Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Monday, November 28, 2005
MABALOZI WA KISWAHILI MAREKANI KUTOKA TANZANIA

UNAOWATAZAMA hapa ni Watanzania wanaofundisha Kiswahili Marekani kwa mwaka 2005/06 katika mpnago unaoratibiwa na Furbright chini ya State Department. Mabalozi hawa wako katika majimbo mbalimbali hapa Marekani, kutoka kushoto ni; Clara Mtei,(Frolida), Subira kabula, (Western Virginia), Jacob Lubuva(Califonia), Boniphace Mazega Makene (Texas), John Mwaipopo (New Jersey) na January Afadhali John (Ilinois).

Kukutana kwa mabalozi hawa kulifanyika hivi karibuni huko Washington D.C. Kazi yao nasikia ni njema sana na wamekuwa wakijitahidi kupaza sauti ya bara la Afrika baada ya kugundua kuwa Tanzania hii uchi kama hakuna Afrika moja huru inayokubaliana na kuheshimiana. Nawapongeza kwa masaibu wanayokabiliana nayo huko maana inapokuja suala la wewe kuwa mweusi kwa mliowahi kufika nje ya nchi mnaweza kuwa na picha njema na mlio nyumbani mwatakiwa kuamka na kuchana na ubaguzi toka katika lugha na mwatakiwa kujenga kujali watu kwa sababu ni watu na sio rangi zao. Nadhani ujumbe huu unaweza kuwa muwali kwa Mfalme wa Jamhuri ya Tanzania ndugu Benjamin Mkapa.
 
© boniphace Tarehe 11/28/2005 12:35:00 PM | Permalink |


Comments: 6


 • Tarehe 11/28/2005 2:12 PM, Mtoa Maoni: Anonymous Mwaipopo

  Na hatuishii hapo tu. Pamoja na kujifunza yaliyo mema kutoka hapa Marekani, ambayo yapo mengi tu, na kuyaacha machafu hapa hapa, kazi nyingine ni kuwafuta ujinga hawa wamarekani kuhusu mtazamo wao kuhusu Afrika. Kwa mfano fikira ya walio wengi wao kuwa Afrika ni nchi moja na kwamba bado tunaishi vichakani, taswira wazipatazo kupitia filamu wanazopelekewa, ambazo zimesheheni uwongo na uzindiki mkuu. Kisha kuwachengua tu mimi niliwaambia namiss sana kamsosi ka panya (chamaki nchanga wa kule Ntwara, ingawaje sijawahi kuonja licha ya kutamani kufanya hivyo). Halafu nimewaambia kuwa kasehemu ka ziada waliyo nayo wasisahau,wakipenda, kukainvest kwenye elimu barani Afrika badala ya kupoteza kwenye miradi hasi mingi waliyonayo.

   
 • Tarehe 12/01/2005 5:45 PM, Mtoa Maoni: Blogger Ndesanjo Macha

  Suala la kufuta ujinga wa wamarekani ni kweli. Si unajua akina CNN ni vyombo vya habari za maafa. Tena maafa yanayotokea nchi za wengine sio yanayotokea MArekani. Na kuhusu chakula umenena...jamani...ugali wa kisamvu cha nazi...mtori...chipsi mayai pale kinondoni "american chips", au chipsi za usiku usiku kariakoo zinazomiminiwa ukwaju! We, na maji ya ukwaju na miwa. Na madafu. Vitu vyote hivi wengi tunaona kuwa ni vya ovyo kumbe akili zetu zinazotufanya tufikirie hivyo ndio za ovyo.

   
 • Tarehe 12/01/2005 5:48 PM, Mtoa Maoni: Blogger Ndesanjo Macha

  Makene, sasa nakupa kazi moja rahisi sana.

  Naomba hawa ndugu zetu, yaani Clara Mtei, Subira kabula, Jacob Lubuva, John Mwaipopo na January Afadhali John, uwaingize mmoja mmoja kwenye ulimwengu wa blogu. Mawazo yao, uzoefu wao, uelewa wao wa lugha tunahitaji katika kuimarisha "shihata" hii mpya ya umma ambayo haihitaji usajili toka kwa mtoto wa mtu!

   
 • Tarehe 12/01/2005 6:07 PM, Mtoa Maoni: Blogger Boniphace Makene

  Nimetuma ujumbe wako kwa ndugu hawa tayari. Nimekuwa katika hamu ya kuwaona nao wakijianzishia magazeti yao kama hili langu. Nimewakumbusha kuwa si lazima wawe na magazeti ya kila siku walau hata lile la mara moja kwa wiki na ninaona wananunua mawazo haya. Asante tena

   
 • Tarehe 12/01/2005 6:23 PM, Mtoa Maoni: Anonymous mwaipopo

  Ndesanjo nimekupata. Mwanazuoni mkamilifu Makene ananipa mafunzo kamili ya kufungua blogu. Mafunzo mengine tayari nimeshayapata kwenye blogu yako. Nafikiri sasa ni wakati wa pambazuko jipya Tanzania.

   
 • Tarehe 12/03/2005 11:34 AM, Mtoa Maoni: Blogger Ndesanjo Macha

  Mwaipopo, kweli huu ni wakati wa pambazuko jipya. Umesikia Tanzania Waziri Mkuu kafungua magazeti mawili, Tanzania Daima na jingine nimesahau jina. Sasa huku kwenye blogu sijui akitaka kutufungia atafanyaje!

  Watu wengi wanadhani kuwa teknolojia ya blogu bado haina nafasi kwa Tanzania na Afrika kwakuwa watu wengi hawana uwezo wa kupata kompyuta. Lakini kama mtu anafuatilia kwa karibu masuala ya teknolojia za kisasa atajua kuwa hivi sasa ili uweze kuingia kwenye intaneti sio lazima uwe na kompyuta, hata ukiwa na simu za mkono unaingia kwenye kompyuta, unatuma barua pepe na kusoma ulizotumiwa, unasoma blogu, n.k. Simu za mkono hivi sasa zimekuwa ni 1.simu 2. kamera 3. kompyuta 4. intaneti 5. shajara (notebook) 6. saa 7. kituo cha mawasiliano cha jamii (kutokana na tabia ya matumizi ya simu kijamaa katika jamii zetu za Afrika)....na kadhalika na kadhalika. Kwahiyo watu wanaodhani kuwa eti watu wa kawaida watakuwa wanasikia mambo ya mtandao kwenye bomba wamekosea maana simu za mkono zinakuwa kama njugu.

  Halafu sijui kama mmesikia kuhusu mradi wa "kompyuta kwa kila mtoto" wa Negroponte wa chuo cha MIT. Negroponte anatengeneza kompyuta za dola 100 au chini ya hapo, yaani itakuwa kama vile kununua simu ya mkono.

  Halafu faida ya kitu chochote kwenye jamii sio lazima kila mtu awe nacho. Faida ya magazeti sio mpaka kila mwananchi awe anayasoma, faida ya redio sio lazima kila mtu asikilize, faida ya kitabu sio lazima kila mtu akisome. Na faida ya intaneti na blogu sio lazima kila mwananchi awe na kompyuta.

  Hata viwanda vya vitabu vilipoanza kama kile cha Guttenberg kuna watu walisema,"aah, watu wengi wala hawajui kusoma faida yake nini?"

  Ninadhani kuwa teknolojia hizi kadri siku zinavyokwenda watu wengi watakuja kuona faida zake na pia watunga sera walio makini watapitisha sera ambazo zitawezesha watu wengi kufaidika. Kwa sasa hatuwezi eti kuacha kuzitumia kwakuwa asilimia kubwa ya watu wetu hawana uwezo wa kuzipata, tutatumia, watakapozipata watajiunga nasi au watakuwa tumetengeneza njia bora kwao.

  Ndugu Mwaipopo na wenzako, tunawasubirini.

   
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved