Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Tuesday, November 15, 2005
NIMEFUNIKA KOMBE
NIMETOKA muda si mrefu kuchonga kuhusu Afrika na kidogo Tanganyika. Maelezo yangu yameuteka umma kama nilivyotarajia. Niliyekuwa naye ni huyu Jamaa kutoka Saudi Arabia, Kizungu chake hafifu hivyo alianza kumwaga sera yeye.

Alipomaliza nikaachiwa fursa, nikawauliza wapiga kura, samahani wasikilizaji kisha wakacheka kutokana na matani yangu na hapo nikaanza kulonga juu ya Historia ya Kiswahili na baadaye kuchonga mambo mwengi ya Afrika. Sikuona noma kumaliza kazi hiyo chini ya dakika kumi ili nipate kipindi nikipendacho, maswali na majibu!

Kumbuka na tena nataka ukumbuke, si maswali na majibu wanayoulizwa wafalme wa Bongo. Maana yale yanatakiwa kuandikwa miezi sita kabla kisha kutafutiwa majibu kabla ya kujibiwa hadharani. Yangu ni ya hapa kwa hapa na huu ni uwanja niupendao sana, sijui mnakubaliana nami jamani?

Kuna hili swali la namna tunavyoifikiria Marekani juu ya nchi zetu. Kaliuliza Profesa mmoja. Anaanza kujibu huyu jamaa wa Saudia na kupigia mayowe ugaidi huku akiapa kuwa magaidi si waislamu. Nachukua kipaza sauti na kuanza kuponda vyombo vya habari vya huku kuiandika vibaya Afrika. Nachonga na kuwakumbusha namna wanavyosahau mambo muhimu kama Iraki na Katrina lakini wanajirusha na vita na njaa katika Afrika.

Kabla sijamaliza kuna kajamaa kamenyoosha mkono. Nakaruhusu kutwanga swali jingine. Kanauliza kuhusu World Bank na IMF na athari zake katika Afrika. Hapa naamsha fikra mpya za wasilikizaji kuhusu kutamka bayana kuwa vyombo hivi vinalihujumu Bara la Afrika. Nawakumbusha mikataba feki wanayosainisha Wafalme wetu kiasi kwamba inatughalimu uhai kulipa madeni. Nakumbushia madeni ya Tanzania tangu uhuru na pia nawakumbusha kuhusu geresha ya kufuta madeni na kubainisha kuwa haina faida kabisa kwa Afrika.

Nimekumbuka, kuna wakati nilijibu swali na kumtetea Mkapa, nilitamka naye apewe nafasi sawa katika vyombo vya habari vya huku kama apewavyo Bush. Nawataka hawa jamaa wamtambue huyu kuwa naye ni Rais na pia kuwa Bush hatawali ulimwengu. Wanacheka na kutingisha vichwa, kisha nawakumbusha demokrasia ya Tanzania, ghafla nabanwa na kigugumizi kuhusu Zanzibar na kisha kuiepa habari hiyo.

Nilipomaliza nikaanza kufuatwa kama kawaida na Waandishi wa gazeti la Rumbo Valley na wengine. Utadhani mwanasiasa kabisa maana nimetinga tai yangu ya Bendera ya Taifa. Usiniulize niliipataje maana wasije wakajua wale Wafalme wakaiathiri familia yangu huko Bongo. Hizi huvaliwa na Mawaziri na Wabunge wa ufalme wa Tanzania. Wengine ni watoto wao na ndugu wa karibu. Niliipata kama miujiza hivi na niliitunza ili niivae siku hii. Pia nimeweka beji kali yenye bendera ya Marekani na Tanzania. Ama kweli kwa pamba hizi navutia lakini je suala la mkataba wa Muungano hiyo dokumenti kaificha nani maana nataka kulichukulia suala hili kuwa la kisiasa kampeni zikizinduliwa tena.
 
© boniphace Tarehe 11/15/2005 12:20:00 PM | Permalink |


Comments: 6


 • Tarehe 11/15/2005 6:09 PM, Mtoa Maoni: Anonymous mwaipopo

  Hapa kwenye dokumenti za muungano patamu kwelikweli. Sijui kawapa nini wazo hili wale wanzanzibari 10. Kigagasiko kilichopo sasa katika kutowapa dokumenti kinanifanya nidhanie kuwa yawezekama ama hakukua na maandishi kabisha ulu mwaka wa 1964 na hivyo tumekua tukipumbazwa miaka yote hiyo. Ama wakubwa fulani katika wakati fulani waliyakiuka yaliyoandikwa na kutiwa saini hivyo basi wanaogopa vidole vya kuambiwa: "Mbona hapa hamkufanya kama ilivyoandikwa?"

  Hivi inawezekanaje mkataba ule ulioandikwa na kufikiwa katika nchi ndogo ya Bongo (sio Umoja wa Mataifa Marekani) ufanywe siri namna hii. Jipu liko katika maungo ya sirini sasa ni sharti daktari alione wazi litibiwe.

   
 • Tarehe 11/16/2005 1:14 AM, Mtoa Maoni: Blogger Indya Nkya

  Hongera kwa kuwapasha hao. Hasa hili suala la IMF na WB. Vyombo vya ajabu sana vinavyohamasisha demokrasia wakati vyenyewe vimetawaliwa na udikteta wa hali ya juu. Kiini macho cha madeni kusamehewa nacho ni vizuri kama uliwapakilia vizuri. Safii kabisa

   
 • Tarehe 11/16/2005 6:43 AM, Mtoa Maoni: Blogger Boniphace Makene

  Hizo Dokumenti zitolewe na baada ya hapo tunazitafutia wakaguzi wa kimataifa ili zisigushiwe! Zapaswa kuonekana nzee na zaweza pimwa kwa Carbon 14 ili kuthibitisha kweli kuwa ni za kipindi hicho.

  Baada ya hapo tunatazama kama hazikufanyiwa ilivyotakiwa, ili tuhakikishe hakuna ulaghai katika haka katamthiliya ka Muungano.

  Idya, nimewapasha, walibaki kimya na nilitazama wakiangalia chini, sikubakiza chochote niliona muhimu kutimiza nafasi yangu.

   
 • Tarehe 11/16/2005 11:21 AM, Mtoa Maoni: Blogger Indya Nkya

  Hakuna kitu kibaya duniani kama mtu kusaliti nafsi yake. Kwa hivyo kila upatapo nafasi inabidi umwage yale unayojua na unayoamini ni sahihi. Kama yatakasirisha wengine ni sawa lakini umeitendea nafsi yako haki. Endeleza kuna siku vitaingia masikioni mwa wengi. Nashindwa hata kuchangia kuhusu huo uigizaji wa hati za muungano. Kama si igizo tuiteje? Makene tafuta jina la huo mchezo. Halafu nasikia hakuna kitu kibaya kama kutunga igizo na kulicheza mwenyewe.

   
 • Tarehe 11/23/2005 5:31 AM, Mtoa Maoni: Blogger mloyi

  Tanzania bila bendera, ndivyo tulivyo, tunasema utanzania wetu kama tutafaidika, tuambie ukweli boniphace hivi wewe ukiwa mbali hivyo na nyumbani unakosaje bendera yako? au ilikuwa ni sehemu ya mafunzo yako kuongelea kuhusu Tanzania na soi kawaida yako kufanya hivyo? naona chumbani mwako unayo bendera ya marekani na ya uingereza.,
  Somo jingine lianzie hapa, ninabandika nakala kwenye kibaraza changu(motowaka.blogspot.com) unaweza kupitia na kuisoma baadae kidogo.

   
 • Tarehe 11/25/2005 5:11 PM, Mtoa Maoni: Blogger Ndesanjo Macha

  Nakubaliana nawe. Unaweza kuitetea Afrika na Tanzania usiku kucha ila ikifika kwenye suala la demokrasia (au mkumbokrasia kama anavyoita Nkya) inabidi upate kigugumizi. Hasa kule Zanzibar...
  Asante kwa kutupasha yaliyojiri huko.

   
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved