
HAPA Texas sasa ni kipindi cha kampeni za uchaguzi wa awali kabisa. Gharama zake ni kubwa maana hata Mbowe hafiki na Herikopta lake katika chaguzi hizi. Kwa Tanzania chaguzi nkama hizi ni zile za vitongoji, lakini huku wagombea nao hununua matangazo katika Televisheni na mmoja juzi aliniacha hoi alipokuwa akitumia ndege kabisa kupeperusha bango lake. Huu ni utamu kabisa hasa kwetu vichaa wa siasa.
Tumepata bahati ya kutembelewa na wabunge wa Texas mara kwa mara katika madarasa yangu. Humo nashukuru sibaguliwi maana kila mgeni akifika Profesa wangu anamtambulisha kwangu na kumueleza kuwa natoka Tanzania. Anampa walau picha ya kujitahidi kuweka mawazo ya kimataifa ili nami niambulie jambo. Mwisho unakuwa muda wa sisi kuwatwanga maswali. Nimewatwanga maswali kisawasawa na moja kubwa ni mafunzo ya aina ya siasa zinazotakiwa kufanyika. Kama unataka kuwa mwanasiasa unatakiwa kutafuta darasa hili. Baragumu anazo taarifa juu ya nini ukifanye na hii naitamka ili yakitokea mambo kinyume na matarajio yangu, basi muoneni Baragumu atawafafanulia!
Kibaya zaidi ni kila ninapopita katika kona ya barua zangu za mtandaoni. Nakutana na barua ya kijana wa sekondari moja toka eneo lenye ukame wa maji na njaa aliyeweza kufika katika intaneti na kupata wasaa wa kuniandikia waraka. Huyu kajituma kweli maana kipindi hiki chenye umeme wa mgao mtu kufika katika mtandao kunataka moyo kama unabisha muulize MIRUKO atakueleza! Kibaya na kinachonikera ni huyu kijana mbichi kabisa anayepaswa kuwazia masomo kuamua kuvuka nafasi ya mipaka ya nidhamu ya Afrika kwa kuniomba nimtafutie mchumba wa kizungu? Hivi hao mabinti waliojaa hapo Tanzania hamuwaoni? Kama mnashiriki kuwachukia dada zenu kiasi hiki nani atawapenda? Huyu kijana anawakilisha kundi kubwa linaloamini kuwa kitendo cha kuwa mweupe tayari ni kuukata kimaisha. Fikra hizi za kikoloni bado zinaikabili sana Afrika na kuna kazi kuziondoa.
Natulia, kidogo na kufungua barua nyingine. Hii inatoka kwa binti naye anataka nimtafutie mchumba wa kumuoa lakini awe mzungu! Najiuliza hivi kulikoni hapa? Kama dada zetu nao hawatupendi sisi tutaoa wapi? Ina maana kuna mapigano ya sisi kwa sisi au ni yale ya dhana ya kuchanganya mapenzi na mali? Nani kasema kuwa mzungu ni maana ya kuwa na mali? Kuna kazi hapa...
Wakati haya yakiendelea nakumbuka hadithi za mwalimu wangu nikiwa shule ya msingi. Alinambia, "Soma Makene, mabinti hawa watajilerta wenyewe." SIJUI NAYE ALIWAAMBIA AKINA DADA KUWA WASOME KWA KUWA WANAUME WATAJILETA WENYEWE! Nilifaulu shule ya msingi na kuingia sekondari, huko napo nikaambiwa soma mabinti watajileta. Sikuwaona wakijileta hadi nilipoamua nami kuwatafuta. Upweke wa ughaibuni mkali sana na ndio kisa cha mimi kuandika makala haya yaliyokuwemo kichwani kwangu siku nyingi. Nifanyeje wakati sina jiko na umri unakimbia kwa kasi mpya, nguvu mpya na ari mpya? Nguvu za mwili zinazidi na matamanio yanautesa moyo...nawaza huku kukiwa na hoja za kuchanganya kuhusu maamuzi ya kuheshimu tamaa ya mwili wangu au kuacha nafasi ya umma iniamulie matakwa yanayohusu moyo wangu.
Ok narudi nyuma tena, nikafika Sekondari ya juu na huko binti niliyempenda nilimfata na yeye akanitangazia kuwa ana "Boi Furendi" wake Chuo Kikuu. Nikaona bado hadithi za kusoma kwanza zinatakiwa kuendelezwa. Nilipofika Chuo Kikuu sikuwahi kusikia kuwa kuna binti anajisifu kuwa mimi ni "Boi Furendi" wake kwa kuwa nipo Chuo Kikuu. Nikavuta subira, upweke ukaendelea..
Hapo napo nikaamua kumtongoza binti, bila aibu sasa huyu wa chuo kikuu akanambia kuwa ana "Boi Furendi" wake Marekani. Sijui nani kawaloga hawa mabinti, kama ni kusoma si tayari nipo Chuo Kikuu au mwalimu wangu alimaanisha ni mabinti wa aina ipi watakaonifata. Huenda alimaanisha wale niliowaacha kijijini Sitimbi! Siwawezi tena wale maana hawajui losheni na pafyumu, na enjo fesi. Sababu hii inaweza kuwa chuku lakini hasa nao walishanisahau na kikweli hata majina yao sina sasa. Nikabaki kinywa wazi, siku si haba nikahitimu huko na kuja Marekani sijasikia kuwa kuna mtu ananitajataja kuwa mimi ni boifurend wake kwa kuwa niko Marekani. Zaidi ni hizi barua ninazopokea zinazonitaka kuwatafutia wao waume au mabinti wa kizungu. Hivi kila hatua nakumbana na vipingamizi hivi, kuna swali lingine hili limefika sasa hadi nalichukia. Sidhani kama lina lengo la kiubaguzi lakini kwani mahusiano kati ya mtu wa rangi moja na nyingine yanaihusu jamii katika lipi? Hivi kama ni mke nitakayeamua kuoa mimi anaihusu jamii nini, hawa wanaonitaka kuwatafutia mabinti na waume wa kizungu je nao ni wabaguzi wa rangi au wanataka kuvuka mipaka ya rangi zao? Je kwa nini sasa huyu aniulize bila soni swali hili, JE UMESHAOA MZUNGU?
Ina maana Makene wale mabinti wa ndanda sekondari,warembo wa complex mkwawa na mamiss wako wa UDSM umewasahau au unataka tuamini kua huna bahati katika hii fani???
Ninayo mengi ya kusema juu ya mtandao wa wanawake wako lakini naashia hapa kwanza nikisubiri michuzi aweke picha zako ulizokua nao hao mabinti kwenye fuko za coco,kipepeo na land mark hadharani!!!!!!!!!