Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Wednesday, November 23, 2005
NAWASHUKURU SANA
SAFARI yangu kuja Marekani imefungua nami kutambua umhimu wa kushukuru wenzangu. Hii ni sikukuu kubwa sana waweza isoma hapa. Ninaishukuru familia ya Mzee Benard Makene na wote ninaoungana nao na kile kinachobainishwa kuwa undugu wa damu. Binadamu wote ambao siku zote kwangu mu sawa licha ya rangi zenu. Nawashukuru sana mliowahi kuchangia fadhila zenu na kushindwa kurejeshewa nami. Natambua mmefanya haya kwa sababu tu ya undugu wenu na sio stahiki yangu kutendewa nanyi hivyo.

Nishukuru walioweka taaluma hii ya Blogu na sasa naweza kuandika na kuacha jina langu kuwafikia wengi. Nitaje huyu mmoja kwanza maana mchango wake katika Blogu ni mkubwa kuliko anavyofahamu. Ndesanjo Macha Niendelee na safari, rafiki zangu mpo wengi hasa wasomaji wangu katika maandishi yangu yanayochapishwa na Gazeti la Mwananchi, waandishi wa Habari wenzangu, Wanablogu na Walimu wote mliopata kufundisha kichwa changu na pia kunipa utajiri huu ninaolinga nao sasa.

Niwashukuru wanafunzi wangu, poleni maana mlitaka kukaa na mwalimu wenu muda mwingi lakini amekuwa na tabia ya kurukaruka kama chura, hatulii kila siku yuko katika njia hii mara ile. Niwashukuru wanafunzi wote mliopata kusoma nami tangu pale aliposomea Nyerere, Mwisenge hadi aliposomea Mkapa, Ndanda, sijasahau Mkwawa, TSJ na Mlimani na sasa Texas Pan American.

Shukrani zangu za dhati zaidi zikufikie wewe unayedhani huu mdogo sana katika kuchangia mafanikio ya ulimwengu. Niwashukuru pia raia wa nchi za nje ambao pia wamekuwa mbele kurutubisha fikra zangu nikianza na serikali ya Marekani chini ya State Department inayoratibu ukaaji wangu hapa sasa. Rafiki zangu wa Canada, Mellisa, Ernesto, Renee na wengine vile vile mlio Mexico salamu sana. Natambua nguvu zenu katika kuchimbua almasi ya masuala ya nje.

Ntambua pia uwepo wenu wakazi wa Musoma Vijijini, sijafanya kazi yoyote ya kuunganisha nguvu zenu na zangu lakini siku si nyingi nitakuja huko. Natambua mmnilea tangu nikiwa mdogo na sasa umri wangumaridhawa ila bashasha lile nililokuwa nalo lazidi kutoweka jinsi nionavyo kero zile mlizoahidiwa kutatuliwa tangu nikiwa mdogo bado zinanisubiri. Nitafika, nitafika na sina namna ya kuja kuanza safari mpya yenye uvumilivu, unyenyekevu na upole kwenu mlioishi tabu hizo kwa karne sasa.

Tanzania na hata Tanganyika yapaswa kutambua kuwa ina kazi ya kuiweka Afrika katika ramani. Ilishindikana wakati huo lakini safari yatakiwa kufikiwa hata kama hakutakuwa na taifa liitwalo Afrika. Tunatakiwa kuanza safari hiyo sasa na kumbukeni nafasi ya wakati huu uliopo. Nasikia Watanzania mnapiga kura siku si nyingi. Hapo kuna kura za aina mbili, mosi zile za wananchi na pili zile za Tume ya uchaguzi. Kuna haja ya kujifunza tunayoyaona Kenya kuwa kura za TRume ya uchaguzi hazitatufikisha mbali sana na badala yake tuangalie namna ya kupata kura za wananchi. Slamu wanachama wa chama changu, Kasri la Mwanazuo. Nakusalimuni na poleni kwa makal ndefu sasa lakini safari ya kula fikra haitaishia hapa chukueni nafasiyenu.

Nitoe wito na ombi lwa Jalia, mwenyezi Qudusi, tambua kazi za mwanao na boresha fikra zake ili ajue kuwa tumbo lake moja haliwezi kujaza kuliko binadamu wote na pia maisha yake mafupi sana na yaweza refuka kama ataunganisha nia na wenzake. Nihepushie tamaa za mwili na mali, nipe weledi na urazini zaidi. Nipe hofu ya maovu na hasa rushwa!!! Niongoze katika njia ya majaribio na kamwe usiniache nijiamini na kujifanya mfalme kama hawa niwatukanao. Nikumbushe siku zote vazi safi la nakshi utkalonivisha baada ya kutwaa uhai wangu nikiwa nimeshinda vita vikubwa hapa duniani.

Wasalaam,

Makene Bonipahace Washington, DC
 
© boniphace Tarehe 11/23/2005 05:40:00 PM | Permalink |


Comments: 1


  • Tarehe 11/27/2005 4:55 PM, Mtoa Maoni: Blogger Jeff Msangi

    Makene,
    Hili wazo lako la kushukuru watu ni muafaka.Ingawa lina "umarekani" ndani yake haijalishi,ni muhimu.Sio mtu usubiri mpaka fulani afe ndio uanze kumsifia na kumshukuru.Kazi njema.

     
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved