Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Sunday, March 19, 2006
NI KWELI HAYA YATATOKEA...
NIMEJIFUNZA sana siku hizi kuheshimu kazi za watu. Msanii Ebbo aliimba wimbo akitaja maneno na kuomba kusamehewa. Nimeona nami nianze kuomba msamaha maana siku hizi kumeongezeka wachangiaji mada wanaojiita ANONIMASI. Hawa tunaweza kuwadhibiti na hasa ndugu Issa Muhidin Michuzi anapaswa kufanya hivyo mara moja. Mawazo yangu yanaweza kutopokelewa vema lakini niliahidi nilipotoa maoni yangu katika Gazeti Tando la Michuzi kuwa nitalaani matukio ya hoja za udhalilishaji utu. Nafanya hivi na imani yangu wamiliki wa Magazeti Tando wengine nao watafuata harakati zangu... hata kwa kutikisa vichwa tu pale wasomapo maandishi yangu haya leo.

Awamu ya nne, ipo madarakani kufuatia nguvu ya vyombo vya Habari na wasomi wachache waliotumia nafasi zao za kuihadaa jamii kwa kipindi kirefu. Kama walifanya hivyo kwa wema, basi sasa wako madarakani na ni imani ya wengi kuwa haya yanayozungumzwa sasa yanaweza kuwa vitendo na sisi tukaamini kuwa lengo lao lilikuwa kuujali umma na sio matumbo yao. Kama hawatafika mwisho vema...tutajiuliza nini kilifanyika, hakukuwa na mikakati ya ubainishaji matatizo na kupata masuluhisho yake?

Nimeona umuhimu wa kuandika nafasi ya Magazeti Tando katika awamu ya tano ya serikali ya Tanzania. Kuna watu huku wana nafasi ya kuunda agenda, kuna wengine wanataka kupoteza agenda hiyo pia...hawa wasitukwamishe kujengeana uwezo! Kuna watu nawaona machoni kabisa kuwa wanafanya maandalizi ya kushika dola. Kuna wengine nawaona wanajiandaa kabisa kushawishi wale wanaodhani wanaweza kupeleka mashua yetu mbele kujitokeza. Kizuri wamekuwa wakihamasisha uchakatuaji wa hoja na utafiti wa masuluhisho ya matatizo. Siku zote nimewatazama wakifanya kazi ya kuangalia uchafu na kuupigia kelele. Kuna jamaa mmoja aliwahi kunieleza juu ya siri ya kuwa muongo, alisema na hapa namnukuu bila kumtaja "Ukiwa muongo jenga tabia ya kutunza kumbukumbu."

Blogu, jina ninalolikataa lakini limekuwa tayari na kuzoeleka, zinatoa kumbukumbu ya fikra na itikadi na mitizamo ya watu ambazo zitatunzwa kwa miaka mingi. Zitakuwa hazina isiyopotea na zitatumika kuonyesha nani anasema nini huko tuendako, alitoka wapi, na je amehama imani na misingi yake. Tutaweza kumuuliza vema, na pia kuweza kuhoji waliojificha wakidhani kuwa ni muhimu kudanganya na kujificha ili uingie kama mtakatifu katika madaraka ya dola.

Nimetazama sana na nimejitahidi kuhamasisha, baadhi ya wale ambao wanaonyesha kutaka kuingiza nguvu zao kuijenga Afrika wakianzania na Tanzania. Kizuri wametapakaa sana na kweli wanaonekana hapa. Jamii inawaona na mimi nawakilisha jamii hiyo nikiwataka sasa kugeuza mipango yao kutoka kuandika hoja tu bali kuwa na tafakari na hasa kujifunza kusoma na kusikiliza hoja za wengine pia. Kuna watu nadhani wanatakiwa kujifunza uvumilivu maana hii ni sifa kubwa kama wanataka na wanakusudia kushika madaraka ya dola. Ninawaona na hili wanatakiwa kulifanya sana, sipendi kunukuu maandishi ya Biblia maana Upadre ulinishinda zamani, hii haina maana kuwa nimeshaukimbia ukapera...la hasha niko single mie, nasaka katika mitaa ya dunia hii! Hapa nataka kudonoa tu hoja hii tu toka kwenye hilo Buku jeusi, "jifunzeni toka kwangu na ishini kama mimi" tena hapa "akupigaye shavu la kushoto mgeuzie na la kulia."

Nadhani kuna jamaa anatakiwa kuanzisha Blogu ya masuala ya dini ili kuwanoa viongozi wetu wajao. Afanye hivi bila woga maana kuna kazi ya kwanza ya kunoa mwili na baada ya hapo ni kunoa moyo/roho. Utawezaje kuwa juu ya rasilimali za nchi kisha uvumilie kutozidonoa wewe kwanza. Mtazame mfanyakazi wa Benki unapomtembelea afisini kwake na kumuomba fedha..huchomoa zilizoko mfukoni mwake! Kwa nini asibugudhi burungutu zilizopo mbele yake hapo kaunta?

Kuna kuandaa moyo kama kulivyo na kuandaa kuandaa fikra. Kuna kuandaa imani na itikadi na msimamo wa mtu binafsi kisha kuitazama jamii, haya si mambo mzaha, ya msingi sana kuwa nayo ili uendelee. Kuna kipindi maandishi tuandikayo yatabadilika ili kutunza amali za jamii yetu. Kutunza utu, kuheshimu jamii na kutojiunganisha na matabaka yasiyo na msingi katika umma. Maana halisi hapa ni kujiandaa maisha ya kubeba misalaba. Nina maana misalaba kubebwa na viongozi na sio wananchi, sinukuu kabisa kauli ya Msuya kuhusu kila mtanzania kubeba msalaba wake mwenyewe.

Mimi naamini kwa Profesa aliyepewa jina la Yesu, aliyeamua kubeba msalaba yeye kwa ajili ya umma. Hawa ndio viongozi tunaotaka Afrika. Kiongozi aliye radhi kugawa chakula kwa raia kwanza wale kisha masalio ambayo yameharibika ndiyo ayageuze kuwa kitoweo chake. Hapa namkumbuka Padre Biseko wa Jimbo la Musoma na kituo chake cha wagonjwa wa Ukoma pale Nyamiongo. Nikifika Musoma nitamtembelea, kumsabahi na kisha na mimi kunywa kahawa na familia yake hiyo anayoithamini na kuipenda sana.

Kuna mengi yatatokea, lakini moja ni kubwa kwa tunaowatazama jiandaeni sana. Msife moyo maana mafanikio myatakayo yanaweza kutotoka katika mikono yenu na badala yake yakaletwa na watoto au wajukuu wenu. Kama unachukia kujigawia nyumba za serikali basi tazama uko ulipo umejiuzia vingapi? Jifunze kuanzia hapo na rekebisha maana muda bado upo, nikamilishe kwa nukuu yangu ya mara nyingi, "Inawezekana, cheza karata yako."
 
© boniphace Tarehe 3/19/2006 02:15:00 PM | Permalink |


Comments: 5


 • Tarehe 3/19/2006 6:46 PM, Mtoa Maoni: Blogger John Mwaipopo

  Umeongea mengi mema kama kawaida yako Bonny lakini la msigi ni hili la hawa Anonimasi. Hakika wamenipa changamoto sana juu ya sura yangu na maoni yangu kule kwenye kibaraza cha michuzi. Hivi sasa nimeshapata dawa -cream- ya kujipaka na kujichubua huenda nikawa mzuri kama watakavyo wao na sio yeye aliyeniumba. Sikujua kuwa vibaraza hivi ni vya kuchangia hoja na masuala jadidi. Kumbe ni mashindano ya ama urembo ama kujificha mithili ya askari wa mwituni.

  Lililonikera sana ni kuingilia mawazo ya mtu mwingine ambayo hata hayadhihaki mtu. Mathalani lugha na nakshi ambazo ndani yake hayana ukakasi bali sanaa na weledi wa namna fulani. Mwenye blogu mwenyewe ndiye alihamasika kunisabahi kwa kiluga changu (bahati njema anazungumza lugha karibu 10 hivi- hili aliniandikia mwenyewe). Akiandika yeye vema nikimjibu nongwa.

  Kazi ipo na inahitaji busara na uvumilivu kama Mark Msaki na Ndesanjo walivyonena kule kwa bwana Muhidin.

   
 • Tarehe 3/20/2006 9:16 AM, Mtoa Maoni: Blogger mark msaki

  nisiliache hili lipite hivi hivi. ninausifu mtiririko wa hiki kisa...kuanzia na kule kwenye suala la anonimasi kushindwa kuchuja mawazo yao kabla ya kusema...kila mtu huwaza vitu, huanza na kufikiri na mwisho kutoa vitu hadharani, vitu ambavyo vitamsema yeye ni nani...na anataka nini (kama ulivyoainisha baadaye)...hivyo ndivyo baada ya muda vitawafanya wanadamu wengine kupata mahali pa kujenga uwezo, kutetea, kutetewa n.k. mawazo na uwezo wa kufikiri ni hazina, uwezo hujengwa, mara nyengine kupitia shule, au matukio(kula chumvi), au wa kuzaliwa..hatima yake tunautumia uwezo huo kujiendelea sisi kama jamii ya wanadamu...je Einstein aliyegundua matumizi ya Nuclear angeyaficha kapuni, leo hii tungeona mapinduzi yaliyopo katika nyanja za nishati? je aliyegundua injini na mungine akatumia kanuni hizo hizo kuendeleza hadi likatokea gari, mashine ya kusaga, meli na hata baadaye ndege ..... wangekuwa wamejengwa kwenye concepts za uchoyo, tungeweza kuwepo hapa tulipo kama wanadamu???

  mapambano ya kifikra ni kitu cha muhimu sana, na lazima kiheshimiwe, kwa mfano ni nani huathiri system? je mwanzo wa kila kitu huwa ni mkubwa? (umeishasema teyari kuwa hata mtoto ataanzia alipoachia baba)....kitu ninachokiona hasa kwa wananchi na wanablogu, ni kuwa je kwa sababu sisi tuliteseka bila sababu ya msingi na watoto wetu wateseke hivyo hivyo? je tuache mambo yaendelee kuharibika na sie tupige makofi? je tunawezaje kumuepusha binadamu na machungu? hasa zaidi wale waliokwenda ughaibuni wanafikiria je, ni laana gani tumepigwa kule nyumbani? hii huuma zaidi baada ya kujifunza kuwa uharibifu unaotokea huko nyumbaniu unatengenezwa na sisi wenyewe!!!!

  tofauti na kizazi kilichopita ambacho kinaangalia kupona wao tu, fullstop, kizazi cha sasa huwezi kidanganya kirahisi, kizazi hiki kinaelewa kuwa hata kama unatembelea "Prado" na homu kwako ni raha masaa 24, bado kuna mjomba, shangazi, jirani ambao wanateswa bila sababu za msingi, kwa sababu tu fulani ndiye ameamua iwe hivyo, kizazi hiki kinapiga picha kule kilipotoka na kinapokwenda... kina uzoefu ... kwa ujumla hakitaki makosa yarudiwe....kizazi hiki kimeona wengine wanavyoishi kwenye nchi zao, kimeona uzalendo wao, je nyumbani kunani???

  lakini basi kama ilivyosemwa ni kwamba kuna haja ya kuongeza kasi ya kuelimisha raia ili basi wawe wanatumia fursa chache zilizopo kujenga na si kubomoa. uhuru wa kusema kutoa maoni au kuamua unapotumika vibaya ndio chanzo cha kufikiri kuwa kuna umuhimu wa kunyamazisha kundi fulani ikibidi kutumia nguvu ili mambo yaende sawa....umeishasema mfano kundi la wanamtandao wakakamata madaraka, ili kurekebisha mambo (tuombe ibakie kuwa hivyo)....

  ukweli lakini unabakia. ni lini Watanzania tutapenda kuwa serious na matatizo yanayotukabili? mbona tukiwa bado wakubwa michezo ya chekechea tunaipenda? je tunamtambua adui wetu kweli? ninahisi na ninateseka sana kama sio kuona tabu, nikifikiria siku utandawazi utapopanda chati bongo!! watu hawataki wala kujiandaa kwa hilo!! hadi leo wanagombana kule mbagala eti "Yesu na mohhamad SAW nani zaidi"!..ninadhani hawa wanaotukana basi tuwaonee huruma na tusijibishane nao...watakuja kugundua kuwa wanachofanya si sahihi... na watajifunza kuargue, pia jinsi ya kutumia fursa chache kwa umakini kutoka kwa wengine

   
 • Tarehe 3/21/2006 4:18 AM, Mtoa Maoni: Blogger nyembo

  hakika Mark sina cha kuongeza baada yako, nimesoma fikra za mwaipopo na wewe basi yatosha kuniwakilisha

   
 • Tarehe 3/21/2006 11:59 PM, Mtoa Maoni: Blogger Fikrathabiti

  Ndugu wanablog wenzangu wenye majina na hekima katika kuchanganua hoja na kutoa mchango mahsusi katika makala za watu, hili wimbi la kuongezeka mijadala ya kashfa katika makala inayofanywa na watu wasio na majina inanitia wasiwasi.

  Inakua vigumu kuamini mtu mwenye akili timamu anaweza kukaa na kutumia mda wake kuandika mambo yasiyo na msingi wowote katika jamii.Nikiwa naamini kua wenye busara bado mnatafakari hatua za kuchukua dhidi yao ili kulirudishia heshima gazeti hili tando tarajiwa inabidi tuendelee kua wavumilivu ili kuepusha majibizano na hao wendawazimu yasiyo na mantiki yoyote.

   
 • Tarehe 3/22/2006 11:46 AM, Mtoa Maoni: Blogger Jeff Msangi

  Makene,
  Ulichokiandika hapa ni kitu muhimu sana.Nikisema nakupa hongera itakuwa kama huko nyuma ulikuwa huandiki kama hivi.Kuchelea fikra hizo mimi nitakuambia mwendo ni ule ule ingawa kuongeza spidi sio vibaya.
  Nimefuatilia kwa kiasi hoja zinazotolewa na hao kina anyonimous.Zingine kwa kweli zinakera kwa sababu sio tu hazitusogezi hata hatua moja mbele bali zinakatisha tamaa vichwa vyenye dhamira njema.Lakini kwa bahati mbaya kabisa dunia si dunia bila mchanganyiko huu.Na siku hizi dhana ya uhuru wa habari ndio changamoto yetu mpya..yaani habari na maoni bila mipaka.Cha muhimu sana ni mimi na wewe kutambua wajibu na nafasi yetu katika jamii.Hapo ndipo panapokuwa na maji kujitenga na mafuta.Uhuru wa habari na mawasiliano usikukere hata kidogo.Kama unavyosema,cheza karata yako.Haya mengine ni pumba katika mchele!

   
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved