Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Tuesday, November 08, 2005
WIKI YA KIMATAIFA TEXAS: TANZANIA BILA BENDERA
WIKI hii niko katika harakati za kuitangaza Tanzania. Hii si ajira yangu kwa sasa lakini kuna wanaokula mishahara ya kodi zetu huku ili wafanye kazi hii. Nimekumbuka kuwa fursa hii ina majukumu mengi lakini ushirikiano wa Ubalozi wa Tanzania, Marekani ulinikatisha siku ya kwanza tu, Wajua sababu, eti wana bendera tatu tu ambazo wanaazimisha wakazi zaidi ya elfu kumi toka Tanzania wanaoishi hapa Marekani kwa shughuli za kuitanga za Tanzania.

Kwa wasioifahamu Marekani vema, tambua kuwa Marekani ina nchi 50 zilizoungana na kila moja ina sheria na taratibu zake. Mfumo wa elimu wa huku, umefunga uwezo wa kuona yanayotendeka katika mataifa mengine, na akipatikana kalubandika kama mimi hapa kwao ni furaha tele. Sasa wiki ijayo nitakuwa na mhadhara wa zaidi ya wananchi elfu kumi na tano kutoka nchi mbalimbali.

Unakumbuka sakata la vifaa vya serikali ikiwemo hiyo Bendera. Bado hujasahau kauli ya Waziri Omari Kaburi juu ya uhalali wa yeye na wafalme wenzake kumiliki vitambaa hivyo! Sikuchukia lakini nimechapisha yangu kwa karatasi kutoka katika mtandao, nitaitumia.

Pembeni yangu atakuwepo mwakilishi wa Saudi Arabia akiwa na yake kubwa, atafuata huyu wa Mexico, Ufaransa na Ujerumani na ile ya Marekani itapambwa kila kona. Mimi nitakuwa kati yao na kikaratasi chenye kufanana na bendera. Natamani nisikitumie au nichukue hii ya Marekani tu lakini moyoni naumia.

Sitoki katika familia za wafalme, hivyo nikikutwa na bendera katika Begi langu naweza kutoruhusiwa kupanda ndege. Niliogopa hilo maana siunajua kuja majuu namna kila mtu anavyotamani. Nilishaonywa mapema kabisa juu ya nyaraka za wafalme wa Tanzania, nikatulia kimya! Hapa sasa nasikia naweza kununua bendera ya Marekani yaani lile kubwa analokuwa nalo Bush wakati akizungumza. Nasikia ni zuri sana kupamba nyumbani, pembeni yake nitapamba maandishi yangu ya Gazeti la Mwananchi! Hivi vitakuwa viwakilishi vyangu maana sidhani kama hata mjomba wangu anaweza kumudu tafrani la mabadiliko ya kura za wananchi na zile za tume ya uchaguzi.

Hawezi kushinda kura za tume, achilia mbali uwezo wake katika kutoa rushwa iliyobatizwa jina la Takrima. Napumua sasa, nina jukumu la kuandika taarifa za Tanzania na masuala ya elimu na utalii. Naogopa maana sikuwahi kufika katika Mbuga yoyote. Shule za Tanzania hazina utaratibu wa wanafunzi kutembelea mbuga na kama upo unatakiwa kulipia gharama kubwa na mimi sikuwa nazo hali iliyonifanya wakati fulani kushinda njaa nikijifanya nimeshiba hapo Chuo Kikuu Mlimani!

Nimekumbuka, nitazungumzia Afrika, hii haina haja ya Bendera maana ninayo aliyonipa mama. Unaijua hii, ni ngozi yangu, nitasema juu ya ukandamizaji wa Mtaifa makubwa dhidi ya ngozi yangu. Nitasema kuhusu kununua viongozi wetu ili watekeleze miradi waipendayo hawa wakubwa. Nitawapasha kuhusu kutochangia demokrasia ya kweli ulimwenguni. Sitasahau kuchomeka mfano wa mauaji ya Iraki japokuwa hayako katika mada yangu!

Nimesahau, nitakumbushia suala la kuwakumbusha kuja Afrika, watazame namna wafalme wetu wanavyoishi kwa anasa huku raia tukifa. Nitawakumbusha kufanya hivyo mapema halafu waseme kama si haki wananchi Afrika kutwangana ngeu baada ya kuona wamechoka kumalizwa na hawa wazungu waliojivika bendera ya bara la Afrika.

Niliwahi kuona mtoto wa katibu kata mmoja akivinkwa nepi ya bendera ya chama kimoja wakati ule. Huyu sasa anajinadi hasa kuzaliwa katika hicho, Bendera hizo kalieni, mapambazuko yanakuja kama upepo na hakuna wa kuyazuia, amkeni wanafunzi ni wakati wa kuandika makala mpya!
 
© boniphace Tarehe 11/08/2005 02:00:00 PM | Permalink |


Comments: 0


   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved