Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Saturday, April 22, 2006
WAHUSIKA KATIKA KAZI ZA SHAABAN ROBERT NA HATMA YA MAGAZETI TANDO YA KISWAHILI
NILIPATA kusoma kazi nyingi za Shaaban Robert na kubaini tabia ya gwiji huyu katika kuchagua majina ya wahusika wake. Riwaya ya "Utubora Mkulima" ina mhusika mkuu aitwaye UTUBORA anayeonekana kujawa maarifa na fikra chanya kwa umma wakati unakutana na jina lake la pili likiwa UJINGAHASARA. Kama ulisoma KUSADIKIKA pia utakutana na KARAMA na Majivuno. "Adili na Nduguze" kina majina kama Adili na Mwema. Wahgusika wenye tabia mbovu Shaaban alikuwa akiwapa majina yanayofanana na tabia wanazobeba, kama Mwovu au Majivuno nk.

Tangu kupitishwa kwa Azimio la Dodoma tulitarajia kuungwa kwa Azimio hilo linalowalenga wamiliki wa Magazeti Tando kutafuta dhana ya kuchuja tabia zao na za wasomaji wao.Kipengele cha azimio hilo chasema na hapa nakinukuu: "Tumeafikiana kuwa wasomaji wa magazeti yetu wanaopenda kuchangia mijadala mbalimbali bila kutaka kutaja majina yao (anonymous), wasinyimwe uhuru, bali tuendelee kuwakemea baadhi yao kwa lugha za kashfa, matusi na mambo mengine ambayo hayafurahishi walio wengi, kwani kinachoandikwa leo katika mtandao hakitapotea, kitasomwa na watu wa vizazi vijavyo. Tumetambua kuwa akina anonymous wanaficha majina yao kwa sababu za ama kujitetea katika mambo yaliyowagusa binafsi au
wanataka kutoa hoja fulani nzito ili wasijulikane kutokana na nyadhifa zao."


Hoja inayoibuka ambayo haikujadiliwa na kifungu hicho ni teknolojia hii kuweza kuruhusu mtu kutumia jina la mwenzake na kisha kutoa matusi. Tukio hili nimelibaini haraka sana katika Gazeti Tando moja hivi karibuni. Ni tukio hili linalonipa kuanza kutoa rai kuhusu kutazama namna ya kutunza majina ya watu yasiweze kutumiwa na wakora kwa ajili ya kujifurahisha wao na kisha yakawakosanisha watu waliokwisha kujijengea heshima kati yao kwa wao na jamii yao. Kwa mtindo huu tunaweza kabisa kukuta majina hata ya wafu, viongozi wa nchi zetu na watu wengine tunaowahitaji kuthamini kazi hii ya kupanua taarifa kwa umma kisha wakatupuuza na kutuingiza katika kundi la wahuni wasio na dira.

Gazeti Tando la Jikomboe liliwahi kutoa taarifa ya kupingwa kwa teknolojia hii katika nchi kadhaa na kisha nikapata fursa ya kuchangia mjadala huo huko. Baadaye hoja hiyo ilijadiliwa sana ikiwa ni muendelezo tu wa kile nilichokifanya mwezi Machi, 2006 katika gazeto tando hili. Uvunjaji wa taratibu katika Magazeti Tando hautamuhusu sana mchangiaji hasa anapokuwa ana kivuli cha kuficha utambulisho wake, au anapoamua kwa makusudi kutumia jina la mtu mwingine au lile ambalo halipo kabisa. Hapa mhusika wa dhambi ya mchangiaji wa aina hii itabaki mabegani mwa mmiliki wa Gazeti Tando husika.

Tusidhani kuwa tuko juu ya sheria na kuwa hatuwezi kuhukumiwa kwa kosa la udhalilishaji (defamation). Katika kesi ya muundo huu muathirika wa kwanza ni mmiliki wa Gazeti Tando kwa kushindwa kuhimili mijadala na wachangiaji wake. Huku ni sawa na kuchukua jukumu lililokuzidi kimo hivyi huwezi kujinasua kuhusu adhabu zitakazotokana na madahara unayoweza kusababisha kutokana na uzembe wa wewe kutotambua athari kabla ya jambo kutendeka! Tukumbuke tuko chini ya sheria na kwa sisi watanzania sheria yetu inayotulinda na kutuongoza popote tulipo inafahamika ilipo!

Si lengo langu kuwatishia wamiliki wa Magazeti Tando au kupindisha kipengele cha pili cha Azimio la Dodoma, bali ni kutoa angalizo kama ambavyo imekuwa kawaida yangu kufanya ili kunusuru balaa siku zijazo. Kuna umuhimu wa baadhi ya watu kutazama miaka mia ijayo, hata kama hawatafanikiwa kufika huko. Tena kuna sababu ya watu kujenga mihimili ya wakati huo sasa kuliko kuusubiri wakati huo ujijenge wenyewe. Nafasi hii inaweza kufanywa na wamiliki wa Magazeti Tando ambayo hasa yanakumbwa na tabia ya kukiuka maadili ya utu wa watu hasa kwa wachangiaji wao.

Tazama Nkya Idya ana maelezo muhimu sana kwa kila mtanzania kuhusu IPTL. Huko huwezi kuona mtu akitukana mwenzake maana maudhui ile indhaniwa kuwa ya kundi fulani tu kama alivyokuwahi kubainisha Shaaban Robert katika "Kusadikika na Kufikirika."

Jamii kubwa kukimbia majukumu na kudhani kazi yao ni kucheza, kucheka na sio kutafakari na kutafuta masuluhisho ya masuala magumu ni kosa ambalo likiachwa liambae litatuathiri wote. Tunatoka katika nchi maskini sana duniani, na kibaya hatukuwahi kupima umaskini wa fikra ambao mimi nimeegeza dira yangu zaidi katika huo wa mali ambao unaweza kuupunguza tukitumia vema rasilimali zetu na unaonekana kwa macho! Huu wa fikra hautazamiki kabisa na haukuwahi kupata ikibali njema hata kwa muumba! Tuna jukumu la kuonyesha njia pale tunapodhani inafaa na hasa tunapotazama jamii yetu inapotea kutokana na kupenda vitu vyepesi vyepesi. Wanaoweza kutambua au kuona ugonjwa huo wanatakiwa sasa kubadili maudhui ili kuifanya jamii ikose pa kupata taarifa nyepesi nyepesi kama ambavyo Azimio la Dodoma linavyobainisha kama umelisoma kwa umakini. Si kila mtu atambua namna vipofu wawili wanavyoongozana huku wakikosa anayeona kuwaonyesha njia! Nini huzuni yao hawa huku wanabaini kuwa duniani kuna watu wanaotazama lakini hawataki kutazama masaibu yanayowakabili wao?

Nitoe wito sasa kuandaliwa kwa sehemu maalum ambapo tutaweza sasa kuweka majina ya wanaokubali kuingia katika jumuiya yetu. Waziri wa Teknolojia ndugu MK anaweza kutusaidia na Katibu wetu Miruko anaweza pia kutupa mwongozo baada ya kuwasiliana na Komredi Mwenyekiti wetu.

Nibainishe hapa ndugu zangu kuwa kunitukana mimi si jambo linaloninyima usingizi hata kidogo! Natambua si kila nifanyalo ni jema na kama ambavyo si kila wewe ufanyalo ni jema. Tena nafahamu si kila jambo langu unalipenda, sawa sawa na kila jambo ufanyalo kuwa ni lazima mimi nilipende. Tena naelewa kuwa, tuko tofauti sana na nabaini kuwa nina Gazeti Tando langu hapa ambalo halitavumilia hata siku moja kuona utu wa mtu unavuliwa kama ambavyo nimekuwa nikifanya huko nyuma ikiwa ni pamoja na kutoshiriki kuwavua nguo wengine popote niwapo! Kutumiwa jina la mtu kumtukana mwingine ni dhambi isiyosameheka haraka! Mnaotazama sasa tazameni na chukueni hatua kabla hatujaangamisha huku tukidhani tunajenga! Ubaguzi si ule unaofanyiwa zaidi ya huo unaofanya wewe! Nikamilishe kwa kauli yangu ya siku zote, "inawezekana, cheza karata yako"

Komredi Boniphace Makene
Leo Jumamosi, Apr 22, 2006 UT PANAM
 
© boniphace Tarehe 4/22/2006 09:15:00 AM | Permalink |


Comments: 8


 • Tarehe 4/22/2006 4:56 PM, Mtoa Maoni: Blogger Jeff Msangi

  Komredi Makene,
  Kama kawaida umeandika mambo ya msingi sana hapa.Nadhani mambo kama haya ndio yale ambayo kina anonymous huwa hawana muda wa kuyasoma wala kuyachangia.Hili linatupa picha juu ya aina ya watu tunaopishana nao lugha na maono.Wasikunyime usingizi,nimependa kauli hiyo.Lakini nadhani wakati umefika sasa wa kutumia tekinolojia kuwadhibiti watu hao.Hakuna uhuru usiokuwa na wajibu.Tusishindwe kuweka "this blog does not accept comments from anonymous people".Ni jambo rahisi sana na wakati umefika nadhani.Nia ni kujenga na wala sio kubomoa.Hii itasaidia kila mtu kuwa na uwanja wake,kufungua blogu zao.

   
 • Tarehe 4/22/2006 5:22 PM, Mtoa Maoni: Blogger John Mwaipopo

  Jeff nia tunayo na namna tunayo ila tumeshindwa. Tupo miongoni mwetu tunaofurahia hii maneno. Nafikiri unanielewa. Kuna namna ipo pale Kwa Bwaya CN ya kuhariri comment lakini ama tunajifanya maamuma ama hamnazo.

  Jeff nilipata habari (sijui kweli au urongo) kuwa wewe ulisoma-ga Afrika. Ile elimu wewe ni shahidi. Sio hii ya kuandika vya uongo na kupata A. Ndio hii ya hawa anonymous ambao katu hawana nafasi ya kujisumbua mathalani na maandiko ya Rashidi pale kwako. Maandiko ama vitabu vya nini wakati baba zao waliwafundisha video tokea hata Tanzania hakuna TV.

  Wanataka picha tena hata hizo picha sio zote. Ni zile za ama watu maarufu wa mtaani ama nani kavaa shanga nyingi ama kapaka hina ya kutoka Abudhabi ama Saudia. Weka picha ya kupungua kwa theluji Mlima Kilimanjaro kama hautaona hoja inabadilishwa kushabihiana na mapenzi yao.

  Ndio ndugu zetu hawa wala wasitunyime usingizi, ingawaje ni ule wa mang'ang'amu.

   
 • Tarehe 4/23/2006 1:31 AM, Mtoa Maoni: Blogger MK

  Ni jambo zuri sana kuweza kuzungumzia jinsi hii techonology inapo tupeleka sisi watanzania na wana-blog kwa ujumla.

  Katika kipindi hiki tulicho nacho na kuendelea jamii yetu itaweza kulelewa na hii technology inayo kua kwa kasi kubwa ktk dunia nzima hivyo basi tunabidi kuweza kujenga maadili yaliyo mema yatakayo wezesha kujenga hii jamii ya mtanzania na jamii ya muafrika sababu siku zote technology ni kitu kizuri na vile vile ni kitu kibaya, bila kuliangalia hili jambo kwa undani tunaweza kuelekea pabaya na wakuraumiwa tutakuwa sisi kizazi cha sasa.

  Katika upande unao husu wale watu wanao changia kwa kutumia lugha chafu za matusi ni vizuri kuweza kuwaonya na vile vile ili kuweza wana-blog wote kuwa salama ktk mambo ya sheria mimi natoa mawazo yangu ya kwamba ktk kila blog tunabidi kuandika maandishi kama haya yafuatayo:-
  "Vijimamboz.blogspot.com (Unaweza kuweka jina la bog yako) haitahusika kisheria au kwa namna yoyote ile na maoni ya msomaji yeyote aliyotuma katika blog hii kuhusiana na habari yoyote" na mnaweza kuandika kwa kiswahili au kiingereza na basi hapa tutakuwa salama ktk maswala yoyote yale ya kisheria.

  Tuweze kukemea yale maswala yote yanayo endana kinyume na jamii yetu ili kuweza kujenga kizazi chetu maana maendeleo ya taifa letu na wananchi wake yanategemea kutoka ktk hiki hiki kizazi.

  Pia mbali ya kuandika habari za kufurahisha au starehe tu, tunabidi tuweze kutoa mchango wetu kwa kuandika habari zitakazo muelimisha au kumsaidia hata msomaji atakayekuwa kule Songea, Mwanza, Mtwara au mkoa wowote ule ndani ya tanzania na afrika nzima.

  Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

  Nashukuru,
  ©2006 MK

   
 • Tarehe 4/24/2006 1:37 AM, Mtoa Maoni: Anonymous charahani

  Makene

  Hili nalo lingefaa kuwa tamko la Texas, maana lina mambo mazito yanayozungumzia mustakabali wa magazeti yetu. Hoja imekwenda kifalsafa kidogo hasa pale inapoanzia na kina Shaaban Robert, labda unahitaji idhini tu ili tuweze kuliweka katika miongozo yetu.

   
 • Tarehe 4/24/2006 3:40 AM, Mtoa Maoni: Blogger mwandani

  Katika kuchangia - hoja nadhani kuna njia nyingi tu za kuweza kuzuwia au kuondosha maoni yanayodhalilisha au kutukana watu.

  Njia ya Bwaya na Innocent ni nzuri tu, kwamba maoni yanabandikwa pale tu mwenye blogu anapoamua maoni gani ya kubandikwa.

  Ila kwa hisia zangu binafsi saa nyingine nakuwa nakata tamaa kabla ya kuchangia - hivyo kughairi kuchangia - kwani nakosa ile furaha ya kusoma maoni yangu papo kwa papo

  Au pengine nisiyaone kabisa na wala nisione wengine waliochangia wana mitazamo gani juu ya mada husika.

  Kadhalika nakosa uhuru fulani - that somebody has control here

  Starehe na manufaa ya chombo - kama zilivyo blogu -kinachoshirikisha watu moja kwa moja katika mjadala vinaweza kukinzwa namna hiyo.

  Njia ya Bwana Bwaya itakuwa nzuri ikiwa mhariri ana imani na nia njema - na kuzuwia matusi tu na mikwara mingine mingine.

  Kuna njia nyingine ya kuhariri maoni, kama vile unavyofanya kama umekosea kuandika maoni kwenye blogu yako na kutumia picha ya debe la taka kufuta maoni pale chini ya kidirisha cha maoni uliyoandika.

  Mimi binafsi kama ningekuta matusi kwenye maoni ndani ya blogu yangu ningetumia njia hii ya pili. Njia hii ya pili inategemeana na vile mwenye blogu anapata muda mara ngapi kwa siku au kwa wiki kuhariri - kama muda utapita sana kwabla ya kuhariri, matusi yanaweza kuwa yameshamdhalilisha mlengwa kabla ya kufutwa.

  Jambo la tatu, nafikiri teknolojia ya blogu imeweza kunipatia uhuru mkubwa ambao sikuwahi kuupata kwenye teknolojia nyingine zinazotumia moderator au kamati mbalimbali za kufanya maamuzi.

  Bila ya shaka wengi wetu tumefurahia - au kwa uhakika zaidi mimi binafsi nimefurahia - hali ya kutokuwa na uongozi au kujiandikisha mahala kokote.

  Ninakiri kuwa tangu zamani nina matatizo ya kutoa maoni na waalimu, uongozi, organised religion na vyombo kama hivyo.

  Hivyo basi suala la kujiandikisha katika chombo fulani chenye namna ya kudhibiti uhuru wa blogu ninaoufurahia au wachangiaji wenye nia nzuri wanavyoufurahia... hapo nahitaji kufikiria na kuelimika zaidi juu ya hilo ili niweze kutoa maamuzi yanashawishi moyo wangu kwa dhati.

  La mwisho, kuhusu watu wanasoma na kuchangia nini, kama ulivyotolewa mfani wa ripoti ya IPTL kwa Nkya - watu wengi wanaona hayo mambo ya maana ni michosho, yanawapigisha miayo.

  Kwa bahati mbaya hivyo ndivyo watu walivyo na safari hatua, natumaini baada ya muda, blogu zinavyozidi kuongezeka kutoka kwetu nyumbani nayo makundi ya wachangiaji pia yataongezeka na watachangia kwa kadiri ya mapenzi ya mada zinazoandikwa.

  Ninaamini pia kuwa inawezekena kabisa wenye matusi sio wengi ila wanatumia vitisho kuogopesha wengi.

   
 • Tarehe 4/24/2006 7:03 AM, Mtoa Maoni: Blogger Reginald S. Miruko

  Umesomeka Makene. Hawa watu, kina Anonymous mimi binafsi wananikera sana, hasa pale wanapotumia uhuru huu vibaya. Niliwahi kupendekeza katika michango yangu ya hoja mbalimbali (kwenye magazeti tando), kuwa tuweke kifungo cha kuwabana watu hawa. Nilipojaribu kuuza wazo hilo katika kikao cha Azimio la Dodoma, nikashawishiwa kuwa wapo watu ambao kwa nyadhifa zao watashindwa kuchangia hoja, na badala yake tutakuwa tunapata maoni ya wenye magazeti tando pekee. Mfano, nilifikiria, mfano, kama mtu aliyesoma na Waziri fulani, na waziri huyo akafeli mtihani na kununua cheti, akitaka kuweka hoja hiyo itakuwa vigumu kuandika jina lake. Lakini ukiangaliwa kwa Ndesanjo sasa, huwezi kutuma maoni bila kujitambulisha. nadhani sasa imefika wakati tufumbe macho, tuwazuie bila kujali kipengele kimojawapo cha Azimio la Dodoma, kwa kuwa lile ni pendekezo na lipo mezani kwa mjadala.

   
 • Tarehe 4/25/2006 6:50 AM, Mtoa Maoni: Blogger Bwaya

  Uhuru wa teknolojia hii usipokuwa na mipaka, unaweza kuibua kasheshe zisizokuwa za lazima.

  Nadhani tukitaka kulipunguza tatizo hili, tuanze na sisi wenye blogu. Tuwe makini na maandiko yetu manake tusipoangalia, blogu zinaweza kugeuka blogu udaku. Nimekuwa nijiuliza kama anavyojiuliza Makene, "Hivi kwa nini hawa anonymous wanakuwa na nguvu mahala fulani zaidi kuliko kwingine?". Nadhani tunawavutia kwa content za blogu zetu.

  Hata hivyo anonymous anaweza asiangilie anakochangia. Hivyo umuhimu wa kudhibiti maoni bado unaendela kuwapo. Awali nilifikiri njia yangu ya kuthibiti uchangiaji wa wasomaji, ni nzuri. Lakini njia hiyo imekuwa ikinipa matatizo kidogo maana mara nyingine huwa napotea kwa juma zima na tatizo analolidokeza Mwandani hapo juu linajitokeza. Nimeshawishika kuibadili.

  Nadhani itapendeza kama ile namna anayotumia Ndesanjo na Mwaipopo itatumika. Kwamba kila anayechangia ni lazima afahamike! Sioni kama kuna ulazima wa kuruhusu watu wasioleweka wanaandika mambo yao amabyo mengine yanakera wasomaji wengine.

  Kama uhuru huo wa kuwapa nafasi watu wasio na blogu kutoa mawazo yao unasababisha matatizo ya kuvuana utu, sioni sababu ya kuuendeleza uhuru huo.

  Mwenye simu ndiye awe na ruhusa ya kusikika asiyenayo awe pembeni.

   
 • Tarehe 7/07/2018 3:19 PM, Mtoa Maoni: Blogger collins williams

  Mimi Kwa ujaini Johnson Tamara yetu. Ninaishi Marekani, Kati ya HII Nataka Kutum Ili kuwaonya washauri Wote Sana wa Mpango wa mkopo Kuwait Makin Sababu KUNA Kashfa Kwa Kila Mahal. Nimeshambuliwa si wakopaji Kadhaa mtandaoni. Nilikuwa nimepoteza Tumaini Kwa Hadi Rafiki Yangu alipokuwa akanipeleka wakopaji Sana wa kuaminika aitwaye Mr Collins Williams Loan Company Ambay alinipa Mpango wa mkopo usio wa Salama ya Chini 75,000 Dola meza 24 Shida yoyote mpira. Ikiwa moja Haja Aina ya ya yoyote Mpango wa mkopo wewe wasiliana Naye sasa-kupitia Barua Pepe: HII Nitumia bigloan15@gmail.com Kati Ili kuwaonya Kwa Wote wanaotafuta Mpango wa mkopo Sababu ya ya Jahannamu niliyopita katika Mikono wakopaji bandia.Mimi sisi Tamara Johnson Kwa ujaini. Ninaishi Marekani, Kati ya HII Nataka Kutum Ili kuwaonya washauri Wote Sana wa Mpango wa mkopo Kuwait Makin Sababu KUNA Kashfa Kwa Kila Mahal. Nimeshambuliwa si wakopaji Kadhaa mtandaoni. Nilikuwa nimepoteza Tumaini Kwa Hadi Rafiki Yangu alipokuwa akanipeleka wakopaji Sana wa kuaminika aitwaye Mr Collins Williams Loan Company Ambay alinipa Mpango wa mkopo usio wa Salama ya Chini 75,000 Dola meza 24 Shida yoyote mpira. Ikiwa moja Haja Aina ya ya yoyote Mpango wa mkopo wewe wasiliana Naye sasa-kupitia Barua Pepe: HII Nitumia bigloan15@gmail.com Kati Ili kuwaonya Kwa Wote wanaotafuta Mpango wa mkopo Sababu ya Jahannamu niliyopita katika wakopaji Mika Band.

   
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved