MWAKA 2005/06:

8. Mheshimiwa Spika, mwenendo wa viashiria muhimu vya uchumi kwa kipindi cha Julai 2005 hadi Machi 2006 ulikuwa wa kuridhisha, licha ya janga la ukame ambalo lilisababisha uhaba mkubwa wa chakula na upungufu mkubwa wa maji kwa ajili ya kuendesha mitambo inayozalisha umeme. Aidha, kupanda mfululizo kwa bei ya mafuta ya petroli katika soko la dunia kumeongeza gharama za uzalishaji na huduma mbalimbali. Matukio haya yalisababisha mfumuko wa bei nchini kupanda kutoka asilimia 4.3 mwisho wa Julai 2005 hadi asilimia 6.9 mwezi Aprili 2006. Hata hivyo, kama alivyoelezea Mheshimiwa Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, uchumi umekua kwa asilimia 6.8 mwaka 2005 ikilinganishwa na asilimia 6.7 mwaka 2004. Vilevile, akiba ya fedha za kigeni kwa mwaka 2005 ilikuwa inatosha kulipia bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi cha miezi 6.4.

9. Mheshimiwa Spika, tathmini inaonyesha kwamba utekelezaji wa Bajeti ya 2005/06 kwa miezi tisa ya mwanzo ya mwaka wa fedha umekuwa wa kuridhisha licha ya madhara ya ukame na kupanda kwa bei ya mafuta. Hata hivyo, upungufu wa chakula ulilazimu Serikali kufanya marekebisho ya ndani kwa ndani katika bajeti yake ili kununua na kusambaza chakula cha njaa kwa wananchi wa maeneo yaliyoathirika zaidi na uhaba huo, na pia kuiwezesha TANESCO kumudu gharama hasa kununua umeme wa IPTL na Songas. Hatua nyingine ni pamoja na Serikali kutoa msamaha wa kodi kwa nafaka kutoka nje ya nchi ili chakula kipatikane kwa wingi na kwa bei nafuu kwa walaji. Kwa pamoja, hatua hizi zilipunguza makali ya uhaba wa chakula, na kuokoa maisha ya wananchi wengi. Hatua hizi zilisaidia pia kuzuia mfumuko wa bei usipande sana.

10. Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2005/06, Serikali ililenga kukusanya mapato ya ndani yasiyopungua Shilingi trilioni 2 bilioni 66, milioni 751 (shilingi 2,066,751 milioni). Ili kuboresha ukusanyaji wa mapato, hatua kadhaa zilichukuliwa ambazo ni pamoja na kuimarisha utendaji na usimamizi katika Idara ya Forodha; kurekebisha Muundo wa Mamlaka ya Mapato ili kuboresha zaidi usimamizi wa vyanzo vya ndani vya mapato, kuimarisha Idara ya Walipakodi Wakubwa ili ihudumie walipakodi wengi zaidi; na kufanya marekebisho ya mfumo wa kodi katika maeneo kadhaa ili kurahisisha ukusanyaji na ufanisi wa usimamizi wa kodi. Hadi mwezi Machi, 2006 jumla ya Shilingi trilioni 1, bilioni 544, milioni 366 (Shilingi 1,544,366 milioni) zilikuwa zimekusanywa sawa na asilimia 100.5 ya lengo la kipindi hicho. Mwelekeo unaonyesha kwamba lengo la mapato kwa mwaka 2005/06 litafikiwa. Yafuatayo ni maelezo ya baadhi ya hatua zilizochukuliwa katika mwaka wa 2005/06 kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali:-






(i) Marekebisho ya Kodi ya Mapato: Serikali ilirekebisha viwango vya kodi ya mapato yatokanayo na ajira (PAYE) katika Sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004, kwa kuongeza kiwango cha chini cha mapato ya ajira yasiyotozwa kodi, kutoka Shilingi 60,000 kwa mwezi hadi Shilingi 80,000 kwa mwezi. Hatua hii ilitoa unafuu wa kodi kwa wafanyakazi wa kipato cha chini kwa kuwaondoa katika wigo wa kodi.
(ii) Marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa Sura Namba 147: Viwango vya Ushuru wa Bidhaa kwenye vinywaji baridi; bia; mvinyo kutoka nje ya nchi; vinywaji vikali, na sigara viliongezwa kwa asilimia 5 ili kwenda sambamba na mfumuko wa bei. Mapato yaliyokusanywa kutokana na kianzio hiki katika miezi tisa ya Julai 2005 hadi Machi 2006 yaliongezeka kwa asilimia 16.5.











(iii) Marekebisho ya Mfumo wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT): Serikali ilifanya marekebisho katika Sheria ya VAT Sura Namba 148 kwa nia ya kutoa unafuu kwa sekta ya usafirishaji na kuziba mianya ya ukwepaji kodi. Marekebisho hayo ni pamoja na kutoa msamaha wa VAT kwa vipuri vya treni na vifaa vingine vinavyotumika katika treni ili kupunguza gharama za usafirishaji na kusaidia Mashirika yetu ya reli, yaani TRC na TAZARA, kumudu gharama za matengenezo. Serikali pia ilitoa msamaha kwa magari maalum ya kutoa huduma za afya (Mobile Health clinics) ili kuvutia huduma hizo katika maeneo yasiyo na Vituo vya Afya au Zahanati. Hali kadhalika, Serikali ilitoa msamaha wa kodi kwa mafuta ya ndege ili kuziwezesha kampuni za ndege za hapa nchini kuhimili ushindani, kutokana na ongezeko kubwa la gharama za kuendesha ndege.

(iv) Marekebisho ya Ushuru wa Forodha: Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zilianza kutekeleza mfumo wa viwango vya ushuru wa Forodha wa pamoja mwezi Januari, 2005. Katika kipindi cha Julai 2005 hadi Machi 2006, mapato kutokana na Ushuru wa Forodha yalikuwa asilimia 52 zaidi ya mapato ya kipindi kama hicho mwaka wa fedha wa 2004/05. Huu ni uthibitisho kwamba, Tanzania ilifanikiwa kulinda mapato yake ipasavyo wakati wa majadiliano ya kuanzisha Itifaki ya Umoja wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

(v) Marekebisho ya Mfumo wa Leseni za Biashara: Hatua zilizotekelezwa katika eneo hili ni kufanya marekebisho ya viwango vya baadhi ya ada zinazotozwa na vyombo mbalimbali ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji. Hatua hizi ni pamoja na kufuta ada za leseni za usafirishaji zinazotozwa na mamlaka mbalimbali kwa magari yasiyochukua abiria (kama vile magari ya mizigo – madogo na makubwa).

11. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2005 hadi Machi, 2006, misaada na mikopo ya nje ya masharti nafuu ilifikia shilingi trilioni 1, bilioni 364, milioni 244 (shilingi 1,364,244 milioni) ikilinganishwa na makadirio ya shilingi trilioni 1, bilioni 443, milioni 580 (Shilingi 1,443,580 milioni) katika kipindi hicho. Kati ya hizo, misaada na mikopo inayopitia kwenye bajeti ya Serikali ilifikia jumla ya shilingi bilioni 575, milioni 956 (shilingi 575,956 milioni) ikilinganishwa na makisio ya shilingi 589,913 milioni (shilingi bilioni 589, milioni 913). Mikopo na misaada ya miradi ya maendeleo ilifikia shilingi 731,711 milioni (shilingi bilioni 731, milioni 711) ikilinganishwa na shilingi 783,467 milioni (shilingi bilioni 783, milioni 467) zilizotegemewa awali. Misaada na Mikopo ya nje haikufikia lengo katika kipindi hicho kutokana na sababu mbali mbali. Sababu kubwa ni, kwamba baadhi ya nchi wahisani zilikuwa na chaguzi ambazo zilibadilisha Serikali na hivyo kukawa na ucheleweshaji wa kutoa misaada iliyoahidiwa.

12. Mheshimiwa Spika, mapato kutokana na ubinafsishaji yalifikia shilingi milioni 33,309 (shilingi bilioni 33 milioni 309) ikilinganishwa na makisio ya Shilingi bilioni 5, milioni 210 (shilingi 5,210 milioni) kutokana na mauzo ya hisa za Serikali katika Benki ya NMB.


13. Mheshimiwa Spika, hadi mwisho wa Machi 2006, matumizi yote yalifikia shilingi trilioni 3, bilioni 180, milioni 542 (Shilingi. 3,180,542 milioni) karibu sawa na makisio ya Shilingi trilioni 3, bilioni 171, milioni 84 (Shilingi 3,171,084 milioni) katika kipindi hicho. Matumizi ya kawaida yalifikia Shilingi trilioni 2, bilioni 199, milioni 632 (Shilingi 2,199,632 milioni), na matumizi ya miradi ya maendeleo yalikuwa Shilingi bilioni 980, milioni 911 (shilingi 980, 911 milioni). Malipo ya madeni na pensheni yalitumia Shilingi bilioni 440, milioni 623 (shilingi 440,623 milioni) na mishahara ilitumia Shilingi bilioni 486, milioni 511 (shilingi 486,511 milioni). Malipo ya pensheni ni pamoja na madai ya wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo ilivunjika mwaka 1977. Uchambuzi bado unaendelea kwa wale wanaojitokeza na madai, hasa wale wa mirathi. Inatarajiwa kwamba zoezi hili litakamilika ifikapo mwisho wa Juni 2006. Kama watakuwepo wadai watakaosalia, malipo yao yataendelea kushughulikiwa katika mwaka wa fedha wa 2006/07.

14. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mwenendo wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali katika kipindi cha Julai 2005 hadi Machi 2006, Serikali inaamini kwamba lengo la mapato la mwaka wa 2005/06 litafikiwa bila shaka yoyote. Mapato ya ndani yanatarajiwa kufikia trilioni 2, bilioni 66, milioni 751 (Shilingi 2,066,751 milioni) sawa na asilimia 14.3 ya Pato la Taifa kwa mujibu wa takwimu za Pato la Taifa zilizokuwepo. Hata hivyo, kwa kuzingatia marekebisho ambayo yamefanywa hivi karibuni ya takwimu za Pato la Taifa zilizotolewa na Wakala wa Takwimu, uwiano huu unakua asilimia 13.6 badala ya 14.3. Malengo ya misaada na mikopo kutoka nje ikijumuisha misamaha ya madeni, pia yatafikiwa. Kwa upande wa matumizi, mwelekeo unaonyesha kwamba matumizi ya kawaida yatakuwa kama yalivyopangwa baada ya marekebisho kutokana na uhamisho wa ndani kukidhi mahitaji mbalimbali ya dharura yaliyotokana na sababu nilizoeleza awali. Aidha, matumizi ya maendeleo yanategemewa kuwa kama yalivyopangwa.


UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI:

15. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa 2005/06, Serikali imeendelea kuimarisha mazingira ya soko la fedha na la mitaji. Miswada ya Sheria mpya ya Benki Kuu ya mwaka 2006 na Sheria ya Mabenki na Asasi za Fedha ya mwaka 2006, iliwasilishwa Bungeni na kupitishwa mwezi Aprili 2006. Moja ya malengo muhimu ya sheria hizo ni kuipa Benki Kuu uwezo na uhuru zaidi wa kusimamia kikamilifu benki na asasi za fedha nchini ili kupanua huduma za sekta hiyo, hasa kuwezesha wananchi kupata mikopo ya masharti nafuu ili washiriki kikamilifu kujiondolea umaskini. Ikumbukwe kwamba sekta ya fedha imara ni nguzo muhimu ya uchumi imara, na inapaswa kutoa mchango wake katika kuwezesha wananchi kupata mikopo hasa ya uzalishaji. Marekebisho hayo ya Sheria ni sehemu ya utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mpango wa Uboreshaji wa Sekta ya Benki. Maeneo muhimu ya Mpango huo ni pamoja na:

Kuimarisha mazingira ya kisera na Sheria ili kuwezesha sekta ya benki kukua zaidi ili huduma ya benki iwafikie wananchi walio wengi;

Kuimarisha masoko ya fedha ili kuongeza ushindani na tija;

Kuboresha usimamizi wa Mifuko ya Mafao ya Uzeeni;

Kuimarisha sekta ndogo ya bima;

Kujenga mazingira ya upatikanaji wa huduma ya mikopo midogo midogo;

Kuwezesha ardhi kutumika kama dhamana kwa ajili ya mikopo; na

Kuwezesha upatikanaji wa mikopo ya muda wa kati na muda mrefu.

16. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kudhamini mikopo ya mabenki kwa wananchi kupitia Mfuko ya Dhamana ya Mikopo ya Mauzo ya Nje, na Mfuko wa Dhamana ya Mikopo kwa Biashara Ndogo Ndogo. Mifuko hii inaratibiwa na Benki Kuu. Aidha, Serikali iko katika hatua za mwisho za kuanzisha rasmi Mfuko wa Dhamana ya Mikopo ya Maendeleo. Serikali inakiri kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi ya kutoridhishwa na utendaji wa mifuko hiyo ya dhamana iliyokwishaanzishwa. Katika mwaka wa fedha 2006/07 mifuko hiyo itafanyiwa tathmini ya kina na marekebisho yanayotakiwa yatafanywa.

17. Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kutekeleza Mpango wa Kurasimisha Biashara na Mali za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), ili kuzipa uhai kisheria rasilimali mfu zinazomilikiwa na kutumiwa na wananchi wa kawaida katika shughuli zao za kujikimu. Mpango huu unatambua ukubwa wa sekta isiyo rasmi, thamani ya mtaji mfu katika sekta hiyo, taratibu zake za kiutendaji, na mchango mkubwa unaoweza kutolewa na sekta hii katika kukuza uchumi wa nchi. Mapendekezo ya jinsi ya kurasimisha sekta isiyo rasmi yanaandaliwa ili kutambua rasilimali za wananchi na kuwapa hati miliki zinazoweza kutumika, pamoja na mambo mengine, kama dhamana ya kukopa fedha kutoka benki kwa ajili ya kuboresha mitaji na maisha yao kwa ujumla.

18. Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa fedha, Serikali ilianza mchakato wa kuigeuza Benki ya Rasilimali (TIB) kuwa Benki ya Maendeleo ambayo itaratibu upatikanaji wa mikopo ya uwekezaji na uzalishaji kwa sekta zote zikiwemo sekta za kilimo na viwanda. TIB imeongezewa mtaji kwa hatua ya mwanzo, na sasa inajikita katika kuimarisha uwezo wa raslimali watu kabla ya kupanua shughuli zake. Aidha, Serikali inaboresha mazingira ya kuwezesha uanzishwaji wa vyombo vingine vya kuwapatia wananchi mitaji kwa ajili ya shughuli za uzalishaji kama nitakavyoeleza baadae katika Hotuba hii.

CHANGAMOTO ZILIZO MBELE YETU:

19. Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio mengi ya kiuchumi na kijamii, nchi yetu bado inakabiliwa na changamoto nyingi, zikiwemo zifuatazo:
Kwanza, Uwezo wa Serikali wa kutatua matatizo ya umaskini bado ni mdogo. Kwa hivyo, tunalo jukumu kubwa la kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuimarisha utawala wa kodi, kuiingiza sekta isiyo rasmi ndani ya wigo wa kodi, kuziba mianya ya ukwepaji wa kodi, kuimarisha masoko ya ndani ya kifedha ili kuwezesha wananchi kukopa na kupata mitaji ya kujiendeleza, na kuendelea kuboresha mazingira ya kuvutia uwekezaji, ambao ndio utapanua wigo wa kodi, na ajira.

Pili, Sehemu kubwa ya mapato yetu ya fedha za kigeni inatokana na misaada na mikopo ya masharti nafuu kutoka nje. Mauzo ya bidhaa na huduma za Tanzania nje ya nchi ni kidogo sana. Hatuna budi kuweka nguvu mpya katika kukuza mauzo ya nje. Kazi hii sharti ianze kwa kutambua na kuyafanyia kazi maeneo ambayo yanaweza kutupatia mafanikio kwa haraka na kutuongezea uwezo wa kiushindani katika soko la dunia.

Tatu, ni vyema tutumie misaada ya Wahisani kwa njia ambazo zinatusaidia kujenga uwezo wa nchi wa kujitegemea siku za usoni. Kwa sababu hiyo, maamuzi ya wapi misaada ielekezwe ni ya muhimu sana.
Nne, ingawa nidhamu ya matumizi ya fedha za Serikali imekuwa bora kuliko huko nyuma, bado uko udhaifu katika kusimamia fedha za Serikali, na hatua za kuondoa udhaifu huo zinachukuliwa.


UHUSIANO WETU NA WAHISANI:

20. Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa fedha, Serikali imeendelea kuboresha uhusiano wetu na nchi wahisani pamoja na mashirika ya fedha ya kimataifa chini ya Mikakati tuliyojiwekea. Tumeendelea kupata misaada na mikopo yenye masharti nafuu. Lengo kubwa la mikakati hii ni kuhakikisha kwamba Serikali ya Tanzania inamiliki agenda ya maendeleo ya nchi yetu badala ya wahisani, kuhakikisha misaada ya nje inapatikana na inaendelea kuongezeka, na kwamba fedha nyingi zaidi zinapitia kwenye mfumo wa bajeti ya Serikali.

21. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2005/06, Tanzania imeanza kunufaika na mpango wa kuzifutia kabisa nchi masikini duniani madeni ya Taasisi za Fedha za Kimataifa kufuatia kundi la nchi nane tajiri duniani (G8) kukubali kufutwa kwa madeni ya nchi 22 masikini ikiwemo Tanzania. Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) tayari limeifutia Tanzania deni lake kwa Shirika hilo lenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 336. Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) pia zimetangaza kwamba zitaifutia Tanzania madeni yake kwa Mashirika hayo. Kiasi kitakachofutwa kitafahamika kwa uhakika kabla ya Julai, 2006. Aidha, Serikali ya Marekani kupitia Shirika lake la Millennium Challenge Corporation (MCC) imeiingiza Tanzania katika kundi la nchi zitakazofaidika na msaada wa ”Millennium Challenge Account” na tayari tumefaulu katika awamu ya kwanza ya “Threshhold” na sasa tunatayarisha mpango wa awamu ya pili (Compact Programme).

22. Mheshimiwa Spika, Serikali iko katika hatua za mwisho za utekelezaji wa Mpango wa PRGF unaodhaminiwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ambao utamaliza muda wake mwezi Desemba, 2006. Uhusiano kati ya Tanzania na IMF umekuwa mzuri katika miaka kumi iliyopita. Uhusiano huo umekuwa kichocheo muhimu katika kuvutia wawekezaji, kupata misamaha ya madeni, na ongezeko kubwa la misaada ya wahisani ikiwemo Benki ya Dunia, na kupanda kwa akiba ya fedha za kigeni. Hivi karibuni, IMF imeanzisha mpango mpya wa ushirikiano na nchi maskini ambazo zimeonyesha kuwa na uwezo wa kupanga na kusimamia chumi zao pasipo kuhitaji mikopo kutoka katika Shirika hilo. Serikali imeanza mchakato wa kujiunga na mpango huo ujulikanao kama “Policy Support Instrument” (PSI) mara baada ya mpango wa sasa kufikia ukomo mwezi Desemba 2006. Kujiunga na mpango huu kutaleta manufaa ambayo ni pamoja na:-

Kuvutia uwekezaji;

Gharama ndogo za usimamizi kwa kuwa kutakuwa na tathmini mbili tu kwa mwaka ikilinganishwa na ziara nyingi za maafisa wa IMF chini ya mpango wa PRGF;

IMF haitatoa mikopo tena kwa Tanzania, isipokuwa kama kuna dharura, hivyo tutapunguza utegemezi kwa Shirika hilo.

MISINGI NA SHABAHA YA BAJETI ZA MWAKA 2006/07:

23. Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza hapo awali, bajeti ya mwaka 2006/07 ni ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Nne, kufuatia Uchaguzi wa Rais na Wabunge uliofanyika mwezi Desemba 2005. Bajeti ya mwaka 2006/07 imelenga kuanza kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005. Aidha, bajeti hii inaendeleza utekelezaji wa MKUKUTA ili kufikia malengo ya Milenia na hatimaye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Kama alivyoeleza leo asubuhi Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Malengo ya uchumi mpana ni pamoja na:-


(i) Pato halisi la Taifa litakua kwa asilimia 5.9 mwaka 2006, asilimia 7.3 mwaka 2007, na asilimia 7.7 mwaka 2008.

(ii) Kasi ya upandaji wa bei haitazidi asilimia 4.0 (kwa bei za mwaka 2001) ifikapo Juni 2007.

(iii) Ukusanyaji wa mapato ya ndani sawa na asilimia 14.5 ya Pato la Taifa mwaka 2006/07, asilimia 14.7 mwaka 2007/08 na asilimia 14.8 mwaka 2008/09.

Ongezeko la ujazi wa fedha (kwa tafsiri pana, M2) litawiana na ukuaji wa uchumi, na kasi ya mfumuko wa bei.

ILANI YA UCHAGUZI YA CCM YA 2005:


24. Mheshimiwa Spika, bajeti hii inaanza kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005. Baadhi ya mambo yaliyoko kwenye Ilani ya Uchaguzi yanayozingatiwa katika bajeti hii, ni pamoja na haya yafuatayo:-

Bajeti ya 2006/07 inachochea ongezeko la kasi ya kukua kwa uchumi;

Ruzuku ya mbolea, mbegu, na pembejeo za kilimo na mifugo, pamoja na miundombinu ya umwagiliaji imeongezwa katika bajeti hii;

Bajeti imetenga fedha za kuanzisha maeneo maalum ya uwekezaji na uzalishaji wa bidhaa za kuuza nchi za nje (SEZ na EPZ);

Fedha zimetengwa kwa ajili ya zoezi la kutambua mipaka ya vijiji, Hati za kumiliki ardhi, ili matumizi ya ardhi yawe endelevu nchini kote;

Zimetengwa fedha pia kwa ajili ya upimaji wa maeneo ya wafugaji ili kudhibiti uharibifu wa mazingira;

Serikali itaendeleza dhana ya kuunda mifuko ya udhamini wa mikopo, na kuboresha uendeshaji wa mifuko ambayo tayari ipo;
Ziko hatua nyingine nyingi katika marekebisho ya kodi ambazo nitazielezea baadae katika Hotuba hii.

MKUKUTA:

25. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi unakwenda sambamba na utekelezaji wa MKUKUTA, Dira ya Maendeleo hadi 2025 na Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs). Kuanzia katika bajeti ya mwaka 2005/06, fedha kwa ajili ya utekelezaji wa MKUKUTA ziligawanywa kwa kuzingatia maeneo makuu matatu ya kimatokeo (Outcome Clusters). Mwaka 2005/06, asilimia 39 ya matumizi yote ya kutekeleza MKUKUTA zilielekezwa kukuza uchumi na kupunguza umaskini wa kipato; asilimia 43 kwa ajili ya kuboresha maisha ya watu na ustawi wa jamii; na asilimia 18 iliyobaki ilitumika kuimarisha utawala bora na uwajibikaji. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2006/07, maeneo yote makuu yameongezewa fedha, ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa MKUKUTA. Aidha, bajeti hii pia inazingatia umuhimu wa kuongeza rasilimali kwa ajili ya kukuza uchumi, kama msingi wa mkakati endelevu wa kuondoa umaskini. Kwa hivyo, asilimia 45.8 ya fedha za kutekeleza MKUKUTA zitatumika kwa ajili ya kukuza uchumi. Maeneo yanayohusika ni pamoja na miundombinu, kama kuendeleza na kukamilisha miradi ya barabara na kukamilisha mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda katika miji ya Shinyanga na Kahama, fedha kwa ajili ya kuongeza uwezo wa TANESCO kuzalisha Megawati takribani 145 zaidi za umeme ili kukabiliana na upungufu wa nishati hiyo kila panapotokea ukame. Kwa ujumla, bajeti hii imetenga asilimia 26 ya mapato ya ndani kwa ajili ya matumizi ya maendeleo, ikilinganishwa na asilimia 18 zilizotengwa mwaka 2005/06. Lengo ni kujenga mtandao mzuri wa miundombinu, ili kupunguza gharama za uzalishaji nchini, na hivyo kuvutia uwekezaji zaidi kutoka ndani na nje. Tukifanikiwa katika hilo, tutaweza kuanza kusindika sehemu kubwa zaidi ya mazao yetu. Aidha, hatua za kuboresha huduma za jamii, kuboresha maisha na ustawi wa kila Mtanzania, zimetengewa asilimia 35.8 za fedha za kutekeleza MKUKUTA. Asilimia 18.4 iliyobaki imetengwa kuimarisha utawala bora.

UWEZESHAJI:

26. Mheshimiwa Spika, uwezeshaji wa wananchi ni sehemu muhimu ya mpango wa kuhakikisha maisha bora kwa kila Mtanzania, kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2005. Ili kufanikisha azma hii, bajeti ya 2006/07 imezingatia mambo yafuatayo:-

Kwanza, mifuko iliyoko ya dhamana za mikopo itaimarishwa ili wananchi wengi zaidi waweze kuitumia kujiletea maendeleo.

Pili, taratibu za kuanzisha Mfuko wa Dhamana kwa Mikopo ya Maendeleo zitakamilishwa ili mfuko huo uanze kutoa dhamana ndani ya mwaka wa 2006/07.

Tatu, Serikali inaandaa taratibu ambazo zitawezesha uanzishwaji wa SACCOS za makundi mbalimbali ya jamii, ambayo yatawezeshwa kupata mikopo kutoka benki za kibiashara mikoani, nchini kote.

Nne, hatua za dhati zitachukuliwa kuongeza wigo wa kuzalisha umeme nchini na kuboresha mtandao wa usambazaji wa umeme.

Tano, fedha zimetengwa kwa ajili ya maandalizi ya kutengeneza vitambulisho vya Uraia ili kuwawezesha Watanzania kudhibiti maliasili yao.
Sita, kuendeleza juhudu za kuiwezesha TIB kutoa mikopo ya uzalishaji kwa sekta za uchumi, zikiwemo sekta za viwanda, kilimo na utalii. Hatua ya kwanza ya kuipatia benki hiyo mtaji ni kutumia fedha za Serikali zilizokuwa zinasimamiwa na benki hiyo, zisizopungua shilingi 17 bilioni. Kwa mujibu wa mizania ya vitabu vya hesabu za TIB, benki hiyo ina mtaji wa shilingi bilioni 7.4, unaotokana na faida ambayo benki imekuwa inapata katika miaka ya hivi karibuni. Ukiongeza shilingi bilioni 17.5 za Serikali ambazo TIB imeruhusiwa kuziingiza kwenye mtaji, benki hiyo sasa ina mtaji wa shilingi bilioni 24.9. Hata hivyo, ili benki hii iweze kuanza shughuli za “Benki ya Maendeleo” mtaji wake hauna budi uongezwe ufikie angalau shilingi bilioni 50 kwa kuanzia.

Saba, suala la mikopo ya nyumba (mortage finance), mikopo ya mali ya kukodi (lease finance), mikopo midogo midogo (micro-finance) nalo litapewa kipaumbele katika utekelezaji wa bajeti ya 2006/07. Serikali imekubaliana na Wakuu wa benki zote zilizoko hapa nchini, kuunda Kamati Maalum ya kutafuta muafaka wa majawabu ya malalamiko kuhusu ukosefu wa mikopo, riba kubwa za mikopo, na ndogo kwa amana, huduma za benki kujikita kwenye miji mikubwa tu, benki nyingi kupendelea wateja wakubwa, benki kupendelea kununua dhamana za Serikali badala ya kukopesha, na mengine mengi. Kamati hiyo itaundwa ndani ya mwezi mmoja na itatoa mapendekezo yake kwa Serikali mwezi Oktoba, 2006.

27. Mheshimiwa Spika, hatua nyingine za uwezeshaji nitazielezea chini ya marekebisho ya Mfumo wa Kodi na ada mbalimbali.

MAZINGIRA:

28. Mheshimiwa Spika, miezi michache iliyopita, Serikali ilitangaza hatua mbalimbali za kulinda mazingira ili kuweka msingi endelevu wa shughuli zetu za maendeleo. Hatua hizo ni pamoja na kupiga marufuku usafirishaji wa magogo ili kulinda misitu na vyanzo vya maji, kuondoa mifugo katika maeneo ya vyanzo vya mito, na pia kupiga marufuku utengenezaji na uingizaji nchini wa mifuko myembamba ya plastiki. Bajeti ya 2006/07 imetenga shilingi 9.4 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa Mkakati wa Kutunza Mazingira.

29. Mheshimiwa Spika, ziko hatua nyingine kadhaa za kulinda mazingira ambazo nitazitangaza baadae kidogo.

MASLAHI YA WAFANYAKAZI:

30. Mheshimiwa Spika, azma ya kuboresha maslahi ya wafanyakazi wa Serikali imezingatiwa katika MKUKUTA na pia katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Kwa hiyo, bajeti ya mwaka ujao wa fedha imetenga shilingi trilioni 1, milioni 4 kwa ajili ya mishahara, ikilinganishwa na shilingi bilioni 682 zilizotengwa mwaka 2005/06 – ongezeko la shilingi 318 bilioni. Fedha hizo ni kwa ajili ya nyongeza ya mishahara pamoja na ajira mpya ya walimu, watumishi wa afya, wahasibu, wakaguzi wa ndani, na wengine. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Utumishi, ataelezea kwa mapana zaidi matumizi ya fedha hizo, wakati atakapowasilisha bajeti yake.

MAPATO YA NDANI:

31. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2006/07, Serikali inalenga kukusanya mapato ya ndani yasiyopungua Shilingi trilioni 2 bilioni 460, milioni 995 (shilingi 2,460,995 milioni) sawa na asilimia 14.5 ya Pato la Taifa, ikilinganishwa na mapato ya shilingi trilioni 2, bilioni 66, milioni 752 (shilingi 2,066,752 milioni) mwaka 2005/06 – ongezeko la asilimia 19.1. Ili kuendelea kuboresha ukusanyaji, hatua zifuatazo zitatekelezwa:

Kuendelea kupanua wigo wa kodi, kwa kusajili walipakodi wapya na kuimarisha uchumi tulivu, pamoja na kuweka mazingira bora ya biashara kuwezesha sekta binafsi kukua.

Kusimamia kwa karibu mageuzi makubwa yanayoendelea ndani ya Mamlaka ya Mapato (TRA) chini ya Mpango wake wa Pili wa Maboresho wa Miaka Mitano, ambao umekuwa msingi wa kukua kwa mapato ya ndani mwaka hadi mwaka.

Kuendelea kurekebisha mfumo wa kodi na kuimarisha Idara ya Walipakodi Wakubwa kwa kuboresha utendaji.

Kuweka nguvu zaidi katika kuboresha usimamizi na utendaji wa Forodha kwa kuongeza uwajibikaji, matumizi ya teknolojia, na kupunguza mlolongo wa taratibu ndefu ambazo ni kero kwa walipa kodi.

Kupitia upya msingi na taratibu za misamaha ya kodi kwa lengo la kuziba mianya ya kukwepa kodi.
Kufanya tathmini ya makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi kwa lengo la kubaini mapungufu yaliyopo na kufanya marekebisho ili kuongeza ufanisi wa kukusanya mapato hayo.


MISAADA NA MIKOPO YA NJE:

32. Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza awali, utekelezaji wa Mkakati wa Pamoja wa Kusimamia Misaada (Joint Assistance Strategy) na ule wa madeni (National Debt Strategy), utaendelea kuisaidia Serikali kuboresha uhusiano wetu na nchi wahisani pamoja na mashirika ya fedha ya kimataifa ili tuendelee kupata misaada na mikopo yenye masharti nafuu kugharamia mipango yetu ya maendeleo. Misaada na mikopo kutoka nje itachangia takribani asilimia 39 ya bajeti ya 2006/07 ukiondoa misamaha ya madeni ya Mashirika ya Fedha ya Kanda na Kimataifa.


MATUMIZI:


33. Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema awali, bajeti hii inadhamiria kuanza utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005 kwa kuzingatia vipaumbele katika maeneo yaliyoainishwa katika Ilani hiyo na katika MKUKUTA. Aidha, Serikali itaendelea kuongeza ujuzi wa watumishi wake, kuimarisha nidhamu katika matumizi ya fedha za umma na kuhakikisha uwajibikaji katika ngazi zote za Serikali, zikiwamo Halmashauri za Serikali za Mitaa. Mtandao wa IFMS ambao umeonyesha mafanikio makubwa katika udhibiti wa matumizi ya Serikali utasambazwa katika Halmashauri nyingi zaidi ili usaidie katika kuweka uwazi na uwajibikaji. Mtandao wa IFMS ni teknolojia ya mawasiliano inayozuia mtumishi kutumia fedha ambazo hakuruhusiwa, yaani ambazo hazikukasimiwa. Ni vyema Halmashauri, kupitia sheria ndogo ndogo, zikajipanga vizuri kusimamia fedha zinazopelekwa huko ili zitumike kama inavyokusudiwa. Waheshimiwa Wabunge mnayo nafasi ya kusaidia kusukuma jambo hili, hasa kwa kuwa ninyi pia ni Madiwani katika Halmashauri zenu.

34. Mheshimiwa Spika, napenda kusisitiza umuhimu wa kuchuja watumishi ili wale ambao sio waadilifu, na wanaofuja fedha za Serikali wachukuliwe hatua za kisheria. Halmashauri zinahimizwa kutoa taarifa za mapato na matumizi kila mwezi. Aidha, wananchi wanakumbushwa kuzingatia wajibu wao wa kuhoji matumizi ya Halmashauri zao kwa kufuatilia taarifa za mgao wa fedha kwa Halmashauri hizo. Kwa upande wake, Serikali Kuu itajitahidi kutoa msaada wa kila aina kuziwezesha Halmashauri kujenga uwezo wa utendaji na utaalam hasa katika fani ya uhasibu na ukaguzi wa ndani. Hivi sasa, Serikali ipo kwenye zoezi la kuajiri wahasibu na wakaguzi wa ndani kwa ajili ya Halmashauri ambao wanategemewa kuanza kazi mwezi Julai mwaka huu 2006. Aidha, Wizara ya Fedha imeunda kitengo maalum cha kufuatilia kwa karibu matumizi ya fedha katika Halmashauri.

35. Mheshimiwa Spika, katika kupanga mgao wa fedha za bajeti kwa mwaka wa fedha 2006/07, mambo yafuatayo yamezingatiwa:-


Shilingi bilioni 641, milioni 766 (shilinigi 641,766 milioni), sawa na asilimia 26 ya mapato yatokanayo na vianzo vya ndani, zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Kati ya hizo, shilingi bilioni 219, milioni 240, (Shilingi 219,240 milioni) zimetengwa kwa ajili ya miradi maalum ya kuzalisha umeme wa gesi katika vituo vya Ubungo na Kinyerezi, na ukarabati wa miundombinu ya kusambazia umeme.


Sekta ya kilimo pia imepewa kipaumbele kwa kiwango cha kuridhisha katika bajeti ya 2006/07 kwa kutambua kwamba ni sekta yenye uwezo mkubwa wa kukuza uchumi na kuongeza ajira. Bajeti ya maendeleo ya kilimo imesambaa katika Wizara nyingi – Kilimo, Chakula na Ushirika, Mifugo , TAMISEMI, Halmashauri za Wilaya, Miundombinu, na nyingine.

Bajeti ya 2006/07 imetenga Shilingi bilioni 21 milioni 196 (shilingi 21,196 milioni) ambazo ni mgao wa asilimia 4.5 ya misaada ya nje kwa ajili ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ). Utaratibu wa sasa wa kugawa misaada na mapato mengine utaendelea kutumika hadi hapo utaratibu mwingine utakapopendekezwa na Tume ya Pamoja ya Fedha na kuridhiwa na Serikali zetu mbili.

Bajeti inaendelea kutenga kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya huduma za jamii – (elimu, afya, maji n.k).

Bajeti hii imezingatia mahitaji ya msingi ya sekta za ulinzi na usalama wa raia, pamoja na ufufuaji wa makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa.

Bajeti ya 2006/07 imetenga fedha kwa ajili ya mikoa ya pembezoni; na ununuzi wa magari kwa Wilaya zenye mahitaji zaidi, hasa Wilaya mpya.

Mahitaji ya miradi maalum yamezingatiwa katika bajeti ya 2006/07:- Kwa mfano Mradi wa Maeneo Maalum ya Kiuchumi (Special Economic Zones); Mradi wa Maji Ziwa Victoria hadi Miji ya Shinyanga na Kahama; ujenzi wa barabara, na Ununuzi wa mitambo ya kuzalisha umeme.

MAREKEBISHO YA MFUMO WA KODI, ADA MBALIMBALI NA HATUA NYINGINE ZA MAPATO:

36. Mheshimiwa Spika, Serikali inapendekeza kuchukua hatua mpya za kurekebisha mfumo wa ukusanyaji wa mapato kwa lengo la kuboresha mfumo wa kodi, kuziba mianya ya uvujaji wa mapato ya Serikali, kuongeza mapato ya Serikali, kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kuweka mazingira mazuri ya uwezeshaji wa wananchi kujiletea maendeleo yao.

Hatua zinazopendekezwa zinahusu kurekebisha sheria za kodi zifuatazo:-

Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura Namba 148.
Sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004.
Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura Namba 147.
Sheria ya Ushuru wa Barabara, Sura Namba 220.
Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004.
Sheria ya Uwekezaji Tanzania, Sura Namba 38.
Sheria ya Madini, Sura Namba 123.
Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura Namba 290.
Kodi na Usimamizi wa Mafuta ya Petroli, na
Usimamizi wa Kodi ya Michezo ya Kubahatisha.

Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani:-

37. Mheshimiwa Spika, inapendekezwa kufanya marekebisho yafuatayo katika Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani:-

Kufafanua bayana katika Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kwamba ada ya kukodi ndege (aircraft leasing fees) inayolipwa na Kampuni ya Ndege iliyosajiliwa hapa nchini haitozwi kodi ya Ongezeko la Thamani, sawa na ilivyo kwa gharama ya kununua ndege. Kodi hii iliondolewa ili kupunguza gharama za uendeshaji wa kampuni za ndege nchini na hivyo kuyaongezea uwezo wa ushindani;


Kupunguza ukomo wa muda wa kuomba marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kutoka miaka mitano hadi mitatu ili kuondoa mianya ya kukwepa kodi;

Kuongeza kiwango cha adhabu kwa kosa la kutotoa stakabadhi kutoka Shilingi 200,000/= za sasa hadi Shilingi 500,000/=;

Kurekebisha kiwango cha adhabu kwa kosa la kukwepa kodi kwa njia ya udanganyifu, kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 2,000,000/= tu ili kiwe kiwango kisichopungua shilingi 2,000,000/= au mara mbili ya kodi iliyokwepwa kutegemea kipi ni kikubwa, au kifungo cha miaka miwili, au faini na kifungo kwa pamoja;

Kurekebisha kiwango cha adhabu kwa kosa la kushindwa kulipa kodi au kushindwa kuwasilisha fomu za marejesho ya kodi kwa wakati unaotakiwa kutoka Shilingi 200,000/= hadi shilingi 500,000/= au kiasi cha mara mbili ya kodi husika kutegemea kipi ni kikubwa.


B. Sheria ya Kodi ya Mapato:-


38. Mheshimiwa Spika, inapendekezwa kufanya marekebisho yafuatayo katika Sheria ya Kodi ya Mapato:-

Kupunguza kodi ya mapato, kwa makampuni mapya yatakayojisajili katika Soko la Mitaji la Dar es Salaam (DSE) na kuuza angalau asilimia 35 ya hisa zao kwa wananchi ili kiwango cha kodi kiwe asilimia 25 badala ya asilimia 30 ya mapato. Punguzo hili litakuwa kwa muda wa miaka mitatu. Lengo ni kushawishi makampuni mengi ya binafsi kujiunga na Soko la Mitaji na kuongeza umiliki wa wananchi katika makampuni ya Tanzania;

Kutoa unafuu wa kodi ya mapato kwa watu binafsi wanaochangia Mfuko wa Elimu kama ilivyo hivi sasa kwa biashara. Wachangiaji watatakiwa kujaza fomu za marejesho ili kudai nafuu hii ya kodi;

Kubadilisha utaratibu wa kutoza kodi ya mapato ya hitimisho la ajira -terminal benefits (isipokuwa pensheni ambayo haitozwi kodi), ili mapato aliyolipwa mstaafu katika kipindi cha miaka sita ya mwisho au kipindi halisi cha ajira, ndio yatumike kukokotoa kodi badala ya utaratibu wa sasa wa kutoza kodi mapato hayo kwa mkupuo kama mapato ya mwaka mmoja. Hatua hii itapunguza sana mzigo wa kodi kwa wafanyakazi wanapostaafu; na

Kupunguza kiwango cha kodi ya zuio, kwa mapato ya riba ya Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja (Collective Investment Schemes), kutoka asilimia 30 hadi asilimia 10 kama ilivyo kwa watu binafsi, ili kuhamasisha uwekezaji wa pamoja nchini.
Sheria ya Ushuru wa Bidhaa:-

39. Mheshimiwa Spika, inapendekezwa kufanya marekebisho yafuatayo katika Sheria ya Ushuru wa Bidhaa.


Kupunguza kiwango cha Ushuru wa Bidhaa kwenye mafuta ya taa, kutoka Shilingi 122 kwa lita hadi Shilingi 52 kwa lita ili kuhamasisha wananchi kutumia mafuta ya taa badala ya mkaa na kuni kwa matumizi ya nyumbani na hivyo kulinda mazingira. Hatua hii ya kupunguza kodi kwenye mafuta ya taa inaweza kuongeza tatizo la ukwepaji wa kodi kwa kuchanganya mafuta ya taa na mafuta mengine ya petroli (Fuel Adulteration). Kwa hivyo tutahitaji kuimarisha udhibiti katika biashara ya mafuta ya petroli;

Kuongeza viwango vya Ushuru wa Bidhaa kwenye bidhaa mbalimbali zisizo za petroli kwa asilimia 7, sawa na kiwango cha sasa cha mfumuko wa bei. Lengo ni kulinda thamani halisi ya mapato ya Serikali kutoka kwenye vyanzo hivi. Viwango vya sasa na vinavyopendekezwa ni kama ifuatavyo:-

(a) Vinywaji baridi kutoka shilingi 41.50 kwa lita hadi shilingi 45 kwa lita,

(b) Bia inayotengenezwa kwa nafaka ambayo haijaoteshwa; kutoka shilingi 150 kwa lita hadi shilingi 161 kwa lita,

(c) Bia nyingine zote, kutoka shilingi 256 kwa lita hadi shilingi 274 kwa lita,

(d) Mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25, kutoka shilingi 820 kwa lita hadi shilingi 878 kwa lita,

(e) Vinywaji vikali kutoka shilingi 1,216 kwa lita hadi shilingi 1,302 kwa lita, na

(f) Kurekebisha viwango vya ushuru wa bidhaa kwenye sigara kama ifuatavyo:

Sigara zisizo na kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka shilingi 4,170 hadi shilingi 4,462 kwa sigara elfu moja,

Sigara zenye kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka shilingi 9,840 hadi shilingi 10,529 kwa sigara elfu moja,

Sigara nyingine zenye sifa tofauti na (a) na (b) kutoka shilingi 17,870 hadi shilingi 19,195 kwa sigara elfu moja,

Tumbaku ambayo iko tayari kutengeneza sigara (“cut filler’) kutoka Shilingi 9,025 hadi shilingi 9,657 kwa kilo; na

(iii) Kuongeza kiwango cha Ushuru wa Bidhaa kwenye huduma za mawasiliano ya simu za mkononi (mobile phone airtime) kutoka asilimia 5 hadi asilimia 7 ya mauzo ili kikaribiane na kiwango cha asilimia 10 kinachotozwa Uganda na Kenya – Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki;

(iv) Kurekebisha Sheria ya Ushuru wa Bidhaa ili bidhaa zinazouzwa nje ya nchi ziandikwe “Kwa Kuuzwa Nje tu” au “FOR EXPORT ONLY” ili kuzuia bidhaa hizo kuuzwa hapa nchini bila kulipiwa kodi;


(v) Kuongeza kiwango cha Ushuru wa Bidhaa kwa mifuko ya “plastic” inayoruhusiwa kutoka asilimia 15 hadi asilimia 120 ili kupunguza uchafuzi wa mazingira; na

(vi) Kuweka Ushuru wa Bidhaa kwa kiwango cha asilimia 20 kwa magari madogo chakavu yenye umri wa miaka 10 au zaidi.

Sheria ya Ushuru wa Barabara:-

40. Mheshimiwa Spika, ili kulinda mapato ya Mfuko wa Barabara kwa kuzingatia ongezeko la gharama za matengenezo, inapendekezwa kuongeza Ushuru wa Barabara kutoka Shilingi 90/- kwa lita hadi Shilingi 100/= kwa lita, na kuweka kifungu katika Sheria kinachoruhusu marekebisho ya kiwango hiki kila mwaka kulingana na kiwango cha mfumuko wa bei.

Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki:-

41. Mheshimiwa Spika, kikao cha pamoja cha Mawaziri wa Fedha wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, kilichofanyika tarehe 8 Juni 2006 mjini Arusha kilipendekeza marekebisho ya viwango vya Ushuru wa Forodha kwa mwaka 2006/07 kama ifuatavyo;

Kurudisha ushuru wa asilimia kumi (10%) kwenye mafuta ghafi ya kupikia (Crude Palm Oil) kwa lengo la kuwalinda wazalishaji wa mbegu za mafuta hapa Afrika Mashariki, na kuziba mianya ya kukwepa kodi.

Kupunguza kiwango cha ushuru unaotozwa kwa malighafi ya kutengeneza sabuni (RBD Palm Stearin) kutoka asilimia ishirini na tano (25%) hadi asilimia kumi (10%). Lengo ni kuwawezesha wazalishaji wadogo wa sabuni kumudu ushindani usio wa haki kutoka nje.

Kufuta Ushuru kwenye mitungi ya gesi (LPG Cylinders) ili kuhamasisha matumizi ya gesi kwa nia ya kulinda mazingira.

Kupunguza ushuru kwenye karatasi zinazoagizwa kutoka nje kwa matumizi mbalimbali kama vile kuandikia na kuchapisha makala za magazeti, kutoka asilimia ishirini na tano (25%) hadi asilimia kumi (10%). Hatua hii inategemewa kupunguza gharama za uzalishaji viwandani na uchapishaji wa makala mbalimbali kama magazeti n.k.

Kutoa msamaha wa Ushuru kwa vifaa vinavyotumia mionzi ya jua kuzalisha umeme. Hatua hii itahamasisha wananchi kutumia nishati hii mbadala na kuhifadhi mazingira.

Kuongeza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia thelathini na tano (35%) hadi asilimia hamsini (50%) kwa viberiti vinavyoagizwa kutoka nje ya Afrika Mashariki. Lengo ni kulinda kiwanda chetu cha viberiti kutokana na ushindani usio wa haki.

Kuondoa ushuru unaotozwa kwenye “globu” zinazohifadhi umeme. Hatua hii inategemewa kupunguza matumizi ya nishati ya umeme na gharama za umeme.

Kupunguza Ushuru viunganisho (unassembled completely knocked down) vya baiskeli na pikipiki kwa waunganishaji wanaotambuliwa na mamlaka husika kuwa asilimia kumi (10%) kwa pikipiki na asilimia sifuri (0%) kwa baiskeli. Hata hivyo, pikipiki na baiskeli ambazo huagizwa kutoka nje zikiwa zimekwisha unganishwa zitaendelea kutozwa ushuru wa asilimia ishirini na tano (25%) kwa pikipiki na asilimia kumi (10%) kwa baiskeli.

Kuingiza kwenye jedwali la tano la Sheria ya Ushuru wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kutoa msamaha kwa vifaa na madawa yanayotumika kwenye maabara kufanya uchunguzi wa magonjwa.

Kuongeza Ushuru wa mazulia ya sakafuni (floor carpets) hadi asilimia ishirini na tano (25%) kwa kuwa hii ni bidhaa inayotengenezwa kwa kiwango cha kutosha katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kupunguza Ushuru kutoka asilimia kumi (10%) hadi sifuri (0%) kwenye malighafi zinazotumika kuzalisha karatasi zinazotambulika katika HS Code 2507.00.00, HS Code 2526.10.00, HS Code 2526.20.00.

Kupunguza Ushuru kwenye jamii ya mkaa wa mawe (HS Code 2704.00.00) kutoka asilimia kumi (10%) hadi sifuri (0%) ili kuendana na kiwango cha ushuru wa mkaa.

Kupunguza ushuru kwenye malighafi itumikayo kutengeneza bidhaa mbalimbali kama vile dawa ya mswaki (HS Code 3402.13.00) kutoka asilimia ishirini na tano (25%) hadi asilimia kumi (10%).

Kupunguza ushuru kwenye malighafi zinazotumika kutengeneza vipuri vya magari (Oil/Air/Fuel Filters – HS Code 4805.40.00) kutoka asilimia kumi (10%) kwenda sifuri (0%).

Kufuta Ushuru wa Malighafi inayotumika kutengeneza nyaya za kuchomelea (welding electrodes) HS Codes 7223.00.00, HS Code 7505.11.00, 7505.12.00.

Kutenganisha bidhaa za kioo (HS Code 7019.90.00) ili kufuta ushuru wa forodha kwenye nyuzi za kioo zinazotumika kutengeneza vifaa vya kusagia na kukata (HS Code 7019.90.10)

Kutenganisha karatasi za aluminia (HS Code 7607.19.00, 7607.20.00) ili kutofautisha kati ya zile zilizochapishwa na zisizochapishwa. Lengo ni kuongeza ushuru kwa zile zilizochapishwa kutoka asilimia kumi (10%) hadi asilimia ishirini na tano (25%).
Marekebisho haya ya Ushuru wa Forodha yatatangazwa rasmi kwenye Gazeti la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

42. Mheshimiwa Spika, inapendekezwa kutoza kodi sukari inayoingizwa nchini kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya SADC kwa viwango vinavyotozwa bidhaa hiyo kutoka nje ya Afrika Mashariki chini ya Itifaki ya Umoja wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Katika Jumuiya ya SADC, biashara ya sukari haipo kwenye utaratibu wa kawaida wa kupunguziana ushuru bali imewekewa utaratibu wa pekee ambapo baadhi ya nchi zimepewa viwango maalum (quotas) vya kuuza Sukari katika soko la Afrika Kusini. Katika utaratibu huo, Tanzania haikupewa kiwango maalum (quota) kwa vile haijitoshelezi mahitaji yake ya ndani. Aidha, kuruhusu sukari kuingia nchini kwa kiwango kidogo sana cha kodi (asilimia 25) kunaweza kudumaza jitihada za uzalishaji wa ndani zenye lengo la kujitosheleza kwa bidhaa hiyo.

Sheria ya Uwekezaji Tanzania:-

43. Mheshimiwa Spika, inapendekezwa kufanya marekebisho katika Sheria ya Uwekezaji ili:

Kifungu Na. 19(2) cha Sheria hiyo kinachoikataza Serikali kubadili mfumo wa kodi kwa wawekezaji kitumike kwa Wawekezaji Mahiri tu kama waliowekeza kwenye kilimo, miradi mikubwa ya kuzalisha kwa ajili ya kuuza nje, miundombinu, na mingine ya namna hiyo;

Kuondoa msamaha wa kodi unaotolewa sasa kwa magari madogo ya binafsi (non utility vehicles) kwa wawekezaji. Msamaha uendelee kuweko kwa magari ya kazi (utility vehicles).
Sheria ya Madini:-

44. Mheshimiwa Spika, inapendekezwa kutoa msamaha wa mrahaba kwa wazalishaji wa chumvi wanaotumia rasilimali zinazojirejesha (renewable resources) ili kusaidia kampeni ya kupambana na magonjwa yanayotokana na ukosefu wa madini joto mwilini.

Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa:-


45. Mheshimiwa Spika, inapendekezwa kufuta ada ya magari yanayotumia barabara za miji (city plying fees) inayotozwa chini ya Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa ili kuondoa kero na kuboresha mazingira ya biashara.

Kodi na Usimamizi wa Mafuta ya Petroli:-

46. Mheshimiwa Spika, inapendekezwa kufanya marekebisho yafuatayo katika eneo hili:

Kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye bei ya mafuta ya petroli ili kupunguza mzigo wa ongezeko la bei za mafuta hayo, lakini bila kuathiri mapato ya Serikali.

Kurekebisha viwango vya ushuru wa bidhaa kwa mafuta ya petrol kama ifuatavyo: -

Petroli (MSP na MSR) shilingi 315 kwa lita;
Diseli (GO) shilingi 292 kwa lita;

Mafuta ya taa (IK) shilingi 52 kwa lita;

Mafuta mazito ya mitambo (HFO) shilingi 109 kwa lita;

Diseli ya kuendeshea mitambo viwandani (IDO) shilingi 366 kwa lita;

Gesi ya kupikia ya LPG haina kodi;

Mafuta ya ndege (JET A1 na AVGas) hayana kodi.


Kuongeza muda wa usafirishaji wa mafuta ya petroli kwenda nchi za jirani kutoka siku 15 hadi siku 30. Hatua hii itarahisisha biashara ya mafuta ya petroli bila kuathiri mapato ya Serikali;


Kuboresha utaratibu wa kurejesha kodi za Ushuru wa Bidhaa (excise duty) na Ushuru wa Barabara (fuel levy) kwenye mafuta ya petroli kwa makampuni ya madini yenye msamaha ili uzingatie uzalishaji na mauzo ya madini nje ya nchi, kulingana na uwiano uliopo kati ya matumizi ya mafuta na uzalishaji wa dhahabu. Hatua hii inalenga kudhibiti mianya ya ukwepaji wa kodi; na

Kuunda kikosi maalumu ndani ya Mamlaka ya Mapato kitakachosimamia utaratibu wa marejesho ya kodi kwa makampuni ya madini.

Usimamizi wa Kodi ya Michezo ya Kubahatisha:

47. Mheshimiwa Spika, inapendekezwa kufanya marekebisho yafuatayo katika eneo hili;

Kuipa Bodi ya Michezo ya Kubatisha Madaraka ya kukusanya Kodi kutoka kwenye kianzio hiki kwa niaba ya Mamlaka ya Mapato; na

Kubadilisha utaratibu wa kutoza kodi ya michezo ya kuhatisha ili, badala ya utaratibu wa sasa wa kutoza viwango maalum kwa vifaa vya kuchezea michezo hiyo, kodi hiyo itozwe kwa kiwango cha asilimia 13 ya mapato yote yatokanayo na Michezo ya Kubahatisha.

Muda wa Kodi Mpya Kutumika:-

48. Hatua hizi mpya za kodi zitaanza kutumika tarehe 1 Julai, 2006 isipokuwa pale ilipoelezwa vinginevyo.



MAJUMUISHO:

49. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia misingi na sera za bajeti nilizoeleza hapo awali, Serikali inatarajia kukusanya mapato ya ndani ya jumla ya Shilingi trilioni 2, bilioni 460, milioni 995 (shilingi 2,460,995 milioni) katika mwaka wa fedha 2006/07.

50. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa matumizi, Serikali katika mwaka 2006/07 imepanga kutumia jumla ya Shilingi trilioni 4, bilioni 850, milioni 588 (shilingi 4,850,588 milioni). Kama ilivyokuwa kwa miaka kadhaa iliyopita matumizi ya Serikali Kuu pamoja na Serikali za Mitaa, yanajumuisha malipo ya kodi zote zinazotozwa kwenye bidhaa zinazotumiwa na Serikali.

51. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa maelezo haya, sura ya bajeti ya mwaka 2006/2007 inakuwa kama ifuatavyo:-


Mapato Shilingi Milioni A. Mapato ya Ndani 2,460,995 B. Mikopo, Misaada na misamaha ya madeni ya nje 2,226,116 C. Kupunguza akiba (reserve draw down) 163,477 JUMLA YA MAPATO YA NDANI NA NJE 4,850,588 Matumizi D. Matumizi ya Kawaida 3,116,121 (i) Deni la Taifa
(ii) Wizara
(iii) Mikoa
(iv) Halmashauri 287,786
2,037,536
60,514
730,285 E. Matumizi ya Maendeleo 1,734,467 a) Fedha za Ndani
b) Fedha za Nje 641,766
1,092,701 JUMLA YA MATUMIZI 4,850,588
MWISHO:

52. Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Nne imejipanga kutekeleza kwa dhati Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambayo inasisitiza kuongeza kasi ya kukua kwa uchumi na ajira ili kupunguza umasikini, hasa kwa pato. Bajeti ya 2006/07 pia ni mwendelezo wa jitihada za Serikali katika kufikia malengo ya MKUKUTA, malengo ya Millenia, na hatimaye Dira ya Maendeleo 2025. Hata hivyo, ili kufikia lengo letu mapema zaidi, kila mwananchi anapaswa kushiriki kikamilifu kwa kutumia fursa zinazojitokeza kwa kuzalisha mali na kujiongezea vipato. Ni vizuri ieleweke kwamba Serikali haitoi fedha kwa mwananchi mmoja mmoja katika kupiga vita umasikini, bali jukumu la Serikali ni kuboresha mazingira yatakayowezesha wananchi kuongeza uzalishaji, ajira na kujiletea maisha bora. Serikali iko tayari kutimiza wajibu wake huo.

53. Mheshimiwa Spika, ushiriki katika uzalishaji kwa mwananchi mmoja mmoja au katika vikundi ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wetu. Aidha, sekta ya viwanda ikiboreshwa na kutilia mkazo usindikaji wa mazao ya kilimo, ina nafasi kubwa ya kuchangia Pato la Taifa na kukuza ajira. Bajeti hii pia inalenga kuendeleza jitihada za Serikali za kuunganisha nchi yetu kwa njia ya miundombinu ya barabara, reli, mawasiliano na nishati. Ni matumaini yangu kwamba Waheshimiwa Wabunge wataniunga mkono katika bajeti hii inayolenga kufikia matumaini ya wananchi wetu waliotuchagua.


54. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
Kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa inategemewa kupungua kutokana na ukame na ongezeko la bei ya mafuta ya petroli na bei ya umeme mwaka 2005/06
Inajumuisha fedha zitokanazo na kufutwa kwa madeni yetu kwa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) TShilingi. 219.24 bilioni sawa na USD 180 milioni.
 
© boniphace Tarehe 6/15/2006 09:14:00 AM | Permalink |


Comments: 1


   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved