Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Thursday, March 16, 2006
SALAMU ZA WABONGO ATLANTA
NIMEFARIJIKA sana nilipopata bahati ya kufika ATL. Pale nitapakumbuka mno kutokana na Watanzania wa pale kuonyesha ukarimu wa hali ya juu ambao sikuwahi kuuona. Heshima hii iliyotukuka, imenipa fursa kuandika makala hii. Zawadi yangu kubwa ilikuwa Juisi ya Maembe (Kwa mlio Atlanta najua hamfamamu, huu ni utani wa pombe) Tulipiga juisi ile na kisha kugoma kwenda disko ili tuendelee kujadiliana masuala ya siasa ya nchi yetu. Nafarijika ninapopata fursa ya kujadili masuala haya na mtu yeyote. Wapo wasiopenda kabisa kusikiliza masuala haya lakini kwa Atlanta hapana...hawa walifika mbali zaidi, kujadili Kiswahili na nafasi ya Sanaa ya Tanzania kwa ajili ya Watanzania na kuwatambulisha nje.

Atlanta jirani kabisa na Alabama, Hapa kama unakumbuka Mmiliki wa Gazeti Tando la Baragumu aliwahi kula ugali hapo. Kuna rafiki zake nimewakuta huko na wao kunialika kusoma Gazeti Tando lililopo mtandaoni liitwalo KASRI LA MWANAZUO. Ilinibidi kucheka maana natambulishwa kusoma Gazeti Tando ninaloliandika na kulimiliki mimi. Nikacheka na kuwapa taarifa ya kuwa ni mimi mwenyewe, basi ujumbe wa JEFF Msangi kuwa nihakikishe anapatikana mmiliki mwingine wa Gazeti Tando toka upande huo zinaweza kuzaa matunda. Nina kila sababu ya kujipongeza kutokana na kasi ya kuyatangaza magazeti haya. Yanapendwa na kila anayetambulishwa kutokana na kubeba maudhui mzito zenye kuonyesha dira na muelekeo wa nini kifanyike. Niwapongeze wamiliki wa Magazeti Tando wengine maana kama mnaweza kufanya kazi hii kwa kujitolea tu je mtashindwa kuinyanyua nchi yenu katika majukumu mtakayopatiwa na umma?

Kuna ujumbe kwa MWANDANI ambao umetokana na habari ya Gazeti la Nipashe kuhusu kuli ya JK. Hii ni kauli njema lakini JK anataka kuleta urasimu usio na umuhimu kabisa. Kwani hao viongozi wa serikali hawawezi kumiliki Magazeti Tando kama yetu haya ili tuweze kuwafikia moja kwa moja. Kuna haja gani ya kuwa na Mtandao mmoja kisha awepo mtu wa kukusanya maoni na kuyapeleka? Tutaaminije kuwa yamefika na tutapata lini majibu? Tunahitaji namna ya kuweza kuwasiliana moja kwa moja, nipe nikupe na viongozi wa serikali. Michuzi najua uko karibu huko kazi hii sasa fika hapo Ikulu, gonga hodi , singizia unapeleka picha ama vingine sijui ili tu uweze kuepusha urasimu na matumizi yasiyo na umuhimu. Kumuweka mtu hapo ina maana tunafungua ajira isiyo na umuhimu na kuongeza matumizi ya serikali. Tena kutatakiwa kuwa na matumizi ya mafuta ya kuchoma bure kabisa kwa yule atakayekuwa anapeleka maoni hayo katika ofisi mbalimbali. Yote haya ya nini, kazi hizi zaweza kufanyika bure kabisa! Niliwahi kuuliza ndugu yangu mmoja kuhusu kushindwa kwa Serikali ya Wanafunzi DARUSO kukosa Mtandao wao. Nilikuwa kiongozi wa chini kabisa hadi juu kabisa huko. Sasa hivi naweza kuandika na kuhariri KASRI LA MWANAZUO peke yangu lakini pale tulishindwa maana kila mmoja alidhani jambo hili ni gumu na haliwezekani. Kuongezeka kwa warasimu kama atamkavyo Max Weber kunaongeza pia matatizo ya fikra. Jambo linalowezekana sasa lachukua muda mrefu kufikiwa maamuzi yake. Kila jambo lina athari lakini kinachotakiwa ni kuvunja utepe mwekundu Red Tape katika urasimu kama alivyowahi kubainisha, Bill Clinton katika "The National Perfomance Review." Nikirudi hapa ni kuweka picha za safari hii awamu ya kwanza.
 
© boniphace Tarehe 3/16/2006 10:21:00 AM | Permalink |


Comments: 2


  • Tarehe 3/18/2006 11:45 AM, Mtoa Maoni: Blogger FOSEWERD Initiatives

    Makene, suala la kuwakabidhi maelezao hata mie naona lina mauza uza.... nimetoa maoni pale kwa mwandani.

     
  • Tarehe 3/26/2006 6:40 PM, Mtoa Maoni: Anonymous Anonymous

    una mawazo yaliyopevuka ndugu. Haya ni mawazo ya mzalendo kamili, mhakiki wa sera potovu za magharibi. Lau viongozi wetu wangejua wangewekeza katika mawazo kama haya.

    Daudi Kyeu

     
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved