Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Friday, February 17, 2006
JAMALA LANGU LI WAPI?
NATUMIA shairi hili kulipa deni nililotoa katika dirisha la maoni ya Harakati. Lakini pia shairi hili nililolitunga nikiwa Ndanda linajibu tungo za Malenga Mkwinda na Nyembo ambao wote wamekaa kimya kusubiri nijibu tambo zao kabla ya kuandika makala nyingine katika Baraza zao.


Nimekosa kitu gani, mimi malenga mfupi?
Mwanitia mashakani, enyi shetani wakopi
Pingu mmenifungani, jamala langu li wapi?
Licha nikuta roshani, mwanila kama makapi
Shetani hebu semeni, kwa nini mwameza pipi!
Makware ninyi haini, iweje mnipe nepi?

Hapa nipo gurufuni, semeni acha kugwaza
Gunge mmenipendeni,mwataka niguruguza
Bado nipo upofuni, Munkari kujiitiza
Mwataja mimi haini, kwa lipi nilotendeza?
Enyi Nduli maskini, mbona mwapenda jiponza!
Wakili nimefateni, lazima tawatuliza
Licha letwa kizimbani, jamala langu li wapi?

Malenga sikilizeni, kisa cha kuajabia
Mimi kuishinda fani, latosha nikamatia?
Kasema mtu razini, wizara yamtambua
Hataki nitambueni, fani mimi jifunua
Shida pate sabihini, weledie tangazia
Kapiga saksafoni, mimi nilipotulia
Licha letwa kizimbani, jamala langu li wapi?

Yanikumbusha zamani,Yesu waliposhikia
Licha wagonjwa ponyani, walo njaa kushibia!
Macho waliyafumbia,wema jamala lipia
Nilianza kwa kubuni,watu kufurahishia
Huyu aso sarakani,mabomu kanitupia
Licha jifanya sajini,ndiye alinishikia
Licha letwa kizimbani, jamala langu li wapi?

Mwanitia machozini, kila napofikiria
Uwazi siutamani, tazama nimeachia
Sitaki fanya sakia, hapa kupumzikia
Sasa ninatesekani, ukweli kufichilia
Vipi niwe matatani, kwa fani nilojulia?
Japo ningali zuoni, matope menitupia
Licha letwa kizimbani, jamala langu li wapi?

Nawajua mashetani, wivu mwausumbukia
Mimi sinyoi sekini, kichwa nalinganishia
Vita vyangu ogopeni, majini mtajutia
Japo bado mdogoni, rufaa meshakatia
Sihiri zenu toeni, kichaa nawaapia
Kesho msije juteni, kalamu kuwachapia
Licha letwa kizimbani, jamala langu li wapi?
 
© boniphace Tarehe 2/17/2006 12:15:00 PM | Permalink |


Comments: 3


 • Tarehe 2/18/2006 8:02 AM, Mtoa Maoni: Blogger Rashid Mkwinda

  Du! Makene ndivyo ulivyokuja? na agenda hiyo ngoja nikuvutie pumzi lakini sio mbaya, naona deni lako umelipa, tuendeleze libeneke.

   
 • Tarehe 2/18/2006 3:44 PM, Mtoa Maoni: Blogger Jeff Msangi

  Ushairi bab kubwa.Malenga,kazi kwenu,hivi na mie nimo??

   
 • Tarehe 2/20/2006 5:57 AM, Mtoa Maoni: Blogger nyembo

  nimeona, kaka nalazimika sasa kukaa mkao wa kula!maana kazi yako si mchezo! nimepokea ujio wako na sasa ninaahidi kudili nawe mpaka saa ya mwisho ambayo TIME KEEPER...atakapo sema saa ya kwenda nyumbani imefika ngoja nigonge kengele!

   
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved