Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Tuesday, November 08, 2005
MIAKA 40 NA NDOTO YA MAJI KUSINI TANGANYIKA
WARAKA huu kaniandikia rafiki yangu. Kwa sasa nitahifadhi jina lake lakini nitajitahidi kutouvunja waraka huu hata neno. Haya ndiyo maisha ya Tanzania na nafarijika sana kuona kila siku wanaongezeka watu wanaoyachukia huku wakijenga fikra za kubadili uelekeo.

TumeiShi miaka mingi na kero hizi zimezidi kuongezeka kuliko kupungua. Ushuhuda wangu wa hivi karibuni ni pale nilipotazama hali ya kuchoka kwa mji wa Iringa baada ya kutoka pale miaka mitano iliyopita. Wakazi wa huko ambao zamani walionyesha bashasha mathalani baada ya kubugia guduria la Ulanzi hivi sasa wanazidi kunyong'onyea na kujawa fikra za namna watakavyopata mapambazuko mapya.

Nisijaze sana maneno yangu sasa soma WARAKA huu na pia changia uwezavyo ikiwa ni kujenga tafakari kabla ya uchaguzi mkuu Tanganyika Desemba 14, 2005.

KAKA.
Naanza kupungukiwa na kiza kinene baada ya kutimia siku 40 toka msiba unipate, pasipo mzazi wangu kurejea kama nitumainivyo. Naanza taratibu kuvuta kasi nikisaka pa kuanzia. Ndipo baada ya kimya kirefu katika mitandao ghafla nakutana na blogu ya

Mwanazuoni. Tuyaache hayo.

Kubwa ni pitapita yangu katika kona za nchi hii hususan mikoa ya kusini. Kabla sijakueleza niliyoyaona huko, ni hiki kipindi cha propaganda za CCMkinachoruka hewani huku sauti ya Selestine Kakele ikirindima mithili ya mtu atoaye ushuhuda wa kutokewa na masiah. Ni mwana CCM mzuri amwagaye sera za chama chao, chama ambacho hata mimi nilikihubiri kuwa ndio haswa chama cha kutuongoza milele.

Sidhani kama nawe umebadili fikra zako za kugombea ubunge kupitia chama hiki. Sina hakika. Wako wengi.

Safari yangu ya mkoani Mtwara kupitia mikoa ya Pwani na Lindi ilijaa huzuni kuu na chuki ya dhahiri dhidi ya tabaka tawala. Ni safari ya takribani saa 30 mpaka kijijini kwangu kunakoitwa makao makuu ya wilaya ya Tandahimba. Safari hii ndefu imepambwa na barabara mbovu iliyojaa mashimo na vumbi ambayo magufuli na bosi wake wamekua wakiimba mithili ya chiriku aonaye mvua wakati wa ukame.

Njiani ni vibanda vya nyasi vilivyokaa upande na kukaribia kuanguka huku vikivutia kwa kupambwa bendera nzuri zenye neema-kijani na njano, na juu kidogo zina nembo maarufu kuliko zote kwa watu hawa-jembe na nyundo!!

Wasafiri wote tunafanana baada ya takribani masaa5 toka DSM. Tunajikuta katika sare isiyo rasmi-vumbi jekundu mpaka kwenye kope, wote tuliopangwa kwenye mabasi haya ambayo hayastahili kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine, zaidi ya kutoka Misungwi kwenda Kwimba ama Nzega siku za minada.

Alhamdullillah nafika salama, nikiwa ndani ya hiyo sare niliyokueleza. Baada ya kuwa ndani ya sare hiyo kwa saa 30, nagundua wanakijiji wananywea ghafla pale wanapokumbuka kuwa mgeni wao napaswa kuoga na kuondoa hiyo sare. Kisa?maji. Dumu hili la lita 20 hapa linauzwa kwa pesa taslimu, isiyopungua hata senti 5 wala kuruhusu mkopo. Ni pesa halali kwa malipo halali ya shilingi 500/= kwa dumu! Upo hapo.

Ni miaka takriban 44 ya uhuru, na uongozi wa chama chetu milele (CCM) mwanakijiji asiye na hata senti ya dona analazimika kutoa mia 500 anunue maji. Na hapa napata kujua kwanini wahenga walisema mgeni aje mwenyeji apone. Mahali hapa ambapo nazungumzia ni kama kilomita 15 toka mto Ruvuma(Ruvu-DSM ni km 71).

NAREJEA DSM nikiwa nimejaa makovu yatokanayo kurushwa na kujigonga katika gari. Kwa hasira namvaa huyu kada mpya wa chama chetu milele aitwaye NAWANDA. Bila haya namwambia mbele ya Kakele na Mbogoyo, kitendo chake kukumbatia chama hiki ni usaliti kwa nduguze ambao hawana ufunuo, elimu na upeo wa kuona kutokana na kutotembea, huku wakimaliza wiki bila kuoga.

Naendelea kumwambia kuwa heri wachaga wakipende maana japo barabara shemeji yao kawajengea, lakini hao nao hawakitaki. Sembuse wewe chinga?

Ni heri umwachie Mbogoyo maana babaye anagombea ubunge kule katika jimbo la Mihambwe. Na wewe Kakele?Twendeni huko vijijini ambako chama chetu kinapendwa na kuwa na ngome kuu, ili tukirudi hapa bodi kwenye foleni ya mkopo, tutakuwa na uwezo wa kujitizama na kujua kama kweli baba yetu ametulea vema, kiasi tunakwenda redioni na kumwimbia nyimbo lukuki.

Nakomea hapa kukupa tafakari, na kukujibu swali lako la kwamba-Mamwetta na Kakele lao moja? Naendelea kutafakari KASRI LA MWANAZUONI, mtandao ambao umekuwa maarufu ghafla kwa wanafunzi wenzangu wa MA-DS hapa mlimani.
Wasalaam
.
Siku chache zijazo:HUYU NDIYE RAIS WA TANZANIA...nani huyo?TEGA SIKIO.

NB. Sehemu nilizowekea wino ni kwa lengo la kutia mkazo tu: Makene

 
© boniphace Tarehe 11/08/2005 01:40:00 PM | Permalink |


Comments: 0


   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved