Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Thursday, February 23, 2006
BARUA YA KOMREDI IDDI SIMBA KWA WAZAWA
NIMEPOKEA waraka huu, naona niubandike ili nisichafue kabisa waraka wenyewe na kisha kukupa fursa msomaji wangu kuweza kuingia au kuchangia mjadala huu. Mawazo usiyoyapenda au kuyaamini katika Waraka huu hayana uhusiano wowote na KASRI LA MWANAZUO hivyo tazama umuhimu wa agenda lakini maelezo ya kupalilia agenda hii waweza yachukua au yaweka kando. Umuhimu wa kutanua nafasi ya uchumi wa mzawa wa Afrika na Tanzania ni kauli mbiu ya KASRI LA MWANAZUO na hii ni imani yangu siku zote. Nitashukuru kama nawe utatafuta taarifa zaidi na kuungana na Komredi Simba ili kumkuza Mtanzania mzawa ambaye amegeuka mtumwa wa kiuchumi katika nchi yake kwa miongo mingi

Kwa kupitia vyombo vya habari inawezekana ukawa umeona kuna kundi dogo la wabunge wa kipindi kilichopita waliokutana Dodoma tarehe 27 Desemba 2005 na kuamua kuunda Taasisi walioipa jina la “TANZANIA ECONOMIC FORUM”.

Kwa heshima, napenda kukuarifu rasmi kwamba jambo hilo lilitokea, na kwamba Taasisi hiyo inakusudiwa iwe ya kuwaunganisha wananchi wa kila aina wataohamasika kujiunga nayo.

Madhumuni ya barua hii ni kujaribu kukushwawishi, kwa namna ya peke kwako, uwe mmoja ya waasisi wa chombo hiki, ambacho kitashugulikia zaidi masuala ya kiuchumi kwa jinsi yanavyogusa maisha ya Mtanzania wa kawaida.

Katika kipindi cha miaka kumi ya awamu wa tatu ya utawala wa Mheshimiwa Rais Benjamin Mkapa, nchi yetu ilishuhudia mambo makubwa matatu yaliyoathiri hali ya maisha ya Mtanzania.

Mabadiliko ya mfumo wa kisiasa na kiuchumi ambayo yalileta demokrasia ya vyama vingi pamoja na utekelezaji wa sera za uchumi.

Ndani na muongo huu nchi ilikabiliwa na misukosuko ya kisiasa baina ya vyama tofauti na ndani ya vyama vyenyewe. Kadhalika kipindi hiki kilionyesha dhamira ya serikali kujitoa katika umilikaji wa rasilimali za Taifa na udendeshaji wa uchumi. Sekta binafsi ilipewa fursa ya kushika hatamu na kununua mashirika yaliyokuwa ya umma

Juhudi za kufufua Ushirikiano wa Africa ya Mashariki pamoja na kubadilisha mfumo wa ushirikiano na nchi za kanda ya kusini mwa Afrika.

Ni Katika kipindi hiki hatua za kisheria zilifikiwa na kuielekeza nchi yetu kwenye soko la pamoja na nchi za kanda ya Africa Mashariki (EAC) na nchi za kusini (SADC)

Utandawazi ulipamba moto kwa kasi kubwa zaidi katika kipidi hiki cha utawala wa awamu ya tatu.

Athari za mtindo wa biashara huria ya kimataifa zilijitokeza kwa nguvu sana wakati huu. Kushiriki kwa Rais Mkapa katika tume ya kongamano mbalimbali za kimataifa sio tu kuliipatia heshima nchi yetu, lakini pia kuliwafungua macho baadhi ya Watanzania juu ya ushindani mkali wa kibiashara na kiuchumi unaotukabili na nchi zingine.
Haya Mambo matatu hayakuwa mapya kabisa. Yote yalikuwapo siku zilizopita kwa kiwango Fulani, lakini yalipata nguvu sana kuitekelezaji katika muongo huo.

Athari iliyojitokeza zaidi kwa maisha ya Tanzania, Juu ya mambo haya matatu, ilikuwa ni kiuchumi. Serikali za awamu zilizopita kwa vipindi mbalimbali zlijaribu kubuni na kutekeleza mbinu za kusaidia.

Pamoja na juhudi za serikali zetu zilizopita, wabia wetu wa kimataifa nao walitoa fursa mbalimbali ambazo zilikusudia kutuwezesha kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi. Mifano michache itafaa kuiangalia :-

“Open General License” – OGL ( Tangu awamu ya Kwanza)
“Commodity Import Support” CIS
“Debt Conversion Programme”
“Microfinance Policy”
“Economic Empowerment Policy”
“MKUKUTA, MKURABITA, AGOA, EBA N.K”
Sambamba na hayo, awamu ya tatu ya Rais Mkapa ilijitahidi sana kujenga misingi imara ya uchumi wa Jumla (Macro-economy). Baada ya kuimarishwa utaratibu na tabia ya kulipia madeni, kuongeza ukusanyaji wa kodi, kudhibiti mfumuko wa bei na thamani ya sarafu ya Taifa, kuboresha miundo mbinu ya usafiri na mawasiliano, na baada ya kuonyesha dhamira ya kuipa nguvu sekta binafsi na kuitambua kama mtambo wa kuzalisha mali na kukuza pato la Taifa, wawekezaji walivutiwa na kuanza kuwekeza katika sekta mbali mbali za uchumi.

Serikali ya awamu ya tatu ilifanya marekebisho makubwa katika sekta ya fedha na kuvutia mabenki ya nje kuingia nchini. Huduma za aina hii zilisisimua kwa kiasi kikubwa biashara ya kimataifa katika sekta hasa za madini, Utalii na uchuuzi wa bidhaa na nje na ndani.

Haya yote ni mazuri na lazima yaendelezwe kama ambavyo Mheshimiwa Ras Kikwete ameahidi kuyaendeleza katika awamu ya nne. Lakini ni vema tutambue kwamba mafanikio haya kwa kiasi kikubwa sana yamewagusa Wananchi wachache waliomo katika sekta rasmi ya uchumi.

Watanzania wengi bado wana hali duni ya kimaisha na hawajaguswa na faida zilizopatikana katika sekta ya uchumi wa kisasa. Rais Kikwete ameahidi juhudi za kuinua hali ya maisha ya Watanzania kwa kuwaingiza kwenye njia kuu za Uchumi wa kisasa.

Tunaamini kwamba, kwa misingi iliyokwishawekwa katika awamu zilizopita, hasa awamu ya tatu kiuchumi na tukizingatia neema za maliasili ambazo tunazo nchini, awamu ya nne imekuja na ari ambayo inaweza kabisa kutimiza matarajio ya wananchi. Lakini uwezekano wa kutimiza matarajio hayo utategemea sana juhudi za tawala katika ngazi za serikali kuu, Tawala za Mikoa, Mamlaka mbalimbali za dola, Taasisi mbalimbali za kiraia (Civil society) na hasa juhudi za wananchi kwa jumla wao.

Tukienda pamoja na kushirikiana na kwa kueleweshana juu ya vita vya kiuchumi inavyoikabili nchi yetu, ni dhahiri Serikali ya awamu ya nne itaweza kutimiza ahadi zilizotolewa kwa wananchi. Neema za maliasili tunazokusudia hapa ni pamoja na watu wenye fani mbalimbali, na wenye moyo wa uzalendo unaowahurumia Wananchi masikini wanaotafuta riziki zao katika sekta ya uchumi isiyotambulika.

Ili tutambue uzito wa tatizo la maendeleo ya wananchi wa Tanzania, ni vema tuchambue jinsi tulivyo!

Katika Wananchi takriban milioni 35, nusu yetu ni wazee wenye umri wa miaka 65 na zaidi, pamoja na watoto na Vijana mpaka umri wa miaka 18. Waliobaki ni wananchi milioni 17.5 wa umri kati ya miaka 18 na 65 ambao ndio nguvu kazi wanaobeba mzigo wa kuwatunza watoto, Vijana na wazee.

Takwimu na taarifa rasmi zilizofikishwa katika kamati ya Fedha na Uchumi ya bunge mwaka jana zilionyesha kwamba wananchi wanaotambulika katika sekta rasmi ya uchumi ni milioni mbili tuu.. Hawa ndio wanaofanya kazi za Kuajiriwa na ujiajiri. Ndio wanaolipa kodi kwa utambulisho rasmi, pamoja na kutumia huduma za kibenki na fursa mbalimbali zilizoandaliwa na dola kwa ajili ya maendeleo ya sekta binafsi

Wananchi milioni 15.5 wanafanya kazi za kila aina, katika sekta zote za uchumi bila kujulikana na vyombo vya dola. Hii ndiyo sekta kuu ya pili ya uchumi usiojulikana kwanjia sahihi na rasmi. Wananchi hawa wana rasilimali zao ambazo hazitambuliki na kwa hiyo haziwasaidi katika maendelo ya kisasa. Hawakopesheki, hawalipi kodi na hawawezi kutumia fursa nyingi zilizoandaliwa na serikali kwa ajili ya maendeleo yao. Hata hivyo wanaona jinsi nchi ilivyobadilika sura kwa maana ya majengo mapya, mabarabara, magari, umeme, usafiri na mawasiliano.

Wananchi hawa milioni 15.5 wanatambua faida zinazopatikana katika sekta rasmi. Wachache wanaojaonja anasa za utandawazi kwa matumizi ya simu za mkono, TV, na radio. Lakini wengi wao bado wako mbali sana na faida za uchumiwa kisasa ambazo kama tunavyoona zinawagusa wananchi milioni mbili tuu. Na hata hao milioni mbili, ni wachache miongoni mwao ambao ni wachezaji wa kweli katika shuguli za uchumi wa sekta rasmi.

Katika Kipindi cha mwaka uliopita wa fedha 2004/2004, idadi ya akaunti katika mabenki yote nchini ilikadiriwa kama laki tatu tuu (300,000). Sehemu kubwa sana ya hata wao wananchi milioni mbili waliomo katika sekta rasmi ya uchumi hawapati faida ya huduma za benki. Nao pia hawakopesheki katika mazingira yaliyopo hivi sasa.

Suala la mzingi, ambalo ni lazima tulipatie jawabu haraka, ni jinsi tutavyoweza kuvuta nguvu zetu za kitaifa ili nchi yetu ikabiliane na ushindani wa kibiashara na kiuchumi katika mazingira haya ya utandawazi.

Tanzania imo vitani. Ni vita ya kiuchumi inayolazimisha tufungue mipaka yetu, siyo tu kwa jili ya bidhaa za kutoka nje lakini pia kwa ajili ya wafanyakazi na wawekezaji ambao wanavutiwa na fursa nyingi za kujitajirisha zilizomo nchini mwetu.

Hii ni hali ambayo haiepukiki na wala si busara kujaribu kujiepusha nayo.

Tunachotakiwa kufanya haraka sana ni kuwashitua wananchi wetu, kuwasisimua na kuwaanda kwa vita kali ya kiuchumi. Mahindano yetu na nchi zingine yanatutaka tuzalishe mali katika sekta zetu zote za uchumi zitazoongeza pato la Taifa kwa kasi kubwa zaidi.

Tanzania ina nafasi na fursa ya kufikisha katika masoko ya Dunia bidhaa zinazotakiwa duniani. Tusipozalisha bidhaa hizo sisi wenywe pamoja na kushirikiana na tuwatakao kwa mtindo utaolinda maslahi ya taifa letu hivi sasa, baadaye (na baadaye hii ni miaka kama kumi na tano hivyi) Dunia itatulazimisha tufanye kama Dunia inavyotaka.

Kazi ya kuwatayarisha wananchi kwa mapambano haya ya kiuchumi, na kazi ya kuvuta nguvu zote za Taifa kwa ajili ya vita hii, haiwezi kufanywa na Serikali peke yake, Bunge peke yake, Vyombo vya wafanyabiashara au kundi lolote peke yao.

Tunadhani ni bora tuunde chombo kitachowajumuisha watu wa fani mbali mbali, makundi ya kila aina, viongozi wa Taasisi za kisiasa, Kibiashara, kiroho na taaluma, Chombo ambacho kitachambua kwa undani mipango yote na fursa zilizoandaliwa na serikali kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kujiendeleza. Kwa mfano, ni watu wachache mno wanaojuwa habari za MKUKUTA, MKURABITA na mifuko mbali mbali yenye malengo ya kuwasaidia wananchi.

Chombo hiki kitatafiti taratibu zote na fursa zote zilizowekwa na serikali yetu, na hata Taasisi za kimataifa, ambazo zinakusudia kutuwezesha kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi. Taarifa sahihi juu ya yote haya itakuwa inatolewa kwa namna ya kuwaelimisha watu ili waweze kuchacharika katika sekta zote za Uchumi.

Tunakusudia kuwashwawishi wananchi wanaharakati wa maendeleo, wajiunge na chombo hichi ambacho madhumuni ya msingi ni kuhimiza maendeleo ya wananci kwa kujenga taratibu sahihi za ushirikiano endelevu baina ya serikali na watu.

Tarehe 18 Machi 2006, Jumamosi saa nne asubuhi tutakutana katika ukumbi wa hoteli ya Royal Palm Movenpick, Dar es salaam

Ni maombi na matumaini yangu kwamba utakubali kujiunga na chombo hiki cha kiraia ambacho azma kuu ni kujenga ushirikiano wa dhati na vyombo vya dola ili kwapamoja tupigane vita vya kuondoa umasikini na kujenga uwezo wa nchi yetu kwa mashindano ya kiuchumi na mataifa mengine. Kujiunga kwako nacho kutakipatia chombo hiki heshima na kutuwezesha tuaminike na tuwe msaada mkubwa kwa serikali katika juhudi za kuwaletea wananchi maendeleo.

Tunamini kwamba, pamoja na wewe, idadi kubwa ya wananchi wasiopungua mia moja watakuwa amejiunga na kulipia ada za uanzilishi wa Taasisi hii. Rasimu za katiba inandaliwa ili baada ya kukubaliwa na kikao, ambacho kitachagua uongozi, tutachukuwa hatua za usajili na kuanza shuguli zitazokusudiwa.


Idd Simba
(Mwenyekiti wa Muda)

Kwa maelezo zaidi wasiliana nasi info@tanzaniaeconomicforum.org
--
 
© boniphace Tarehe 2/23/2006 09:15:00 AM | Permalink |


Comments: 3


 • Tarehe 2/25/2006 4:20 AM, Mtoa Maoni: Anonymous Anonymous

  Naam,

  Nitaichapisha ili niisome kwa ufasaha zaidi.

  F MtiMkubwa Tungaraza

   
 • Tarehe 2/25/2006 5:57 AM, Mtoa Maoni: Blogger mwandani

  Nimesoma. Nadhani hili ni wazo zuri sana. Nitanukuu kwenye waraka wa MTU KWAO panapozungumzia nia ya mwafrika au mtanzania ughaibuni:

  "Pengine kundi kubwa katika mseto huu matata wa mwafrika anayevinjari ughaibuni ni lile lenye visifa vyote vya hapo juu kwa reja reja na kwa vipindi tofauti.

  'Kundi linalounganishwa kwa dhana kubwa moja – wote ni waafrika na wote wana nia ya kufanya kweli lakini hawajakamata mkondo. Kama mto uliofurika baada ya mvua kali nao wamejaa njozi nyingi tu."

  Pengine huu ndio wakati wa kuweka mambo sawa, huu ndio wakati wa kukamata mkondo, kushiriki kwa vitendo.

  Barua hii imenitia moyo na hisia kali. Shukrani.

  Tufuatilie kwa karibu.

  (Nadhani hii barua ni ya kweli na siyo 'kanyabwoya' au 'spam')

   
 • Tarehe 3/08/2006 4:23 AM, Mtoa Maoni: Blogger Michuzi

  hapana. ni barua ya kweli na si kanyabwoya. mie nna nakala yake halisi na nishaongea na wapambe wa m'kiti na wamethibitisha. kwenye kikao nategemea kwenda, ntawapasha yatojiri...

   
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved