Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Saturday, March 11, 2006
NIKO SASA ATLANTA
WANAKASRI wametuma lawama kuwa hawasomi somi maandishi mapya hapa. Niliwaacha waendelee na hekaya ya kisa cha kuoa wazungu. Kisa hiki chema sana maana imani ya Kasri ipo kwa binadamu wote. Kasri limetanuka nje ya mipaka ya rangi na hii inalipa fursa kujali utu kwanza na rangi baadaye. Madhara yanayotokana na rangi na hasa fikra zake hasi zina athari zaidi ya faida yake. Kuna haja ya masuala haya kupimwa na kuyapatia majibu anuwai ili binadamu tuigeuze dunia kuwa sebure njema kwetu kukaa na kuishi.

Hapa Atlanta nimefika baada ya safari kutoka Edinburg iliyochukua saa kama kumi kufika Houston. Huko niliyoyaona njiani katika barabara zinazokatiza baharini yamenipa maswali na hoja nitakazoziandia siku nyingine. Nikaondoka tena Houston na kuanza kukatiza Luoisiana nirani kabisa na New Orleans, kisha Misisipi, Alabama na kuingia hapa Georgia Atlanta jana jioni.

Nimefika na kuzitangaza Blogu huku kwa watanzania na mjadala wetu jana umenichukua saa nyingi huku tukipata maji ya bahari yaitwayo Heineken. Tumeendelea kujadili siasa ya Tanzania na kila mara nikiwakumbusha watanzania wenzangu nafasi yao huko nyumbani. Nimefurahi wengi wanalijua somo lakini wanahitaji kuongezwa kwa fikra zaidi na kuwezeshwa kimtazamo.

Nimebaini itikadi inaua taifa, hapa nina maana ya vyama vya siasa Tanzania. Vyama hivi vimefanya watendaji wengi wazuri kuwa nje ya serikali wakati tuliwahitaji sana. Mfano wetu hapa leo ni Mrema, huyu tutake tusitake tunamhitaji sana, wa pili ni Seif Hamad. Pemba na Zanzibar inamuhitaji huyu kuwa serikalini lakini swali ni moja aingieje? Itikadi za vyama vingi zimefanya mtindio wa ubongo kuingia Tanzania. Fikra za watu wetu zimegeuzwa katika makundi, waoga ama wanaopenda kujikomba kuingia chama tawala, na majasiri kuwa upinzani. Hivi sasa vinageuka vita vya nini si mnatupinga sisi, hivi nini kinachotoa mwanya wa tofauti za fikra kugeuzwa vita na kutanuliwa katika lindi la kunyimana nafasi za kuiwajibikia nchi ikiwa kila mmoja ana lengo la kufanikisha maendeleo yetu?

Inakuja suala la utaifa, na maendeleo kwanza. Je kura ni kigezo tosha kwa raia kutumia kufikia maendeleo. Uchaguzi una maana gani kama washindi walishajulikana kuwa ni matajiri fulani tu? Kuna haja gani ya watanzania walio ughaibuni kubakia huku badala ya kutumia nafasi ya ushawishi wao kusaidia kuendeleza nchi yetu? Lakini kwa nini walioko ndani nao wawatenge kwa kuwaita majina ya kila bezo, wanyamwezi, wanajiona, machizi nk?

Nitarudi baadaye hizi ni salamu za Atlanta, mji mwenyeji wa Olimpiki mwaka 1996. Hapa leo vijana wangu Sajo na Gladdy wanafunga pingu za maisha. Nitafafanua harusi hii baadaye baada ya ndugu zangu hawa kunipa fursa ili Gazeri Tando langu liweze kutumia maelezo haya katika makala zake.
 
© boniphace Tarehe 3/11/2006 08:54:00 AM | Permalink |


Comments: 5


  • Tarehe 3/11/2006 9:26 AM, Mtoa Maoni: Blogger Jeff Msangi

    Salamu zao Atlanta,
    Hakikisha kabla hujaondoka huko utupatie japo mwanablogu mpya kutoka kibande hiyo.

     
  • Tarehe 3/12/2006 10:28 PM, Mtoa Maoni: Blogger Fikrathabiti

    Hiyo habari ya SAJO na GLADDY ni njema makene kwani inakamilisha safari iliyoanza miaka ya 1999 kule Iringa na kuthibitishia wengi kua hawakua wakifanya masihara kama wafanyavyo vijana wengine!!

    Hili nalo linapaswa kua funzo kwako kwani tumechoka kutambulishwa mashemeji wapya kila mwaka.

     
  • Tarehe 3/13/2006 5:59 AM, Mtoa Maoni: Anonymous Anonymous

    Makene, tuma salamu za wanablogu kwa ndugu zetu wanaooana. Tunawatakia heri na fanaka.

    Suala la kuwa na watu taifa linawahitaji ambako kwakuwa wako upinzani, wanakuwa nje ya uongozi na utawala nami nimekuwa nikilifikiri muda mrefu. Au suala jingine la wabunge wa chama twawala kuwa washabiki wa sirikali baada ya kuingia kwa wapinzani bungeni. Ule upinzani bungeni kama enzi zile za kundi la wabunge 55 sijui tutauona lini tena.

    Sasa tufanyeje kuhusu suala la itikadi kuzuia watu wenye uwezo kushiriki kujenga taifa na kuongoza?

     
  • Tarehe 3/13/2006 10:43 AM, Mtoa Maoni: Anonymous Anonymous

    aisee fikra thabiti umemuamulia makene...mwambie aangalie sana yasije mkuta yale ya kwenye daladala ya mwaipopo kule kwa michuzi.

     
  • Tarehe 3/18/2006 11:41 AM, Mtoa Maoni: Blogger FOSEWERD Initiatives

    Makene na Ndesanjo, hili suala la itikadi kuweka mipaka kwa kweli mie huniumiza sana kichwa....upande wa pili ni matokeo ya "the mwenzetu syndromme" ambapo mwenye makosa atakuwa huru alimradi yuko upande wa walioshika jag poti!! - syndrome hii huisha ikiwa tu tutapata populal leader, ambaye hakuwekwa madarakani na systems....huyu hatamnyenyekea yoyote kuwa ndio kampa nguvu, na atatenda kazi kwa kufuata kanuni...kwa kweli bado ni gumu sana.....wenzetu wa Zambia wamefanikiwa.... kwamba nchi ni ya watu wenyewe na si ya fulani.....

    sijui sana lakini nahisi serekali ya sasa kama vile imeanza kulistukia hilo, labda kwa vigezo kadhaa

    1. Kitendo cha JK kutoendekeza magwanda ya kijani akiwa kwenye kazi zake za uraisi

    2.Kitendo cha JK kukubali kuwa tofauti za fikra za wanaCCM ziheshimiwe kwani ndio kujenga chama

    3. Kitendo cha Magufuli kutamka wazi wazi kuwa atadili na waliohodhi majumba ya NHC bila kuangalia kama ni CCM au CHADEMA inaonyesha dalili za kukataa kuendeshwa na itikadi

    4. kitendo cha Waziri mkuu kuwataka wanaKaratu kuacha kuvutana kuhusu legitimacy ya mbunge wa CHADEMA (dr. Slaa) na kuwekeza kujenga wilaya...ambayo ni tofauti na zile tulizozoea za Sumaye kupinga miradi ya maji ya wanakaratu na uwajibishwaji wa halamashauri na akina Slaa..

    kukwangua makunyanzi serekalini na kukiri kuwa kuna uovu....zamani watu wengi waovu walikuwa salama kwa kuwa tu wana kadi za kijani....

    hili ni la msingi sana...na hili kweli ni kasri la mwanazuo....

    nikimalizia ningeomba serekali ya wanablogu ilishikie hili kidedea NA IKIWEZEKANA HATA NYUMBANI KUZUIA ITIKADI KUUPIKU UTENDAJI UMAARUFU!!

    NAOMBA KUTOA HOJA!

     
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved